Profesa Abdulrazak Gurnah ni mwafrika wa saba kupewa Nishani ya Fasihi ya Nobel. Alipotangazwa, furaha ya wengi haikufichika kwani pongezi zilitapakaa kila mahali mitandaoni. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar, Dakta Hussein Mwinyi waliwaongoza wengi kutoa pongezi zao.
Waandishi na wanajamuiya ya uandishi wa Tanzania nasi tunampongeza. Hapa wapo waandishi nguli pamoja na waandishi chipukizi ambao tuzo hii imewahamisha sana waendelee kuandika. Pia wapo wadau wa tasnia ya uandishi kama vile wahariri, wachapishaji na watafsiri.
Waliotuma pongezi zilizokusanywa humu ni Shafi Adam Shafi, Ida Hadjivayanis, Ahmed Rajab, Anna Manyanza, M.G. Vassanji, Sandra Mushi, Walter Bgoya, Demere Kitunga, Richard Mabala, Ayeta Wangusa, Fadhy Mtanga, Nahida Esmail, Amil Shivji, Laura Pettie, Hussein Tuwa, Neema Komba, Said Ahmed Mohamed, Zuhura Yunus, Joseph Mbele na wengine wengi. Kwa hakika, ni heshima kubwa. Na ni jambo la faraja kuona waandishi wa Afrika wakiwa mstari wa mbele kumpongeza kwa kutunukiwa nishani hii.
Waandishi wengine kutoka barani Afrika ambao wamewahi kupokea heshima hii ni pamoja na Albert Camus (1957), Wole Soyinka (1986), Naguib Mahfouz (1988), Nardine Gordimer (1991), J.M Coetzee (2003), na Doris Lessing (2007).
Nilipoona jarida la mtandaoni la Brittle Paper likimpa hongera Prof. Gurnah kwa kupaza sauti za waandishi 103 kutoka barani Afrika, nilifurahi sana. Nilitamani na sisi Watanzania tuseme neno kwa pamoja tena kwa lugha yetu. Tumpe pongezi mwenzetu kwa heshima kubwa aliyopokea. Binafsi nimefurahi sana. Na kwa hakika, jambo hili limeweka alama kwa waandishi sio tu wa Afrika bali wa Tanzania, wa sasa na wa vizazi vijavyo.
Andiko hili nimeliandaa kwa Kiswahili lakini pongezi zina tafsiri ya Kiingereza itakayochapishwa baadaye humu Udadisi ili ulimwengu mpana zaidi nao ushiriki katika pongezi hizi.
Hongera sana Prof. Gurnah!
Sisi waandishi wa Tanzania tunakupongeza, tunakushika mkono, na tunafurahi pamoja nawe.
Pongezi hizi zimepangwa kwa kufuata majina ya waandishi kialfabeti.
Pongezi kwa Gurnah, ni kitu kila mtu anasema na watasema. Mimi nilikuwa nataka kuangalia namna gani tutapata Gurnah wengine. Si kwa kufanya vurugu za siasa ili watu wakimbie nchi kwenda kuandika ughaibuni kuhusu mashaka waliyokutana nayo. Hapana. Tuangalie ni nyenzo gani muhimu ili kupata waandishi bora. Nyenzo ni umahiri wa lugha.
Hivyo, ni muhimu tufundishe Kiswahili bora na Kiingereza bora. Umahiri wa lugha unatokana na kusoma vitabu vingi vya kila aina. Hii itawezekana tu ikiwa kuna mashirika mengi ya uchapishaji vitabu bora vitakavyonunulika. Katika nchi zinazoendelea mchango wa serikali ni muhimu. Kwa mfano, kuna shule za msingi zipatazo 17,000 na sekondari takriban 4,000 kati ya hizo ngapi zina maktaba zenye vitabu vinavyosomeka, si vile vya msaada kwa lugha ngeni?
Ingawa wapo wenye maoni tofauti, ushindi wa Abdulzarak Gurnah ni ushindi wa taifa letu. Binafsi nimeguswa sana, na ninatarajia mambo makubwa kwenye tasnia ya fasihi hapa Tanzania. Na ni matumaini yangu kuwa tamaduni zetu, vyakula vyetu, lugha na kila kinachoujenga utanzania wetu vitaendelea kumfanya msomaji aendelee kufungua kurasa na kusoma.
3. Ahmed Rajab
Zanzibar na Afrika inajivunia kuwa nawe mwandishi nguli. Hongera sana. Kwa hakika, unastahili heshima hii. Ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwapa hamasa waandishi chipukizi barani Afrika kuendelea kuandika.
4. Amil Shivji
Ni jambo la furaha sana kuwepo mmoja wetu, haswa kutoka Zanzibar – kitovu cha lugha ya Kiswahili kushinda tuzo ya fasihi ya Nobel. Natumaini hili jambo litarudisha haja ya kusoma na kuchambua kazi zetu wenyewe na kuleta msukumo upande wa waandishi kushika kalamu na kusimulia hadithi zao.
Kama Mtanzania na mwanafasihi, nimefurahi sana kupokea habari za kipekee kuwa mwaka huu mwanafasihi nguli, Prof. Abdulrazak Gurnah, ameshinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi. Tuzo hii ni tuzo ya kifahari sana, na imewahi kutunukiwa kwa wanafasihi maarufu, wakiwemo Toni Morrison (1993) na Wole Soyinka (1986). Ni ufahari mkubwa sana kwetu sisi Watanzania kufahamu kuwa tuzo hii hatimaye imefika nyumbani.
Kazi za Prof. Gurnah ambazo nimepata kuzisoma kabla ya ushindi huu ni Gravel Heart na Paradise. Ninamshukuru mlezi wangu wa Kiswahili, Mwalimu Abdilatif Abdalla, kwa kunitambulisha kuhusu kazi za Prof. Gurnah. Kupitia ushindi huu, fasihi kutoka Tanzania na Afrika nzima kwa ujumla, imethibitisha kwa mara nyingine tena umuhimu wake duniani kote.
Pongezi za pomoni zikufikie Prof. Abdulrazak Gurnah.
Hongera sana Prof. Gurnah kwa kupewa Tuzo ya Nobel katika Fasihi. Mawazo unayoyachambua kuhusu ukoloni, kumbukumbu na uhamiaji yanawagusa watu duniani kote na huonekana dhahiri kwa namna ambavyo kumekuwa na uhamiaji mkubwa wa Waafrika kwenda Ulaya kupitika Bahari ya Mediterranean; wafanyakazi wa kazi za ndani wanavyonyanyasika huko Mashariki ya Kati; Waafrika wanavyobaguliwa kwa kuwa raia wa nchi tofauti na ile wanayoishi barani Afrika. Asante kwa kusimulia simulizi zetu kwa ulimwengu.
Hongera sana Prof. Gurnah, umepeperusha bendera ya Tanzania vilivyo. Acha na sisi hapa nyumbani tupekue karatasi za vitabu vyako na kujivunia talanta za mzawa mwenzetu.
Ushindi wa Prof. Gurnah ni heshima kubwa kwa tasnia ya uandishi wa kazi za fasihi. Lakini pia unatutia ari waandishi tuendelee kuandika hata kama tusipopata chochote kwa sasa, tunaweza kutambuliwa au vipaji vyetu vinaweza kutambulika tukiwa hai, na hata kama tukiwa na umri mkubwa kama ilivyojitokeza kwa Prof.
Aidha, ushindi wake unafuta dhana iliyojengeka miongoni mwa waandishi au jamii kwamba mara nyingi katika nchi zetu waandishi hutambulika zaidi baada ya kufariki. Wakiwa hai hakuna anayewathamini. Pia, kuna kitu cha kujifunza; ni wakati muafaka na sisi tukaanzisha tuzo zetu kuwatunuku watu waliofanya mambo makubwa tukiwatengea zawadi nono zinazokaribiana na Tuzo ya Nobel. Kwa kufanya hivyo tutawapa motisha watu wetu na kuwajengea Watanzania utamaduni wa kuthamini kazi za sanaa na waandishi, kusoma vitabu na kuandika.
Ushindi wa Gurnah ni ushindi mkubwa kwa waandishi wa Tanzania. Sio tu kwamba tuzo hii imeleta hamasa kubwa kwa waandishi Tanzania, imeleta hamasa kwa wengine kuchochea vipaji vyao na kuandika. Nimefurahi sana, kama Mtanzania. Mlango umefunguka sasa kwetu sisi tuliopo diaspora.
10. Demere Kitunga
Nakumbuka kusoma kitabu chake cha Paradise zamani sana. Nilikipenda na nilitamani kusoma vitabu vyake vingine lakini sikujua nivipate wapi. Kile kitabu kilikuwa tofauti na vitabu nilivyowahi kusoma, na nilitamani kuuelewa huo utofauti zaidi, nimfahamu mwandishi zaidi. Lakini hata watu walionizunguka kwenye tasnia ya uandishi hawakuwa wanamfahamu vizuri kwa wakati ule. Nikajikuta nimeliweka hilo kando.
Tuzo hii imemleta tena kwangu, pamoja na kazi zake. Nimeshanunua vitabu vyake vyote na nitavisoma kwa miezi iliyobaki mwaka huu. Tuzo hii imerudisha kazi zake nyumbani, na kuwapatia ulimwengu pia.
Historia yetu imesimuliwa na mwenzetu ambaye baadhi yetu hatukumfahamu vema, na huenda waliomfahamu hawakuzipa simulizi zake umuhimu stahiki, ama pengine wachapishaji wake hawakuilenga jamii yake ya nyumbani kama ‘soko’ la kazi zake. Tofauti zetu na jinsi ambavyo taathira na tafsiri za historia yetu zinavyojitokeza zaweza kudhihirisha tofauti hizo. Binafsi ninaona kuwa ni wakati wa kuirejelea historia yetu iliyonyamazishwa, au kusimuliwa kwa mtazamo wa wageni, kwa manufaa yao.
Nimewasikia watu wakijadili kuhusu utaifa wake, nadhani hili ni jambo la ajabu sana! Mimi niliondoka kijijini kwetu nikiwa na umri wa miaka tisa. Nikaishi wilaya nyingine ya mkoa nilipozaliwa, lakini hadi leo kule nilikozaliwa ndiko ninakokuona kuwa ni nyumbani. Nyumbani ni nyumbani. Hakuna anayeweza kukupokonya au kukutunuku tafsiri yako ya nyumbani. Ni haki yako.
11. Diana Kamara
Prof. Gurnah kwangu ni kama Freddie Mercury. Anajulikana mno kimataifa lakini si jina maarufu sana nyumbani. Tumeufurahia ushindi wake wa tuzo lakini hatuna hakika tunautumiaje katika historia yetu. Tunajivunia kuwa tunatoka nchi moja lakini ni kweli tunaweza kusema tumechangia mafanikio yake?
Labda la muhimu ni serikali kufuatilia historia ya familia yake na kutunza kumbukumbu ya nyumba na mahali alipokulia. Ila hasa ni jukumu la wanahabari na wanahistoria kuuonesha ulimwengu kwa jinsi gani udugu wetu wa kihistoria na Bwana Gurnah umezalisha nyota huyu wa kimataifa.
Kwa wakati huu tunachofanya ni kuimba, “Hongera mwanangu, nami nihongere.”
12. Dotto Rangimoto
Nimeandika. Nimefuta. Nimeandika tena. Nikafuta tena. Nimeandika nini basi? Si kingine. Ila ni pongezi. Huku kufuta kwingi ni kwa sababu ya kukosa maneno toshelezi ya kuweza kuwasilisha pongezi zangu za dhati; na huu ndio usuli wa kuchelewa kutoa salamu zangu za pongezi. Hata hivyo leo wacha tu nizitoe pamoja na kwamba bado sijapata maneno ya kubeba pongezi zangu halisi.
Kutoka ndani kabisa ya kiini cha moyo wangu napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwako wewe Bwana Abdulrazak Gurnah kwa kushinda Tuzo ya Nobel katika kipengele cha Fasihi. Ushindi wako una maana kubwa sana kwa nchi yako ya Zanzibar na kwa Taifa letu la Tanzania.
Mimi kama mwandishi chipukizi wa Fasihi ya Kiswahili, Bwana Abdulrazak Gurnah umenishajiisha mno kuichonga kalamu yangu uzuri; na kwa kweli hivi sasa nimo katika kuichonga na niko na imani nayo itachongeka, Inshallah!
Aidha nina hakika jana wakati mshindi wetu unaandika riwaya zako hukujuwa kama kesho yako; ambayo sasa ni leo yako ingekuwa hivi ambavyo sote tunaishuhudia na kuisheherekea. Pengine cha mno ulichokuwa wakijua ni kuwa, kalamu yako itawakomboa wengi kifikra na kimtazamo; na pasina na shaka imeshafanya hivyo na nina yakini kwamba hata sasa yaendelea kufanya hivyo.
Ahsante sana Abdulrazak Gurnah kwa kulitangaza jina la Zanzibar na la Taifa letu la Tanzania katika anga za kimataifa. Hakika umeweza kutuheshimisha wenzako. Nakutakia kila heri na ninakuombea makubwa zaidi.
13. Elias Kasunga
“Inawezekana.” Ni neno la kwanza kuja akilini mwangu pale jina lako lilipotangazwa kama mshindi wa Tuzo ya Nobel katika Fasihi. Kujua kwamba tunachoandika sisi kama Waafrika kinaweza kugusa dunia ya fasihi na kwamba historia yetu inaweza kugusa mioyo ya walio nje ya mipaka yetu ni uhakikisho pekee niliohitaji mimi kama mwandishi chipukizi. Hongera sana na asante kwa kushirikisha dunia sanaa yako.
14. Elias Mutani
Ni fahari kwetu kwamba miongoni mwetu wana wa Afrika Mashariki, mmoja wetu amechomoza kuwa kinara. Imenipa msukumo wa ajabu wa kusonga mbele. Gurnah na waandishi nguli wenzake wanaotia maudhui ya Kiafrika katika medani za dunia ni kioo kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho. Hongera sana kwake.
Mimi Elizabeth Mahenge almaarufu Mamaaridhio/Mamakaifa, nakupongeza sana mtunzi Gurnah kwa kutukuka katika kazi zako. Mwenyezi Mungu azidi kukufanikisha katika ndoto zako ulizojiwekea. Amina!
16. Fadhy Mtanga
Sisi Watanzania, kwa hakika tunajivunia sana Mtanzania mwenzetu Prof. Abdulrazak Gurnah kushinda tuzo hii mufti ulimwenguni. Licha ya umbali wa maelfu ya maili kutoka mahali anapoishi, sisi Watanzania twaona raha.
17. Farida SomjeeHongera sana kwa Abdulrazak Gurnah kwa kupewa Nishani ya Tuzo ya Nobel katika Fasihi. Kila la heri.
18. Gloria Gonsalves
Sikuwahi kumsikia wala kumsoma Abdulrazak Gurnah hadi aliposhinda Tuzo ya Nobel katika Fasihi. Labda ni kwa sababu ya aina ya uandishi ninaopenda kusoma zaidi. Athari za baada ya ukoloni sio chaguo langu la kwanza. Hivyo, kumpongeza wakati sijawahi kusoma kazi zake za uandishi kwangu ilikuwa kama sio uaminifu. Vichwa vya habari vilizingatia hisia zangu kwa kunipa ufunuo mmoja mkuu. Kama mshindi wa Kitanzania, amewatunuku kwa pamoja Watanzania na Waafrika. Nilijawa na sifa.
Mimi pia nilipokea pongezi kutoka kwa wanafamilia na marafiki. Simu yangu ilijaa jumbe za kushinda kwake na pia hongera. Siku hiyo baada ya kutangazwa mshindi, nilihisi kama nimeshinda pia. Wakwe zangu Wajerumani waliniandikia barua pepe ya pongezi. Walisema (kwa hisani iliyotafsiriwa), “Tunakupongeza kwa ushindi wa Mtanzania mwenzako Abdulrazak Gurnah kutoka Tanzania/Zanzibar, ambaye amepewa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya 2021. Kweli, labda hamjuani lakini nyote mnapenda uandishi. Hongera.”
Ushindi wa Profesa Gurnah umeumba uwezekano wa kupata tuzo ya kifahari zaidi ya fasihi ulimwenguni, sio kwangu tu bali pia kwa waandishi wachanga. Kilichochochea uandishi wangu hapo awali ni kutaka kuthibitisha kuwa waandishi wa Kitanzania wapo hata katika nafasi ambazo sio kawaida kwa Waafrika. Hadi leo, siwezi kuelewa kile nilichowahi kusoma mtandaoni kwamba mtu hakujua Tanzania ina waandishi. Ushindi wake Gurnah umeongeza nguvu kwenye dhamira yangu ya kuonesha kwamba waandishi wa Kitanzania wapo na ulimwengu unawaheshimu.
Hongera Profesa Abdulrazak Gurnah. Asante kwa kutuletea sifa nyumbani.
19. Hussein Tuwa
Nampongeza sana Prof. Gurnah kwa kupewa Tuzo ya Nobel mwaka huu. Yeye amekuwa mwanga wa kuiangazia sio tu Tanzania, bali pia Afrika Mashariki, kwenye ulimwengu wa fasihi andishi duniani. Bila kujali kuwa ametumia lugha ya Kiingereza kwenye maandiko yake mengi, ni ukweli usiopingika kuwa ametoka kwenye nchi ambayo Kiswahili kimezaliwa. Hii inakiweka Kiswahili chetu kwenye hadhi ya juu zaidi kwa sababu ni lugha mama ya mshindi wa Tuzo ya Nobel kwenye Fasihi.
20. Ida Hadjivayanis
Kama Mtanzania aliyetokea Zanzibar, kazi zake Gurnah zinanigusa kipekee. Ushindi huu ni mkubwa sana! Gurnah hutumia maneno ya Kiswahili kwenye uandishi wake kwa lugha ya Kiingereza, na hivyo kuhimiza umuhimu wa lugha yetu. Husema kweli kwa kuweka kando mtazamo wa kikoloni. Yaani, nimefurahi kuliko maelezo.
21. Nahida Esmail
Hongera sana kwa Mtanzania mwenzangu Abdulrazak Gurnah kwa kushinda Tuzo ya Nobel katika Fasihi. Kwa bahati mbaya, kazi zake hazifahamiki sana na Watanzania. Lakini, pengine hilo litabadilika sasa. Na inasikitisha kwamba anatunukiwa heshima na Afrika baada ya kushinda Nobel. Hata hivyo, ni jambo la faraja kuwa ameirudisha tuzo hii kwa Waafrika. Na ninaamini ushindi huu utaongeza hamasa ya usomaji Tanzania.
Ninajisikia fahari sana kwa sababu ya ushindi huu, Mtanzania mwenzetu ameshinda Tuzo ya Nobel katika Fasihi. Kama mwalimu anayefundisha Kiingereza kwa mfumo wa Cambridge hapa Tanzania, nimeona umuhimu wa kuchagua vema kazi za fasihi kwa ajili ya wanafunzi wangu. Ndani ya miaka 2 iliyopita, tulianza kumsoma Wole Soyinka (aliyeshinda Tuzo ya Nobel katika Fasihi mwaka 1986).
Nimeona mabadiliko ndani ya wanafunzi wangu wakiwa wanasoma kazi za waandishi Waafrika ambazo zinaakisi mazingira na tamaduni zao. Kwa kutambua kule anakotoka mwandishi, ile kazi inakuwa na uhai mpya! Nina shauku kubwa kuona kazi za Gurnah zikianza kutumika kwenye mfumo wa ufundishaji wa Cambridge na NECTA hapa Tanzania!
Hongera Profesa Gurnah!
23. Joseph Mbele
Nampongeza sana mwandishi Profesa Abdulrazak Gurnah kwa kushinda tuzo adhimu ya Nobel katika fasihi. Katika Afrika nzima kuna waandishi wachache tu waliotangulia kupata Tuzo ya Nobel katika Fasihi. Wako ambao wameitamani tuzo hii kwa miaka na miaka, lakini imetua kwetu. Ni heshima ya pekee. Tufanye kila linalowezekana kuzitumia fursa zinazotokana na ushindi wa tuzo hii. Nampa pongezi nyingi mwandishi wetu.
24. Laura Pettie
Tunapoiongelea tuzo ya Nobel, tunaongelea kitu kinachotambulika kimataifa. Tena ikiwa ni tuzo kubwa zaidi duniani. Hili si jambo dogo.
Ikiwa mshindi wa tuzo hiyo upande wa fasihi, Profesa Abdulrazak Gurnah, anatajwa kuwa mtu mwenye asili ya Zanzibar ambayo ni nchi mmojawapo inayounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, basi, binafsi naona fahari na ninafikiri wanafasihi wa pande zote tuna kila sababu ya kumpongeza na kujivunia.
Ni kutambulika kwa mwanafasihi mmoja kimataifa, ambaye jina lake linapotajwa, Zanzibar au Tanzania inatajwa pia. Hii inafungua milango ya fasihi yetu kuanza kufuatiliwa kwa umakini has ukizingatia kuwa baadhi ya kazi zake zimegusa historia ya alikotoka. Hili si jambo dogo asilani.
Kupitia ushindi huu, uwanja ni wetu kucheza na fursa. Uwanja ni wetu wa kufanya kazi bora zaidi. Uwanja ni wetu kujifunza kitu chanya kupitia ushindi huu. Asili yake ni zawadi kwetu. Tuzo yake ni ramani kwetu.
25. Lello Mmassy
Niliposikia Mtanzania ameshinda tuzo ya Nobel nilipasuka kwa furaha. Nikasema, ‘alaa ivoo’ kumbe haya mambo yanawezekana ati? Nampongeza sana Prof. Abdulrazak Gurnah kwa ushindi huu. Ameinua ari yangu na hamasa yangu katika uandishi. Sitachoka, sitakata tamaa. Siku akija Tanzania natamani kukutana nae.
Nimepata tumaini kushuhudia mwandishi kutoka nchi yangu akipeleka hadithi zilizotokana na mazingiza yetu duniani kote. Tuzo imemfikia kwa wakati muafaka na kwa haki zote. Hongera na asante sana Prof. Gurnah. Namtakia kheri kila mwandishi atakayefuata nyayo zako.
27. Lubacha Deus
Hongera kwake Abdulrazak Gurnah kwa kushinda tuzo hii ya heshima. Ni jambo kubwa kwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla. Naamini wengi wamepata hamasa mpya kuhusu uandishi. Ni ujumbe kuwa haijalishi rangi yako na mahali gani unatokea, bado unaweza kutambulika na kuheshimika kama mwandishi ukiamua kusimamia ukweli.
Hata hivyo, waandishi wasiandike ili washinde tuzo. Waendelee kuandika mambo yatakayodumu kwa ajili ya bara hili na dunia kwa ujumla. Kwa njia hiyo waandishi tutatambulika kama watu tuliotoa mchango katika kuifanya dunia mahali salama zaidi.
28. M.G. Vassanji
Hongera sana, Abdulrazak. Unastahili tuzo hii.
29. Mkuki Bgoya
Asante sana ndugu Gurnah kwa kushinda tuzo hii ya kimataifa ambayo pia imemulika jamii yetu ya wanafasihi ambayo imesahaulika kwa muda mrefu hapa Tanzania. Umeziinua kazi zetu za fasihi, hususani za utunzi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikipuuzwa. Umeonesha kuwa unaweza kuitangaza nchi yetu duniani kwa kutumia kalamu tu na ubunifu wa akili yako. Umewaonesha Watanzania kuwa waandishi wetu wanastahili kulelewa, kulindwa na kusheherekewa kwanza hapa nyumbani ili tuwezeshe kuwepo akina Abdulrazak Gurnah wengineo huko mbeleni.
Hii ni kumbukumbu nzuri kwa serikali na jamii yetu kwa ujumla kuwekeza kwenye kununua vitabu vya waandishi wetu na kuvisambaza kwenye maktaba, kuanzisha programu za kusoma na kuandika kwa watoto mapema, kusimamia hakimiliki za waandishi na kulinda kazi zao kutokana na uharamia na mwisho kuwekeza zaidi kwenye kujenga taifa la wasomaji ili iwe chachu ya kuongeza matumaini kwa waandishi chipukizi. Ni mzigo mzito kumbebesha mtu mmoja lakini tunashukuru kwa kuwa yeye ni alama ya ubora unaowezekana kutoka Tanzania.
Hongera sana Mzee.
Kama Mzanzibari, namuadhimisha Abdulrazak Gurnah kama mwakilishi na msimulizi wa hadithi ya nchi na watu wangu kwenye jukwaa la kimataifa. Tuzo yake ni tuzo kwa hadithi yetu na alama ya kudumu kwa utambulisho wetu.
Mimi nataka kusema zaidi ya fakhri kubwa aliyotupa Watanzania wote. Namshukuru kutuonesha kwamba kuandika masuala ya kwetu yaani maisha ya kukua Zanzibar, mahusiano na mambo ya kila siku sio jambo dogo ama la kupuuziwa, bali ni elimu kwa dunia. Kupata ushindi huu mkubwa inaonesha kwamba msomaji anaweza kuvaa viatu au kofia japo kwa muda mchache na kuwa Mzanzibari na Mtanzania. Hilo sio jambo dogo bali ni la ustadi mkubwa.
32. Mwafrika Merinyo
Nampongeza kwa dhati Abdulrazak Gurnah kwa kupewa tuzo ya Nobel katika Fasihi. Tuzo ya Nobel ni moja ya tuzo zenye heshima kubwa duniani, na hivi Waafrika na Watanzania tunaona fahari kubwa kwa mzawa huyu wa Afrika kuipata tuzo hii.
Yawezekana kwamba kazi za Gurnah si bora kuliko kazi za waandishi wengine wote katika Afrika au Tanzania, lakini tuzo hii yaweza kuwa utambuzi wa namna kazi yake katika fasihi ilivyoweza kugusa maisha ya wasomaji, na huenda maisha ya watu wa jamii yake pia. Naona fahari ya kipekee kwa tuzo hii kufika katika mikono ya Mwafrika mwenzangu!
33. Nancy Lazaro
Nimefurahi sana na najisikia fahari kuishi katika zama ambazo mshindi wa Tuzo ya Nobel ametoka miongoni mwetu sisi wenyewe, Mtanzania, Mwafrika. Asante kwa kututengenezea njia kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Mafanikio yako yanatusukuma kushikilia ndoto zetu na kuendelea kufanya kazi kuhakikisha zinatimia.
Umefanya iwe rahisi kwa watoto wetu kuwa na ndoto juu ya maisha yao, na kwa vizazi kuendelea kustawi. Umetukumbusha umuhimu wa kuelezea hadithi zetu, katika kweli na kwa shauku. Umetupa sababu ya kuendelea kukuza na kutumia sauti zetu.
Hongera, Bwana Abdulrazak Gurnah kwa kushinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi mwaka 2021. Hakika unastahili tuzo hii. Wakati umewadia!
34. Neema Komba
Hongera sana Prof. Abdulrazak Gurnah kwa ushindi huu, hakika unastahili. Ni furaha kubwa na matumaini pia kwa waandishi wote wa Afrika, Tanzania na duniani. Mimi kwama mwandishi ninehamasika sana na ushindi huu.
35. Ngasuma Kanyeka
Gurnah ametutoa kimasomaso Waafrika na Watanzania. Mbali ya kumpongeza pekee, hii iwe fursa ya kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye uandishi si tu kwa sababu ya kushinda tuzo, bali kwa sababu hadithi zetu, historia yetu na uhalisia wa maisha yetu unastahili kuelezwa. Kuna thamani kubwa katika hilo.
36. Ngollo Mlengeya
Kwako Prof. Gurnah,
Hongera sana kwa kushinda Tuzo ya Nobel katika Fasihi. Umefanyika mfano wa kuigwa kwa wengi wetu na kutujengea hali ya kuthaminiwa.
37. Pepita Mwanga
Asante kwa mchango wako kwenye fasihi. Unastahili pongezi, hongera Abdulrazak Gurnah.
38. Richard Mabala
Pongezi zangu za dhati zimwendee Abdulrazak Gurnah kwa kushinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi. Anawakilisha mwelekeo ambao kwa bahati mbaya umeshamiri mno wa waandishi wa Kiafrika ambao hupata masaibu na kuishi uhamishoni. Lakini hufanikiwa kugeuza waliyoyapitia kuwa fasihi bora ambayo hutupatia sisi sote mafundisho mengi.
Nina furaha kubwa kumpongeza Mzanzibari na mwandishi mwenzangu kwa kushinda tuzo ya fasihi ya Nobel. Ni matumaini yangu kuwa waandishi chipukizi watapata hamasa kuendelea kuandika na kuchapisha vitabu vyao.
40. Sandra Mushi
Salamu za pongezi kwako Mzee Gurnah!
Umetunukiwa tuzo hii ya heshima na ni wazi kuwa umestahili. Umetumia talanta yako ya uandishi kujulisha na kuelimisha jamii juu ya muktadha usio rahisi kuwasilisha kiyakinifu. Nimehamasika kwa namna isiyoelezeka, kwani wewe ndiyo Mtanzania wa kwanza kutunukiwa tuzo hii na sasa ni hamasa kwa waandishi wengine wengi pamoja na wenye ndoto ya uandishi.
Tuzo hii ya Nobel ni utambuzi wa mchango mkubwa ulioshiriki na jamii kwa njia ya riwaya. Umeacha alama kubwa sana hususani kwa jamii ya Watanzania na itakumbukwa na vizazi vingi.
Kwa heshima, taadhima, pongezi na shukhrani tele – hongera sana, Mzee Gurnah!
41. Sauda Simba
Hongera kwa Abdulrazak Gurnah kwa kushinda tuzo hii ya heshima ya Nobel katika Fasihi. Ameiweka Tanzania na Zanzibar kwenye ramani na Afrika kwa mara nyingine tena. Tunamkaribisha nyumbani kwa mikono mikunjufu, sio tu kumpa tena alichokipoteza miaka mingi iliyopita lakini pia aweze kujihusisha na kazi za fasihi, wapenzi wa vitabu Tanzania bara na Zanzibar. Tunajivunia.
42. Shafi Adam Shafi
Mimi nampongeza sana Gurnah. Sikumjua leo, nimesoma kazi zake karibu miaka mitano/sita iliyopita. Nimesoma kitabu chake Paradise, Admiring Silence, Desertion. Kwa hiyo nimeanza kumsoma siku nyingi Gurnah na nimeanza kumpenda sana siku nyingi. Na nazidi kumpenda kwa sababu ni Mtanzania na ni Mzanzibari.
Nafikiri mimi nilikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupata habari kuwa alipata hiyo Nobel Prize. Na jambo la kwanza nililofanya nilipopata hiyo habari ni kuwasiliana na watu wanaohusiana na tasnia ya vitabu, Watanzania tuseme chochote kuhusu kushinda kwake. Sasa nimefurahi kwanza kuona kwamba Rais wetu wa Zanzibar ni miongoni mwa waliompongeza rasmi na amemwalika Gurnah aje Zanzibar ambako ni kwao.
Mimi nampongeza, nampongeza sana sana. Nasikia fahari. Naona kama mimi ndiye niliyeshinda.
Hatujawahi kukutana. Ila nawajua kwao. Yeye ni mdogo kwangu. Na hatujawahi kukutana uso kwa uso tukaongea. Ningefurahi sana kukutana naye uso kwa uso kama angekuja huku.
Kwako Abdulrazak Gurnah,
Jina langu ni Shimbo Pastory William. Ni mwandishi chipukizi kutoka Tanzania. Nimehamasika sana na ushindi wako ambao kwa hakika unastahili. Kwa hakika, umetupa hamasa kubwa haswa sisi vijana wenye mapenzi ya dhati na uandishi unaohusu huku kwetu. Ninaandika kwako kutoka Glasgow, Scotland.
44. Sima Mittal
Heshima kwako Mzee,
Ninakupa pongezi nyingi kwa mafanikio yako!
Wasalaamu!
45. Sylvia Ilahuka
Ndugu yetu Abdulrazak Gurnah, hongera sana kwa kutunukiwa hii tuzo ya kifahari. Tunakusifu kwa kuiweka Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwenye ramani katika fani ya uandishi. Ni tumaini letu kuwa huu ushindi wako utawahamasisha na kuwafungulia njia waandishi wengine kutoka pande zetu za ulimwengu.
46. Walter Bgoya
Nakupongeza sana Profesa Gurnah kwa kutunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi. Kama ilivyo kwa wananchi wengine, na haswa kama mchapishaji vitabu, Mkuki na Nyota, tunafurahia na kujivunia heshima na umaarufu ambao Tanzania imepata kupitia vitabu vyako. Hakuwezi kuwa na ushahidi bora wa nguvu ya fasihi, kuliko jinsi jina lako na kazi zako zinavyosherehekewa nchini Tanzania, Afrika kwa ujumla na ulimwenguni kote. Na hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa. Fasihi ni chemchemi iliyojaa maarifa na ufahamu wa kila kinachohusu maisha ya mwanadamu haswa mwandishi wake anapokuwa na kipaji kama chako.
47. Wilbard Makene
Ni Afrika tena. Bara lililosemekana kujaa giza. Kwa muongo mmoja uliopita hili halikuwa kweli. Afrika inang’ara.
Wana wa Afrika wanaiangazia Afrika. Ni Abdulrazak Gurnah, mshindi wa Tuzo ya Fasihi ya Nobel kutoka Tanzania. Amepewa tochi, tochi ya kuiangazia Tanzania na Afrika kwa mara nyingine tena. Hongera Prof. Abdulrazak Gurnah!
48. William Mkufya
Mimi nampongeza kwa kuliletea Taifa heshima kubwa mno ya kifasihi. Vijana wajitahidi kufuata nyayo zake. Wasome fasihi kwa dhati.
49. Zuhura Seng’enge
Moyo unasikia raha kusikia kuwa mwandishi, tena Mtanzania amefanya mambo makubwa! Ni wasaa wa kujivunia kwetu sote. Nami binafsi nimehamasika kuendelea kujijenga kiuandishi.
Hongera kwa Gurnah!
50. Zuhura Yunus
Nilipata furaha isiyo na kifani niliposikia kuwa Profesa Gurnah ameshinda tuzo hii adhimu. Natumai Watanzania na Wazanzibari tutaitumia hadhi na heshima hii kuzitangaza nchi zetu na kuchochea hamasa ya kusoma na kuandika zaidi. Hongera sana Mwananobel!
Hongera kubwa isiyo kifani kwa mwandishi wetu mahiri profesa Gurnah kwa kupata tuzo hii ya kimataifa. Nilijisikia furaha na kuongeza kujiamini katika tasnia ya uandishi ninayoianza. Hakika umeliletea Taifa na Bara letu sifa kubwa. Umekua ni moja ya chumvi inayokuza vipaji kwa waandishi wetu.
Pongezi nyingi Abdulrazak Gurnah. Pongezi kwako Esther kwa kukusanya salamu hizi za pongezi. Pongezi kwa waandishi kwa pongezi na kuhamasika. Tuendelee kuienzi fasihi yetu.
Hata Nami nashiriki kwenye pongezi hizo. Kushinda kwake iwe ni chachu ya kutupa bidii ya kufanikisha malengo yetu.
Hata Nami nashiriki kwenye pongezi hizo. Kushinda kwake iwe ni chachu ya kutupa bidii ya kufanikisha malengo yetu.
Nimefurahi sana aliyeunganisha umaarufu wa kimataifa alioupata Prof. Abdulrazak Gurnah na ule wa Freddy Mercury. Iko siku naye Fredy Mercury tutamuenzi tu hapa nyumbani. Anastahili and I can’t wait for that day to come!
Hongera Abdulrazak Gurnah kwa ushindi wa Nobel Prize.
Pole sana kwa kukimbilia uhamishoni. Natumaini ushindi wako utatufundisha sisi sote watanzania umuhimu wa kutengeneza mazingira rafiki kwa watanzania wote bila kujali tofauti zetu, na pia kuwaenzi watanzania wenzetu kwa umahiri wao popote walipo duniani.
Shukrani kwa Esther na waandishi waliotuma salamu zao za pongezi kwenye makala hii. Natamani orodha ya waandishi hawa isambazwe mashuleni na kwenye maktaba ili wengi zaidi wasome kazi zao za uandishi na kuwaenzi bila kusubiri dunia iwatambue kabla yetu.
Shukrani pia kwa Udadisi kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuwatangaza watanzania mbalimbali katika fani za uandishi na nyinginezo.