Leo tulitembelewa na Mwanazuoni Mkongwe, Profesa Ali A. Mazuri. Alikuja kutoa mhadhara kuhusu Uislamu Barani Afrika – Ukuaji, Uamsho na Uchachuaji Wake. Kama kawaida yake aligusia masuala mengi, watu wengi na nchi nyingi. Kuhusu Tanzania/Zanzibar aliusifia muungano kuwa ndio muunganiko pekee wa nchi za Afrika uliobaki na kuitolea mfano nchi yetu kuwa imeweza kuwa na ‘ustaarabu’ katika miingiliano na migongano ya dini ya Uislamu na Ukristo. Hapa alikuwa anamaanisha kuwa hata tukiwa na migongano ya kidini bado huwa tunaijadili na kujaribu kuitatua ‘kistaarabu’ tofauti na nchi zingine ambazo zimefikia hatua ya kuwa na machafuko na mapigano ya kidini.

Alipoulizwa kuhusu suala la udini Tanzania na malalamiko ya kihistoria kuhusu upendeleo wa kisiasa na kielimu alisema nchi yetu ilikuwa na afadhali katika hilo kuliko nchi kama Ivory Coast. Hapa alikuwa akimaanisha kuwa pamoja na kuwa nchi zote mbili zilikuwa na Marais wa kwanza Wakristo tena Wakatoliki lakini Tanzania haikufikia kwenye kiwango cha ubaguzi wa kidini katika kutoa nafasi za kielimu na kisiasa ambacho kilifikiwa huko Ivory Coast. Pia alisema mlolongo wa kuwa na Rais Mkristo kisha Muislamu ambao umeweza kufanyika katika awamu nne ni jambo zuri na amejaribu kutoa ushauri huo kwa Nigeria ambayo inakabiliwa sana tatizo la udini katika medani ya kisiasa. Lakini alikiri kuwa kuna umuhimu wa kutatua tofauti hizo za kihistoria ndani ya nchi za Kiafrika ila sio kwa namna ambayo inapelekea jamii fulani ya kidini au kikabila kuilipa jamii zingine kama ambavyo wanadai nchi za Magharibi zizilipe nchi za Kiafrika. Hivyo, changamoto ni kujaribu kutafuta njia mbadala inayofaa zaidi kutatua matatizo na tofauti za kihistoria yanayosababisha kuwe na udini n.k.

Profesa Mazrui pia alitumia muda mwingi kujaribu kutofautisha ustaarabu wa kiislamu na dini ya uislamu. Alitumia mifano ya jinsi ambavyo wazungumzaji mbalimbali wa Kiswahili wamerithi ustaarabu wa Kiislamu katika maneno ya lugha yao japo sio waislamu. Katika kuweka msisitizo alitoa mifano ya maneno mbalimbali ya Kiarabu na jinsi yalivyokuwa sambamba na maneno ya Kibantu kana kwamba kulikuwa na fundi muashi aliyekuwa anajaribu kuhakikisha kuna uwiano fulani. Kwa mfano, majina ya nambari tano za kwanza – yaani moja, mbili, tatu, nne na tano – yote ni ya Kibantu ilhali namba kama ishirini, thelathini na elfu ni ya Kiarabu. Pia maneno ‘mashariki’ na ‘magharibi’ yanatokana na Kiarabu wakati ‘kusini’ na ‘kaskazini’ yanatokana na Kibantu’. Neno ‘Rais’ linatokana na Kiarabu ilhali ‘Bunge’ linatokana na Kibantu. Hali kadhalika neno ‘jioni’ linatokana na Kiarabu ilhali ‘asubuhi’ linatokana na Kiarabu. Mfano mwingine alioutoa kama changamoto ni wa neno ‘amani’ linalotokana na Kiarabu na neno ‘vita’ linalotokana na Kibantu. Kwa ujumla, alikuwa anajaribu kuonesha kuwa kuna masuala mengi ambayo jamii zimerithi kutoka kwenye ustaarabu wa kiislamu – kama vile mavazi yanayotumika wakati wa kuhitimu shahada za chuo kikuu na numerali – ambayo sio lazima yamfanye mtu awe muislamu na kuna umuhimu wa kulitambua hilo.

Maswali mawili aliyoyaibua ambayo anadai yanapaswa kufanyiwa kazi na watafiti wa historia ya Uislamu na ambayo huwa anawauliza wanafunzi wake ni: (1)Kwa nini Irani na Misri ambazo zilivamiwa na Waarabu katika vipindi vilivyopishana kidogo sana zilifuata mkondo tofauti ambapo Misri iliarabishwa ilhali Irani haikuarabishwa? (2) Kwa nini waislamu kutoka Asia waliohamishiwa Afrika Kusini waliweza kuendelea na Uislamu wao kwa takribani karne 3 ilhali waislamu waliohamishwa kutoka Afrika kwenda Marekani walipoteza Uislamu wao?

Kuhusu yanayojiri Libya alioneshwa kusikitishwa sana na mapambano yaliyojikita katika ubaguzi wa rangi na kudai kuwa hali hiyo katikaa kiwango hicho haijawahi kutokea tangu wakati wa mapinduzi ya Zanzibar. Ilhali mapambano ya Zanzibar yalikuwa kati ya ‘Waafrika Weusi’ waliokuwa wamenyimwa fursa dhidi ya Waarabu, Profesa Mazrui alisisitiza, yale ya Libya ni ya Waarabu dhidi ya ‘Waafrika Weusi’ wasio na fursa. Aliongeza msisitizo kuwa kuna Walibya wengi sana ambao ni ‘Waafrika Weusi’. Katika kusisitiza hilo alihoji mbona katika mapambano ambayo Wamarekani na Wayahudi wanahusika neno ‘mamluki’ halitumiki? Japokuwa hakumtetea Gaddafi alikiri kusikitishwa sana na kitendo cha kumuua kwa namna ile na kutoa mfano wa wauaji wa Kinazi wa Ujerumani ambao pamoja na mabaya yao yote walipewa fursa ya kuhukumiwa kule Nuremburg kama wanadamu wenye haki hiyo.

Kuhusu Jos na Boko Haram huko Nigeria alisikitishwa na hali hiyo. Japo alikiri kuwa pamoja na kuelimishwa katika elimu ya kimagharibi na yeye ni mpinzani wa masuala mbalimbali ya elimu hiyo ila hakubaliani na upinzani wa elimu unaondeshwa na kikundi hicho. Na kuhusu Somalia na Kenya alionesha wasiwasi mkubwa kuhusu Wasomali wa Kikenya wasiohusika kwa lolote na mashambulizi ya Al-Shabab kujikuta wanahukumiwa na jamii bila hatia yoyote.

Ombi lake kubwa ni kurejea kwa hali ya ubinadamu.