YAH: USHAURI NA MAPENDEKEZO JUU YA NAMNA NZURI YA UDHIBITI WA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA KORONA
Mheshimiwa Rais,
PASIPO kumung’unya maneno, ugonjwa wa Korona ndiyo changamoto kubwa zaidi ya kiuongozi, kiuchumi na kibinadamu kwa viongozi na serikali zote duniani katika kipindi cha miaka 100 iliyopita. Tangu ugonjwa hatari wa Spanish Flu uue takribani watu milioni 50 duniani kote mwaka 1918, hakujatokea tishio linguine zaidi ya hili la Corona.
Ndiyo sababu, katika nyakati kama hizi, ni muhimu kwa viongozi wa aina zote; dini, siasa, sekta binafsi, serikali na makundi yote mengine, kuweka tofauti zetu pembeni na kuungana ili kupambana na tishio hili.
Boti tunayosafiria ni moja na ikizama tutakufa wote. Huu ndiyo msingi wa barua yangu hii kwako; ambayo ni ya kwanza kukuandikia tangu uwe Rais wetu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Kwanini Corona ni hatari?
Nafahamu kwamba unajua lakini kwa ajili ya kukupa ule utakaokugusa zaidi, naomba nitumie mfano wa Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines). Natumia mfano huu kwa sababu nafahamu kiu yako ya kutaka kupanua biashara ya anga hapa nchini.
Katika miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, Shirika la Ndege la Ethiopia halikuwahi kusimama kuacha kazi ingawa taifa hilo limepita katika njaa na ukame wa kutisha, vita ya wenyewe kwa wenyewe, vita dhidi ya Eritrea na majanga yote mengine ya kibinadamu. Bado shirika hilo liliendelea na kazi.
Lakini juzi, watawala wa taifa hilo wametangaza kwamba kwa sababu ya Corona, hatutaona tena ndege za shirika hilo zikipaa angani. Ndege za shirika letu la Air Tanzania tayari zimetangaza kusitisha safari zake za kwenda katika maeneo yaliyoathirika na Corona.
Changamoto za Tanzania
· Uchache wa Vyumba vya Wagonjwa Mahututi (ICU spaces): Takwimu rasmi za serikali zinaonyesha kuwa nchi yetu ina ICU chache sana na muda mwingi zinakuwa zimejaa.
· Uchache wa Vifaa Tiba za kutibu wagonjwa wa Korona kama vile mashine za kusaidia kupumua – ventilators, PPE, kwa ajili ya watoa huduma za afya na kadhalika.
· Uchache wa Wataalamu wa Afya ambapo tuna nakisi ya wataalamu wa ngazi zote wanaozidi 150,000. Wataalamu wa kuendesha ventilators ni wachache mno.
· Hatari kwa wenye UKIMWI na Wazee: Korona hushambulia mfumo wa kinga ya mwili. Kwa watu ambao tayari kinga yao ya mwili iko hatarini; kwa mfano wenye UKIMWI, wazee, wenye magonjwa kama kisukari na kansa, hali ni ya hatari. Kuna mamilioni ya Watanzania wako hatarini. KINGA NI BORA KULIKO TIBA.
MAPENDEKEZO
Mimi kama Mtanzania mzalendo, Mbunge na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo chenye wanachama zaidi ya milioni moja Tanzania Bara na Zanzibar, nina wajibu wa kutoa mapendekezo machache ili kupambana na adui huyu aliyetuvamia.
Kwa heshima na taadhima, ninapendekeza yafuatayo;
I. Umoja wa KITAIFA: Hakuna wakati nchi yetu inahitaji umoja kama wakati huu. Wewe kama Mkuu wa Nchi una wajibu mkubwa wa kuwaweka Watanzania pamoja kwa vitendo.
II. Wataalamu: Ni muhimu kwa viongozi kuacha kutoa kauli za jumlajumla na badala yake tuwaachie wataalamu watoe maelekezo ya kitaalamu.
III. KUPIMA: Kwa sababu sasa tumepata msaada wa vifaa kutoka kwa taasisi kama CDC na tajiri Jack Ma, ni muhimu kuendesha kampeni kubwa ya kupima watu. Nchi zilizofanikiwa kupambana na tatizo hili, ni zile zilizopima zaidi.
IV. UWAZI: Mheshimiwa Rais, tusione aibu hata kidogo kuweka wazi idadi ya Wagonjwa wa Korona kwani kuna faida zaidi kuliko kuficha.
V. TUEPUKE MAELEKEZO YANAYOPINGANA: Serikali ilichukua hatua mwafaka kufunga mashule na vyuo kote nchini ili kuzuia maambukizi. Hata hivyo, tangu wakati huo, viongozi wamekuwa wakihutubia mikusanyiko ya watu na kutoa kauli zinazokinzana na ujumbe huo.
VI. MAHABUSU na WAFUNGWA: Ni muhimu kuondoa zuio la dhamana kwa kesi zote ambazo zimewekewa zuio au ambazo hazina dhamana kisheria lakini upelelezi bado unaendelea watuhumiwa wasubiri upepelezi wakiwa majumbani mwao ili kupunguza msongamano magerezani. Watuhumiwa au Wafungwa wenye umri zaidi ya miaka 65 na wagonjwa wenye magonjwa hatarishi kwa Korona (underlying conditions) waachiliwe warudi majumbani mwao ama kumalizia vifungo au kusubiri upelelezi wa kesi zao.
VII. Shughuli za kila siku: Kuendelea na maisha kama kawaida ni hatari. Ni muhimu hatua kama za kufunga mipaka na kuzuia msongamano katika vyombo vya usafiri zichukuliwe kwa haraka.
VIII. TUHAMI UCHUMI: Hatua tutakazochukua kuzuia mashambulizi ya Korona lazima zitaathiri Uchumi wetu. Nakusihi sana Rais kuwa timu ya wataalamu wa uchumi nchini iundwe na kuanza kazi mara moja. Bahati mbaya sana tulivunja Tume ya Mipango kwani ingekuwepo ingefanya kazi hii na kulishauri Taifa mara moja hatua zinazofaa kuchukua. Haidhuru, unaweza kuunda timu ya muda kukidhi haja za sasa.
Mheshimiwa Rais,
Mimi na wenzangu kutoka chama ninachokiongoza, tuko tayari kutoa ushirikiano wowote unaohitajika katika kupambana na janga hili.
Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
ACT Wazalendo