Na Neema Komba (@Neysk)
Wanahoji alikuwa nani.
Ni mtu maarufu hapa mjini, au mtoto wa nani?
Maisha yake yalikuwa vipi,
Ni mrembo, mcheshi, au mambo safi?
Alivaa nini?
Alikunywa nini?
Alikuwa wapi?
Alifanya nini hadi wamfanyie ukatili?
Usiulize alikuwa nani.
Yeye ni dada yako,
Aliyekua njiani kwenda dukani kununua mahitaji
Lakini bila sababu wakamvuta kwenye kichaka,
Wakaiiba thamani yake na kumtupa kama ni taka,
Haiba yake wakaichana mithili ya nguo yenye kiraka,
Lakini wale vijana walisema eti kisa ni khanga,
Haikuwa ngumu ya kutosha kuficha maumbile yake machoni mwao,
Mwendo wake wa upole uliwaita,
Wakatamani, wakachukua kwa nguvu,
Kama vile mwili wake ni mali yao.
Walimgaragaza chini kwenye kokoto,
Lakini hata ncha za mawe zilizochoma mgongo wake
Hazikua kali kuzidi macho yao,
Yaliyomvua thamani na kumfanya
Si mtu, si kitu, bali mzoga
Mwanamke asiye na haki ya kuishi huru na salama ndani ya mwili wake.
Usiulize alikuwa nani.
Ni mama yako nyumbani kwake,
Anayejipa moyo kuwa zimwi likujualo halikuli likakwisha,
Na siku moja hapana yake itakuwa halali kwa mume wake,
Lakini sauti yake haisikiki,
Na kilio chake cha kwikwi hakimsikitishi,
Anaendelea kumpiga kama mwizi,
Tena pamoja na maumivu
Anamlazimisha ale zake mbivu
Bila kujali bado ni mbichi.
Huyatazama madonda yake kwa uchu,
Na kusema,
Yeye si mtu, si kitu, bali mzoga
Mwanamke asiye na haki ya kuishi huru na salama ndani ya mwili wake.
Usiulize alikuwa nani.
Ni binti yako wa miaka sita,
Ambaye hajatambua kuwa jinsi(a) yake kumbe ni mwiba.
Jirani yako wa karibu ameamua kumfundisha,
Somo lake la kwanza ni kuwa-
Katikati ya miguu yake kuna uwanja wa vita,
Na jirani ndiyo komando mkakamavu,
Anafyatua risasi bila ya wasi,
Anamlipua na bomu la woga,
Kisha kuuzima mwanga wa nafsi yake ya utoto,
Na kumuachia giza totoro,
Lenye mizimu yenye kumkebehi,
Eti yeye si mtu, si kitu, bali mzoga,
Msichana asiye na haki ya kuishi huru na salama ndani ya mwili wake.
Usiulize alikuwa ni nani,
Wala usihoji alikuwa wapi, alivaa nini, alikunywa nini, alifanya nini?
Ukatili hauna sababu zaidi ya ukatili;
Wala si mavazi aliyovaa,
au njia aliyopita,
au umri alio nao,
Kimini, suruali na baibui zote si salama
Barabara kubwa na uchochoro, zote si salama,
Binti mdogo na bibi kikongwe, wote si salama.
Nasi tumechoka lawama zenu.
Si muwakamate hao walioasi,
Na kulaani matendo yao?
Usiulize tena alikuwa nani.
Ni mimi,
Ni wewe,
Ni wao,
Ni sisi,
Binti salaam,
Wanawake wenye haki ya kuishi huru na salama ndani ya miili yetu.
Comments are closed.
Moving poetry, a song, a reflection but also a social commentary in figurative and symbolic language. Mistari hii itabaki nami nikirudia rudia kama tasbihi: Ukatili hauna sababu zaidi ya ukatili;Wala si mavazi aliyovaa,au njia aliyopita,au umri alio nao… Jazakallah kheir Neema
Asante sana!
Ni janga kuliko la Ukraine!
Ni jinai kuliko uhaini!
Ni kisu kikatacho maini!
Dunia imefika kiamani!
Dada zetu, binti zetu hatarini!
Mama zetu bibi zetu wa jangani!
Na tuusake muarubaini!
Wa kuwatoa wanaume uhayawani!
Na tuisake dripu ya kwinini!
Kuwatibu homa ya ukatili uso soni!
Tuungane sote kaumuni!
Kuwasema hadharani kuwalaani!
Sheria tuitunge bungeni!
Kuwaweka wanawake salamani!
Asante sana kwa shairi hili. Kwa kweli, dripu ya kwinini inahitajika.
This is so beautiful and sad. Thank you
Thank you Manka.
This is splendid👏🏾, amongst a few well inked swahili poems.
Thank you very much.
A lovely piece of poetry. Hongera Neema
Thank you :)
This poem holds a very deep message that everyone must read. Indeed, It is me, it is you, it is them, it is us…. The women of this world that must be protected and given their right to freedom.
Thank you Pesh :)
Moving beyond words!
Asante sana