Na Anna S. Manyanza (@annasamwel7)

1

Mara ngapi umenyanyasika?
Mara ngapi umedhalilishwa?
Mara ngapi umedharaulika?
Mara ngapi umeteseka?
Binti wa Afrika 

2

Historia imekutesa
Historia imekusahau
Historia imekufuta
Historia haikutambui
Binti wa Afrika

3

Siasa imekulaani
Siasa imekuasi
Siasa imekukebehi
Siasa imekukufuru
Binti wa Afrika

4

Karne ya 1500, historia imekutia utumwani
Karne ya 1700, historia imekutia ukoloni
Karne ya 1800, historia imekutia aibu
Karne ya 1900, historia imekuvunja moyo
Binti wa Afrika


5

Utumwa umekusambaza dunia Mashariki
Utumwa umekusambaza dunia Magharibi
Ukoloni umekusambaza dunia Kaskazini
Ukoloni umekusambaza dunia Kusini
Binti wa Afrika

6

Mashamba ya katani umehenyeshwa
Mashamba ya miwa umemenyeshwa
Mashamba ya pamba umetaabishwa
Mashamba ya karafuu umesoteshwa
Binti wa Afrika 

7

Jua limekuwamba
Mvua imekulowesha
Njaa imekudhoofisha
Kiu imekuvyausha
Binti wa Afrika

8

Moyo wa damu
Mwili wa damu
Roho ya damu
Uke wa damu
Binti wa Afrika

9

Kisu rohoni
Kisu moyoni
Kisu mwilini
Kisu ukeni
Binti wa Afrika

10

Roho ya majuto
Roho ya machungu
Roho ya majonzi
Roho ya hofu
Binti wa Afrika

11

Roho ya maombolezo
Roho ya utumwa
Roho ya mashaka
Roho ya wasiwasi
Binti wa Afrika

12

Binti mkimbizi
Binti wa kupekua
Binti wa mateso
Binti wa kuchakaa
Binti wa Afrika

13

Umezaa
Umelea
Umezika
Umeomboleza
Binti wa Afrika

14

Umejua vita
Umejua mauaji
Umejua maradhi
Umejua ufukara
Binti wa Afrika

15

Umebakwa, wana umezalishwa
Umebakwa, maradhi umeambukizwa
Umebakwa, moyo imedhalilishwa
Umebakwa, roho imeumizwa
Binti wa Afrika


16

Hulalamiki, nani atakuamini?
Hulisemi, nani atakuafiki?
Huripoti, nani atakusaidia?
Huliongelei, nani atakutetea?
Binti wa Afrika


17

Umenyimwa elimu
Umenyimwa amani
Umenyimwa penzi
Umenyimwa haki
Binti wa Afrika


18

Ukabila umekubagua
Utamaduni umekulemaza
Mila imekupumbaza
Dasturi imekufunga
Binti wa Afrika


19

Lolote baya, sababu ni wewe
Lolote baya, shutuma ni wewe
Lolote baya, lawama ni wewe
Lolote baya, adhabu ni wewe
Binti wa Afrika


20

Si kitu, hufi moyo
Si kitu, hufi roho
Si kitu, hufi faraja
Si kitu, hufi taraja
Binti wa Afrika

 

21

Weye u kisima cha majonzi na furaha
Weye u mto wa majonzi na furaha
Weye u ziwa la majonzi na furaha
Weye u bahari ya majonzi na furaha
Binti wa Afrika

 

22

U waridi jangwani
U waridi kondeni
U waridi nyikani
U waridi milimani
Binti wa Afrika


23

Malkia sawa na Miriam Makeba
Malaika sawa na Waris Dirie
Shupavu sawa na Michelle Obama
Shujaa sawa na Wangari Maathai
Binti wa Afrika


24

Mithili ya mbuyu, mkakamavu umesimama
Mithili ya mpingo, mweusi umesimama
Mithili ya mwembe, mpana umesimama
Mithili ya mnazi, mrefu umesimama
Binti wa Afrika

 

25

Binti wa Afrika umetoka mbali
Binti wa Afrika bado uko safarini
Binti wa Afrika usife tumaini
Binti wa Afrika siku moja utafika
Binti wa Afrika

 

26

Kuwa binti wa Afrika, si utumwa tena
Kuwa binti wa Afrika, si ukoloni tena
Kuwa binti wa Afrika, si kuambukizwa tena
Kuwa Binti wa Afrika, si kubakwa tena
Binti wa Afrika

 

27

Kuwa binti wa Afrika, si kisu ukeni tena
Kuwa binti wa Afrika, si kufa njaa tena
Kuwa binti wa Afrika, si hofu tena
Kuwa binti wa Afrika, si kufa upesi tena
Binti wa Afrika

 

28

Kuwa binti wa Afrika, si laana tena
Kuwa binti wa Afrika, si kosa tena
Kuwa binti wa Afrika, si lawama tena
Kuwa binti wa Afrika, si aibu tena
Kuwa binti wa Afrika, si shutuma tena
Binti wa Afrika

 

29

Binti wa Afrika ana haki ya kuthaminiwa
Binti wa Afrika ana haki ya kupendwa
Binti wa Afrika ana haki ya uhuru
Binti wa Afrika ana haki ya kuishi
Binti wa Afrika

 

30

Binti Afrika una haki ya kufurahi
Binti Afrika una haki ya kuelimika
Binti Afrika una haki ya kutibiwa
Binti Afrika una haki ya kuajiriwa
Binti wa Afrika

 

31

Zaa wanao upendavyo
Lea wanao upendavyo
Elimisha wanao upendavyo
Tetea wanao upendavyo
Binti wa Afrika

 

32

Fundisha wanao upendo
Fundisha wanao amani
Fundisha wanao hekima
Fundisha wanao kuwajibika
Binti wa Afrika


33

Ni haki yako kukubali
Ni haki yako kukataa
Ni haki yako kukosoa
Ni haki yako kupinga
Binti wa Afrika


34

Ni haki yako kutaka ndoa
Ni haki yako kufunga ndoa
Ni haki yako kukataa ndoa
Ni haki yako kuchoka ndoa
Binti wa Afrika

  

35

Pinga ukame
Pinga UKIMWI
Pinga ufukara
Pinga umasikini
Binti wa Afrika


36

Pinga ubaguzi wa rangi
Pinga ubaguzi wa jinsia
Pinga ubaguzi wa wazee
Pinga ubaguzi wa watoto
Binti wa Afrika

 

37

Yako sauti paza
Wako moyo paza
Wako mori paza
Yako roho paza
Binti wa Afrika


38

Sifa yako simulia
Elimu yako simulia
Hisia yako simulia
Maisha yako simulia
Binti wa Afrika

 

39

Jitahidi binti wa Afrika
Jaribu binti wa Afrika
Wajibika binti wa Afrika
Pambana binti wa Afrika
Binti wa Afrika

 

40

Ruka milima, upendo peleka
Vuka bahari, ujasiri peleka
Vuka mito, amani peleka
Vuka mabonde, furaha peleka
Binti wa Afrika

Hatimiliki

Udadisi imetumia picha kwa hisani ya pixabay.com.
  1. Joshua Lukonge September 4, 2021 at 4:44 pm

    Utunzi mzuri, asante

  2. Maryam September 5, 2021 at 2:04 am

    Binti wa Africa ameshasikia hivi villio kwa wingi sana. Sasa no wakati wa kusikia vicheko na mafanikio vya mabinti Africa walioonesha mfano. Mbona hawasikiki?. …oh! Nimeelewa. Wanafunikwa na tango zinaelezea machozi na udhaifu.
    Tafadhali leta Tungo ingine yenye nderemo, vicheko, mafanikio, ushupavu, uthubutu, ubunifu, wa Binti Africa, ndani na nje ya Africa.

  3. Mary September 6, 2021 at 5:39 am

    Utunzi murua na unaofikirisha

  4. Velma September 6, 2021 at 12:39 pm

    Binti Was Afrika afute machozi ainuke, asubuhi mpya imepambazuka.

    Beautiful piece

    • Ruth September 8, 2021 at 11:53 am

      Kabisa kabisa dadangu umenena. Hongera sana kwa kuwa sauti ya binti wa Afrika🙌🙌

  5. David Alila September 7, 2021 at 10:19 am

    Utunzi mzuri sana.Hongera!

  6. Angira O. Angira September 7, 2021 at 12:27 pm

    Nimependa mawazo yalo ndanimwe mwa shairi hili. Ima Binti wa Afrika,ipo siku✊

  7. Aneth September 7, 2021 at 1:04 pm

    Shairi limenigusa sana kama binti wa Afrika, asante kwa kutushirikisha dada Anna 🙏

  8. Camillus Kassala September 8, 2021 at 10:29 am

    Mpaka hapo mwanamke atakapodhihirisha anaweza kumfundisha mwanaume kuwa kama mama na kama dada naye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, ndiyo atakuwa amejenga msingi madhubuti wa ukombozi wake kama mwanamke anayeweza kumakamilisha mwanaume katika utu na ubinadamu!

  9. Gadi Nuru October 5, 2021 at 12:29 am

    Nimejikuta nasoma Mara 2 mbili

    Ahsante mama kwa Utunzi murua

Comments are closed.