Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kifo cha mwandishi maarufu, Ben Mtobwaama ‘Joram Kiango’. Taifa limepoteza kinara mwingine wa kutumia fasihi andishi kufichua masuala mazito yaliyoigubika jamii yetu. Hivi karibuni nilimwona gwiji Ben pale kwenye Mkahawa wa Vitabu wa Somaakipanga mikakati ya uandishi na uchapishaji.

Nilidhani huo ni mwendelezo wa kumwona mpiganaji huyu akiwa katika harakati za kutumia ‘mtutu wa kalamu’ kufichua uzandiki na ufisadi katika jamii. Lakini upeo wa mwanadamu una kikomo. Hivyo, sikujua kuwa hiyo ilikuwa mara ya pili na ya mwisho kumwona mwanaharakati huyo ambaye pia alijitosa katika fani ya uhariri wa gazeti la Heko na uchapishaji kupitia kampuni yake ya Heko Publishers.

Nawasihi tumpe mtunzi huyu‘Zawadi ya Ushindi’ kwa kusoma kwa undani vitabu vyake ili tutambue ni nini hasa amejaribu kutufunulia ‘Nyuma ya Mapazia’ ya jamii yetu iliyozingirwa na ‘Malaika wa Shetani’ na mafisadi wenye ‘Roho ya Paka’ wanaomsulubisha ‘Mhariri Msalabani’ na kudiriki kusema ‘Najisikia Kuua Tena’ kupitia mikataba mibovu wanayoisaini ‘Dar-es-Salaam Usiku’ pasipo kumwambia mwekezaji uchwara ‘Peza Zako Zinanuka’ na tena bila kuogopa ‘Salamu Kutoka Kuzimu’ au kilio chetu cha ‘Tutarudi na Roho Zetu?‘ Buriani Ben Mtobwa!