BURIANI MWL. YOHANA J. MUGANYIZI: BINGWA WA HISABATI NA FIZIKIA ALIYEWAJALI WATOTO WA WANYONGE
Na Mwl. Sabatho Nyamsenda
“Bwana rubani wa ndege ya Rais,
umesikia kauli ya Waziri Mramba? Kwamba ndege ya Rais lazima inunuliwe hata
kama itawalazimu Watanzania kula nyasi!” Aliniuliza mwalimu Yohana Muganyizi,
ambaye alikuwa akinifundisha fizikia na hisabati nilipokuwa kidato cha tatu na
cha nne, katika shule ya sekondari Kahororo iliyopo mjini Bukoba. Siku hiyo
ndiyo ilikuwa mwisho wa ndoto yangu ya utotoni ya kuwa rubani. “Siutaki tena
urubani,” nilimjibu, moyoni nikiwa nimejaa hasira. “Utasoma nini sasa?”
aliniuliza. “Nitasoma siasa. Na nataka kuwa mwalimu kama wewe!” Wengi tuliokuwa
katika darasa lile la sayansi hatukuendelea tena na sayansi licha ya kufaulu
masomo ya sayansi kwa alama A katika mtihani wa kidato cha nne. Wengi wetu sasa
ni walimu, tangu sekondari mpaka vyuo vikuu.
Mwalimu Yohana J. Muganyizi alihamia
shuleni Kahororo mwaka 2003, akitokea shule ya wavulana ya Bwiru iliyopo jijini
Mwanza.Alikuwa mwalimu bora wa sayansi, na hasa katika masomo ya hesabu na
fizikia. Sayansi kwake haikuwa nadharia tu, bali pia vitendo. Aghalabu
ungemkuta akitembea na bisibisi akijaribu kurekebisha taa na mifumo ya umeme
shuleni hapo. Kubwa kuliko yote ni kwamba hakuwa mwalimu wa sayansi wa kawaida:
alichanganya sayansi na siasa.
Wengi wetu tulivutiwa na hadithi zake
kuhusu siasa, na jinsi alivyoichambua historia ya nchi hii. Si ajabu kwamba
ujio wake shuleni Kahororo uliamsha vuguvugu la kupigania haki na usawa
miongoni mwa wanafunzi, na baina ya wanafunzi na walimu.
Binafsi nilikuwa karibu naye, huku
akinishauri namna ya kuendesha vuguvugu la kupigania haki na usawa. Nilikuwa
kiongozi wa taaluma, na baadaye kiranja mkuu, huku yeye akiwa mwalimu wa
taaluma, hivyo tulikuwa karibu sana.
Mapambano
ya dhidi ya uonevu
Kufikia mwaka 2004, viongozi wa
wanafunzi shuleni Kahororo tulikuwa tumegawanyika katika makundi matatu. Kundi
la kwanza, ni lile miungu watu. Hawa walijiona wako juu ya sheria. Waliwapiga
wanafunzi, walipora chakula, na hasa wali na sukari, na walifurahia zaidi kuwa
karibu na walimu madikteta, na hasa aliyekuwa mwalimu mkuu msaidizi. Kundi hili
lilitengenezwa na mwalimu mkuu msaidizi, na wengi wao wakiwa ni watu wa dini
yake na kabila lake.
Kundi la pili ni lile lililojibainisha
kama kundi la wanamapinduzi. Tulikuwa wachache katika kundi hili. Tuligoma
kuweka sahani zetu katika meza ya viongozi na tukajichanganya na wanafunzi
wenzetu. Ilipofika zamu yetu, na hasa siku ya wali, tulihakikisha kuwa
wanafunzi wenzetu wanapata chakula cha kutosha. Tuliongoza kwa upendo, na
hatukuwahi kumpiga mwanafunzi.
Kundi la tatu ni lile la mrengo wa kati
ambalo halikutaka kuchukua upande. Hivyo basi mgongano mkubwa ulikuwa kati ya
wanamapinduzi na madikteta. Walimu pia waligawanyika katika makundi hayo
matatu. Mwalimu Muganyizi alikuwa katika kundi la walimu wanamapinduzi.
Mgomo
mkubwa wa wanafunzi
Migongano kati ya makundi hayo mawili
ya wanafunzi yalipelekea mgomo mkubwa wa wanafunzi mwaka 2004. Viogozi
madikteta walikuwa wamempiga mwanafunzi mmoja na kumjeruhi vibaya sana, huku
waking’oa ngozi ya kiganja cha mkono wa kulia. Kilichoumiza zaidi ni kuwa
mwanafunzi yule alitakiwa kufanya mtihani wa majaribio (MOCK) wa kidato cha
pili siku inayofuata. Wanafunzi waliingia katika mgomo na kuanza kurusha mawe
katika ofisi kuu ya viongozi, huku madikteta wakiwemo ndani. Ni mwalimu
Muganyizi aliyeshirikiana na wanamapinduzi kutuliza urushaji wa mawe.
Tulimwambia Muganyizi kuwa auambie uongozi wa shule, unaowalinda madikteta, kuwa
hatutaingia darasani mpaka viongozi wale wafukuzwe shule.
Hivyo jioni ya siku ile kikaitishwa
kikao cha viongozi, pamoja na mwalimu mkuu msaidizi na mwalimu Muganyizi. Cha
kushangaza ni kuwa mwalimu mkuu msaidizi alitugeuzia kibao wanamapinduzi na kusema kuwa
tunataka kuchoma shule na ni sisi ndio tunaosababisha mgomo. Tulimwambia wazi
kuwa mgomo anausababisha yeye na kundi lile la madikteta. Sisi jukumu letu ni
kuhakikisha haki inatendeka. Alipojaribu kupindisha haki, na hata kumnyima
mwanafunzi aliyejeruhiwa ruhusa ya kwenda hospitali, wanafunzi walikasirika na
kuanza kurusha mawe. Kwa mara ya kwanza katika historia ya shule ile ulitokea
mgomo mkubwa uliosababisha uharibifu mkubwa wa majengo na mali za shule, na
hata kusababisha polisi kuingilia kati ili kutuliza vurugu.
Mapambano
yanaendelea
Gharama za mgomo ule walizilipa
wanafunzi wasio na hatia, ambao walifukuzwa shule. Wengine walisimamishwa
masomo na kulipishwa faini ili kufidia uharibifu. Madikteta ambao ndio
waliosababisha wanafunzi kufanya vurugu hawakuguswa.
Wanamapinduzi tulisakamwa, na hasa mimi
niliyekuwa kiongozi wa kundi hilo, ambaye pia nilisingiziwa kuchochea wanafunzi
kufanya uharibifu. Kama isingekuwa ujasiri wa walimu wanamapinduzi wakiongozwa
na Mwl. Muganyizi, ilikuwa tufukuzwe shule.
Japo ulisababisha uharibifu, mgomo ule
ulikuwa mwanzo wa kipindi kipya. Madikteta walipunguza uonevu dhidi ya
wanafunzi. Lakini baadhi yetu tuliendelea kusakamwa, huku mwalimu mkuu msaidizi
akitutamkia kuwa hatukupaswa kuwepo shuleni pale. Kwa kuongozwa na Mwl.
Muganyizi, tulipeleka malalamiko yetu kwa mkuu wa shule, marehemu Mwl.
Lutanjuka. Baadhi ya walimu waliokuwa wakitunyanyasa na kututisha walionywa na
kutakiwa kuja kutuomba msamaha. Yupo mwalimu mmoja ambaye tulihakikisha kuwa
anavuliwa nyadhifa zake za uongozi wa bweni na nidhamu.
Walimu madikteta wakiongozwa na mwalimu mkuu
msaidizi walikuwa wamemdanganya mkuu wa shule kuhusu chama cha wanafunzi
wavukao ziwa, kilichoitwa Kahororo Overlakers’ Association (KOA) ambacho
kilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kusaidia wanafunzi waliotoka mikoa ya mbali
pale wanapopata shida, hasa katika gharama za matibabu, nauli na hata ada. Mimi
nilikuwa mwenyekiti wa chama hicho, na mwl. Muganyizi ndiye aliyekuwa mlezi
wetu. Walimu madikteta walimlisha sumu mkuu wa shule na kumfanya akifute. Kwa
kushirikiana na Mwl. Muganyizi tulikwenda mbele ya mkuu wa shule na kuhakikisha
kuwa anabadili uamuzi wake. Aliubadili. Tukashinda. Walimu madikteta wakabaki
wamepigwa butwaa.
Ualimu
bila viboko
Yapo megi ya kusimulia juu ya mapambano
tuliyofanya na Mwl. Muganyizi. Yalikuwa ni mapambano ya kupinga uonevu, uporaji
na dhuluma. Nje ya mapambano ya kimapinduzi, yeye alikuwa ni mfano mzuri wa
kuigwa katika uongozi. Licha ya mwili
wake ulioshiba katika ujazo na urefu, pamoja na mazoezi ya viungo aliyofanya,
alikuwa mvivu wa kushika kiboko. Katika miaka mitatu tuliyokuwa pamoja sikuwahi
kumwona ameshika fimbo, au kumchapa mwanafunzi. Kinywa chake chenye simulizi
nyingi hakikuwa kikitoa amri za kiimla au makaripio ya ukali. Kwa ufupi,
alikuwa ni mwalimu wenye utu na aliyejiheshimu. Hii ilimjengea heshima kubwa
miongoni mwa wanafunzi, ambao walimpenda na kumthamini.
Utumishi
uliotukuka
Mwalimu Muganyizi alijitolea
kuwatumikia wanyonge kwa moyo wake wote. Yeye, kama ilivyo kwa walimu wengine,
alikuwa na familia kubwa (mke mmoja, watoto saba na wajukuu wanne) na ndugu
wanaomtegemea. Malipo aliyopata mwisho wa mwezi, kama ilivyokuwa kwa walimu
wengine, yalikuwaya kijungu jiko, na kwa kweli hayakutosha hata kuihudumia
familia yake. Lakini uhafifu wa malipo hayo haukumfanya awachukie na kuwaadhibu
watoto wa wakulima wasio na hatia. Hivyo, alitumia muda mwingi kutafuta maarifa
katika vitabu, na kisha kuyahamishia maarifa hayo katika vichwa vya wanafunzi.
Alitumia muda mwingi wa ziada kutufundisha na kutupatia mazoezi.
Katika fikra za Mwl. Muganyizi,
ukombozi wa pekee kwa wanyonge wa nchi hii utapatikana kwa kuwapa elimu bora
watoto wao. Elimu bora ni zaidi ya kufundisha kanuni za hesabu na fizikia, bali
kuwafungua macho wauone uonevu na unyonyaji unaofanywa na watawala, pamoja na
kuwaongezea hasira ili wakapambane na unyonyaji huo. Mapambano dhidi ya
udhalimu yanaanza katika jamii na taasisi uliyomo.
Pumzika
kwa amani
Mwl. Muganyizi hatunaye tena. Alikoma
kufundisha fizikia na hesabu Jumatano 5 Machi 2014. Alianguka akiwa anatoka
darasani kusimamia mtihani, na kukimbizwa hospitali ambako alikata roho baada
ya muda mfupi. Amefariki tarehe ambayo wanyonge duniani kote walikuwa
wakiadhimisha mwaka mmoja tangu kuondokewa na shujaa wa mapambano ya wanyonge,
El Commandante Hugo Chavez, aliyekuwa rais wa Venezuela. Chavez alihakikisha
kuwa utajiri nchi hiyo unawanufaisha watu wa tabaka la chini, ambao ndio wengi.
Naam, Mwl. Yohana J. Muganyizi naye alihakikisha kuwa maarifa yaliyomo kichwani
mwake yanawanufaisha watoto wa wanyonge.
Twakuhakikishia
Muganyizi,
Ulotufunda
tutakuenzi,
Si kwa kununua
mabenzi,
Au maghorofa ya
Mbezi.
Tutawajali wanyonge,
Ambao ndio wengi.
Historia
itakukumbuka,
Kwa utumishi
uliotukuka.
Kwa amani, pumzika.
Mwandishi wa tanzia hii ni mwalimu wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya sayansi ya siasa na utawala wa umma.
Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com
Kaka inauma sana,
ni kama ninayaona,
yote uloyasema,
Nimekumbuka ya nyuma,
Enzi tupo tunasoma
Muganyizi ni mlima,
Utakaokuwepo daima,
mchana na siku nzima,
Buriani wetu Mwalimu,
Uliyetupa Timamu.
Kaka inauma sana,
ni kama ninayaona,
yote uloyasema,
Nimekumbuka ya nyuma,
Enzi tupo tunasoma
Muganyizi ni mlima,
Utakaokuwepo daima,
mchana na siku nzima,
Buriani wetu Mwalimu,
Uliyetupa Timamu.