Utangulizi
Mnamo tarehe 16 mwezi Machi mwaka 2020, jijini Dar es Salaam, serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ilitangaza kesi ya kwanza ya mgonjwa mwenye virusi vya corona, aliyepatikana mjini Arusha, siku moja kabla. Kwa kuzingatia Kanuni ya 46 ya Sheria ya Afya, Waziri alitoa maelekezo kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi ya kirusi huyo. Hii ikijumuisha, kupunguza safari zisizo za lazima, kuweka vyombo vya kunawia mikono katika taaasisi kubwa, vyombo vya usafiri, na maeneo yenye mikusanyiko; kuepuka kushikana mikono, kukumbatiana, kubusiana; kuepuka kushika pua, mdomo na macho; na kuweka zuio la ndugu kutembelea wagonjwa hospitalini.
Siku moja baadaye, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliuhakikishia umma kuwa serikali imejipanga kirasilimali, kitaalamu na kimiundombinu kupima na kutoa huduma za kitabibu. Zaidi, akatangaza msimamo wa serikali, wenye udhibiti zaidi, kwamba shule zote zitafungwa kwa siku 30, na wakati huo huo, kupiga marufuku mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kuanzia shughuli za kisiasa, michezo, na mambo ya kijamii. Tamko hili lilifuatiwa siku ifuatayo na la kufunga vyuo vya kati na juu nchini.
Ukisikiliza vizuri maagizo ya serikali, taarifa hizo zina sehemu kubwa tatu. Mosi, serikali imewahakikishia watanzania kwamba imejidhatiti katika kukabiliana na ugonjwa uletwao na virusi vya corona, yaani COD-19. Pili, mfumo wa huduma ya afya wa dharura umeshajengwa kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma ya kihospitali katika maeneo maalumu. La tatu, ambalo ndio msingi wa makala haya, serikali imetoa mwongozo juu ya kupunguza michangamano ya watu ili kudhibiti maambukizi mapya. Maagizo ya serikali yanaitaka jamii kupunguza mikusanyiko na michangamano isiyo ya lazima ili kuzuia au kupunguza maambukizi. Hii dhana kwa kiingereza inaitwa social distancing na kwa kiswahili tunaweza kuiita, kujenga umbali wa kijamii. Lengo la makala haya ni kujibu, je, ni kwa nini dhana hii inatiliwa mkazo?
Dhana ya Kudhibiti Mlipuko
Ugonjwa uletwao na kirusi cha corona siyo tu umekuwa tishio katika usambaaji wake wa haraka, bali umewafanya madaktari kukiri kwamba, hakuna hospitali yoyote duniani, kwa sasa, iliyo na uwezo wa kumudu huo ugonjwa vilivyo kama haudhibitiwi kwenye ngazi ya jamii. Hivyo, madakatari na wataaalamu mbalimbali, wakati wanaendelea na michakato ya kutafuta tiba na chanjo, wameziomba serikali, taasisi, na jamii kutumia dhana ya afya ya jamii itwayo kwa kiingereza, flatten the curve au flattening the curve, kwa ajili ya kuzuia maambukizi mapya. Wito huu lengo lake ni kupunguza kasi ya usambaaji wa ugonjwa huu ili usiuelemee mno mfumo wa afya unaoujumuisha watoaji huduma na taasisi zao.
Dhana hii bado haijatafsiriwa kikamilifu kwa kiswahili ila, kwa matumizi ya sasa, tunaweza kuiita kudhibiti mlipuko. Na ili kuielezea kirahisi nitatumia mfano kwa kusawazishaji mlima au tuta. Msingi wa dhana hii ni kupunguza kasi ya usambaaji wa maambukizi ya virusi ili kufanya wanaohitaji huduma ya tiba dhidi ya ugonjwa huu, wakati wowote, wawe wachache. Hii itawezesha hospitali, madaktari na wataalamu mbalimbali, kuwahudumia wagonjwa kwa ukaribu na kuokoa maisha yao. Lakini wagonjwa wanapokuwa wengi, hutengeneza kitu tunachoweza kukiita mlima wa maambukizi kama picha hapo juu mwanzoni inavyoonesha, na hivyo kufanya upatikanaji wa huduma za hospitalini kuwa mgumu.
Kwa mantiki hiyo, dhana hii inatumika kama kinga ya kujiepusha na maambukizi katika ngazi ya kijamii ili kuzuia msongamano wa wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya corona ambao unapelekea mfumo wa afya usiwe tena na uwezo wa kutoa huduma itakiwavyo. Kimsingi, dhana hii inazungumzia mambo makubwa mawili. Mosi, ni uwezo na ukomo wa hospitali, kitaalamu na kirasiliamali, katika utoaji wa huduma yoyote, na hasa katika magonjwa ya mlipuko. Hii inamaanisha, kila hospitali ina uwezo wa kutoa huduma kwa idadi fulani ya wagonjwa. Kila aina ya ugonjwa nayo ikihitaji wataalamu wake, dawa zake, vifaa vyake, na malazi yake. Hivyo, wagonjwa wakiwa wengi, katika ugonjwa wowote ule, kuzidi uwezo wa hospitali, kifedha, kitaalamu na kimazingira, basi fursa ya kutoa huduma ili kuokoa maisha ya binadamu, hasa katika wakati wa magonjwa ya mlipuko, unakuwa mdogo. Ufinyu huu ukihusisha hospitali zote katika eneo fulani, basi hali inakuwa ni nje ya uwezo wa mfumo wa afya wa eneo hilo.
Pili, ni usambaaji wa ugonjwa wa virusi vya corona, ambao umewatia mashaka sana wataalamu wa afya maana unakua katika kasi kubwa na kwa sasa umesambaa zaidi ya nusu ya dunia, kwa muda mfupi. Katika hali ya kushtua, ugonjwa huu uligundulika China mwishoni mwa mwaka 2019 na, hadi kufika mwanzoni mwa mwaka 2020 .ulikuwa umeshafika mabara ya Amerika, Ulaya na Afrika. Hii ni kwa sababu maambukizi ya kirusi cha corona huenea kwa urahisi kupitia mtu aliye na virusi pale anapopiga chafya au kukohoa na matone yake yanaposambaa yanakuwa tayari kwa maambukizi, pale mtu apoyashika na kujigusa katika pua zake, midomo au kinywa chake. Hali hii imefanya maambukizi kuongezeka zaidi ya maradufu. Kwa mfano, ndani ya mwezi moja kuanzia tarehe 18 Februari hadi leo tarehe 18 Machi mwaka huu idadi ya wagonjwa duniani imetoka ~73,332 hadi kufikia ~207,518.
Umuhimu wa Dhana ya Kudhibiti Mlipuko
Dhana ya kudhibiti mlipuko, au kusawazisha tuta ama mlima wa maambukizi, ni muhimu sana kwa sababu kubwa mbili. Mosi, uzoefu unaonesha kuwa nchi zilizoathirika mno zinapata changamoto kubwa sana kitabibu, kiafya na kirasilimali katika kupambana na ugonjwa huu. Kwa mfano, huko China ambapo ugonjwa huu uligundulika, ongezeko la wagonjwa liliwafanya wajenge hospitali mbili kubwa ndani ya mwezi mmoja katika mji wa Wuhan jimboni Hubei kulipokuwa na mlipuko mkubwa. Lakini pia walijenga hospitali 16 za dharura katika ambazo wanasema saa wamezifunga baada ya kufanikiwa kupunguza idadi na wagonjwa na wengine kuhamishiwa kwenye hospitali za kudumu. Pamoja na mafanikio waliyoyapata katika kukabiliana na ugonjwa huo, wingi wa hospitali pekee haujamaliza tatizo la ongezeko la wagonjwa nchini humo kwa ujumla bali mchanganyiko wa hatua mtambuka zilizojikita katika kudhibiti mlipuko. Hadi kufikia leo, kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha John Hopkins, watu 69,755 wamepona kati ya 81,102 huku 3,241 wakipoteza maisha yao na wachache wakiugua.
Huko Italia inasemekana wao walichelewa kuudhibiti ugonjwa, hivyo, hali yao kwa sasa inaonekana ndio mbaya kuliko taifa lolote duniani. Ndani ya siku nne, kuanzia tarehe 11 hadi 15 mwezi Machi 2020, wagonjwa waliongezeka maradufu, kutoka 10,149 na kufikia hadi 21,157. Hii imeilazimu serikali ya Italia kufikia maamuzi magumu ya kuruhusu vyumba vya dharura kutumika kuhifadhi wagonjwa, kuajiri mamia ya madaktari wapya na wastaafu pamoja na kuomba msaada wa vifaa vya matibabu. Na bado idadi ya wagonjwa inaongezeka na hivyo kuzilazimu hospitali kushindwa kupokea wagonjwa wapya. Hivyo, wengi wao wanapoteza maisha. Jumapili ya tarehe 15 mwezi Machi 2020 iliripotiwa kuwa ndani ya masaa 24 vifo 368 vitokanavyo na virusi vya corona vilitokea nchini humu. Na kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha John Hopkins, hadi kufikia leo hii Italia ina wagonjwa 35,713 ambapo waliopona ni 4,025 tu kati ya hao na ambao wamepoteza maisha yao ni 2,978.
Pili, ulimwengu umetambua kwamba hakuna mtu wala taifa lilipo salama kwa sasa. Hivyo, udhibiti wa ugonjwa huu unahitaji juhudi za pamoja. Ulianza ndani ya nchi moja, huko uchina, lakini kutokana na miingiliano ya mataifa katika masuala mbalimbali, kama ya kibiashara, kiutalii na kiuchumi, watu katika nchi 156tayari wameambukizwa corona, na hakuna takwimu zinazoonyesha ugonjwa huu ukipungua kiujumla kwa sasa. Ni katika muktadha huo, dhana hii ya kudhibiti mlipuko inahitaji kutiliwa mkazo, kwani inaweza kutumika kama kinga au njia ya kupunguza maambukizi katika mazingira tofauti. Kwa maeneo yaliyoathirika sana, dhana hii hutumika kupunguza au kusimamisha msongamano wa wagonjwa katika mahosipitali na kuupunguza usambaaji wake.
Katika maeneo yenye maambukizi madogo au yaliyoko hatarini kuathirika zaidi, dhana hii hutumika katika kuzuia kasi na kupunguza ukuaji usiende katika hali hatarishi, ambayo ni mlipuko wa maambukizi mapya. Na kwenye maeneo ambayo bado hajaathirika, dhana hii inaweza kutumika katika kupunguza uwezekano wa usambaaji wa virusi vya ugonjwa huu, yaani kujikinga. Hivyo, waataalamu wanapozungumzia dhana hii ya kudhibiti mlipuko, inahusisha idadi halisi ya wagonjwa wa corona iliyopo na idadi ya makisio ya wagonjwa watakaoweza kupata maambukizi, kupitia taarifa za awali za maambukizi, pale ambapo ugonjwa hautaweza kudhibitiwa. Katika msingi huo, dhana hiyo inatumika kuonesha kuwa hospitali peke yake haziwezi kutunusuru na janga la corona bila kuchukua hatua stahiki za kuhakikisha tunasawazisha tuta au mlima wa maambukizi unaoneshwa katika picha iliyopo mwanzoni mwa makala. Dhana hii inapendekeza namna gani tunaweza kupunguza maambukizi mapya katika ngazi ya jamii ili kuhakikisha kuwa hilo tuta au mlima huo unasawazika.
Namna ya Kudhibiti Mlipuko
Tanzania tuna bahati maambukizi ya virusi vya corona nchini bado ni madogo. Hivyo, uwezo wa kuzuia ongezeko kubwa la maambukizi hayo tunao kwa kutumia uzoefu wa wenzetu juu ya dhana ya #DhibitiMlipuko. Ni vyema tujikumbushe kuwa mpaka sasa chanjo au dawa ya kutibu COVID-19 haijapatikana. Leo wagonjwa wenye virusi vya corona wanapokwenda hospitali, wanapewa vitamini, dawa za kushusha homa au kutibu homa ya mapafu ama mashine za kupumulia kutegemeana na hali yao ili kuiwezesha miili yao iwe na nguvu za kupambana na virusi hivyo.
Ila tiba bado hamna. Ufumbuzi peke yake wa kuaminika ni kutekeleza dhana ya kudhibiti mlipuko inayobebwa na dhana kubwa mbili. Kwanza, ni dhana ya kujikinga mtu mmoja moja kwa kubadilisha tabia. Pili, ni dhana ya “kujiweka mbali na jamii”, ambayo tumeona kwa kiingereza ikiitwa social distancing. Dhana hizi zinasisitiza kubadilisha tabia kwa kupunguza mchangamano wa mtu na mtu katika matukio ya kijamii na kuwaelekeza watu kukaa majumbani kwao. Na pale ambapo mtu anahisi anakuwa anaumwa au kutoka maeneo hatarishi, basi anatakiwa “kujitenga” na watu wa karibu. Kwa lugha nyingine hii inaitwa kujikarantini.
Mabadiliko ya Tabia za Mtu Mmoja Mmoja
Inasemekana mtu anapopiga chafya au kukohoa, virusi vinaweza kurushwa hata zaidi ya mita moja na kufikia kwenye nguo, sahani, magari, milango n.k.. Hivyo, inashauriwa kukaa umbali wa mita 2 au futi 6 na wengine kama unajisikia kuwa na dalili ya maambukizi ya virusi vya corona au kama uko na mtu mwenye dalili hizo. Pia kwa ambaye ni mgonjwa, akipiga chafya ni jambo la kawaida kabisa, hivyo, watu kutumia mikono yao kuzuia chafya au kikohozi ni muhimu. Basi mtu huyo akishika kikombe, sahani, mlango, gari, gazeti, kitabu na kadhalika, kirusi kina uwezo wa kubaki na kuishi kati ya masaa 6 hadi 72 kwenye vitu hivyo. Kwa hiyo kila mtu anashauriwa kuosha mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji masafi na ya kutosha. Hata pale maji yanapokuwa shida, mikono isuguliwe vizuri na kusuuzishwa ama kutawazwa hadi itakate hasa.
Jambo jingine ni gumu kiasi maana linahitaji kujifunza kutojishika machoni, mdomoni wala puani kwa kutumia mikono yetu hasa pale tunapokuwa hatujanawa kwa maji yanayotiririka au vitakasishaji.
Kujitenga na Wajibu wa Kukinga Wengine
Mtu yeyote yule ambaye atapata dalili mchanganyiko wa yafuatayo, kikohozi, shida ya kupumua, na homa ana majukumu makubwa mawili. Mosi, kuwakinga watu wanaomzunguka kwa kujikinga kuwa nao karibu. Hivyo, mtu anapaswa akae eneo la peke yake kama inawezekana. Iwapo mazingira ni magumu ina maana mtu huyo inampasa achangamane lakini ni lazima kufunika kinywa na pua wakati wa kukohoa na kupiga chafya. Pili, mtu huyo inapendekezwa atoe taarifa kwa vyombo vya afya. Kuna baadhi ya maeneo yamependekezwa kwa wanaohisi wana dalili za kuumwa. Ni vyema wapige simu kabla ya kwenda ili wapate maelezo kutoka kwa wataalamu. Na kuna mahali wagonjwa wenye dalili wanahitajiwa kwenda hospitali moja kwa moja ila kwa tahadhari ya kutosambaza virusi kwa watu wengine maana kukingana ni wajibu.
Umbali wa Kijamii
Kujenga umbali wa kijamii ni mbinu mojawapo muhimu sana ya kudhibiti mlipuko. Hii, kama nilivyogusia hapo juu, inamaanisha kutokujenga mazingira ya mkusanyiko mkubwa wa watu, kuzuia matembezi ambayo sio ya lazima, na kuondoa ukaribu kati ya mtu na mtu wanapokutana ama wakiwa katika maongezi. Kutokujenga mkusanyiko wa pamoja inamaanisha watu waache kwenda kwenye shughuli zozote ambazo zinavuta watu wengi kwa wakati mmoja. Hii inajumlish, mikutano, mashule, kazi, harusi, sinema, mpirani n.k. Kutokutembea kusiko kwa lazima ni pamoja na kutokwenda kwa jirani kupiga soga na mashosti na washikaji kijiweni, au kwenda kariakoo kununua jeans au dera. Hali kadhalika ni kuondoa ukaribu wa kupeana mikono, kukumbatiana au kukaa karibu bila sababu ya msingi. Kujenga umbali wa kijamii pia kunahusu safari za ndani na za kimataifa. Hivyo, nchi nyingi zimefikia maamuzi ya kuzuia wasafiri ili kujiweka mbali na watu wa maeneo fulani fulani.
Katika kutimiza dhana ya kujenga umbali wa mwingiliano wa kijamii, nchi nyingi sasa zimechukua hatua mbalimbali. Zipo nchi zilizotoa maagizo makubwa kwa kutoa mwongozo wa nchi juu ya namna ya kuishi, kufanya kazi na kuchangamana katika maisha na juu ya ugonjwa utokanao na virusi vya corona. Miongozo hiyo imetoa tafsiri mpya za mikusanyiko hatarishi. Pia zimetoa maagizo ya baadhi ya taasisi kufungwa hasa za mashule, vyuo na ofisi ambazo hazina ulazima wa watu kwenda maofisini kila siku, hivyo, watu kufanya kazi kutoka nyumbani au mitandaoni ikiwezekana.
Miongozo mingine ni juu ya usafiri wa anga, watalii na mipaka. Utekelezaji wa hatua hizi unatofautiana kutoka nchi kwenda nchi nyingine kutokana na tathmini za nchi hizo n.k. Wapo ambao wamefunga mashule kwa muda, kati ya wiki 8 hadi 12. Pia kuna uhamasishaiji wa hali ya juu wa watu kutumia muda mwingi majumbani mwao isipokuwa kwa vitu muhimu tu, kama kazi, chakula au dawa. Yote hayo ni katika kujaribu kuudhibiti mlipuko.
Hitimisho
Wahenga walinena, heri kinga kuliko tiba. Kama makala ya Joakim Paschal Ishengoma humu Udadisi inavyoonesha, methali hiyo pia inaendana na dhana ya dhibiti mlipuko. Maadam uwezo wa kujikinga na maambukizi mapya tunao, nia tunayo, na sababu tunayo, basi tuendelee kufanya hivyo kwa kujenga umbali wa kijamii na kutekeleza ushauri tuliopewa na madaktari na wataalamu wengine kuhusu kujikinga na kirusi corona. Kwa kufanya hivyo, kama anavyositiza Dokta Frank J. Minja, tutadhibiti mlipuko na kuuwezesha mfumo wetu wa afya usielemewe bali ustahimili. Hili ni suala langu na lako-ni wajibu wetu sote, tujikinge na kukingana.










Jamani tusikilize maelekezo ya wataalam wa Afya ili tuweze kujikinga na gonjwa hili hatari pia tuendelee kumwomba Mungu atuepushie balaa hii.