USULI WA RIWAYA
Nina furaha kusema kuwa, riwaya yangu ya pili, FARADHI YA MOYO, imetoka. Imechapishwa na Shirika la Uchapishaji la Mkuki na Nyota @MkukiNaNyota. Kwa sasa unaweza kuagiza nakala yako hapa, TPH bookshop, 24 Samora Avenue, Dar es salaam. Simu nambari: +255 742 556 446. Au agiza moja kwa moja kupitia tovuti yao: https://tph-bookshop.business.site/
Turudi kwenye kazi yenyewe sasa, Faradhi ya Moyo ni riwaya imhusuyo binti mmoja, kwa jina, Wasila. Mumewe wasila, Maulidi, anang’amua kuwa kumbe Wasila mgumba! Talaka ikacharazwa, talaka hiyo inabadilisha maisha ya Wasila moja kwa moja. Sasa pata nakala yako ujionee mwenyewe misukosuko anayopitia binti huyu. Ninalishukuru kwa moyo wote Shirika la Uchapishaji la Mkuki na Nyota @MkukiNaNyota kwa kuniamini, wakaikubali kazi yangu.
Kabla ya kutoa FARADHI YA MOYO, nimebahatika kutoa riwaya ya kwanza kabisa ambayo ni PENZI LA DAMU. Ni riwaya iliyobahatika kujinyakulia Tuzo ya Kimataifa ya Fasihi ya Afrika ya Safal Cornell, 2015. Katika riwaya hii tunafuata safari ya binti Malaika anayebahatika kwenda ughaibuni kimasomo huku akimwacha nyuma mpenzi wake, Ben. Utengano huu unawaletea wote wawili changamoto nyingi zinazotishia kuvunja penzi lao. Riwaya hii inapatikana pia katika duka la vitabu la TPH Bookshop au kupitia tovuti yao: https://mkukinanyota.com/product/faradhi-ya-moyo/.
WASIFU WA MTUNZI
Anna Samwel Manyanza ni mwandishi wa riwaya na hekaya za watoto. Ni mzawa wa Tanga, Tanzania. Ana shadaha ya Uzamili ya Siasa, Lugha na Uandishi wa Habari kutoka Chuo Kikuu cha Leibniz Universität Hannover, Ujerumani.
PENZI LA DAMU (2015) ni riwaya yake ya kwanza iliyonyakua ushindi wa kwanza kabisa wa Tuzo ya Kimataifa ya Fasihi ya Afrika ya Safal-Cornell.
LUCIA MTOTO WA MAMA (2017) ni utanzu wake mfupi uliochap-wa kwenye diwani ya Vazi la Mhudumu. Diwani hil imechaguliwa kuwa kitabu cha kiada chini Kenya. (East African Educational Publishers).
KAKOFIA KEUSI (2020) ni hekaya yake ya kwanza ya watoto ambayo imebahatika kufasiriwa katika lugha ya Kingereza, Kijeruma-ni na Kifaransa. Amewasilisha kazi zake katika warsha ya kimataifa ya Waandishi wa Afrika iliyofanyika jijini Berlin, Ujerumani, 2022.
Mwaka 2023, amehariri na Edison Wanga, diwani ya BODA MPYA na Hadithi Nyingine, kazi yake katika diwani hii inaitwa CHOZI LA SAMAKI (Adizan Publishers).
FARADHI YA MOYO (2024) (Mkuki na Nyota Publishers) ni riwaya yake ya pili iliyozinduliwa katika sherehe ya Kalam Salam inayofadhiliwa na Shirika la Uchapishaji la Mkuki na Nyota, Dar-es-salaam.