Na Nadj (@najiniusnaj77)

Kisiwa kimeingia giza
Nuru kamwe haitafika
Watu wake kuwazika
Kila saa na dakika
Najiuliza:
Shetani gani huyu
Tumbo lake lisoshiba?
Kiu yake ya damu
Hamu yake isokwisha?

Kisiwani majonzi yamesambaa
Yamezagaa, yametandawaa
Watu wake ‘megeuzwa chambo
Na mabango ya kutungia shabaha
Risasi zikitiririka
Bahari yake imegeuka damu
Vilio kamwe havitakwisha

Firauni mguu wake umewekwa
Ardhini kaudidimiza
Hata huko Ging’ingi
Wachawi wameshindwa
Roho yako roho gani –
Iso chembe ya hisia?

Kisiwa kimeingia giza
Nuru kimepoteza
Asumini yatoa damu
Waridi uzuri limepoteza
Mwanga wewe, mwanga gani?
Ukaaye madarakani?
Damu ya Wazanzibari
Kutambaa benderani
Ikipepea waona sifa
Kisiwa kimeingia giza
Nuru kamwe haitafika
©️ Nadj

Comments Off on GIZA! GIZA! GIZA