Hapo zamani…ila sio zamani sana, sio zama za Pontio Pilato; wala zama za naitini (19) kweusi au zama za Mwalimu; bali zama za juzi.

Zama hizo, katika nchi ya Nyika, alifika Yohana, mwana wa Yusufu, aliyeibuliwa kutoka kwa watu, naye akatawazwa na kutunukiwa mamlaka. Alijazwa nguvu na kupewa sifa na utukufu wa kuwa Mtu Mkuu, mkuu kuliko watu wote.

Punde, Yohana, Mtu Mkuu, akaanza kuzozwa na mamlaka yake. Akawa mwenye kutuna na kufura. Hasemeshwi. Haambiliki.

Juu ya mimbari ya utukufu wake aliketi na aliwabatiza wale wote chini yake kwa moto. Akawaamuru, mithili ya maandiko, wamtii yeye mwenye mamlaka; yeye walipaswa wamtumikie, wampapatikie, wamuabudu, kwani yeye ndiye aliyetumwa kuwaokoa wote walio dhaifu na dhoofu hali, wale walio wafu ila hai. Kwa wale waliomkataa na kukaidi jina na neno lake, naye, Mtu Mkuu, akawaonesha ukuu wa mamlaka yake, akafunga vinywa vyao na kuwafungia makufuli ya hila.

Miaka ikazidi songa, Yohana akaendelea “kuwasomea imla yake”, kama alivyoimba ‘kichaa’ mmoja mswahili. Akafumbia macho misingi ya kinachoitwa sheria; akaipuuza dhana ya haki katika namna zote zile. Sheria ikawa kauli yake na haki ikawa fikra zake. Jambo lingine lolote likawa jinai.

Alizozwa na neno demokrasia, hakutaka kulisikia. Akalipiga vita, akalipinga, akaelekeza lifutwe kote, katika fikra na maandishi. Akaliwekea zuio kutamkwa, akasema, neno hilo ni chanzo cha taharuki na tafrani. Akanadi, wale wote walitajalo neno hilo ni sehemu ya kundi kuu la wasokheri, hawana nia njema na nchi yao ya Nyika. Akasema, “Mimi pekee ndio mwanaheri, nanyi hampaswi kamwe kunihoji.”

Punde si punde, Yohana akaitwa na mamlaka kuu zaidi, naye akaitika, akatwaliwa, akaenda. Papo hapo likawafika fumbo wana wa Nyika, “Ikiwa Yohana ametangulia panapo mamlaka kuu kuliko, je nini haswa kitajiri juu yetu sisi tulio watu baki? Ni upi haswa mustakabali wa nchi yetu ya Nyika?”

Wangali wakiwa bado na mashaka, huzuni na majonzi, akainuliwa Makamu, naye kama Yohana, akatawazwa na kutunukiwa mamlaka. Akajazwa nguvu na kupewa sifa na utukufu wa kuwa Mtu Mkuu, mkuu kuliko watu wote.

Akapanda juu ya mimbari na kuketi katika kiti cha enzi. Akakoma kuwa Makamu, hivyo akawa Amiri na Amrati. Kama wenzake, naye akakikwaa cheo cha Ujemedari.

Tofauti na wenzake hata hivyo, yeye, aliyeuvunja mwiko, alikuwa na jukumu la awali la kulifariji taifa kwa kuondokewa na kipenzi chao Yohana; pasi shaka, akalifanya vyema jukumu hili hapo mwanzo. Wengi wakamsifu kwa kuwapatia amani ya moyo na tumaini. Akazidi kuzikonga nyoyo za watu wake kwa mikogo na mikato yake ya hatari.

Waja wakaanza kumnadi, “Jemedari maridadi. Jemedari mahiri wa mitindo na mjuvi wa kudamshi.”  Hapo akawa si tena Jemedari, naye akawa Jemedarling. Angali akizikonga nyoyo za watu wake, Jemedarling akawaonesha umahiri wake katika lugha, akawajaza misamiati ya Visiwani na kuwafunza salamu maridhawa. Akawasalimu, nao wakaitika.

Mithili ya pira biryani, aliziteka nafsi. Mara darizi, kidogo tobo, huyo akatandika mikasi. Mitandao ikaandika, “anaupiga mwingi, yani kama wote”. Si mashabiki wala wanafiki, wote walidemka na kushirikiana kumnadi Jemedarling. Waliona vilemba vyake havimtoshi, hivyo wakaamua kumvisha ‘vilemba vyengine’, vilivyo vya ukoka na kadhalika.

Kwa mara nyingine tena, wana wa Nyika wakahadaika na kuamini ya kwamba, “Wameipata Suluhu.” Wakaridhika kuwa yupo mwana mwingine aliyetumwa kuja kuwakomboa wao maskini na dhaifu. Tena wakajikosha ya kuwa huyu wa sasa ndiye wa kweli na hodari kulinganisha na mwenzake na wenzake. Nao hawakuona tabu kuweka matumaini yao kwake. Wakamkabidhi nafsi na fikra zao. Mzobe mzobe wakajikabidhi kwake, ili nao, kama yeye, wainuliwe na wapate kuketi palipo pakuu kama yeye.

Jemedarling alipodhihiri ya kwamba amefanikiwa kuwachota wana wa nchi yake, akaanza kujifunza lugha ya watu wake na papo hapo akaanza kuizungumza pasipo kuimaanisha. Ndipo hapo akatamka neno “demokrasia” nao wana wa Nyika wakawehuka, hawakujiuliza nini haswa anamaanisha alitajapo neno hilo. Je, alimaanisha ni ushiriki kikamilifu wa wananchi wengi katika kufanya na kuyasimamia maamuzi; au bado aliendelea kurejea katika demokrasia ya maamuzi ya watu wachache, wanaowajibika kwa wachache, kwa maslahi ya hao wachache?

Alipoihubiri haki na sheria nao wananchi walipatwa na mawaa. Walishindwa kuhoji kwa kina, Jemedarling alimaanisha nini aliposema haki huinua taifa. Ni taifa lipi? La Nyikaheri, Nyikahai au Nyikahoi? Linainuliwaje?

Wana wa taifa hilo nalo watainuliwa na haki? Kama ndio, watainuliwa vipi? Kama la, hatma yao ni ipi? Kwa ujumla, wakasahau ya kwamba, ni Jemedarling, Bintie Hazan, ndiye anayeishikilia na mwenye kujua maana halisi ya haki; na yeye ndio sheria.

Alipoyanadi maendeleo, kwa kutoa msisitizo kwamba maendeleo hayo yatakuwa ya watu na sio vinginevyo, hapo ndipo wana wa Nyika wakashikwa na ‘wazimu’. Wakiwa wanazidi kuserebuka, wakishangilia kwa matumaini kuyapata maendeleo, Jemedarling akakazia, “Sharti maendeleo hayo kufikiwa yapaswa waje wahisani”. Akaendelea kusema, “Wakija wao sote tutapata… wao watapata, nasi tutapata.”

Sauti za nderemo na vifijo zikasikika, nazo zilisema, “Hakika sasa tutaiona neema na ahueni ya kweli iwaja.”Hawakuhoji, ni kwa kiwango gani wao watapata na sisi tutapata. Wachache waliojaribu kuliibua swali hilo, wengi wao walionekana kutokuvutiwa nalo. Hawakujali. Walisema… “wacha waje, itafahamika!”

Kila jaribio la kuhoji uhalisia wa ujio wa wageni iligonga miamba ya vijembe, misemo na nahau. Mara baadhi walisema, “Kaa karibu na uwaridi unukie”. Wengine wakarejea maneno ya Mwana Mkuu Mstaafu, “Ukitaka kula, sharti uliwe.” Wanagenzi wengine wakasema, “Fuata nyuki ule asali.” Lakini vipi kuhusiana na manundu yasababishwayo na nyuki hapo watapokuuma? Hilo la pili hawakujiuliza, wao waliyataka maendeleo, kwa udi na uvumba.

Haukupita muda, baadhi ya wana wa Nyika wakiamini Binti Hazan, Mtu Mkuu, Jemedarling, anazoeleka, ndipo hapo wakaamua kupiga makasia kwenye maji ya demokrasia. “Maji haya tulivu, tutayamudu…,” walijiambia. Hakika wahenga walisema na kughani vyema, “Usione Ukadhani!”  Kasia la pili tu, Wana wa Nyika hao wakakumbwa na dhoruba. Nahodha wa chombo chao akatwaliwa kwa kosa la uharamia wa majini.

Wana wa Nyika wakadhoofu, wakaitazamia sauti ya Binti Hazan, Jemedarling; walijawa na shauku kuisikia sauti yake iwapo itakuwa suluhu, yenye kuwatoa kwenye fumbo la shaka na hofu. Hata hivyo, Jemedarlingi hakusema neno, kama aliyemtangulia na waliomtangulia aliyemtangulia, akaendelea, “Kupiga Kazi!” Mithili ya tembo, hakuzozwa na kelele za vyura. Kwa nini azozwe ilihali yeye ndiye Mwana Mkuu?

Baadae, akiwa ameivaa vilivyo sauti ya mamlaka, Jemedarling akauvunja ukimya, akaamuru yeyote amhojie yeye na mamlaka yake, kwa dhahiri na isivyo dhahiri, naye mtu au watu hao hawana budi kusuluhuhishwa na vyombo vyake vya usuluhishi.

Hakimiliki

Udadisi imetumia vibonzo kwa hisani ya wachora katuni Kipanya, Kingo na King Kinya.