Hasira ni Udhaifu
Hasira hazijengi, wahenga walitwambia
Mbona sasa huzitengi, mwenzangu wazikumbatia
Tena kwa makeke mengi, bila hata kujutia
Hasira ni udhaifu
Ulitongoza kwa pole, huku ukinyenyekea
Ahadi tele na tele, na nyimbo kuniimbia
Nikakuchagua tule, dume nimejipatia
Hasira ni udhaifu
Ndoa ya kisheria, dunia ikashangilia
Mizinga na zumaria, vyote wakatupigia
Wadini walihudhuria, baraka kutupatia
Hasira ni udhaifu
Ndani tumeingia, hasira waniletea
Hila zimekuingia, kila kitu wakemea
Vitisho wanitishia, tena kwa kunionea
Hasira ni udhaifu
Wanangu wawachukia, waziwazi wawambia
Vita wawatangazia, eti adabu kuwatia
Huku ukiwatambia, ubabe ulojitwalia
Hasira ni udhaifu
Wewe si mume wa kwanza, wanne wametangulia
Ubabe utakuponza, wana watakuchukia
Hakika watakubeza, dharau kukujazia
Hasira ni udhaifu
Ulezi ni kuwafunda, pale wanapokosea
Kwa mapenzi bila inda, heshima utajijengea
Nasi tutakupenda, mapenzi kufurahia
Hasira ni udhaifu
Hasira ni udhaifu, si sifa wala ujanja
Watu kuwatia hofu, kamwe hutakidhi haja
Waonesha upungufu, wa ubaba wenye tija
Hasira ni udhaifu
Unanipa fadhaiko, ndoani mtikisiko
Kucha huishi vituko, vyenye kuleta sikitiko
Walitafuta anguko, maafa mtiririko
Hasira ni udhaifu
Nakuomba kwa hisani, acha ubabe wako
Amani ilete ndani, nifaidi mke wako
Watoto wawe furahani, Jenga familia yako
Hasira ni udhaifu
@Mwanahamisi ‘Mishy’ Singano