Hayawi hayawi sasa tunaambiwa yamekuwa. Kwa mujibu wa gazeti la leo la The Citizen, uamuzi wa kuvunja uwanja wa kihistoria wa Nyamagana uliopo mjini Mwanza ili kuwapisha wawekezaji umekwishafikiwa. Uwanja huo ulisanifiwa enzi za mkoloni na Dokta John Thoburn Williamson wa Williamson Diamonds Limited. Uwanja huo ulijengwa mahsusi kwa ajili ya wakazi wa Mwanza ambao mababu na mabibi zao walipoteza maisha yao kwa ajili ya wakoloni kwenye Vita Kuu ya Pili. Hivyo, kwa kipindi kirefu wakazi wa mji huo, wakiwamo watoto, walikuwa na uhuru wa kuutumia uwanja huu. Je, sasa wataipata fursa hiyo lini, wapi, na vipi?

Katika dunia ya leo ya ‘utandawazi’ ambayo inahubiri kuwa wawekezaji wana wajibu kwa jamii (corporate social responsibility) kunakuwa na utata pale wawekezaji wanapowezeshwa kwa nguvu za dola kutoiwajibikia jamii. Mkoloni mmoja aliwahi kusisitiza kuwa hakuna kitu chochote kinachoweza kumfidia mwafrika aliyenyang’anywa ardhi yake. Kama wakoloni na ubaya wao wote waliweza kufikiria walau kidogo kuhusu wajibu kwa jamii waliyoitawala je tunapata picha gani kuhusu ukoloni mamboleo pale tunaposhuhudia ukikiuka hata misingi ya huduma kwa jamii iliyoachwa na ukoloni wa kale? Je, ‘Heri Mkoloni kuliko Mkoloni Mamboleo’?