Kama tatizo ni wanafunzi kutojua Kiingereza mbona wanafeli Hisabati inayofundishwa kwa Kiswahili? Hili ni swali linalorudiwa mara kwa mara matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba yanapotoka nchini Tanzania. Linafanana kiasi na lile swali la: Kama tatizo ni Kiingereza kutumika kama lugha ya kufundishia shuleni, mbona wanafeli Kiswahili Kidato cha Nne?
Matokeo ya Darasa la Saba ya mwaka 2023 yameibua tena mjadala huo mitandaoni. Kama picha ya kitakwimu iliyochorwa na The Chanzo na jedwali la matokeo lililotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA)yanavyoonesha hapo, Kiswahili (87.91%) kinaongoza kwa ufaulu ilhali Kiingereza (34.35%) kinashikilia mkia kikisindikizwa kuelekea huko mkiani na Hisabati (48.83%). Pia tunaona ufaulu mzuri kwenye Uraia na Maadili (82.12%), Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi (77.40%) na hata katika Sayansi na Teknolojia (74.08%). Kulikoni?
Hoja yangu leo ni moja tu. Kuwa ugumu wa kufundishwa na kuelewa Kiingereza kama lugha ya kigeni au lugha ya pili ama ya tatu kwa walio wengi nchini Tanzania hautofautiani na unaoitwa “ugumu” wa Hisabati. Kwa nini? Kwa sababu ‘Hisabati nayo ni lugha ya kigeni.’ Hapa siongelei Hesabu za kawaida za kujumlisha, kutoa, kuzidisha na kugawanya ambazo ni sehemu ya maisha ya mtoto wa Kitanzania kuanzia kwa anayechunga hadi kwa anayevua na anayelima. Hao wote wanajua kuhesabu ndama wangapi wamezaliwa au samaki wangapi wamevulia ama mbegu ngapi zimepandwa. “K” ya kuhesabu katika 3K siyo lugha ya kigeni.
Nazungumzia dhana za msingi na kanuni kuu za Hisabati za madarasa ya juu zaidi kama zilivyoorodheshwa katika Muhtasari wa Somo la Hisabati Elimu ya Msingi Darasa la III–VII utolewao mara kwa mara uliopo katika tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET). Hali kadhalika nazungumza kama mtu aliyepata tabu sana kujifunza lugha hii ya kigeni. Mtu aliyeweza tu kufanikiwa kufaulu Darasa la Saba baada ya nguvu nyingi na uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye somo hilo. Jitihada hizo hizo ndizo zilizomuwezesha kupata ya alama ya “A” kwenye Hisabati katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne baada ya kupitia changamoto mpya ya kufundishwa kwa Kiingereza. Pia anazungumza kama mtu ambaye anawafundisha nyumbani watoto Hisabati kama na yeye alivyofundishwa na waliomtangulia.
Sasa baada ya ‘kujimwambafai’ huko hebu tuungazie muhtasari uliotumika kabla hatujapitia kidogo rasimu ya wa mtaala mpya. Bila kumumunya maneno unasema kuwa umahiri mkuu mmojawapo utakaojengwa kwa mwanafunzi katika somo la Hisabati ni “kutumia lugha ya kihisabati kuwasilisha wazo au hoja katika maisha ya kila siku.” Neno “lugha” limetajwa mara 23 katika muhtasari huo. Hii inaasharia unatambua kuwa Hisabati ina lugha yake.
Kwa mfano, ukifika Darasa la Saba muhtasari unasema unapaswa kuwa na umahiri mahususi “wa kutumia stadi za aljebra katika maisha ya kila siku.” Unasisitiza kuwa kufanikisha hilo shughuli za kutendwa na mwanafunzi ni pamoja na “kurahisisha sentensi za kialjebra zinazohusu mitajo ya namba nzima, sehemu na desimali.” Yaani ukishaanza kuongelea mambo ya sentensi basi ujue umeshaanza kuongelea lugha. Hakika hisabati nayo ni lugha.
Nimeweka hapo chini picha inayoonesha muhstari huo unasema nini kuhusu kupima kuwa mwanafunzi ameelewa yanayohusu aljebra. Kama hujui basi kuanzia leo ujue kuwa hilo neno lina asili ya Kiarabu, yaani al-jabr, likimaanisha muunganiko wa vitu vilivyotenganishwa au kuvunjwa vunjwa kutoka kwenye kitu kimoja. Na linahusiana na neno jabaralinalomaanisha kurudisha na kuunganisha vitu vilivyovunjika au kutenganishwa viweze kuwa kitu kimoja tena kama kilivyokuwa hapo awali. Kiingereza kilikopa Algebra kutoka kwenye Kiarabu.
Hivyo, muhtasari unaposema mwanafunzi aweza kubaini, kukusanya, na kuunganisha mitajo inayofanana na isiyofanana ili kurahisisha sentensi za kialjebra unamaanisha kile kile tunachomaanisha tunapomwambia mwanafunzi wa lugha ya Kiswahili au Kingereza ama Kipare aunganishe herufu zinazoleta neno moja lenye maana. Sasa usipofundishwa na kujifunza Hisabati kama lugha lazima uchanganywe na uchanganyikiwe. Ndiyo hali iliyonikuta Darasa la Tano hadi nikaambiwa nini “kichwa kigumu!” na kuulizwa “kwa nini huelewi?” kisa dhana za kihasabati zilikuwa zinagoma kuingia.Aljebra ilikuwa ‘mashikolo mageni’ Kwangu. Nashukuru nilibahatika kupata msaada wa ziada wa kufundishwa kutoka kwa aliyekuwa mwanafunzi wa Hisabati hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Fred Mtenzi.
Ila sasa kulikuwa na dhana za hasi na chanya zilipochanganywa na aljebra kichwa kikazidi kuchanganyikiwa. Mwangaza mkubwa kuhusu aljebra niliupata siku ndugu yangu mwingine aliyekuwa mwanafunzi wa uhandisi hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Anthony Kilimo, alipoaniambia kwenye aljebra ukikutana na alama ya sawa sawa, yaani = , basi ujue alama ya hasi yaani –, ikivuka kwenda upande wa pili inakuwa chanya na ya chanya, yaani +, ikivuka upande wa pili inakuwa hasi. Kwa maana nyingine, ili kitu kibaki kuwa sawa sawa chochote unachofanya kulia kwa alama ya = lazima ukifanye na kushoto na chochote unachokifanya kushoto basi lazima ukifanye na kulia. Hivyo, kama una hasi 1 upande mmoja na unataka isiwepo basi utaijumlisha na chanya 1, kitendo hicho utakifanya pia upande mwingine.
Vivyo hivyo, ukitoa chanya 2 kushoto basi toa chanya 2 kulia. Ukimpa mtoto mmoja aliye kushoto chungwa moja basi mpe na mtoto aliye kulia chungwa moja waendelee kuwa sawa. Lakini usipofanya hivyo basi hakutakuwa na usawa. Hakutakuwa ana kulingana. Hiyo dhana ya usawa/ulinganifu ndiyo hasa msingi wa hesabu hizo za aljebra kuitwa milinganyo sahili.
Tusipozingatia vilivyo hili la kuwa Hisabati ina lugha yake na pia Hisabati ni lugha basi tutaendelea tu kushangaa na kubishana kwa nini ufaulu wa Hisabati ni mdogo ukilinganisha na masomo mengine yanayofundishwa kwa Kiswahili kama Sayansi na Teknolojia. Uzuri kuna machapisho ya kitaaluma mitandaoni yanayoongelea umuhimu wa kuitazama Hisabati kama lugha kimantiki. Pia watafiti mbalimbali duniani wanatafiti kwa nini kuna changamoto kubwa kwenye uelewa wa Hisabati hata kwenye nchi kubwa iliyoendeleea kama Marekani.
Kwa hiyo hoja ile ile ambayo baadhi yetu tunaitumia kusema ili kuelewa lugha ya Kiingereza inabidi ifundishwe vizuri kama lugha ya kigeni au lugha ya pili ama ya tatu ndiyo hoja hiyo hiyo naiweka mezani hapa leo. Hisabati ifundishwe vizuri kama lugha ya kigeni.
Pythagoras ni Mgiriki/Myunani wa kale, jina lake lenyewe ni la kigeni. Sasa unapotaka mwanafunzi aweze “kueleza aina za pembetatu na kanuni ya Pythagoras” kama isemavyo rasimu ya Muhtasari wa Somo la Hisabati Elimu ya Msingi Darasa la III – VI basi mfundishe lugha ya Hisabati kwanza. Mwalimu naye ajue kufundisha lugha ya Hisabati. Kuwa gwiji wa kukokotoa milinganyo ya aljebra siyo kipimo halisi cha kuwa gwiji wa kufundisha lugha ya kihisabati kama ambavyo kuwa gwiji wa kuzungumza Kiswahili au Kiingereza hakukufanya moja kwa moja mahiri wa kuzifundisha lugha hizo kwa mtu asiyezijua kabisa. Jaribu uone.
Rasimu ya Muhtasari inasema “mbinu za ufundishaji na ujifunzaji zinazopendekezwa” ni “waongoze wanafunzi kutumia michoro ya vitu vya maumbo ya pembetatu katika ubao na kadi za manila kueleza aina za pembe tatu na kanuni ya Pythagoras.” Nami nasema kujifunza lugha yoyote huanza na kuumba. Kuumba maumbo. Namba na herufi ni maumbo. Tuumbeni.