Huyu ndio
Lwaitama… Sijashangaa!

Omar Ilyas

Nimesoma andiko la Dr. Lwaitama. Mzee wetu na mwalimu
wetu lakini pia mpambanaji wa kudumu katika mapambano ya kifikra.

Nimeangalia andiko
lake katika angle mbalimbali na kugh’amua sababu ya alichokiandika, sina
uhakika kama ndio msimamo wake lakini nia ya andiko lake linalolenga kuhalalisha
hatua ya CHADEMA kuwasimamisha uongozi Zitto na Kitila.

Naamini andiko lake
linalenga katika kitu kimoja kikubwa. Hofu ya kuwa na upinzani legevu ama
kudumaa kwa nguvu za upinzani zilizokuwa zikionyesha kukua. Hofu ambayo hata
mimi ninayo na inapaswa kuwepo miongoni mwa wote wapenda maendeleo ya
demokrasia nchini kama mimi na ndugu yangu Zitto na pia wale waumini wa ajenda
ya kuing’atua CCM madarakani hata kwa mbadala wowote.

Katika andiko la
Mzee Lwaitama ameangalia kitu kimoja pekee, nacho ni ule mkakati wa mabadiliko
ndani ya chama ulioandaliwa na Samson Mwigamba na kuhaririwa na Dr. Kitila
Mkumbo.

Mzee Lwaitama
amejaribu kufumbia macho sababu zingine zote zilizofikisha hitimisho la kuwavua
nafasi zote za uongozi Zitto na Kitila. Uamuzi ambao sasa unaonyesha wazi kuwa
ni batili kutokana na ukiukaji mkubwa wa katiba ya chama hicho na uchakachuaji
wa taratibu zao, ingawa wahusika wameamua kukubaliana nao.

Ningeliweza kusema
kuwa hiyo yawezekana ni kwa sababu yeye kama walivyo wengi wanategemea habari
za siasa zetu zaidi kutoka na kile kinachoripotiwa ama kuwekwa wazi katika
vyombo va habari. Yaani ametengeneza angalizo lake katika muktadha wa taarifa
rasmi ya uongozi wa CHADEMA pekee. Ningeliweza kusema labda hakusikia utetezi wa
kina Zitto
ambao ulikuwa na ufafanuzi wa kile kilichojiri katika
kikao kilichofikia maamuzi hayo magumu aliyoyasifia. Lakini hapana. Katika
andiko lake pia amewatuhumu kina Zitto kutokana na utetezi wao hivyo ni wazi
amesikia ama kusoma taarifa ya kina Zitto kwa umma kupitia vyombo vya habari.

Mzee Lwaitama kama
ilivyo kwa uongozi wa CHADEMA na pia muasisi wa chama hicho Mzee Mtei wamekwepa
kabisa kukubali ukweli kwamba, moja; uamuzi uliofikiwa ni kilele cha safari ndefu
iliyoanzia mwaka 2009 mara baada ya Zitto kutaka kugombea Uenyekiti wa chama
hicho na kuambulia kuambiwa na mwenye chama kuwa kama anataka uenyekiti aende
akaanzishe chama chake. Pili; uamuzi uliofikiwa ulifuatia mjadala mrefu wa
zaidi ya nusu ya muda wote wa kikao uliohusiana na kinachoitwa usaliti wa Zitto
wa kukiumbua chama chake kwa unafiki wa suala la uwazi na umakini wa matumizi
ya kodi ya wananchi wanayopata kama ruzuku. Tatu; kuwa mbali na tuhuma ya
kuandaa mkakati wa kugombea uongozi kinyume na mipango rasmi ya viongozi na
wenye chama, kilichotokea ni hitimisho la tuhuma na juhudi lukuki za kumtuhumu
Zitto kwa usaliti wa maslahi ya chama chake na hata kumbambikia fitna ya
kuhongwa na CCM na vyombo vya usalama ili kufanikisha hilo.

Mzee Lwaitama
hakufanya hilo kwa kupitiwa bali kwa makusudi ya kuweza kujenga hoja yake ambao
imelenga katika kuilinda CHADEMA na athari za uamuzi wao ambao umekiuka hata
misingi ya katiba yao. Na hapa ndipo namuona Mzee Lwaitama amepitiliza hata ile
hulka yake niliyoizoea. Kwa andiko hilo ni wazi anapambanua kuwa kwake yeye ni
sawa kabisa kuvunja katiba ama kutumia vibaya misingi ya katiba ili kufanikisha
mchakato wa kuonyesha kuwa CHADEMA ni mahiri zaidi ya CCM.

Lakini pia hata
tukiangalia suala hili kwa msingi wa huo mkakati pekee. Hapa Mzee Lwaitama
hajaitendea haki sifa yake ya uanamapinduzi. Labda ndio masuala ya ustaafu
haya, spirit ya uanamapinduzi inapungua kiasi.

Unapohalalisha
matumizi mabaya ya sheria ama uchakachuaji wa misingi ya katiba yako ili kufanikisha
maamuzi unayo amini ni muhimu kwa usalama wa kundi lako na maslahi yake, ni
dalili ya ama kutokuwa muaminifu wa siasa za misingi ama kuwa tayari kuenzi
hulka ya uvunjaji misingi ndani ya kundi hilo na kwa kuwa kundi hilo ni kundi
la kisiasa ina maana kuwa unarasimisha utamaduni hatari ambao utaathiri zaidi
taifa letu kuliko kuliokoa kama ambavyo Mzee Lwaitama anaamini kuhusiana na
utume wa CHADEMA.

Vilevile inaelekea
Mzee Lwaitama ama hajasikia ama hataki kuamini kuwa ingawa Zitto ni mlengwa
nambari moja wa mkakati huo lakini yeye hakuhusika kuandaa wala hata kuona hadi
ulipowekwa wazi katika kikao cha kamati kuu ya chama chake. Ukiondoa ushuhuda
wa Kitila kuwa Zitto hakuuona mkakati huo hapo kabla lakini hilo linajionyesha
wazi hata ndani ya waraka huo ambao unasema wazi kabisa kuwa endapo Zitto
ambaye ndio mlengwa mkuu akikataa kukubaliana na mkakati huo yaani kukubali
kugombea uenyekiti wa chama chake katika uchaguzi unaokuja basi wengine akiwemo
Kitila na Mwigamba na wengineo ndio waangaliwe kuchukua nafasi ya Zitto
kufanikisha mkakati ho.

Vilevile nashindwa
kukubali kuwa Mzee Lwaitama ameshindwa kung’amua kuwa kama ni suala la makundi
basi hata hao waliowashughulikia Zitto na Kitila ni sehemu ya siasa za makundi
ndani ya chama hicho na pia tuhuma hizo pamoja na uamuzi wa uamuzi wa
kuwasimamisha uongozi na kutaka kuwanyang’anya uanachama ni sehemu ya mkakati
wa upande mwingine kuhusiana na mchakato wa madaraka ya ndani ya chama hicho.
Yawezekana kundi lingine ama pia wakawa na waraka wao ama wakawa wamekosa
weledi wa kuweza kujenga mikakati yao kisomi kama inayojionyesha katika mkakati
wa Mwigamba, lakini mkakati upo na unatekelezwa kwa rasilimali na vikao halali
na haramu vya chama chao.

Lakini zaidi, Mzee
Lwaitama anapohalalisha siasa za makundi za upande wa watawala wa chama na
kuwataka kina Zitto kuendelea kukandamizwa na wao kujizuia kutojitetea ama
kupanga mipango itakayokikomboa chama chao kutoka katika hatima inayojongea kwa
chama chao na taifa lao kutokana na fikra potofu na matendo maovu ya walio
madarakani ati kwa kuwa taratibu za chama chao haziruhusu hilo, hapo ni sawa na
kuwaambia ndugu zetu wa Palestina kuwa wana makosa ya kupanga na kutekeleza
mipango yao ya kulikomboa taifa lao kutokana na ukoloni, ukandamizaji na
ubaguzi wa Waisraeli kwa kuwa wanakiuka sheria za watawala wao na waliopaswa
kutokujiona wanaweza bali wafuate taratibu zilizopo.

Lakini pia katika
hili ndipo ninaposema kuwa Mzee Lwaitama ameandika andiko lake kama vile ni
mmoja wa wale wachambuzi wetu mahiri ambao hufanya uchambuzi wao katika masuala
mbalimbali kwa kutegemea hisia zao, maslahi yao na taarifa a.k.a propaganda
zinazopatika katika vyombo vya habari pekee. Kitu ambacho sitaki kukiamini
kwani hakujuana na Zitto na Kitila barabarani kama alivyojuana na Mbowe, Dr.
Slaa na Tundu Lissu hivyo ni wazi anajua masaibu yaliyowakumba ndugu zake hawa
kwa miaka zaidi ya mitano sasa hadi kufikia kilele chake sasa.

Anajua wazi ni
jinsi gani Zitto amejitahidi kunyamazia mengi na hata wakati mwingine kuudanganya umma kuwa hakuna mgawanyiko ndani ya chama
chake au hata kuwa hakuna mipango ya kummaliza kisiasa na kimaisha

pale yanapotokea mambo kama hayo mradi tu kulinda usalama na ustawi wa chama
chake.

Mzee Lwaitama
anapowakemea ndugu na wadogo zake Zitto na Kitila kwa kuthubutu kujitetea
hadharani kutokana na ujahili wa kisiasa wa baadhi ya viongozi wa chama chao
kitu ambacho anakiona kama kinatishia uimara usiokuwepo wa CHADEMA, ni tukio
ambalo kulielewa unapaswa kujua kwa undani jinsi anavyoangalia siasa za nchi yetu na ni jinsi gani anaamini […] ndio inaweza kututoa hapa
tulipo. 

Nakubaliana na
hisia za baadhi ya watu akiwemo Mzee Lwaitama ambao wanaamini kuwa CHADEMA na
mapungufu yake yote ilifikia lile lengo la kuwa na upinzani utakaoweza kuipa
changamoto CCM na serikali yake na hali hii ina athari katika hilo. Lakini pia
kinachoendelea sasa ni zaidi ya kuendeleza nguvu hizo za upinzani mahiri. Ni
mpambano wa kujenga upinzani madhubuti wenye kulenga kuandaa mbadala makini
badala ya bora mbadala.

Mzee Lwaitama
anaungana na wanaojaribu kujidanganya kuwa mapungufu makubwa yaliyopo CHADEMA
yanapaswa kuendelea kuachwa hadi pale ushindi wa kuiondoa CCM madarakani
utakapopatikana. Lakini ukiwauliza baada ya ushindi kupatikana, yaani
waheshimiwa hawa wanaofanya haya sasa watakapokuwa na dola mikononi mwao,
inawezekana kweli wakajirudi na kuondokana na mapungufu yao ya sasa kwa manufaa
ya kuepusha athari zake kwa Watanzania na Tanzania yetu? Mimi naamini hapana.
Kama ilivyo vigumu kwa CCM kujisafisha hivi sasa ndivyo itakavyokuwa vigumu
CHADEMA kusafishika ikiwa madarakani. Cha ajabu yeye kama mmoja wa wanaoamini
kuwa njia pekee ya CCM kujisafisha na uozo uliokigubika chama hicho ni wao
kutolewa madarakani ndio pia mmoja wa wanaojidanganya kuwa CHADEMA ya sasa
itaweza kubadilika itakapokuwa madarakani.

Kwa kifupi andiko
la Mzee Lwaitama halijalenga kujipendekeza kwa watawala watarajiwa wa CHADEMA
bali kujaribu kupunguza athari za mafanikio ya kimtizamo maslahi lakini makosa
ya kisiasa ya kundi la viongozi hao katika kulidhibiti kundi la wanamadiliko
ndani ya chama katika muktadha mzima wa hatma ya chama hicho na nafasi yake
katika kuwabana CCM.

CHANZO:

https://udadisi.com/2013/11/huyu-ndio-lwaitama-sijashangaa.html