MAELEZO YA HOJA BINAFSI JUU YA KUSITISHA
UGAWAJI WA ARDHI HADI TATHMINI KINA ITAKAPOFANYIKA KUJUA KIASI CHA ARDHI
KILICHO MIKONONI MWA WAGENI

[Chini
ya Kanuni ya 54(1) na (2)]

Mheshimiwa
Spika,

Kwa
mujibu wa Kanuni  namba  54(1) , (2) 
na (3) ya  Kanuni za Kudumu za
Bunge, Toleo la 2007 naomba kutoa hoja binafsi ya kuitaka serikali  kusitisha zoezi  la ugawaji wa ardhi  kwa wawekezaji ( wa ndani na wa nje)  mpaka hapo tathmini  ya kina itakapofanyika  kuweza kubaini ni kiwango gani cha ardhi kiko
mikononi  mwa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika,

Katika miaka ya hivi karibuni, kufuatia mtikisiko wa
uchumi duniani uliokwenda sambamba na upungufu wa chakula , tumeshuhudia wimbi
kubwa la  wawekezaji kutoka nje
,wakinunua au kumilikishwa maeneo makubwa ya ardhi nchini, kwa maelezo kwamba  wana nia ya kuwekeza kwa manufaa ya wananchi
wenyeji  na Taifa  kwa ujumla , hali ambayo itaweza saidia upatikanaji
wa ajira , kukuza uchumi na  kupunguza
umasikini .

Kwa kadiri gharama  za Chakula na uhitaji wa Chakula duniani unavyoongezeka
ndivyo na kasi ya mahitaji ya ardhi  yanavyoongezeka
, wawekezaji  wanaona ardhi kama biashara
nzuri na yenye tija katika miaka ya baadae. Na kwa nchi tajiri zinazoagiza
vyakula toka nje ( China,Japan,Korea ya Kusini ,Saudi Arabia nk.) wanaona
umiliki wa mashamba makubwa kama njia ya kujihakikishia usalama wa chakula
katika nchi zao.Na wakati huo huo Makampuni binafsi makubwa ya
kimataifa wanaiona hii kama fursa ya kujitanua kibiashara na kutengeneza faida
kubwa.

Mheshimiwa
Spika,

Inakadiriwa
kwamba kati ya mwaka 2001 hadi 2010 kulikuwa na maombi ya ardhi zaidi ya  hekta 
milioni 203 katika nchi zinazoendelea. Hii ni sawa na  maombi ya hekta 55,616 kila siku katika
kipindi cha miaka 10[1]
Halikadhalika nchini Tanzania katika miaka ya karibuni takriban  hekta milioni nne zimeripotiwa ‘kuombwa’
na  wawekezaji wa nje  kwa kilimo cha mazao  ya mafuta (AGROFUEL) na Chakula. 

Mheshimiwa Spika,

Kasi  ya maombi ya
ardhi ,na hatimaye kumilikishwa  ardhi  
wageni, imegeuka shuruba kwa wananchi , wengi wao wakiwa ni wakulima
wadogo wadogo ambao wamejikuta wakiondolewa 
kwa katika  maeneo yao ya
asili  ili kuwapisha  wageni. Wengi wao wakiachwa hohe hahe, na katika
lindi la umasikini mkubwa. Hii inatokana na ukweli kwamba kumekuwa na tafsiri ambayo sio sahihi, kwamba ardhi wanayopewa
wawekezaji haina wenyewe/haina mtu /haitumiki .
Wakati
ukweli ni kwamba maeneo mengi kama sio yote yalikuwa yanatumiwa n a wakulima
wadogo .

Mheshimiwa
Spika,

Hali
halisi inaonyesha kwamba , ni sehemu ndogo sana ya ardhi inayochukuliwa  na wageni inatumika kwa manufaa ya
kutatua/kupunguza matatizo ya njaa katika nchi husika . Hali kadhalika maeneo mengi ardhi yanayochukuliwa na wawekezaji
hao  huwa hayaendelezwi kama inavyopasa ,
na yale ambayo yanaendelezwa , yanaendelezwa kwa kiwango kidogo sana huku
wananchi wengi wakiachwa pasi na ardhi ya kutosha kwa kilimo. Na katika hatua
nyingine, wawekezaji baada ya kupata /kumilikishwa ardhi kwa bei ya kutupa,
hawaitumii,wanasubiri ipande thamani  ,
kisha kuiuza kwa faida kwa wawekezaji wengine.


Mheshimiwa
Spika,

Ninaliomba  Bunge lako tukufu , likubaliane na hoja ya
kuitaka  Serikali kusitisha zoezi la
ugawaji wa ardhi ili kuweza kutoa fursa ,kama nchi kuweza kujitahmini kwa kina,
wapi tulikosea ili tuweze kujipanga upya kwa manufaa ya nchi na wananchi. Hii
inatokana na ukweli kwamba hata wizara ya ardhi leo wakitakiwa kutoa taarifa
sahihi ya ardhi kiasi gani iko chini ya miliki ya wageni,hawana takwimu
sahihi,zaidi ya zile chache zilizopatikana kupitia Tanzania Investment Centre
(TIC) na ambazo pia zimethibitika kuwa na mgogoro mkubwa kutokana na taratibu
kutofuatwa.

Mheshimiwa
Spika,

Mifano
mingi inaonyesha kwamba  kumekuwa na
ubabaishaji mkubwa sana na kuumizwa sana kwa wananchi , na  mbaya zaidi katika mazingira mengine serikali
imekuwa kuwadi wa wawekezaji dhidi ya wananchi wake. Kuna haja kubwa kwa
waheshimiwa wabunge kutambua kuwa matatizo ya ardhi yanayoikumba Rufiji,
Kilombero, Bagamoyo, Kisarawe na lugufu yanaikumba pia Muheza, Pangani, Katavi
,Meatu, Kinondoni, Njombe na Ngorogoro.Hivyo
basi kuna haja kubwa ya kujenga mshikamano 
kwa kuunganisha nguvu ili kulinda maslahi na rasilimali za umma.Nitatoa
mifano michache, kuonyesha uzito wa tatizo hili:

 Bonde
la Mto Rufiji (Rufiji River Basin)

Hili ni
eneo lenye ukubwa wa Km za mraba 176,000. Linajumuisha Rufiji Delta,
Luwero,Kilombero na Mto Ruaha..93% ya wakazi wa maeneo wanaozunguka  eneo hili wapatao 500,000  wanajishughulisha na kilimo, kama wakulima
wadogo wadogo. Kutokana na umuhimu na unyeti  
wa eneo husika kumekuwa na wimbi kubwa la makampuni ya kigeni,
wakipeleka maombi moja kwa moja kwenye vijiji au kwa kupitia baadhi ya vyombo
vya serikali (RUBADA- Rufiji Basin Development Authority) ambavyo vimeacha
majukumu yake na kugeuka kuwadi wa wawekezaji.

Mheshimiwa
Spika,

Makampuni
yafuatayo; ( SEKAB  Tanzania Ltd
(Sweden), African Green OIL Ltd , SAP Agriculture Ltd (Turkey ), RUBADA na
Korean Rural  Community Corporation ,
Kilombero Plantation  Ltd ( British) ,
Kilombero Valley Teak  Co. Ltd ( British)
, Kilombero Sugar Co. Ltd  (South Africa)
, Kilimo cha Yesu ( Uswiss), na Eurovistas (India)  ni kati ya makampuni yaliyomilikishwa ardhi
iliyokuwa  inatumiwa na wanakijiji kwa
shughuli za kilimo. Wengi wao wakitolewa kwa nguvu ili kuwapisha wawekezaji kwa
kurubuniwa kwa kauli tamu.Wakiahidiwa kuletewa maendeleo. Ahadi ambazo nyingi
zimegeuka za uongo huku tayari vijiji vikiwa vimepoteza uhalali wa kutumia
ardhi yao.

Mheshimiwa
Spika,

Taarifa
zinaonyesha kwamba katika ukanda huu , ukiacha makampuni ya  Kilimo cha Yesu (Uswis) na Kilombero Sugar
Co, kilombero Plantation Co na Kilombero Valley Teak(British), wawekezaji wengine
waliokabidhiwa  maelfu ya ardhi ya
watanzania wameyaendeleza kidogo sana au kuyatelekeza kabisa mashamba !
inawezekana wakisubiri ardhi ipande thamani wawakabidhi wenzao kwa gharama
kubwa .[2]

Kisarawe:

Sun
Biofuels Ltd  ni kampuni ya kiingereza
inayojishughuliza na kilimo Jatropha . Wanahisa wake wakubwa  ni kampuni ya  Sun Biofuels Plc ya Uingereza yenye hisa 88% , Julian ozanne ( mwingereza)
mwenye hisa 10% na watanzania
wawili,  Daudi Makobore  na Herbert Marwa wenye hisa 2% (yaani 1% ).

Inasemekana
mwekezaji huyu  alipanga kuwekeza  kiasi shilingi bilioni 25.3 za kitanzania,
lengo likiwa kujenga mtambo wa kufulia mafuta 
na kilimo cha Jatrofa ( pamoja na mihongo kwa ajili ya kuwalisha
vibarua). Ilikadiriwa kutokana na uwekezaji huo zingepatikana ajira za kudumu  1,500 , na ajira za ziada kwa vibarua hasa
wakati wa uvunaji.

Mwaka
2009 Kampuni ilifanikiwa  kupata eneo
lenye ukubwa wa hekta 8,211 kutoka vijiji 11 vya ( Mtamba, Muhanga,
Marumbo,Palaka, Kidugalo, Kurui (40% ya eneo la kijiji lilichukuliwa ),Mtakayo,
Vilabwa , Mitengwe, Mzenga ‘A’ and Chakaye. Hata hivyo mwezi  Oktoba 2011, mradi husika ulisamama kutokana
na ukosefu wa fedha, na mustakabali wa ardhi ya 
kijiji haujulikani.

Mwanakijiji
mmoja wa kijiji cha  Palaka  , Kisarawe alinukuliwa akisema  kwamba walikubali kuwaachia ardhi wawekezaji
kwa mdomo, pasi kuandikiana popote kwa sababu waliaziamini ahadi zao za kutoa
huduma za jamii i.e maji, barabara,shule nk, lakini hakujua kiasi gani cha eneo
lake kinapaswa kuchukuliwa kwa sababu hawakuwa na nyaraka zozote za kuonyesha
mipaka ya shamba lake. Hakuwa anafahamu
haki zake za kisheria
,hivyo hakujua madhara ya kile alichokikubali mpaka
alipopoteza ardhi yake yote bila  kulipwa
fidia.[3]

Mwananchi
mwingine wa kijiji cha Kurui,
alinukuliwa akisema kuna tofauti kubwa kati ya makubaliano ya kutoa ardhi na kushiriki 
katika mkutano wa kijiji
. Anadai kwamba kushiriki kwao katika kikao
cha kijiji ,kulichukuliwa kama kukubali kutoa maeneo yao . Hakuingia
makubaliano na mtu yeyote kutoa eneo lake.[4]
Eneo lilichukuliwa na mwekezaji , majina ya mahudhurio yalitumika kama
kielelezo kuonyesha kama waliafiki,wakati hawakufanya hivyo.

Rukwa:

Mheshimiwa
Spika

Eneo hili ,linahusisha Hekta 80,317 (Katumba) na 219,800
( Mishamo) kwa ajili  ya  Kampuni ya kimarekani ya Agrisol .Majadiliano
yanaratibiwa na viongozi wakubwa  sana
Serikalini. Mradi huu umejikita kwenye uendelezaji wa mashamba makubwa , na
matumizi ya mbegu zenye viini tete (GMO). Ili kufanikiwa kwa mradhi huu wakulima
wadogo wadogo wapatao  162,000 walitakiwa
kuhama kumpisha mwekezaji huyo wa kigeni.

Licha ya
kelele nyingi kupigwa juu ya makosa ya kiufundi ambayo serikali inayafanya kwa
kutaka kulikabidhi eneo kubwa na lenye rutuba kwa wageni , na licha aliyekuwa mshirika muhimu wa Agrisol IOWA State
University College of Agriculture ,aliyekuwa mhimili muhimu wa mwekezaji huyu
hasa katika kuwasaidia wakulima wadogo kujitoa baada ya kugundua kwamba
mwekezaji huyu hana dhamira ya kuisaidia nchi na wakulima wadogo zaidi ya
kujinufaisha kibiashara.Na kwamba alikitumia Chuo husika ili apate uhalali wa
kukubalika kirahisi kama mwekezaji mahiri. Serikali inaonekana bado imeziba
masikio!

Kigoma

Wawekezaji
walionunua ardhi mkoa wa Kigoma ni Agrisol na FELISA.

FELISA
amenunua ekari 3000 katika wilaya ya uvinza kijiji cha basanza kata ya uvinza.
Wawekezaji hawa wamewakuta wakulima na wafugaji katika maeneo haya. Wafugaji na
wakulima wakagoma kuondoka kwakuwa walikuwa wakiendesha maisha Yao kutegemea
ardhi hiyo Huu ni ushahidi dhahili kuwa hakuna ziada ya ardhi ukilinganisha na
mahitaji. Mwekezaji kwa kushirikiana na vyombo vya dola alianza zoezi la
kuwatoa wananchi mwezi Mei  mwaka huu akitumia
vikosi vya mgambo kupiga wananchi, kuchoma nyumba, kuharibu mazao na halikadhalika
kuwafungulia wananchi mashtaka!

USHAHIDI
ZAIDI KUHUSU MGOGORO HUU TAYARI KUNA KESI MAHAKAMA YA MWANZO MWANDIGA KIGOMA
KATI YA WAKAZI WANAOGOMA KUHAMA NA MWEKEZAJI.

AGRISOL

Mwekezaji huyu
amepewa hekta elfu 10,000 eneo la Lugufu. Eneo hili ndio ili kuwa kambi ya
wakimbizi. Na eneo hili ndio limetengwa kuwa Makao makuu ya wilaya . Kwa mujibu
wa  Mbunge wa Kigoma Kusini (ambaye eneo
lenye mgogoro liko ndani ya jimbo analoliwakilisha), Mhe David Kafulila alipozungumza  na watendaji wa halmashauri walikiri kuwepo
shinikizo kutoka ngazi za juu.

Na hii inatokana na mantiki ya kawaida tu kuwa
uamuzi wa kumpa mwekezaji huyu Eneo hili ni Sawa na kuamua Makao makuu ya
wilaya ya uvinza yazungukwe na shamba na mwekezaji. Hivyo mji ambao ni Makao
makuu hautatanuka kwasababu utakuwa eneo dogo sana lililozungukwa na shamba.
Nasema eneo dogo kwasababu mpaka sasa haijafahamika Makao hayo makuu yatawekwa
wapi wakati eneo lote kashapewa mwekezaji. Labda serikali imwombe Agrissol eneo la kujenga wilaya.

Mheshimiwa
Spika,

Zaidi ya
mkanganyiko huo pia kuna tatizo la mahitaji ya ardhi, wakazi wa eneo la jirani,wanaotoka
Uvinza na Mwamila wanahitaji kulima katika eneo hili lakini wanazuiwa. Taarifa
ya mahitaji ya eneo hili kwa wakulima wakawaida ipo ofisi ya mkuu wa mkoa
Kigoma.Mkuu wa Mkuu wa Mkoa anakiri kuwa ni tatizo, na kupendekeza labda watu
walime kwa muda wakati mwekezaji hajafika. Wakazi mwamila walifanya jaribio la
kutaka kulima mwaka huu wakafukuzwa.

Mheshimiwa
Spika,

Mchakato
mzima wa agrossol kupewa eneo halikuridhiwa na 
wana kijiji,halmashauri na wataalamu walishinikizwa. Na isisitizwe kuwa
uamuzi huu unakinzana na juhudi za serikali yenyewe kusukuma wananchi katika
kilimo kwani wilaya ya uvinza Hivi sasa mbunge amekopa trekta nne ili kusukuma
kilimo kwa yeye kulima na wananchi kulimiwa kwa bei ya chini kuliko bei ya
serikali.Halmashauri awali ili kuwa na kituo chenye trekta mbili hapo lugufu
Kama kituo cha huduma ya matrekta ya kilimo kwanza, pia halmashauri imenunua
trekta tano kwa ajili ya kusukuma kilimo wilaya hii. Juhudi zote hizi ambazo ni
matunda ya mkopo ya SUMA JKT, INAKWAMISHWA NA UAMUZI WA SERIKALI KUUZA ARDHI.

 Mheshimiwa Spika,

Ni muhimu ikaeleweka
kwamba,hakuna anayepinga umuhimu wa uwekezaji, lakini ni muhimu vile vile
ikaeleweka kwamba hatutaweza kuendelea kama tukikabidhi kila kitu kwa wageni.
Sote tunajua ni kwa namna gani dhahabu, almasi 
na Tanzanite zimetumika kujenga uchumi wa mabeberu! Hatuwezi kufanya
makosa tena kwenye rasilimali hii muhimu ya ardhi  inayopanda thamani kwa kasi sana! Uchumi
hauwezi kuachwa uendeshwe na watu wa nje!

Mheshimiwa
Spika,

Kutokana
na uwekezaji kutoka nje wa makampuni makubwa uchumi wa Tanzania unarekodiwa kukua
kwa asilimia 7. Hiki ni kiasi kikubwa kinachoifanya nchi hii kuwa miongoni mwa
nchi 20 kileleni kwa kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi dunia lakInI wakatihuohuo
inasikitisha kuona nchi hii ni miongoni mwa nchi 20  duniani. Hii inatokana na ukweli kuwa kilimo
kinachoajiri 70% ya watanzania kimeachwa, njia ya kuondoka kwenye
mlinganyo(equation) hiyo ni ARDHI. wakulima wadogo wagawiwe ardhi, wawezeshwe
zana na ufundi kwa kilimo.

Mheshimiwa
Spika,

Mambo
kadhaa yamejitokeza :

1)  Uvunjwaji
wa haki za binadamu  

2)  Kutokuzingatiwa
kwa sheria inayotaka wananchi ,waarifiwe mapema washirikishwe na kupewa taarifa
sahihi , ili wafanye uamuzi ulio sahihi kwa maendeleo yao (the principle of
free ,prior and informed concent-FPIC)-kuhusiana na mradi husika.

3)  Mikataba
iliyotawaliwa na usiri mkubwa, na wakati mwingine sheria za nchi kupuuzwa .

4)  Serikali
kulipwa fedha kidogo sana. Wastani wa gharama ya kukodi ardhi ni shilingi 200
kwa hekta kwa mwaka. Na muda wa kukodisha ardhi kisheria ni miaka 99.Gharama
hii haijalishi eneo shamba lilipo au mazao yanayozalishwa.

Mheshimiwa
Spika,

Inawezekana
kabisa Tanzania tukawa hatujafikia  hali
mbaya kama ilivyo kwa nchi nyingine…..zaidi ya  30%  ya
ardhi ya Liberia imekabidhiwa kwa wakulima wakubwa  wa Nchi za magharibi katika kipindi cha miaka
mitano! Halikadhalika katika nchi ya  Cambodia , inakadiriwa  linalokadiriwa kuwa 56-63% ya ardhi yote
inayotumika kwa Kilimo iko mikononi mwa makampuni binafsi ya kigeni. Hivyo basi
Serikali ya Tanzania ina fursa ya kujipanga mapema,kabla hali haijawa mbaya!
Lazima kuwe na mjadala mpana wa kitaifa ili tuweze kupata njia bora ya kusonga
mbele.Hatuta kuwa wa kwanza kufanya hivyo. Jirani zetu wa Msumbiji  wa Msumbiji wamefanya hivyo, halikadhalika
serikali ya Papua New Guinea !

Ni muhimu kufanya maamuzi sasa . Maamuzi tutakayoyafanya
sasa yatakuwa na athari chanya ama hasi kwa kizazi kijacho . Inakadiriwa
ifikapo mwaka 2050 watanzania tutakuwa milioni 150, kama leo ardhi yetu
tunagawa kwa wageni kwa muda wa miaka 99, tunaweka akiba gani kwa kizazi
kijacho? Nini usalama wa Chakula na Uchumi kwa Tanzania ya kesho?

HOJA BINAFSI KUHUSU KUSITISHA UGAWAJI WA
ARDHI KWA WAWEKEZAJI HADI TATHMINI YA KIASI CHA ARDHI ILIYOGAWANYWA
UTAKAPOFANYIKA

[Chini
ya Kanuni ya 54(3)]

Mheshimiwa
Spika,

Kwa
kuwa
rasilimali ardhi ndio urithi pekee wa asili wa mtanzania
katika kujitafutia riziki na kuendesha maisha yake;

Na kwa kuwa  idadi ya watu inaongezeka wakati ukubwa wa
ardhi hauongezeki jambo ambalo linaonesha dhahiri kwamba kuna hatari  ya kiasi cha ardhi kilichopo kisitosheleze
mahitaji halisi ya wananchi;

Na kwa kuwa kumekuwa na ugawaji
ardhi kwa wawekezaji hasa wa nje 
usiojali mahitaji ya ardhi kwa wananchi siku za mbeleni;

Na kwa kuwa  imebainika kwamba  uwekezaji 
katika ardhi unaofanywa na makampuni ya nje haujawasaidia wananchi kwa
maana ya fursa za  ajira na  upatikanaji wa  chakula kwa kiwango kilichoahidiwa na Serikali
na makampuni hayo;

Na kwa kuwa ugwawaji huu wa
ardhi kwa wawekezaji unakwenda sambamba na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu
ikiwa ni pamoja na wananchi waliokuwa katika maeneo hayo kupigwa, kuvunjiwa
nyumba zao na kufukuzwa bila kulipwa fidia;

Na kwa kuwa kwa kiasi kikubwa
zoezi la ugawaji ardhi kwa wawekezaji linakiuka sheria za nchi ambazo zinataka
wananchi waarifiwe mapema juu ya ugawaji huo wa ardhi na kushirikishwa
kikamilifu ili waweze kufanya maamuzi sahihi kwa maendeleo yao jambo ambalo
halifanyiki;

Na kwa kuwa mikataba ya ugawaji
wa ardhi inafanyika kwa usiri mkubwa 
jambo ambalo linaashria mazingira ya rushwa na kutia shaka kama maslahi
ya nchi yanazingatiwa;

Na kwa kuwa  Serikali inapata kodi kidogo sana kutokana na
uwekezaji katika ardhi ( yaani shilingi 200 kwa hekta  kwa mwaka) na ikizingatiwa muda wa kukodisha
ardhi kisheria ni miaka 99;

Na kwa kuwa asilimia 80 ya
watanzania wanategemea ajira katika sekta ya 
kilimo ambacho msingi wake ni ardhi;

Na kwa kuwa Ibara ya 63(2)(c) na
(d) ya Katiba ya Jamjhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inasema kwamba: “Kwa
madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza; kujadili na kuidhinisha
mpango wowote wa muda mrefu na wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika
Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo;
kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria”;

HIVYO BASI, naliomba Bunge
liazimie:

1.   KWAMBA,
zoezi la ugawaji ardhi kwa wawekezaji wa nje na ndani lisitishwe hadi hapo
tathmini ya kina itakapofanyika kubaini ni kiasi gani cha ardhi kipo mikononi
mwa wawekezaji na wasio wawekezaji.

2.   KWAMBA, tathmini
ya kina ifanyike kuweza kubaini raia wa kigeni na wa ndani waliojipatia ardhi
kinyemela kupitia serikali za vijiji kinyume na matakwa ya sheria ya ardhi Na.
5 ya mwaka 1999.

Mheshimiwa
Spika,

Baada ya
kusema hayo,

Naomba
kutoa hoja.

…………………………………..

Halima James Mdee(Mb)

Jimbo la Uchaguzi-Kawe

05.11.2012



[1] ILC ( 2011) ‘Land Rights and the Rush for Land’, http://www.landcoalition.org/cpl/CPL-
Synthesis-report. 

[2] Land
Grabbing in a post investment period and popular reaction in the Rufiji River Basin. A
Research Report by Haki Ardhi, 2011. Study carried out by Dr . Abunuwasi Mwami of the Department of
Sociology , University of Dar es salaam and Dr Ng’wanza Kamata of the
Department of Political Science , University of Dar es salaam

[3]
Participant in Community focus Group discussion , Palaka Village ,
Kisarawe District , December 3 , 2010
cited in Frederic Mousseau et al . “Understanding Land Investment Deals in Africa – Country
Report Tanzania”

[4] ibid