Kongole Emmanuel Amunike, Hongera Taifa Stars – Lakini Hatuna Budi Kujitathmini!
Richard Mbunda
Nilitamani makala haya yawe kwa lugha ambayo Kocha Emmanuel Amunike ataielewa. Lakini, la hasha! Ni andiko la umma, najua ujumbe utamfikia tu. Kwa kweli nampongeza kwa kuweka historia, kwa kuipeleka Tanzania kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Misri baada ya mika 39.
Haikuwa kazi ndogo. Ama kweli wachezaji wetu, viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) na Kamati ya Uhamasishaji wanastahili pongezi. Kwa takribani wiki moja furaha ya Watanzania iliongezeka maradufu. Kwa hakika Watanzania wanapenda michezo. Hasa ukizingatia pia kuwa usiku wa tarehe 23 Bondia wetu Hassan Mwakinyo alimnyuka Muajentina Sergio Gonzalez kwa KO. Hii inatoa changamoto kwa Serikali na taassisi zinazosimamia michezo kuwekeza zaidi. Kuna faida nyingi katika michezo, ikiwemo kuongeza furaha katika jamii ili tuondoke mkiani mwa nchi sizizo na furaha Duniani.
Tumebahatisha?
Naam, hatimaye tunaenda Misri. Ilikuwa kama ndoto tu, maana kimsingi tangu tulipofungwa kule Lesotho, tulipoteza matumaini kiasi. Swali la kujiuliza je, tulistahili au tumebahatisha? Vijana wa Kitaa wangesema tumetusua!
Mimi sitaki kupepesa macho katika hili. Napenda kusema wazi kuwa Tanzania ilistahili kwenda Misri. Nina sababu kuu mbili katika kutetea hoja yangu. Mosi, uzoefu wa kufuatilia kwangu michezo ya kufuzu AFCON. Mara zote huko nyuma, Tanzania ilikuwa ikipangwa na timu angalau mbili ngumu na wazoefu wa michuano hiyo. Kwa namna yeyote Tanzania ilikuwa ndiyo timu nyonge – ‘underdog’. Kwa mfano, mwaka 2016, Watanzania watakumbuka tulimenyana na Misri, Naijeria na Chad (ambayo baadae ilijitoa). Tulimaliza wa mwisho na point 1 tu wakati Misri ilikuwa na pointi 10.
Lakini mwaka huu ulikuwa wetu. Tulipangwa na Uganda, Cape Verde na Lesotho. Japo Cape Verde na Uganda walishawahi kushiriki AFCON hivi karibuni, lakini tulikuwa tunawamudu. Na kimsingi Uganda ndiyo iliyoongoza kundi, lakini historia inaonesha kama wachezaji wetu wakihamasika huwa tunawafunga Uganda. Matokeo ya kundi hili yanadhihirisha wazi kuwa tulikuwa na uwezo wa kupata nafasi. Niliwahi kusema mwaka jana kuwa kama hatutashiriki AFCON mwaka huu kutokana na hili kundi, huenda tusingeshiriki tena miaka 10 ijayo.
Pili, tofauti na siku za nyuma, wachezaji wetu wameongeza ujuzi na ari ya kupambana. Tuna karibia wachezaji 10 wanaocheza katika ligi zenye ushindani Ulaya na Afrika, wakiongozwa na nahodha wao Mbwana Samatta, ambaye ni mfungaji bora wa ligi ya Ubelgiji. Haya si mafanikio kidogo. Kwenda kucheza nje kwa wachezaji kama Simon Msuva, Thomas Ulimwengu, Shaaban Chilunda, na Abdi Banda kumewapa ari, kujiamini na mbinu mpya. Lakini pia tumeona mpira unaochezwa na wachezaji wa ndani umeendelea kukua na kuwa wa ushindani zaidi. Wachezaji hawa wameweza kupambana na kutupeleka Misri. Mtu awaye yeyote asiwabeze na kuwabagaza wachezaji hawa. Wanaweza, na ndiyo maana wanang’ara hata kwenye timu zao nje na hapa nchini.
Wapi Tulichemka?
Watu wakifanikiwa hawataki tena kurudi nyuma na kufanya tathmini ya wapi walikosea. Mimi nitajitahidi kuwakumbusha tu, hata kama hamtaki. Tumeshangilia sana mechi ya mwisho, na wengine kidogo tufe na shinikizo (pressure) kwani tunapenda kwenda Misri. Naam, kuna changamoto tulizokumbana nazo.
Mosi, naikumbuka sana mechi ya kwanza kati ya Taifa Stars na Lesotho. Nilihamasika sana kwenda kuishangilia timu yangu ya taifa pale tu ratiba ilipotoka. Lakini pasi na sababu zenye ushawishi, TFF walipeleka mechi yetu ya ufunguzi Chamazi. Binafsi naona kulikuwa na changamoto za aina mbili. Pamoja na kuwa Chamazi ni Dar es Salaam, na tunajua hamasa wa mashabiki wa soka wa Mbagala, lakini ni ukweli usiopingika kuwa Taifa Stars ilikosa mchezaji wake wa 12 ambao ni mashabiki katika ujumla wao. Lakini vilevile, kwa kuwa mechi ilikosa hamasa, wachezaji wetu walicheza kama wapo ugenini pia. Nilifuatilia mtanange huo kwa runinga, na nikasikitishwa sana na sare. Kama TFF wangefanya maandalizi vizuri kwa kuleta hamasa na kuhakikisha mechi inachezwa kwenye Uwanja wa Ben Mkapa, zile zingekuwa pointi tatu safi kabisa kibindoni.
Changamoto ya pili, inamhusu Kocha Amunike. Mimi nikiri kuwa nilisisimka na kuhamasika sana alipoteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa. Huyu ni kocha mwenye wasifu (CV) (m)kubwa na hasa uzoefu katika soka, na amecheza katika klabu bora zaidi duniani – Barcelona – na ameshiriki Kombe la Dunia. Lakini aliniacha hoi sana alivyoamua kuwaacha wachezaji sita katika mechi yake ya kwanza tulipoenda Uganda. Najua Kocha anapaswa kuhimiza nidhamu, na najua kuna wachezaji wengi walioshindwa kunufaika kwa vipaji vyao kwa sababu ya nidhamu.
Lakini, kwa maoni yangu, siyo majukumu ya kocha wa timu ya taifa kutengeneza vipaji au hata kufundisha nidhamu. Hii ni kazi ya vilabu na makocha wa vilabu. Kocha wa timu ya taifa anakuwa na wachezaji kwa muda mfupi sana. Kwa hiyo, kazi yake yeye ni kuchagua wachezaji walioiva. Kuhusu wachezaji wa Simba tuliambiwa kuwa aliyekosea aliwajibika lakini kocha bado aliwaacha wale wachezaji. Na hawa ndio wachezaji wetu ambao sisi Watanzania tunadhani wangetupeleka Cameroon kabla haijapokonywa uwenyeji wa michuano na kupewa Misri.
Kwa maoni yangu, nilitegemea kocha achukue majukumu kama mlezi wa vijana, awajenge wachezaji kisaikolojia ili wasipoteze morali. Lakini kubwa zaidi, fikra za kila Mtanzania ilikuwa juu ya ushindi wa mechi dhidi ya Uganda ugenini. Mimi sisiti kusema ya moyoni. Niliangalia ile mechi dhidi ya Uganda na, japo tulikosa nafasi moja au mbili za kufunga, nikiri tu kuwa kilichotuokoa ni mvua kubwa iliyokuwa imenyesha ikafanya uwanja usiwe rafiki kwao na kwetu. Tukarudi nyumbani na pointi moja na ikamuongezea Amunike kujiamini na pengine kuhalalisha maamuzi yake.
Naomba nisiongelee yaliyotokea ugenini Estádio Nacional de Cabo Verde, kwa kuwa tulipigwa kipigo cha aibu, lakini tulijifunza. Tuliporudi katika mechi ya marudiano, sijui benchi la ufundi lilipatwa na nini nikaona baadhi ya wachezaji wazoefu waliokuwa katika kiwango cha juu kabisa wakiitwa na kupewa majukumu. Tukashinda 2-0 na kila mtu akahisi sasa ndoto imekaribia. Kimsingi mechi ya Lesotho ndiyo ilikuwa fainali yetu, hasa kama tulikuwa tunataka kujihakikishia ushindi. Namshukuru Mh. Rais Dkt. John Magufuli kwa kuongelea mechi hii, hususani jinsi kikosi kilivyopangwa.
Mh. Rais, si wewe peke yako, Mimi niliangalia hii mechi nikiwa mjini Sumbawanga. Wanasumbawanga walisikitishwa sana, na niliwasikia wakitaja majina ya wachezaji ambao hawaamini kwa nini hawakuwa chaguo la kocha. Timu ilicheza kwa kiwango duni sana, na sijui kocha na benchi la ufundi walikuwa wanawaza nini. Haya, tukafungwa. Lakini hatukuishia hapo. Benchi la ufundi likajifunza tena. Tukaona wachezaji kama John Bocco, ambaye naamini anabezwa kuliko sifa anazostahili kwani amekuwa katika kiwango bora kabisa, akifunga na kutoa mapande (assists) muhimu kwa timu yake ya Simba. Mungu mkubwa na sasa tunaenda Misri.
Tugange Yajayo
Tanzania ni moja kati ya timu 24 zitakazoshiriki michuano ya AFCON kuanzia June 7 hadi Julai 13, 2019. Kwa utaratibu wa michuano ya mwaka huu, kutakuwa na makundi 6 yenye timu 4. Timu mbili katika msimamo wa kundi baada ya mechi za makundi zitaingia hatua ya 16 bora. Hii ni hatua ya mtoano. Lakini kwa kuwa timu zitakazoingia moja kwa moja ni 12 tu, basi zitaongezeka timu 4 zitakazoingia kwa tiketi ya walioshindwa kiasi (best loser), ili kufanya idadi ikamilike 16. Ndipo timu hizi zitacheza mtoano, Timu 8 zitakazofuzu zitaenda robo fainali. Timu 4 zitakazoshinda hatua ya robo fainali zitacheza nusu fainali. Kuna mshindi wa tatu katika michuano hii, ambapo wale watakaotolewa katika hatua ya nusu fainali watachuana tena kupata mshindi wa tatu, wakati washindi wa nusu fainali watacheza fainali Julai 13, 2019.
Sisi tunataka kuishia wapi?
Ni swali gumu. Lakini mimi kama shabiki naona haitoshi kuishia tu hatua ya makundi. Tunapaswa kuutangazia ulimwengu kuwa soka letu limekua na tunapaswa kuangaliwa tofauti na ilivyozoeleka kuwa Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu. Tunapaswa kufika hatua ya mtoano. Hii itasaidia Tanzania kupanda katika orodha (rankings) za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Shirikikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kitu ambacho kitasaidia wachezaji wetu wenye vipaji adimu kupata timu Ulaya na kwingineko. Naamini kama benchi la ufundi likifanya ipasavyo na wachezaji wakapata hamasa, tutafika mbali.
Maangalizo
Mtanisamehe tu kwa kuwa sitawaacha bila vidonge hasa kwa benchi la ufundi. Rukhsa kunipuuza kuwa sijui soka. Lakini nitatumia nafasi yangu kama shabiki kutoa maoni.
Tutaweza kufanya vizuri kama Kocha Amunike na benchi la ufundi wataanza kuamini kama wachezaji wetu wanaweza. Nilikuwa namsikiliza Amunike wakati wa mkutano na waandishi wa habari (press conference) baada ya kuwachabanga Uganda goli tatu kwa nunge, Kocha alionesha wazi hakuiamini timu yake. Ni hatari kwenda vitani na kamanda ambaye hawaamini askari wake.
Nimemkumbuka Kocha Marcio Maximo. Tanzania itamkumbuka kocha huyu Mbrazil kwa kuleta hamasa kwa timu wa taifa. Lakini Kocha huyu hakuwahi kuamini kama Watanzania wanajua kucheza mpira. Moja ya vielelezo katika hili, Maximo hakuwahi kuwa na kikosi cha kudumu [kwa maana ya First Eleven].
Uzoefu wa makocha magwiji duniani, kama Sir Alex Ferguson aliyeifundisha Manchester United kwa miaka mingi ya mafanikio na Arsene Wenger aliyepata kuifanya Arsenal ikawa moja ya vilabu vikubwa Ulaya, unatufundisha kuwa hupaswi kubadili kikosi kinachokupa ushindi bila sababu ya msingi. Sasa unajiuliza Amunike aliwaza nini kubadili kikosi kilichompa ushindi dhidi ya timu nzuri kama Cape Verde?
Hakika ni ndoto ya kila mchezaji kucheza katika timu ya taifa. Na makocha wote wa timu ya taifa wanalijua hili. Hivyo, wanapaswa kuwa na moyo wa ukarimu ili kuwapa wachezaji motisha ya kujituma katika vilabu vyao.
Lakini inanishangaza kuona mchezaji mwenye kipaji kama Ibrahim Ajib, aliyeifungia Yanga magoli muhimu na kutoa assists za kutosha, na akaaminiwa na timu yake kuwa nahodha hata katika umri mdogo, bado haitwi timu ya taifa! Inashangaza pia kuwa Mohammed Hussein, almaarufu Zimbwe Jr., aliyewahi kuwa mchezaji bora wa ligi miaka miwili iliyopita, na anang’ara na timu ya Simba katika kombe la Klabu Bingwa Afrika, na juzi tu alifunga goli na kusaidia kuipeleka Simba robo fainali, lakini hagusi benchi la timu ya taifa!
Wachezaji kama hawa unawajengea mtazamo gani juu ya timu ya taifa? Au kuna mengine ambayo sisi mashabiki hatuyajui? Yepi?
Nimalize kwa kusema kuwa, Tanzania tuna imani na wachezaji wetu na wametuonesha mara kadhaa kuwa wanaweza. Hivyo basi, TFF na Kocha Amunike, tunataka mtuhakikishie kuwa tunaenda kushindana AFCON na si kushiriki tu.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Taifa Stars.