Hotuba ya Rais na Hatma
ya Udhibiti wa Fedha za Serikali

Chambi Chachage

Kwa nini Rais aliagiza Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) kuhusu akaunti ya Escrow ya Tegeta
isambazwe kwa umma? Hili ni swali lililozua utata hasa ukizingatia hilo halijawahi kufanyika kabla. Jibu limepatikana katika Hotuba yake ya jana kwa Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam.

Ni dhahiri kuwa Rais aliamua kuwa
atatumia Hotuba hiyo kutafanya uchambuzi wake (mwenyewe) kuhusu taarifa hiyo ya
CAG. Kwa kuwa yeye ni kiongozi wa Serikali basi ni rahisi kuhitimisha kuwa huo
hasa ndio uchambuzi wa Serikali. Swali ni: Je, una tofauti gani na uchambuzi wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambao kimsingi ndiyo
ulitumika kuja na maazimio nane ya Bunge kuhusu akaunti hiyo?

Wachambuzi, wakiwamo wabunge waliobobea
katika kuifuatilia Escrow, wameshaanza kuchambua tofauti hizo. Mmojawapo ni
David Kafulila ambaye ameainisha
masuala saba
ambayo yanasigana. Sehemu ya kwanza ya suala la nne inasema
hivi: “Hoja
kwamba kutaifisha mitambo ya IPTL kutakimbiza wawekezaji ina mapungufu kwa sababu
kwa mujibu wa ripoti ya CAG, PAP alifanya utapeli wa kughushi katika umiliki wa
IPTL hivyo sio mwekezaji mwadilifu hivyo kutaifisha haiwezi kutisha wawekezaji.”

Mwenyekiti wa PAC anaonekana kuendelea
kutekeleza ushauri aliopewa kuhusu “Unyenyekevu
(kuwa na kiasi )”
kwa kuandika maneno yafuatayo katika ukurasa wake wa mitandao
ya jamii: “Nimemsikiliza Mhe Rais. Ninachoweza kusema ni kwamba maazimio yale
hayakuwa ya Zitto Kabwe, PAC, CAG au PCCB. Yalikuwa ni maamuzi ya Bunge zima.
Bunge la vyama vyote kikiwamo chama cha Rais Kikwete yaani CCM. Sisi kama Bunge
tulitoa maazimio yale kwa maridhiano, uzalendo na bila kutaka kumuonea mtu
yeyote. Suala hili sasa naliacha kwa wananchi. Bunge limefanya kazi yake na
Serikali ambayo ndiyo tulikuwa tunasubiri maamuzi yake imeamua hivyo. Wananchi
wataamua wenyewe.”

Lakini siku moja kabla Mwenyekiti huyo
alisema maneno hayo mazito kwenye Mtandao
wa Wazi wa Wanazuoni
: “Wanazuoni  CAG
kasema bila kuzungusha kuwa PAP kagushi nyaraka, kakwepa kodi, hana umiliki
halali wa IPTL. Kitu ambacho CAG hakusema ni hatua gani zichukuliwe na hiyo sio
kazi yake. Hiyo ni kazi ya PAC. Someni hadidu [za] rejea zote muone ni kwa nini
CAG hakujibu hadidu [za] rejea 2 za mwisho. Hizo ndizo PAC ilijibu. Na hiyo ndio
kazi ya PAC miaka yote.”

Hadidu hizo zinasomeka hivi kwenye
ukurasa wa 50 wa Taarifa ya CAG:  “xii.
Kutoa mapendekezo ya njia sahihi za kisheria zinazoweza kutumika kwa ajili ya
kulinda serikali isipate hasara zaidi katika utekelezaji wa mkataba wa
uzalishaji umeme kati ya TANESCO na IPTL chini ya wamiliki wapya wa IPTL yaani
PAP,  xiii. Kutoa mapendekezo juu ya
hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya wahusika kulingana na matokeo ya
ukaguzi maalum. (Rejea Kielelezo 1).”

Mwenyekiti wa PAC pia aliurejea hivi kwa msisitizo zaidi mgawanyo huo wa majukumu kwenye mjadala huo wa Wanazuoni mtandaoni: “Taarifa ya CAG iligawiwa kwa wabunge siku moja kabla. Taarifa ya PAC iliweka taarifa hiyo kama kiambatisho namba 1 na iligawiwa. Bunge halijadili taarifa ya CAG bali taarifa ya PAC. Huu ndio utaratibu miaka yote. Mwaka 2012 mawaziri 8 waliondolewa kwa taarifa ya PAC na POAC iliyotokana na taarifa ya CAG. Hakuna aliyesema taarifa ya CAG ibandikwe kwenye magazeti.”

Swali zito la kujiuliza ni: Kama hii
ndiyo kazi ya PAC miaka yote, kwa nini mwaka huu (itakikane) ifanywe tofauti? Nini
hatma ya udhibiti na uhakiki wa fedha za umma/serikali baada ya ‘tofauti’ hiyo?
Kwa nini kuna tafsiri tofauti kuhusu Taarifa hiyo ya CAG?

Uzito wa swali hilo na maswali hayo
ya nyongeza unaonekana zaidi pale tunaposoma maneno haya aliyoyaandika
Mwenyekiti wa PAC kwenye ukurasa wake wa mtandaoni siku tatu baada ya agizo la Rais kuhusu usambazaji wa taarifa ya
CAG: “Sasa kuna juhudi kubwa za kutetea waliotajwa na Taarifa ya Kamati ya PAC.
Magazeti, haswa ya Serikali yamekuwa yakiandika habari zenye mwelekeo wa
kutetea. Ikulu imeagiza Taarifa ya CAG ichapwe kwenye magazeti, jambo ambalo
halijapata kutokea huko nyuma kwani sio mara ya kwanza PAC kutumia Taarifa ya
CAG kuwajibishana. Makala zinaandikwa kumshawishi Rais asitekeleze maamuzi ya
Bunge. Nasaha za ‘know where to stop’ na ‘kuwa mnyenyekevu’ zinanivuta na kunishawishi
kutosema lolote. Hekima inataka kumwachia Mkuu wa Nchi kuamua kwa namna
itakavyompendeza. Tumwache aamue. Unyenyekevu unataka hivyo. Wenye ushawishi
tofauti walikuwa na nafasi Bungeni. Walishindwa ndani ya Baraza la Taifa. Unyenyekevu
ni kwa walioshindwa pia.”

Kwenye majibu yake ya juzi (na ya awali) dhidi ya Mwanazuoni mmoja anayedai kwa hamasa na kusisitiza kwa vielelezo mbalimbali kuwa PAC imepotosha/imedanganya (wa)Bunge na (wana)Nchi kuhusu masuala kadhaa na muhimu yaliyomo katika Taarifa ya CAG, kuna sehemu Mwenyekiti wa PAC alienda mbele zaidi na kusema hivi kuhusu migongano na vipaumbele vya kitafsiri: “Wanazuoni – sarakasi za CAG na taarifa ya Tegeta Escrow ipo siku umma utajua yote…. Tumeambiwa Rais anaongea kesho. Tusubiri atasema na kuamua nini. Kutokana na atakavyosema, sisi kama PAC nasi tutasema yetu ambayo hayakuwa kwenye taarifa au yamo hayajaeleweka au kuwekewa maanani.”

Mkanganyiko wa tasfiri/matumizi ya
Taarifa ya CAG katika sakata la Escrow unatokana kwa kiasi kikubwa na jinsi
uchunguzi huo ulivyoagizwa na zaidi ya chombo kimoja, kila kimoja kikiwa na
mahitaji yake. Katika kipengele cha 1.1 cha “Utangulizi” wa Taarifa hiyo kinatuelezea
“Chimbuko la Ukaguzi” ambapo tunaona kuwa: “Ukaguzi huu umetokana na barua…ya
tarehe 10 Juni 2014 kutoka kwa Mh. Waziri Mkuu. Kabla ya barua hii, ukaguzi huu
ulikwishaombwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kupitia barua…ya
tarehe 12 Machi 2014 na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia barua … ya tarehe 20 Machi 2014. Barua ya Mh. Waziri Mkuu imefanya
rejea katika maombi yaliyotangulia kutoka kwa Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi iliwasiliana na Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na Katibu wa Bunge kupitia barua…ya tarehe 17
Aprili, 2014 ili kukubaliana juu ya hadidu za rejea zitakazoongoza ukaguzi huu.
Hadidu za rejea husika ziliridhiwa na taasisi hizo mbili kupitia barua…ya
tarehe 5 Mei 2014 kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na barua
…ya tarehe 03/05/2014 kutoka kwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.”

Kwa maana nyingine, Bunge liliagiza
na Serikali nayo iliagiza uchunguzi huo maalum. Bunge lilipoipata Taarifa utaratibu
tuliojulishwa hapo juu na Mwenyekiti wa PAC kuwa ni wa “miaka yote” ukaanza
kama tulivyoushuhudia kwenye mjadala mkali wa tarehe 28 na 29 Novemba 2014
Bungeni. Serikali ilipoipata Taarifa ya awali, kama tulivyojulishwa katika Hotuba ya Rais, kabla ya safari yake ya matibabu Marekani aliikabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB)
ianze kuifanyia kazi. Lakini pia tumeona Raisi akiitumia kutoa hotuba na
maamuzi ya Serikali.

Hali hii inaashiria nini hasa
ukizingatia kwa kiasi kikubwa tafsiri ya Serikali iliyopelekea kuamua
ilichoamua kupitia Hotuba ya Rais inaonekana ni tofauti na tafsiri ya Bunge
iliyopelekea kupendekeza ilichopendekeza? Na hii ni Serikali hiyo hiyo ambayo
Waziri wake, Stephen Wassira, alisema (kana kwamba anawatahadharisha wanachama
wenzake watakaotaka kupinga) yale maazimio nane ndiyo msimamo wa chama tawala –
yaani chenye Serikali – wakati anachangia hitimisho la mjadala wa Escrow
Bungeni usiku ule. Je, Rais na Serikali yake imepata
kikohozi na kuwa kigeugeu? Au Rais ameona sasa Taarifa ya CAG inatumiwa vibaya
na hivyo kuamua kuweka tafsiri/rekodi sawa kwa wananchi/umma?

Huyu ni Rais aliyesifiwa hivi katika ukurasa
wa mtandaoni wa Mwenyekiti wa PAC
: “Ni Kiongozi pekee wa Tanzania
aliyeruhusu taasisi za Uwajibikaji kufanya kazi zake na hata yeye kujikuta
akichukua hatua kulingana na maamuzi ya taasisi hizo. Kabla yake, hakuna Rais
wa Tanzania aliyetoa nafasi kwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kufanya kazi zake kwa uwazi na umahiri. Hatua yake ya kujadili kwa
uwazi taarifa ya CAG ya mwaka unaoishia Juni 30, 2006 kwa kuwaita Mawaziri,
Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, [kisha] Makatibu Wakuu, Ma RAS na Ma DED
ilijenga msingi mkubwa wa taarifa zinazofuata za CAG. Mwaka 2012 alifukuza kazi
mawaziri 6 na manaibu mawaziri 2 kufuatia Taarifa za Kamati za Bunge za
Mahesabu zilizotokana na Taarifa ya CAG. Haikupata kutokea katika historia ya
nchi yetu Rais kufanya hivyo.”

Baada ya kuisoma kwa kina ripoti ya
CAG, kuwasikiliza ‘mwanzo mwisho’ Rais katika hotuba yake na Mwenyekiti wa PAC
katika mawasilisho yake Bungeni pamoja na mjadala wote ule, ninachokiona ni
‘mbaraka katikati ya laana.’ Mkanganyiko huu wa tafsiri na matumizi ya ripoti
ya CAG japo ni laana pale unapochelewesha uchukuliwaji wa hatua kwa wale
walioshiriki katika ufisadi, ni mbaraka pale unapotusaidia kuweka sawa mipaka
na madaraka ya kutumia Taarifa ya CAG. Inapaswa kutumiwa kutenda haki na
kutetea ukweli, hivyo, haipaswi kabisa watu wachache au mtu mmoja – Serikalini au
Bungeni – awe na nguvu na madaraka makubwa (kupita kiasi) ya kitafsiri na
kimaamuzi.

Wakati tunachambua Tuwaonao
katika Ripoti ya CAG kuhusu ESCROW
wadadisi tulisema hivi: “Ndio maana
kwenye sayansi ya siasa ni vigumu kujibu swali la ‘Serikali ni Nani’?” Ugumu wa
swali hilo usituzuie kujibu ni nani na nani katika Serikali ana jukumu lipi na
lipi katika mchakato wa ukaguzi na udhibiti wa fedha za Serikali. Na jibu hilo linapaswa kuzingatia uhuru wa
mihimili ya Serikali na Bunge kuzuia miingiliano.

Ukurasa wa 5 wa Taarifa ya CAG kwenye
Kipengele 1.7 chenye kichwa cha habari “Matumizi ya Taarifa Hii” unatujulisha
hivi kuhusu wajibu:Taarifa hii ni kwa ajili ya matumizi
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ambao ndiyo waliomba kufanyika kwa ukaguzi huu maalum. Taarifa hii
yaweza kutumika kama ushahidi katika mashauri ya madai au jinai. Pia taarifa hii
yaweza kutumiwa na Mamlaka, taasisi za Serikali au vyombo vya kusimamia
utekelezaji wa sheria kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki pale itakapotakiwa
kufanya hivyo. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi haitahusika na matumizi ya taarifa hii
na chombo, taasisi au mtu mwingine zaidi ya vyombo au taasisi zilizotajwa hapo
juu.”

Hatma ya ukaguzi na udhibiti wa fedha
za umma itakuwa mashakani kama uhalali wake na wa mchakato wa utekelezaji wake
utatiliwa mashaka. Hata ukaguzi ukifanywa kwa dharura, haraka hiyo isiwe sababu
ya kufanya tuhoji nani atamkagua mkaguzi kama tunavyohoji nani atamhariri
mhariri. Uhakiki ni kupata uhakika. Ni kupata majibu siyo kuongeza maswali.
Kukiwa na majibu ya hakika hata uwajibikaji utakuwa wa hakika.

Wawajibikaji wawajibike.
Wasiowajibika wawajibishwe. Wawajibishaji wawajibishe.