Na Diana Kamara

 

Tunapokuwa shule hatufunzwi kuhusu ndoa na hasa wasichana kuhusu umuhimu na/au ulazima wa kuolewa. Lakini bado jamii hiyo hiyo inatarajia sio tu tuolewe, bali tuwe wake wema tunapoolewa. Kama kuolewa ni jambo la muhimu kiasi hiki, mbona hawakuliweka kwenye mitaala? 

 

Mnasubiri tuwe na hao waume zetu ndio mtuambie kama tu wake wema ama la? Walau elimu ya mkoloni ilikuwa wazi wazi, masomo ya wanawake kwa ngazi za chini yalihusisha, ukiacha kusoma na kuandika: ushonaji, upishi na kutunza nyumba. Kwa waliobahatika kwenda ngazi za juu nao kazi zao zilikuwa bayana: uuguzi, ukatibu muhtasi ama ualimu.

 

Wengine tulitengwa na familia tukae shule za bweni. Mjomba alisema ni bora nikae bweni kwani nitapata muda zaidi wa kusoma kuliko kusoma shule ya kutwa na kuhangaika na usafiri. Kwa nini hakuniambia hata nikimaliza shahada zote niwezazo, bado jamii inanitarajia niolewe na kufanya kazi za nyumbani, si kama mjakazi, bali kwa moyo mkunjufu. Alijua nikimaliza shule za bweni na masomo ya juu nitarudi kwenye jamii, kwa nini hakulitilia mkazo jambo la ndoa kwa mwanamke? 

Kila leo naona kampeni za mtoto wa kike: kuzuia mimba za utotoni, kuwasaidia katika hedhi, kuwaweka kwenye programu za kujenga kujiamini na mikakati ya kuongeza ufaulu kwa watoto wa kike. Lakini wadogo zangu hawa wakiniangalia na kugundua sijaolewa, wanasikitika sana kana kwamba kuolewa ni kilele cha mafanikio. Na hata nikitaka kuzungumza nao kuhusu ndoa, naanzia wapi? Nitajenga mtandao na nani maana asasi zinazolikaribia suala la ndoa ni zile zinazowaelimisha kuhusu afya ya uzazi. Natamani ningeweza kuongea nao kuhusu siri za unyago, mabwana, vidumu na waume za watu.

 

Nini maana ya jamii kuweka nguvu kwenye kutusomesha halafu kutuzodoa kwa kutoolewa, kuachana ama kuendelea kuwa na waume na wachumba (sugu) za watu? Inakuwaje jamii inakosa mfumo wa kuhakikisha tuliosoma elimu za juu na kupata kazi kubwa kubwa tunaolewa? Au kuhakikisha kuwa kutoolewa siyo mwisho wa maisha?

Halafu wanaume nao wanatuchanganya. Kwanza wengi wao wakisikia umesoma cha kwanza ni kukuambia hutaolewa. Kweli sitaolewa kwa sababu wewe tunayekaribiana hadhi kijamii, kama alivyowahi kusema shosti angu mmoja, unaenda unaoa mwanamke ambaye hata hutaki kuonekana naye kwa watu kwa sababu we mwenyewe unamuona mshamba mshamba. 

 

Na mwanaume huyo huyo anapenda sana muongelee mambo ya siasa na historia, mkale makange na ukimruhusu na wewe uliwe. Kisha hapo hapo, jumatatu aende kazini akazisake ili amlipie ada ya chekechea milioni mbili mwanae, tena ana miaka mitatu tu. Kwa nini asimnunulie midoli, vikopo vya kupikia na kumfundisha adabu za ‘mwanamke anayeoka’ mapema?  

Mama zetu nawaelewa, nao ni msukumo wa makundi. Wakiona watoto wa wenzao wanaolewa na wao wanatamani harusi. Ila wapo wanaonifurahisha kwa kuwa wakweli, “nimechanga sana jamani olewa na mi nichangiwe.” Wengine wanalia na Muumba, kama amewavusha na kuwafanikisha watoto wao kote huko na hili atawavusha. Cha ajabu, wazazi wetu hawawasongi watoto wa kiume kuoa kama sisi wa kike, kwa nini? 

 

Wanaokuonea huruma kwa kutokuolewa wanazidi kukusaidia kuchimba shimo kubwa la ombwe kwenye akili na moyo wako ambalo utahisi ni mume ndio atalifukia. Wengine watakuzodoa kwa kudhani elimu yako ndio inakupa kiburi. Hivi wasioolewa wote wana shahada ya kwanza na wanafanya kazi kwenye taasisi kubwa kitaifa na kimataifa? 

 

Jamii inatukanganya, tuache kusoma shule na kupata kazi ili tuolewe? Na tukiolewa kuna uhakika gani jamii itatuona wake wema, maana makosa, matatizo ama hata hitilafu ndogo tu za mume au watoto lawama hubebeshwa mke-mtu. Sasa kwa niaba ya manungayembe wenzangu, mtushauri tufanye nini kuhusu suala la ndoa. Tunakaribisha ushauri, maoni na masuluhisho.