Ninaweza nisiwe mwerevu sana katika kufasili neno “utamaduni.” Lakini, sote tunaweza kukubaliana kuwa jamii fulani inaweza kutofautishwa na jamii nyingine kupitia lugha, desturi, imani, kazi za sanaa, maarifa, na utambulisho wa pamoja vikiambatana na historia. Ndiyo maana mara nyingi tumekuwa tukinyoosheana kidole kwa “uzuri” ama “ubaya” kati ya jamii moja na nyingine, ukoo mmoja na mwingine, kabila moja na lingine, nchi moja na nyingine, bara moja na lingine au rangi moja na nyingine.
Moja ya mambo yanayotutofautisha ni utamaduni ambao hudhihirika kupitia vigezo vilivyotajwa hapo juu. Yaani ili kubaini tamaduni fulani, tunatazama desturi zao, imani zao, kazi zao za sanaa, lugha zao, maarifa yao n.k. Ni wazi kuwa utamaduni huathiri fikra na hata namna jamii inavyowasiliana na kujitawala.
Katika maisha ya sasa yanayotawaliwa na uchumi wa maarifa na utandawazi, ni vema watu wakafahamu tamaduni zao na zile za wenzao ili kujiongezea uwezo katika tafakuri tunduizi, yaani uwezo wa kutafakari kwa kina na udadisi. Kama ilivyoelezwa katika aya ya pili, utamaduni huathiri fikra zetu kwani tangu utotoni tumekuwa tukifunzwa mambo mbalimbali na kuaminishwa kuwa huo ndiyo ulimwengu. Tazama vile tunatofautiana katika ulaji wa vyakula mbalimbali. Mathalani, wakati jamii za Kiislamu zinaona nyama ya nguruwe si halali kuliwa, hali ni tofauti kwa baadhi ya madhehebu ya Kikristo ambako nyama hii ni kitoweo maarufu.
Kama haitoshi, wakati baadhi ya Wakristo na Waislamu wakishabikia nyama ya ng’ombe kama kitoweo, katika baadhi ya jamii za Kihindi – hasa ya Wahindu – ng’ombe anapewa hadhi ya uungu. Kwa wale tunaokula nyama ya ng’ombe, utajisikiaje ukiambiwa unamla Muumba? Je, tunatazamwa vipi na wale wenye kumpa ng’ombe hadhi ya uungu?
Tusipokuwa makini tunaweza kudhani kile tunachokijua ama tulichoaminishwa tangu utotoni ndiyo ulimwengu wakati si kweli. Katika mihadhara au mijadala yangu ya aina hii, hupenda sana kumnukuu aliyewahi kuwa rais wa Marekani, Bw. Abraham Lincoln. Yeye alisema:
Mchungaji alimfurusha mbwamwitu kutoka kwenye koromeo la kondoo, ambapo kondoo alimshukuru mchungaji kama mkombozi, wakati mbwamwitu alimshutumu mchungaji kama mwenye kuunajisi uhuru. Ni dhahiri, kondoo na mbwamwitu hawana fasili ya pamoja kuhusu uhuru.
Ni vema kufahamu tofauti zetu ili tujirekebishe kulingana na mazingira tutakayokuwepo kwani si mara zote tunawaza sawa. Jambo ama dhana ileile inaweza kutafsiriwa kwa namna tofauti na watu tofauti kama alivyosema Bw. Lincoln. Mjadala kuhusu ni nani mwenye haki kati ya kondoo na mbwamwitu hapo juu hauna mwisho.
Mzungumzaji bora, mtawala bora, mwandishi bora na mwanajamii bora kwa ujumla ni yule anayefahamu utamaduni wa hadhira anayowasiliana nayo. Vilevile utamaduni si suala la asili kama kuchomoza na kuzama kwa jua. Ni suala la kibinadamu. Linatokana na mafunzo na uzoefu tunaoupata katika mazingira tunayoishi.
Kwa hiyo, inawezekana watu kubadili tamaduni zao kupitia njia mbalimbali. Katika makala haya, tutatazama kwa undani namna jamii zinatofautiana kiutamaduni. Tutatumia vigezo vya mamlaka na muktadha kama vilivyoelezwa na wanazuoni Geert Hofstede na Edward T. Hall, mtawalia.
Kigezo cha Mamlaka
Kuhusu mamlaka, Hofstede anabainisha kuwa tamaduni zinaweza kugawanywa katika makundi makuu mawili: Zile zinazoathiriwa kwa kiasi kikubwa na mamlaka katika mahusiano na mawasiliano yao ya kila siku na zile zisizoathiriwa kwa kiasi kikubwa. Mamlaka katika muktadha huu ni ile hadhi ama uwezo alionao mtu katika jamii au muktadha husika.
Hivyo basi, dhana ya mamlaka inaweza kutazamwa kwa vigezo mbalimbali kuanzia maumbile, uongozi, utajiri, hadhi ya mtu katika jamii n.k. Izingatiwe kuwa tofauti hizi za kimamlaka zipo kwa kila jamii. Kwa hiyo, tofauti ya makundi haya si tofauti ya nyeusi na nyeupe, kwamba kama si X basi ni Y, la hasha.
Tofauti hizi hupimwa kwa kuzidiana, yaani nani au nini zaidi. Aidha, jamii inatazamwa kadri inavyoipokea hali husika na kuitazama; je, ni jambo linalokubalika ama halikubaliki? Jedwali lifuatalo linaonesha jinsi jamii hizi mbili, kwa mujibu wa Hofstede, zinavyotofautiana.
Kwa kutumia vigezo hivi, Hofstede anaona kuwa jamii za Ulaya Magharibi, kwa kiasi kikubwa, zinaangukia katika jamii zisizoathiriwa na mamlaka wakati nchi nyingi za mashariki zinaangukia katika jamii zinazoathiriwa na mamlaka kwa kiasi kikubwa. Kwa vigezo hivyo hivyo, Afrika pia inaangukia kwenye jamii zinazoathiriwa na mamlaka kwa kiasi kikubwa. Hivyo basi, kiujumla, Watanzania tunaangukia kundi hili la pili.
Tazama namna tunalea watoto wetu majumbani. Ni mara chache mtoto hupewa nafasi ya kuhoji. Ni mara chache mtoto hupewa nafasi ya kujieleza. Nafasi na wajibu zimebainishwa. Hata kwenye ulaji, sehemu za mnyama zinajulikana, nani hula nini. Hakuna majadiliano.
Hali ni hiyo hiyo shuleni. Walimu wanavaa nafasi ile ya walezi/wazazi majumbani. Wakati mwingi wanafunzi wamekuwa ni wenye kutekeleza amri tu. Fursa ya kuanzisha jambo ama mjadala ni ndogo sana.
Kwenye uongozi wa nchi na taasisi, hali kadhalika, kiongozi hahojiwi—amri yake haitiliwi shaka.
Kuthibitisha namna mamlaka inaathiri maisha yetu, hebu turejee tukio mojawapo. Akikosoa ushirikiano mbovu wa maofisa wa mkoa kwa hayati Anna Mghwira akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro akitokea chama cha upinzani, Rais Samia Suluhu Hassan alitamka kwamba: “Rais huwa hakosei.” Kauli hii inaakisi tamaduni zetu kama ilivyoainishwa kwenye jedwali hapo juu.
Hata hivi karibuni, akitetea maamuzi ya Bunge kupitisha sheria ya tozo ya miamala ya simu, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alidai yeye ana Shahada ya Uzamivu (PhD) ya uchumi, asitiliwe shaka kwa kile anachokisema. Hapa alitumia mamlaka ya kisomi/kiuwanazuoni kuzima hoja kinzani. Lakini pia alitumia mamlaka ya kitawala kuwazima wasomi/wanazuoni wanaohoji.
Kipindi cha hayati Rais John Magufuli kimejaa mifano lukuki. Tazama matendo na kauli za maofisa waandamizi kabla na baada ya kufariki dunia kwake. Wengi hawakuweza kuhoji kauli za Rais huyo mpaka alipofariki dunia ndipo wanatoa ama kutenda yale waliyopaswa kufanya kipindi cha uhai wake.
Mojawapo ya mifano mizuri ni kauli ya Mh. Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu ujenzi wa bandari ya Bagamoyo. Unaweza kushangaa, kipindi Magufuli akiwa hai, Mh. Ndugai aliwahi kuwa mmoja wa maofisa waandamizi waliopigia upatu/chapuo mradi huo. Lakini, kwa kuwa Rais huyo alionesha kutoridhishwa na mradi huo, Mh. Ndugai hakuendelea na hilo. Baada ya kufariki kwa Magufuli, Mh. Ndugai aliibuka na kusema Rais alishauriwa vibaya kuhusu mradi husika na hivyo mradi uendelee.
Ukitazama tabia hizi ni chache kwa baadhi ya nchi za magharibi kama Marekani. Na pindi zinapojitokeza, kwa kiasi kikubwa wanajamii hawapo tayari kuvumilia. Tuliona namna Rais wa zamani wa nchi hiyo, Bw. Donald Trump, alivyopata shida kwenye maamuzi yale ambayo baadhi hawakukubaliana nayo. Kiujumla, kwenye nchi za magharibi hata mtoto anaweza kumkosoa mzazi ama mlezi wake wakati huku kwetu kitendo hiki huchukuliwa kama ukosefu wa nidhamu ama ‘laana’.
Kigezo cha Muktadha
Ni matumaini yangu sasa tupo pamoja kuhusu namna mamlaka inavyoathiri mawasiliano na mahusiano yetu ya kila siku. Ili kusherehesha dhana hii, ni vema pia tukatazama kigezo cha muktadha kama kilivyoelezwa na Hall. Kwa tafsiri au fasili nyepesi, muktadha ni hali ya jumla.
Kuhusu muktadha, Hall anawagawa walimwengu katika makundi mawili: Wale ambao mawasiliano na mahusiano yao huathiriwa na muktadha zaidi kuliko kilichosemwa (lugha) na wale wasioathiriwa kwa kiasi kikubwa. Labda tuidadavue zaidi dhana ya muktadha. Hapa tunamaanisha hali au mazingira yanayowazunguka wazungumzaji kwa ujumla. Yaweza kuwa ya kufikirika (dhahania) ama ya kimaumbile (yanayoweza kuonekana ama kuguswa).
Ni kawaida lugha kuambatana na mazingira inamozungumzwa. Ndiyo maana si mara zote kuelewa kilichosemwa bila ya kufahamu hali au mazingira aliyozungumza mzungumzaji. Kwa maneno mengine, hata kama umesikia sentensi nzima, kuna wakati huwezi kuelewa bila ya kuufahamu muktadha husika. Muktadha huenda pamoja na utamaduni wa wazungumzaji.
Kwa mfano, kwa watu wenye utamaduni wa gari na viatu aina ya buti, mkitoka sokoni, mkasahau nyanya kwenye gari, ukimwambia mwenzako kachukue nyanya kwenye buti, msikilizaji huyu hawezi kwenda kutafuta nyanya kwenye buti kwa maana ya kiatu kwani muktadha hauruhusu kufanya hivyo. Kwa kuwa wote mna uelewa wa pamoja kuhusu buti ya gari na kiatu, mnafahamu jinsi mlivyofanya manunuzi na kuhifadhi bidhaa zenu, hamuhitaji ufafanuzi kuhusu buti lipi katika muktadha huo.
Hivyo, kuna jamii kwa kiasi kikubwa hutumia muktadha zaidi kuliko kilichosemwa. Pia kuna jamii nyingine ambazo hutumia muktadha pale inapobidi tu. Jedwali lifuatalo linapambanua sifa za tamaduni hizi mbili kwa mujibu wa Hall.
Kama ilivyo katika kigezo cha mamlaka, kwa kiasi kikubwa au kiujumla, nchi za Kiafrika zinatumia zaidi muktadha katika mawasiliano yao ilhali zile za magharibi huathiriwa kwa kiwango cha chini. Kwa mfano, umewahi kuona Mtanzania akikuomba kitu? Mara nyingi atakwambia, “ninaomba chungwa moja.” Ukimpa chungwa moja atalalama, “yaani umenipa chungwa moja kweli, dah!”
Kwa baadhi ya Wazungu, hasa wa magharibi, kiujumla hali ni tofauti kidogo na yetu Waafrika—wao kwa kiasi kikubwa humaanisha kilichosemwa. Nimekuwa nikifuatilia sana tabia za Watanzania katika hili. Hata bei za bidhaa, baadhi hawaweki wazi mpaka mteja achague bidhaa husika. Siku hizi, kule mtandaoni utaona, “bei njoo inbox.” Mambo haya hayajaibuka tu bali ni utamaduni.
Hitimisho
Kwa kuhitimisha, ninafahamu kuna mapungufu mengi katika vigezo au mikabala hii miwili inayobainisha tamaduni za watu duniani. Kuondoa utata, kama nilivyotahadharisha mapema, ni vema vigezo/mikabala hii ikapimwa kwa kiasi, wapi kumezidi kwani mamlaka na muktadha hupatikana kwenye jamii zote. Unaweza kuona hali ileile ikitokea katika jamii mbili tofauti, lakini mtazamo wa wanajamii hutofautiana pakubwa katika kuliendea suala husika. Hapa kwetu, wewe unaetoa wazo jema unaweza kuwa adui miongoni mwa wanajamii ikiwa tu unakwenda tofauti na wanajamii wenzako na huna mamlaka ya kuwabadili au uwezo wa kubadili muktadha wa jamii.
Lakini, nina hakika pia hatuwezi kuvibeza vigezo hivi. Kwa kiasi kikubwa vinaweza kutusaidia hapa tulipo na tuendako. Vinaweza kutusaidia kujitambua na hivyo kufanya maamuzi sahihi hasa kiutawala na kimawasiliano.
Aidha, ukichunguza kwa makini, kila upande una mazuri na mapungufu yake. Ni juu yetu kuchuja mazuri ya kila pande na kuyatumia katika mawasiliano na mahusiano yetu. Kilicho muhimu ni kuwa na uwiano wenye mizania.
Kwa mfano, turejee kigezo cha mshikamano kijamii. Kiujumla, Waafrika tupo vema katika hili, lakini katika zama hizi za ugonjwa wa UVIKO-19 inabidi kulitazama upya hasa muktadha wake. Je, vipi kuhusu kuwaona na kuwauguza wagonjwa wetu majumbani na mahospitalini? Vipi mijumuiko kama ile ya mazishini/mazikoni? Usiposhiriki unaonekana mvunja kanuni, ukishiriki unajiweka kwenye hatari ya maambukizi ya korona.
Je, vipi kuhusu athari za mamlaka? Ni kweli baba, mama, na Rais hawakosei? Je, ni kweli wakati wote jamii ipo sahihi? Ni lini mawazo ya mtu mmoja yataheshimiwa? Je, ni sahihi kwenda na mawazo ya wengi hata kama wanakosea?
Mambo mengi ya kiimla hudumaza uwezo wa watu kufikiri na hivyo kukosa ubunifu na ugunduzi—kifo cha tafakuri tunduizi. Inakatisha tamaa kuona watafiti na PhD zao, wafanyakazi werevu, na wanafunzi hodari wanafanya mambo yasiyoswihi, yaani yasiyo sahihi, ili kuendana tu na matakwa ya mwenye mamlaka. Aidha, ni mambo kama haya yamekuwa yakichangia uonevu wa makundi mbalimbali kwa kuzingatia vigezo kama uchumi (matabaka: asiyekuwa nacho dhidi ya mwenye nacho), jinsia (mfumo dume: wanaume dhidi ya wanawake, vijana dhidi ya wazee, wenye ulemavu dhidi ya wasio na ulemavu n.k.), na uongozi (utawala: mkuu X dhidi ya raia Y ama wafanyakazi Z).
Je, tutafika kweli bila kuubadilisha utamaduni huu tenge wa mamlaka na muktadha?
Makala nzuri sana. Ni ngumu kwa tamaduni kubadilika moja kwa moja. Mabadiliko hutokea kidogo kidogo. Tamaduni zetu ni nafasi ya kusonga mbele na kufika pale tunapopataka kwa ujumla wetu. Kwa kubadili kwa kiasi kidogo, haswa kwenye uwajibikaji wa mamlaka, tutafika
Hakika
Ndugu umenena vema kwenye andiko lako na umeacha maswali nyeti yanayohitaji majibu. Kudos Bro!
Shukrani
Nimeisoma makala kuanzia mwanzo mpaka wisho bila kuacha mstari. Inavutia kama vile naangalia movie ya “Action and Thriller “.
Kudos Kama Mhandeni
Asante mkuu
Inafikirisha. Swali nililojiuliza, Je, tamaduni hizi zaweza kubadilika? Mimi nadhani elimu na malezi yanayolenga kumjengea mtoto uwezo na kujiamini, vinaweza kututoa hapa na kutusogeza mbele. Elimu inayolenga kwenye ufaulu inaweza isibadili sana mambo ya “mamlaka” na “muktadha”.
Inawezekana. Japo si mara moja
Desturi ya kulinganisha tamaduni imepitwa na wakati! Uhalisia wa leo ni kwamba utamaduni ni mambo yote yale katika jamii husika unayopaswa kuyajua na kuyatekeleza ili uweze kukabiliana na changamoto za maisha na hivyo kufanikiwa! Nje ya hapo hakuna utamaduni!
Kiukweli jamii zetu na familia zetu zina dhima kubwa. Tumekuwa watumwa mila na tamaduni ambazo hazina tija na kandamizi kwa makundi ya watu. Ipo haja ya kubadili muelekeo