IFUATAYO NI TAFSIRI YA KISWAHILI KWA NJIA YA MUHTASARI YA MAKALA YA NEEMA M. KOMBA, DEAN A. SHEPHERD NA JOAKIM WINCENT

Rushwa imeendelea kuwa tatizo sugu linalokwamisha ujasiriamali na kudhoofisha ubunifu duniani kote. Rushwa hugharimu uchumi wa dunia kwa matrilioni ya dola kila mwaka na kufanya kuwe na mazingira magumu ya biashara kwa wajasiriamali wenye rasilimali chache. Rushwa ni changamoto kubwa kwa biashara changa na ndogo, na kwa ujumla huacha jamii zikiwa katika hali mbaya zaidi.

Juhudi za kupambana na rushwa zinazotumiwa na nchi nyingi zimeshindwa kupunguza au kuiondoa kabisa katika biashara na maisha ya kila siku. Kwa kufuatisha nadharia iliyopo inayojikita hasa kwenye kuamini kuwa rushwa iliyokithiri haiepukiki, inatarajiwa kwamba wajasiriamali wanaofanya biashara kwenye mazingira ambayo rushwa imekithiri hawana budi kujihusisha nayo. Mantiki ya nadharia ya kutojiepusha na rushwa inadhani kwamba wajasiriamali wataendana na mahitaji ya kitaasisi na kanuni za kufanya biashara za muktadha wao. Hata hivyo, kuna haja kubwa ya uelewa mbadala wa mbinu za kukabiliana na rushwa wakati wajasiriamali wanafanya kazi katika muktadha wenye rushwa iliyokithiri bila kujihusisha nayo.

Watafiti, wataalamu, na watunga sera wamekuwa wakisisitiza utekelezaji wa mikakati ya kupambana na rushwa ndani ya mashirika, wakionyesha jukumu muhimu la sekta binafsi katika kupambana na rushwa na kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Tafiti za hivi karibuni juu ya kupinga rushwa ndani ya mashirika na makampuni zinakinzana na dhana ya kuwa wajasiriamali wa ndani hawana nguvu dhidi ya rushwa iliyokithiri, zikionyesha kwamba mashirika yanaweza kudhibiti rushwa ndani ya shughuli zao.

Licha ya shauku inayoendelea ya wasomi juu ya rushwa, juhudi za biashara ndogo ndogo na za kati (SMEs) kupambana na rushwa zimepuuzwa kwa kiasi kikubwa. Badala yake, tafiti zimejikita zaidi kwenye hatua za ndani za mashirika makubwa (ya ndani na ya kimataifa), bila kuzingatia vya kutosha utegemezi wao kwa mazingira na wadau wengine. Hali kadhalika, hatua za kupambana na rushwa zinazotumiwa na mashirika makubwa mara nyingi hazifai kwa biashara mpya na ndogo.

Tulikusanya na kuchambua taarifa zilizotokana na mahojiano na wajasiriamali wa Kitanzania, tukitafiti motisha na mikakati yao ya kupinga rushwa kwenye biashara zao. Utafiti wetu unachangia maarifa mapya ya kupingana na rushwa kwa kutoa maelezo ya jinsi ya kupambana na rushwa yanayojumuisha motisha binafsi wa wajasiriamali, na jinsi wanavyoweza kutumia rasilimali zao na njia mbadala za kufikia malengo yao bila kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa hasa dhidi ya wadau wanaotegemeana nao katika kufanikisha biashara zao.

Kwa kuzingatia mafanikio ya biashara hutegemea sana jinsi mjasiriamali atakavyoyaelewa na kuyamudu mazingira ya soko, andiko hili linachunguza jinsi gani wajasiriamali wadogo wanaofanya kazi katika mazingira ambayo rushwa imekithiri wanaweza kishindana nayo bila athari hasi kwa biashara hizo.

Kwa kutumia nadharia ya mabadilishano ya kijamii (social exhange theory) kuelewa rushwa, tunachunguza kwa undani namna wajasiriamali wapya na wadogo wanavyoweza kukwepa rushwa. Tunaamini kuwa rushwa hutokea kwenye mapatano baina ya wadau wawili wanaotegemeana, na hasa wenye nguvu tofauti za ushawishi (leverage) kwenye mapatano. Kwa mfano, ni rahisi kwa mjasiriamali mnyonge asiyeelewa sheria kushurutishwa kutoa pesa kupata huduma za bure kutoka kwenye mashirika ya umma, au mjasiriamali asiyekuwa na wateja kutoa rushwa kwa meneja manunuzi wa kampuni fulani ili aweze kuwa msambazaji wao. Wajasiriamali hukutana sana na rushwa wakitaka kurasimisha shughuli zao za biashara, pia kwenye kupata vielelezo au vyeti vya ubora kutoka kwa wadhibiti mbalimbali (regulators), katika kupata wateja hasa wa makampuni, na katika kupata mtaji, hasa mkopo au ufadhili kutoka kwenye mashirika yanayotoa huduma za kifedha.

Ingawa wajasiriamali wengi wana motisha wa kutaka kupingana na rushwa kutokana na sababu mbalimbali za kimaadili na kiuchumi, uwezo wao wa kufanikiwa kwenye kupingana na rushwa unategemea sana rasilimali wanazozihitaji, rasilimali walizonazo au njia mbadala za kufikia malengo yao zinazowapa nguvu ya ushawishi (leverage) kwenye mapatano Wajasiriamali wamenonesha ubunifu wa hali ya juu wa kupingana na rushwa, kwa kuwa na mikakati dhidi ya mashirika, pamoja na mikakati dhidi ya wafanyakazi wa hayo mashirika wanapatana nao kwenye shughuli za biashara.

Utafiti wetu unatoa mwanga juu ya uhusiano tata kati ya motisha na uwezo wa wajasiriamali kupingana na rushwa, na kuonyesha mikakati wanayotumia kupinga rushwa bila kuathiri mahitaji yao ya rasilimali.

Kulingana na nguvu ya ushawishi (leverage) [inayotokana na rasilimali walizonazo pamoja na njia mbadala za kupata rasilimali walizonazo], wajasiriamali wanapinga rushwa kwa namna zifuatazo.

Mikakati ya kupinga rushwa dhidi ya mashirika/kampuni

  1. Kwa kuepuka kujihusisha na wadau/mashirika yenye nguvu sana kushinda wao. Wajasiriamali wanatumia njia mbalimbali kuepuka kujihusisha na wadau au mashirika yenye nguvu kushinda wao. Namna moja ni kwenye usajili wa biashara. Wajasiriamali wengi huepuka kusajili kampuni, na kusajili jina la biashara la mmiliki pekee ili kuepuka urasimu na kuhusiana na serikali kwenye biashara. Hali kadhalika, wajasiriamali wengine huepuka kabisa kuwa wasambazaji wa bidhaa au huduma kwa taasisi kubwa au serikali kwani zinajulikana kwa kukithiri kwa rushwa ya asilimia kumi (10-percent).
  2. Kwa kubadilisha utegemezi wao wa rasilimali ili wasilazimike kutoa rushwa sababu hawana nguvu kwenye mapatano. Kuna namna nyingi ambazo wajasiriamali hujikoki dhidi ya rushwa katika ngazi ya shirika.
  3. Kwa kuziba mianya ya rushwa, yaani udhibiti wa hatari (risk management). Njia hii ya kudhibiti hatari inaweza kuwa kwa kuhakikisha mjasiriamali ana vibali vyote stahiki vya kufanya biashara, kwani kukosa vibali kunafungua mianya ya kudaiwa kitu kidogo. Wajasiriamali wengine hujenga sifa njema na hivyo kuwafanya wapenda rushwa waogope kuhusiana nao, hasa wateja wa namna fulani. Wajasiriamali, hasa watoa huduma, wanaojenga sifa njema na ya kuheshimika kwenye soko huweka mikakati thabiti ndani ya biashara zao inayoziba mianya ya rushwa. Kwa mfano, mashirika huwa na kanuni za maadili (codes of conduct) wanazozisambaza kwa wafanyakazi wao na wateja wao, na kuzifuata.

Mikakati ya kupinga rushwa dhidi ya wafanyakazi/mawakala wa kampuni

Kwa kuzingatia mienendo ya kijamii na uhusiano na wadau mbalimbalu, wajasiriamali pia huweza kuwa na mikakati ya kupinga rushwa dhidi ya wafanyakazi au mawakala wa mashirika /makampuni wanayohusiana nayo kwenye biashara. Mikakati hii ni kama ifuatayo:

  1. Mikakati ya kuepuka mwingiliano na mawakala wanaondekeza rushwa. Kwa mfano, mjasiriamali anayetegemea kupata cheti cha Shiringa la Viwango Tanzania (TBS) au Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ili aweze kuuza bidhaa zake kwa wateja, endapo atadaiwa rushwa na mhusika na hatakuwa na namna mbadala ya kupata cheti ili aweze kufanikisha biashara yake basi ana uwezo mdogo zaidi wa kushindana na rushwa kwenye mapatano hayo. Hivyo, ili kupingana na rushwa lakini bila kuathiri upatikanaji wa cheti cha ubora, mjasiriamali hana budi kutafuta namna mbadala ya kuhakikisha anapata anachokitaka bila kutoa rushwa. Wengine hutumia washauri au mabingwa wa shughuli fulani badala ya kushughulikia kila kitu wenywewe. Namna maarufu ya kuepuka mwingiliano na mawakala au wafanyakazi ni kutumia teknolojia. Yaani, kama kuna uwezekano wa kufanya mambo kwenye mtandao bila kwenda kwenye ofisi fulani, basi mjasiriamali hufanya hivyo ili kuepuka usumbufu wa kuombwa rushwa. Kuepuka rushwa kwenye manunuzi na ugavi, baadhi ya wajasiriamali wanapendelea kufanya biashara na mashirika au kampuni ambazo hatahitaji kuzungumza na wakala, bali mmiliki moja kwa moja. Mara nyingi, mmiliki wa biashara hana sababu ya kukuomba cha juu ili uingie naye kwenye biashara, kwani biashara iliyonyooka humnufaisha na yeye mwenyewe pia.
  2. Mikakati ya kushirikiana na wafanyakazi/mawakala dhidi ya rushwa. Mikakati hii hutumia hulka na tabia za wafanyakazi dhidi ya rushwa. Wengine hutumia mbinu ya kujificha, yaani kama changa la macho, waonekane biashara zao ni ndogo hivyo hazivutii kwa wataka rushwa. Mjarisiamali ataenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  kwa mfano, na bajaji huku akiwa amevaa mavazi chakavu ili mradi mtumishi wa pale amuone mnyonge na asitake mlungula kirahisi. Hata hivyo njia ya kujificha inaweza pia kutumika vibaya kwenye ukwepaji wa kodi. Wajasiriamali wengine walituambia kuwa hutumia unyenyekevu kuomba hisani ya mawakala/wafanyakazi, wakitumia nafasi yao ya unyonge kuepuka rushwa lakini kupata huduma wanayotaka. Njia hii, kimantiki, bado inawakweza wafanyakazi, lakini kwa kuwa kuna watu wanapenda nafasi ya utwana na kukwezwa, basi inaweza kufanya kazi kwenye nyakati fulani. Wajasiriamali watatumia lugha mahiri kuwapamba, na kuwaomba watumishi wawatendee haki.
  3. Mikakati ya upinzani kwa wafanyakazi/mawakala dhidi ya rushwa. Kukosa nguvu ya ushawishi kunaweza kumfanya mjasiriamali aonekane dhaifu, na kusumbuliwa na mawakala/wafanyakazi wanaotaka kujinufaisha binafsi. Udhaifu mkubwa uliotajwa na wajasiriamali ni kukosa taarifa sahihi. Wajasiriamali hujikoki kwa kuwa na taarifa sahihi juu ya michakato na haki zao, ili kuwazuia watu wanaotaka kuwaingiza mjini. Kwa mfano, mfanyakazi wa TRA akimuambia alipe kupata namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN) anaweza kumdaka na kumuambia kuwa siyo sahihi. Turudi kwenye mfano wa awali wa kuombwa rushwa kwa ajili ya kupata cheti. Baadhi ya wajasiriamali hutumia watu wenye nguvu zaidi kwenye mapatano kwa kuandika barua na kuwaweka wakubwa wa mtu anayeomba rushwa, ili kumkata nguvu mtumishi mmoja mmoja. Mikakati hii ya upinzani, mara nyingi inategemea sana jinsi mtu anavyoweza kutumia rasilimali au nguvu ya mahusiano kufikia malengo yake ya kupingana na rushwa.

Utafiti wetu unaonesha kuwa, mjasiriamali mdogo na anayeanza sio dhaifu kupindukia dhidi ya rushwa, na kwamba wengi wao wanajaribu mikakati mbalimbali ya kupingana nayo, ili kupunguza gharama na kujihakikishia mafanikio. Hata hivyo, si kila mwenye nia ya kupingana na rushwa anaweza kufanikiwa. Mafanikio yanategemea sana uwezo wa kirasilimali walionao na ubunifu wa mbinu zinaoweza kuwaongezea nguvu ya ushawishi (leverage) katika mapatano ya biashara.

Watunga sera wanaweza kuwaongezea nguvu wajasiriamali kwa kuhakikisha kuwa wana njia mbadala za kupata rasilimali na uhalali, kuwekeza kwenye teknolojia zinazoweza kupunguza muingiliano na kutoa taarifa sahihi kwa wajasiriamali ili wasiingizwe kwenye mtego. Kwa mfano, kukiwa na mbadala wa kupata huduma kwa njia ya haraka (expedited services) kwa watu ambao hawawezi kusubiri huduma. Ukosefu wa mbadala unawafanya wajasiriamali wakose uwezo wa kupingana na rushwa, hata kama hawaitaki.

REJEA

Makala haya yamechapishwa katika Jarida la Usimamizi (Journal of Management): https://doi.org/10.1177/01492063241259424. Tafsiri imefanywa na Neema Komba na kwa msaada wa Akili Mnemba (AI) ya Microsoft Copilot.