Jipu Kuu 


Kuna jipu na majipu, matabibu hutujulisha

Lipo lilo kama upupu, huwasha kwa bashasha! 

Ukubwae wa kikapu, hutuvimbia kama kasha

Kuu hili la Majipu, lini tatumbuliwa Asha?


Lishaiva hilo jipu, mbona bado twajipasha?

Au hadi twanguke pu, ndo twache kulilisha?

Hatuuchoki huu utupu, wauchekao Watasha?

Kuu hili la Majipu, lini tatumbuliwa Asha?


E Mtumbua Majipu, twaona rasha rasha

Sasa situmie diripu, wasiseme la hasha!

Libane kama tiripu, litoboke bila kubisha

Kuu hili la Majipu, lini tatumbuliwa Asha?


Uchungu wa vijipu, asiyeujua Washawasha

Muwashwa wa Kishapu, utungu wamtosha!

 Jipu Kuu la Majipu, lioshwe kama Muosha

Kuu hili la Majipu, lini tatumbuliwa Asha?

© Malenga Mdadisi



Jipu Hilo Jipu Gani?


Jipu Hilo jipu gani

Jipu lisilo na haiba

Jipu lisilo utani

Wala homa nasaba


Jipu liko ndani

Sistimu hukuna uhaba

Jipu limejaa uvundo usoni

Jipu lazima litumbuliwe


Bara na pwani

Mashariki kusini

Magharibi kaskazini

Mtumbuaji ashike pini

Huruma asiweke moyoni

Apasue jipu pwaaaa


Usaha uondoe nukhsani

Taifa letu adhimu

Lifurahie neema ya Mola mwenye Imani

Alotupa dhahabu na madini

Mito, mabonde, na mengi milimani

Hala Hala Watanzania, 

Shangilia awamu yenye nidhamu


© Leila Sheikh