Swali Tupigie Kura (Referendum) Lugha ya Kufundishia? limechochea mjadala mkali kwenye Mtandao wa Mabadiliko na kuendeleza mjadala huu usioisha kwenye Wanazuoni pamoja na kuakisi mjadala kama huo kwenye Jamii Forum. Bado mgawanyiko uke pale pale japo kuna wanaodai kwa nini suala la kitaaluma lifanywe la kisiasa kwa kupiga kura ya maoni. Pia tupo tunaosema baada ya wataalamu kutafiti na kulisemea kwa muda mrefu toka enzi za Tume ya Makweta wanasiasa wameendelea tu kupiga danadana na kuendekeza sera ndumilakuwili ya lugha ya kufundishia inayomhukumu mtoto kushindwa mapema hasa katika kipindi cha mpito kutoka shule ya msingi na kuendelea kwenye shule ya sekondari. Hivyo basi pengine sasa ni wakati muafaka wa kulifanya hili kuwa suala la kisiasa hasa kwa kulipigia kura katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya maana tunaambiwa kila kitu ni siasa.

Maoni yafuatayo yamemgusa sana Mdadisi hasa hilo linalotumia mbinu ya kejeli kuwasilisha kile ambacho baadhi ya wachangiaji wamekiita ubwege wetu wa kushindwa hata kabla ya kuanza kwa kujiona hatuwezi na hatujiwezi:


KIJAKAZI:

Baada ya kusoma posti yako naweza kusema kwamba nafikiri kama ungekuwepo (Mungu saidia haukuwepo) wakati Wamisionari (ambao walikuwa Wazungu) wanatafsiri biblia enzi hizo ungepigania kuwashawishi wasitafsiri Biblia Kiswahili kwa maana “Kiswahili kinakosa uwezo wa kuelezea fikra”, lakini Wazungu walifanya pamoja na kuwa Biblia ni moja ya vitabu vigumu sana, lakini walifanya na leo hii Watanzania wengi tunanufaika kwa kazi kubwa iliyofanywa ya kuifanya liturjia kuwa kwa Kiswahili (Wazungu walifanya), sasa kama waliweza Biblia kwa nini ishindikane Fizikia au Kemia au Hisabati?

Hii inadhihirisha tu usemi kwamba sisi Waafrika hakuna kitu tunaweza kufanya, nakuhakikishia kama Tanzania ingekuwa bado inatawaliwa na Wazungu (Wajerumani) ambao ndio walileta mfumo wa kutumia Kiswahili mashuleni (sio sisi) leo hii tungekuwa tunatumia Kiswahili kuanzia chekechea mpaka Elimu ya juu, lakini kwa bahati mbaya Mungu hakutupenda sana wakaondoka mapema bila kuendelea kutuelimisha kwa Lugha yetu wenyewe leo hii zaidi ya miaka 100 baadaye tunapinga kwa nguvu zote Lugha (yetu wenyewe na hii utaiona Afrika tu) iliyotufundisha Neno La Mungu!
Na mwisho kuna nchi nyingi sana za Kiafrika zinatumia Kiingereza kabisa, je, hali yao ya kimaendeleo ikoje? kama hali yao ni bora sana kuliko yetu nikimaanisha kwamba hawaibiwi kwenye Mikataba kama sisi au hawauzi rasilimali zao kama sisi kwa kuwa wanatumia Kiingereza na hivyo kuelewa kilichoandikwa kwenye mikataba, basi hoja yako inaweza kuwa na maana kidogo lakini SI KWELI Nigeria bado wanaibiwa ingawaje wanatumia kiingereza, Ghana bado wanaibiwa rasilimali ingawaje wanatumia Kiingereza, Uganda bado, Kenya bado n.k HIVYO TATIZO SIO KISWAHILI

Kama kiingereza ni maendeleo nchi kama Jamaika na nyinginezo wote 100% wanatumia Kiingereza lakini bado ndio wa mwisho kwa Umaskini katika mabara ya Marekani na wanapitwa na nchi ambazo watu wao hawajui Kiingereza kabisa kama Venezuela, Brazili ambayo wanatumia Kireno, sasa sijui hoja yako iko wapi?

Labda tunahitaji wazungu waje tena na sijui safari hii watatumia mbinu gani kuja kutuelimisha na kutuambia kwamba tunaweza kutumia Kiswahili na tukaendelea lakini kwa bahati mbaya bahati haiji mara mbili tuliipata mara ya kwanza toka kwa Wamisionari.


IMMACULATE:

Kwa maoni
yangu kupiga kura kuhusu lugha ya kufundishia ni suala la kisiasa na si la
kitaalam.

Kama kweli tunao wataalam nao
wamefanya utafiti wakatoa matokeo, kama sisi tunaheshimu utaalam basi ni
vyema kuwasikiliza wataalam wetu.

 Wataalam wenyewe wanasema
hivi: MTU/BINADAMU YEYOTE HAWEZI KUFIKIRIA KWA LUGHA ISIYO YA KWANZA KWAKE.
YAANI MFANO: MTANZANIA ALIYEZALIWA NA KUKULIA MAREKANI TO 20 YRS, LUGHA YAKE YA
KWANZA NI KINGEREZA. HUYO HATA AKIJA KUJUA KISWAHILI ATAKUWA ANAFIKIRIA KWA
KIINGEREZA KISHA ANATAFSIRI KWA KISWAHILI. HIVYO KASI YA TENDAJI NA UGUNDUZI
WAKE KATIKA LUGHA YA KISWAHILI ITAKWAMA. ATAKACHOWEZA SANA NI KUTAPIKA VILE
ALIVYOMEZA KWA KISWAHILI.

HILI NDILO TATIZO TULILONALO
WASOMI WA TANZANIA. TUNASOMA KWA KIINGEREZA HALAFU TUNAWAZA KISWAHILI. SO
UGUNDUZI HAPO HAUPO. TUNACHOWEZA NI KUTAPIKA THEORY TULIZOSOMA DARASANI AMBAZO
PENGINE HAZIFANYI KAZI KWENYE MAZINGIRA YETU, UKIZINGATIA TUNASOMA VITU VYA
UTAMADUNI MWINGINE KWA LUGHA NYINGINE HIVYO TUNAKUWA HATUNA MANUFAA SANA KWA
JAMII YETU COZ TUNAENDA KUVITAPIKA KWENYE KAMPUNI ZAO, KWA LUGHA YAO KWA
MANUFAA YAO. UKIVITAPIKA KWETU HAPA KWA LUGHA WASIOJUA WENGI HAVITUFAI.

ELIMU ILI IWE YA MANUFAA LAZIMA
KWANZA: ILENGE KATIKA KUBORESHA MAZINGIRA YA JAMII HUSIKA MF. NYASI ZINAZOTUMIWA
NA WENGI KUEZEKEA NYUMBA ZIBORESHWE KUWA KAMA VIGAE, MTOTO WA MFUGAJI AJUE
BASICS ZA UFUGAJI BORA NA UCHAKATAJI WA MAZAO YA MIFUGO, VIVYO HIVYO KWA
MKULIMA, MCHIMBA MADINI N.K. KUTEGEMEANA NA RASILIMALI TULIZONAZO. Elimu ya
Tanzania kwa sehemu kubwa hufundisha vitu vya ugenini ambavyo havipo katika
mazingira yetu..kwa hiyo tunasoma kwa manufaa ya…?

PILI LAZIMA ELIMU HIYO ITOLEWE
KWA LUGHA MAMA AMBAYO INAELEWEKA KIRAHISI ILI KUCHOCHEA UDADISI, UGUNDUZI,
UVUMBUZI, vinginevyo kutakuwa na jamii ya watapikaji wa walichosoma na
watumiaji wa walichotengeneza wengine mf. magari ya kijapani, kompyuta, dawa,
etc.

KWA KUONGEZEA: LUGHA NYINGINE
KAMA ENGLISH, CHINESE, ETC IKIFUNDISHWA NA WALIMU BORA MWANAFUNZI ANAWEZA
KUIELEWA VIZURI NA HARAKA ZAIDI….(KWA NINI TUNASOMA KWA KINGEREZA NA BADO
WENGI HATUKIJUI?)

KISWAHILI NI MUHIMU KWA MAENDELEO
YETU KAMA TAIFA. LUGHA NYINGINE TUTAENDELEA KUJIFUNZA KULINGANA NA MAHITAJI.


MABALA:

Kama mwalimu moyo
unaumia sana kuingia darasani siku ambayo wanafunzi wamebahatika
kupata mwalimu na kukuta blank faces maana hawaelewi
wanachofundishwa.  Au fanya jaribio la kufundisha kwa Kiingereza
lakini uwape kazi ya kujadili katika vikundi.  Angalia
watakavyochangamkia mada na kujadili kwa kina… kwa kiswahili lakini huku
wakitumia neno la Kiingereza hapa na pale hasa ya istilahi…na
wataelewana vizuri sana.  Siyo siasa kusema kwamba watu wanatakiwa
kusoma katika lugha wanayoilewa, ni msingi wa falsafa zote za elimu. 
Sijui kwa nini sisi tunajiona watakatifu na wenye akili ya kuweza kwenda
kinyume na falsafa hizo.  Angalia hata matokeo ya utafiti wa Uwezo. Hali
ni mbaya katika nchi zote si sisi tu lakini sisi badala ya
kutumia advantage tuliyo nayo ambayo ingejenga vizazi vya watanzania walioelimika
pamoja na kufundishwa vizuri lugha ya Kiingereza pia tunang’ang’ania
yanayofanya tushindwe kupata elimu.

[…]

Kama kawaida wako wengine wanachanganya masuala mawili.

a)  Umuhimu wa kujua Kiingereza.  Nani anabisha?  Lakini kwa mifumo yetu ilivyo hii inazidi kuwa ndoto.
b)  Kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia … hapo sasa.

Msingi wa elimu, msingi wa ubunifu ni uelewa ndiyo maana nchi zilizo nyingi sana duniani wanahakikisha kwamba wanafundisha watoto wao kwa lugha wanayoielewa.  Waholanzi, Waswidi na wengine wana uwezo wa kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia lakini hawafanyi hivyo maana wanajua kwamba msingi wa elimu, msingi wa ubunifu, ni uelewa. Na wanajua pia kwamba mara nyingi wanasayansi ndio wabovu kabisa katika kujifunza lugha.

Iwapo tunatengeneza mazingira yanayofaa (…. bonge la iwapo ….) watoto wetu wanaweza kujua Kiingereza vizuri sana pamoja na kuwa na uelewa wa mambo yote muhimu katika elimu.  Mimi nilikuwa sijui Kihispania kabisa lakini kwa muda wa miaka miwili tu, ndani ya shule tu, niliweza kupata ‘B’ katika A Level.  Kwa sababu ya ufundishaji vizuri, mipango makini na pia juhudi yangu.  Kwa hiyo hakuna linaloshindikana.  Elimu kwanza si lugha kwanza.

Na naomba pia niseme mambo mawili.

a)  Eti wengi wanafeli Kiswahili hivyo Kiswahili si utatuzi. Kwanza wako waingereza wengi sana wanaofeli Kiingereza kwa hiyo wafundishwe kwa lugha ya Kifaransa?  Inatemgea sana unaweka nini katika mitaala na nina madonge sana na mitaala ya Kiswahili maana mara nyingine inafundisha lugha kama injini ya gari badala ya kujenga hamu na ubunifu katika lugha.  Nikiangalia madaftari ya wanafunzi mara nyingine naona wanajifunza hisabati na minyambuliko yote ile.
b)  Eti Wakenya au Wazambia wanajua Kiingereza.  Elite ya Kenya inajua Kiingereza vizuri sana na wanajiamini nacho kwa sababu hawatumii shule tu bali hata nyumbani, dukani, kila mahali.  Lakini nenda sehemu nyingine, kwenye maeneo ya wasio nacho, nenda kijijini uone kama kweli wanajua Kiingereza.

Kwa hiyo, kura yangu iko wazi.  Tusipoteze muda.  Tuanze kuwapatia watoto wetu walio wengi fursa ya kujifunza na kuelewa kwa kutumia lugha wanayoijua.  Na wakati huohuo tuanze kupambana na mfumo wa elimu ambao uko ICU lakini mara ya mwisho niliposikiliza moyo nikaona bado unadunda kidogo.