Lipi likusumbualo, kalamu kuirukia
Au umekosa mlo, sasa umechukia
Lipi hasa ulonalo, unalolisumbukia
Kama shida ni uhuru, tushapata 61

Amani tulonayo, ni tunu ilotufikia
Usitake mapambano, shimoni tatumbukia
Sijeichokoza leo, kesho hutoifikia
Kama shida ni uhuru, tushapata 61

Jaribu kujipa moyo, manani takusikia
Kuwa mtu wa maono, lengo utalifikia
Siwachukie vigogo, nchi wameitumikia
Kama shida ni uhuru,tushaupata 61

Siwatafute wanono, waweza kukuchukia
Mwisho wakakutoa roho, bure kwa kujitakia
Ogopa sana vigogo, chini watakufukia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

Wale uwapiganiao, kesho watakukimbia
Hawatoshiriki mgomo, wala kukuimbia
Tena watakaa kando, huku wakijitambia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

We kula ugali wako, ukishiba tajitapikia
Achana na nia yako, wengine kuhangaikia
We jali maisha yako, wenye shida wajitakia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

Chukua hatua zako, uone utapoangukia
Usitafute maneno, balaa likakufikia
Mwombe sana Mola wako, ‘mana’ takushukia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

Kama hawapendi jambo, hawawezistahimilia
Madhari wanapata tango, shida wanavumilia
Siku wakikabwa shingo, mabosi watasimulia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

Shida zikiwakaba koo, watajua pa kukimbilia
Tena watafanya soo, mabosi watajililia
Patakuwa ni padogo, mawe yatasimulia
Kama shida ni 61, uhuru tushaupata?

© Ayub. R.

  1. Anonymous December 9, 2010 at 11:38 am

    Uhuru tumepata nchi na wananchi masikini mpaka kesho ufisadi juu ya ufisadi.

  2. Baha Bernard December 10, 2010 at 6:53 am

    Mh! kila mtu na ale kwa urefu wa kamba yake? wapo wapi wadhubutu kidole kuwanyoshea? mabathathi wafisadi nchi waifilisi, uhuru kama ni kweli mbona wengi twagaa gaa?

Comments are closed.