Mjadala huu usioisha waWanazuoni kuhusu lugha ipi iwe ya kufundishia unapaswa kuwa sehemu ya mjadala wa Katiba mpya. Maoni haya yatawisilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Maadam kuna Mwanazuoni kwenye tume hiyo ni matumaini ya Mdadisi kuwa maoni haya yatazingatiwa. Masuala ambayo Wanazuoni wanakubaliana kuhusu lugha ni kuwa Watanzania wanatakiwa kujua Kiingereza vizuri na pia wanapaswa kupata maarifa. Mambo ambayo hawakubaliani ni jinsi ya kufundishwa na kujifunza Kiingereza – kundi moja linadai kuwa tukitumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia badala ya Kiswahili basi tutakijua ilhali kundi lingine linasisitiza kuwa ukifundisha Kiingereza kama lugha ya pili basi tutakijua vizuri pamoja na kujua Kiswahili.

TELLI:

Nadhani kuna tatizo kido hapa. Watu wote wanakubali (hata mimi) kwamba lugha ya Kiingereza ni muhimu sana kwa watoto wetu wa Kitanzania. Wanaosisitiza matumizi ya Kiingereza na wanaosisitiza matumizi ya kiswahili kama lugha za kufundishia wote lengo lao ni moja, kwamba, lugha ya kiingereza ni muhimu kwa watoto wetu wote.

Kinachogomba hapa ni process ya kukifahamu hicho kiingereza. Wako wanaoamini kwa nguvu zote kwamba kutumia kiingereza kufundishia ndio njia muafaka wa kukifahamu. Kundi hili wanaamini hivyo sio kutokana na sababu za kisayansi au kiutafiti bali kwa ushahidi wa kihisia na kimaono zaidi (anaecdetol evidence).

Ukweli ni kwamba kutumia lugha ya kwanza (mama) kufundishia inasaidia zaidi sio tu kufahamu masomo ya darasani bali hata kufahamu lugha ya Kiingereza. Kumbuka pia kwamba lugha ya kwanza hata kwa mtoto wa kitanzania inaweza kuwa kiingereza pia.

Mfano, mtoto wa kitanzania aliyekulia Oyster Bay na lugha yake ya mawasiliano ndani ya familia ni kiingereza kitupu (Au kwa mfano halisi wa Rasel ambaye mwanae amekulia Marekani na kiswahili kwake ni lugha ya pili)  kiingereza kinapaswa kuwa lugha yao ya kufundishia. Wale kina siye ambapo wanetu wanasoma Kichwamaji shule ya msingi kiswahili kinapaswa kitumike kufundishia masomo yote, ili wawe na ufahamu wa hayo masomo na wa lugha ya kiingereza pia. 

Kwa hiyo tofauti zilizopo hapa ni kuhusu “process” na sio “outcome”. Wote tunakubaliana na outcome lakini sio kwenye process. Tukielewana hapo mbona mjadala utapendeza.


CHAUKA:

Waskandinavia hata hawakitumii kingereza sana, ila wale ambao inabidi wakijue kutokana na kazi zao wanakijua vizuri kulingana na hitaji. Hapa niko ujerumani, hawakijui kingereza, napata shida kweli. Hapa wananiletea kila kitu kwa kijerumani, mpaka nipeleke madocument kwenye google translate nijue kilichoandikwa. Siku nilipoenda kufungua akaunti benki, nilishangaa kukutana na kijana anayekijua kingereza kweli kweli. Nikashangaa sana kujua kuwa kumbe wako wajerumani wanaokijua kingereza vizuri kiasi hicho. Wao wale ambao wanahitaji kufahamu kingereza kulingana na kazi zao, kwa kweli wanahakikisha wanakifahamu. Mfano mwingine, kwa zile programme chache sana za chuo kikuu ambazo zinaendeshwa kwa kingereza, wale wanaoendesha wanakijua kingereza vema. Waskandinavia hata wasipokifahamu, wanajiweza wenyewe, hawahitaji mtu mwingine labda watakapoenda kutalii Tanzania ndio watahitaji. Sisi ambao hata toilet paper tunaagiza na huenda hata hatuna msamiati wake, nadhani tunahitaji.

[…]

Tusidanganyike jamani, lugha ni jambo la muhimu, linamuongezea confidence mtu. Nimehudhuria mikutano mingi, watanzania pamoja na kuelewa jambo wanakaa kimya, hata hawaulizi maswali, kwa sababu lugha ni kingereza. Pamoja na kuwa tunatakiwa tufahamu kiswahili, bado watanzania wanahitaji kujifunza kingereza na kukijua vizuri, bila hivyo tutashindwa kupambana na wenzetu wa hapa Africa Mashariki. Mimi ningeona hata primari masomo yote yafundishwe kwa kingereza, kwa sababu hakuna mana kumfundisha kwa kiswahili mtu, alafu baadae anafundishwa kwa kingereza, inakuwa kupoteza muda wake.

MKUMBO:

Tuache danadana, watu wafundishwe vizuri wazijue lugha zote mbili za Kiswahili na Kiingereza, kwa kuanzia. Huko mbele na lugha zingine wajifunze za kimataifa na kitaifa. Ni aibu kwa wananchi wetu kuwa na lugha moja huku tukizungukwa na nchi zote zinazungumza angalau lugha mbili au tatu. Sisi ni wazembe wa kujifunza, hasa lugha. Hata humu ndani mtu hata lugha ya kwao hajui. Lugha ya jirani yake hataki kujifunza. Tutabishana weee, na kukisifia sana Kiswahili, lakini ukweli ni kwamba tunazihitaji hizi ligha zote kwa usawia kuliko zenyewe zinavotuhitaji sisi!


MATINYI:

Mimi sioni tatizo lolote kwa Tanzania kuwa nchi yenye lugha mbili huku Kiswahili kikiwa juu ya Kiingereza. Nchi zingine wameweza, kwa nini sisi tushindwe? Ni kwa sababu ya kutojiamini, kutopanga mambo yetu vizuri na mvurugano uliopo sasa. Mataifa ya Ulaya karibu yote, watu wake wanakitumia Kiingereza kama lugha ya pili, mbona wanatushinda mbali kabisa? Watanzania wanaosoma Uholanzi, Ujerumani na hata Italia wanatumia Kiingereza, ingawa wao wanababaisha cha kwao, kwani hao walifanyaje mpaka wakakimudu Kiingereza? Zipo nchi za Afrika kama Misri, Morisi (Mauritius), Algeria, Tunisia, na Morocco ambazo zina lugha kuu mbili, kwa nini sisi hatuwezi? Kwa nini hatuwezi? Shida yetu ni nini hasa? Hivi mna habari kwamba sasa hivi hata Kiswahili vijana wa siku hizi hawakijui Nitatoa mifano hapa:

1. Mwandishi/mhariri anaaandika: ……. katika Tanzania ……. (hakuna kitu kama hiki kwenye Kiswahili).
2. Mwingine: ………polisi jamii ……….. au ……..kikosi kazi…….. au mpango mkakati ………. na juzi nimesikia uchafu mwingine eti “uchambuzi kina”. (Kiswahili hakina muundo huu unaobeba nomino mbili kwa pamoja kana kwamba moja ni kivumishi/kisifa).

Hii ni mifano ya ujuha wetu, kwamba baada ya watu kufahamu Kiingereza kibovu, sasa wanahamishia muundo wa Kiingereza kwenye Kiswhili kwa madai kwamba lugha inakua.

Kama tunashindwa kuijua na kuilinda lugha yetu, kwa maoni yangu hata ikitumika kwenye elimu bado tutabaki majitu majinga majinga tu. Kwa nini hatujui Kiswahili leo hii? Ni kwa sababu elimu imekufa nchini na kwenye somo la Kiingereza ndiyo ilikwua ya kwanza kufa na hatimaye leo Kiingereza ni kama kituo cha polisi kwa Watanzania. 



Kwa kifupi na Kiswahil kwisha habari yake; anayebisha achukue habari yoyote kwenye gazeti la leo lolote na asome.

Dawa yetu ni kufufua elimu bora tu.

TUMAINI:

[A]wali nilisema kuwa kama tutaweza kuiga mfano wa Nchi kama Kenya,Uganda na nk, kwa kuongea lugha ya kiingereza hata wakiwa mitaani itasaidia sana. Hii ni kwasababu wameipa nafasi ya Kwanza Lugha Kiingereza. Na sisi inatupasa Tanzania tuige hilo la sivyo, tutauumbuka na kukosa mengi kwa kutokipa Kipaumbele lugha ya kiingereza. Kiswahili kinaishia TZ tuu, ni kitatusaidia sisi tuu kama watza au wana EA, lakini kiulimwengu wa leo hakitambuliki?

BEDA:

Binafsi siungi hoja ya Tanzania kutumia lugha ya Kingereza kama lugha ya kufundishia, maana ili mtu u-elimike ni muhimu utumie Lugha mama. Na kuigeuza Kingereza kuwa Lugha mama kwa watanzania walio wengi ni ndoto, Kiswahili ndio Lugha pekee inayoweza kuwa-onganisha watanzania wote hivyo kuna tija tuki-itumia…


Swala la wenzetu wakenya kutuacha sio suala la Lugha. Kenya kuna vyuo vikuu vingi kuliko Tanzania, yaani wamewekeza zaidi ya Tanzania katika elimu ndio maana wametuzidi, angali viwanda vya na idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu…


Kama kweli kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa, tukianza kufundisha shule za msingi kwa Kingereza, kitawasaidia walio vijijini ?? Hiki Kingereza tunachosema ni muhimu kufanya tujiamini kwenye ulingo wa kimataifa ni chini ya asilimia tano ya watanzania, wenye uhitaji nacho, kweli sera za nchi zitungwe kunufaisha asilimia tano ya taifa ??? Mi nadhani bora kuongeza nguvu katika somo la kingereza tu. 


Kwa maendeleo ya Taifa, na sio kwa maendeleo ya mtu moja moja, tutilie mkazo kwenye kiswahili. Pengine, kwa kuanzishwa kwa shule za kata, watoto wengi zaidi wanapata fursa ya elimu (bora elimu / elimu bora ?), hawa watoto wangefundishwa mpaka kidato cha nne, na kwa wale wanaoenda veta, wote wafundishwe kwa kiswahili…. Kweli msusi ajifunze ususi kwa kingereza ??? Mpishi ajifunze kupika kwa kingereza ??? Mkulima ajifunze kulima kwa kingereza ??? kweli kuna tija hapo ??? Ni wafanyakazi wangapi kwenye sehemu zao za kazi wanatumia kingereza ?? kuna tija ya kufanya mikutano katika jukwaa ambao wote wanajua kiswahili kwa kingereza ??? Kingereza inatumiwa na asilimia ndogo sana ya nchi yetu kwa ajili maendeleo ya nchi….


Kingereza ni muhimu, tuwekeze katika somo la Kingereza tu.

[…]

Nadhani kuna umuhimu wa kutenganisha Umuhimu, Jukumu na Faida la Lugha kama chombo cha (a) Kupata Elimu na (b) Mawasiliano. 



Nionavyo mimi,,, kama tunataka nchi na watanzania walio-ELIMIKA basi tutumie Kiswahili, na kuna tafiti nyingi ambao inayooanisha hilo. 



Suala la watanzania kuto-kujiamini wakiwa katika uwanja wa kimataifa au mawasiliano kuwa magumu, binafsi sioni kama tatizo ni Lugha iliyotumika kufundishia, bali ni Lugha inayotumika kuwasiliana. 



Kwa familia ambao majumbani kwao wanaongea kingereza na watoto wataongea na kujiamini kuongea kwa kingereza. Nijuavyo, kuwa mahiri katika kuongea Lugha flani, inatokana na mazoea/mazoezi ya kuogea hiyo Lugha. Mfano, mtu ukienda ukaishi amerekani kwa miaka mi-nne hivi, ukirudi Tanzania, Kingereza utaongea vizuri tu. Na nina marafiki wengi ambao wameenda marekani kingereza cha ku-unga unga tu, wamerudi na lafudhi imebadirika kabisa, na wanaongea kwa kujiamini.


Hivyo kama tunataka watoto wetu wajiamini kuongea kingereza, kuna umuhimu wa kubadilisha Lugha inayotumika mtaani. Wenzetu wa zimbabwe, ghana, kenya, wengi wao Lugha wanaongea nyumbani na mtaani ni Kingereza, na sio Lugha zao za asili, pengine ndio sababu ya wao kujiamini kuongea Kiingereza. 

MAZIKU:

[N]i kweli uzoefu huo ndiyo hali halisi inayotukuta Watanzania, si kwamba hatuelewi ila mawasiliano yanakuwa magumu sana inapokuja katika matumizi ya lugha ya Kiingereza, mtu anakosa kujiamini na anachokiongea hasa anapokuwa amekutana na watu ambao wao tayari wanakiongea kama lugha yao ya kuzaliwa.  Huenda hata mikataba mingi ya wawekezaji tumejikuta hatuwezi kujadili na tumesaini kama vipofu


Uzoefu binafsi, Mwaka 2004 nilichukua kozi ya maendeleo ya jamii kule Nairobi, nilipata shida sana kuongea hii lugha ya kiingereza, nilikuwa sina ‘confidence’, si kwamba nilikuwa sielewi, nilijitahidi kuongea lakini ulikuwa ni mzigo mkubwa kwa sababu ‘I felt that my oral English was relatively very poor’.  Lakini tulipofanya mitihani na kuandika ripoti yangu ya utafiti, katika wanafunzi 5 waliopata alama za juu nilikuwa nimo.  Mkuu wa chuo alinipa nafai ya kufundisha pale chuoni, Niwafundishe wanajua lugha ya wote!!!


Lakini ukweli ni kwamba wakati wa kozi na kabla ya mitihani wanafunzi wenyeji (Kenya), Uganda, Zimbabwe n.k walikuwa wame tu write-off sisi Watanzania katika English na katika kozi.  Siku ya Matokeo na Graduation heshima irirudi.  Lakini, uzoefu huu umenisaidia kujenga nadharia kwamba Watanzania tunashida ya kuongea si kuandika Kiingereza, nime conclude kwamba Mtanzania aliyesoma vizuri akaelewa hata kama hawezi kuongea mpe kalamu na karatasi aandike atafanya vizuri, nadhani hata wenzetu wa Afrika mashariki wanajua hilo (but I stand to be criticized).  


Hili suala la lugha ya Kiingereza/Kiswahili ni gumu sana kufikia muafaka, kwa sababu watu tuko ‘cynical’, hatusemi kile kilicho mioyoni mwetu, tuna advocate kiswhili lakini hatutendi kile tunachosema.  Tunajua kabisa jinsi mfumo wa lugha za kufundishia Kiswahili (katika ngazi ya awali/primary schools) na kiingereza katika ngazi zinazofuata (upili/secondary, na utatu/Tertiary (Vyuo vikuu/vyuo vya elimu ya juu) ulivyotuweka njia panda katika kupata umahili wa lugha ya kiingereza.  


Katika dunia ya utandawazi (Globalization) umahili wa lugha, hasa lugha ya Kiingereza kama lugha ya kimataifa unabaki palepale kwa hiyo ili tuweze kufaidi matunda ya utandawazi ni muhimu kuwa na umahili wa lugha hii.  Afrika, na hasa Tanzania sasa inavutia wawekezaji wa kigeni na lugha yao ni Kiingereza sasa kama vijana wetu waliotoka UD, Mzumbe, Sokoine nk hawawezi kujenga sentensi ya kiingereza ikaeleweka, tunategemea nini?.  


Labda tushinikize usaili uwe wa kiswahili au waandike (written interview).  Ndugu Yona aligusia suala la ajira na lugha ya kiingereza, binafsi nakubaliana naye kwa asilimia fulani, kwamba lugha ya Kiingereza ni kikwazo katika kupenyeza kwenye mashirika ya kigeni.  Kwa sababu kama mtu hana umahili wa lugha ya kiingereza, anaweza akawa na sifa zote lakini kama hajiamini katika kueleza kile unachouulizwa, au unapoulizwa unashindwa kuelewa wanachotaka lazima utashindwa katika usaili.  


Kwa uzoefu wangu, katika matangazo ya ajira katika mashirika ya kigeni hapo Tanzania moja ya ‘Essential minimum requirements’ huwa ni communication skills (Fluency in Oral and written English), swahili huwa ni added advantage.  Ukitaka ajira UN, wanakuambia uwe na lugha mbili za UN, English na French, Swahili ni added advantage kama ajira iko maeneo ya DRC, Rwanda au burundi (Ukanda wa Afrika ya kati)


Kwa hiyo mpaka tutakapo amua kwamba ni Engish au ni Kiswahili iwe lugha ya kufundishia katika ngazi zote, tutataendelea kuapata shida ya kuwa njia panda.  Tungeiga mfano wa mataifa yanayotumia lugha moja katika mfumo wa elimu badala ya kuwa Mshika mbili moja humponyoka.  Mimi sina shaka na Kiswahili kama lugha ya umoja wa Taifa letu, lakini nina mashaka kama lugha ya kufundishia kwa hiyo tuitishe kura ya maoni tuone mawazo ya Watanzania wengi wanasemaje kuhusu lugha gani itumike kufundishia kwenye ngazi zote za elimu.

MUTEMBEI:

Msingi wa hoja yetu (kama ninavyokubaliana na mwalimu wangu Richard Mabala) ni kuwa: ili mtu apate ufahamu, uelewa na elimu, NI LAZIMA AJIFUNZE KWA LUGHA anayoielewa, iliyo karibu yake na iliyo katka utamaduni wake. Hii ndiyo hoja ya msingi.


Na msingi wake ni kuwa: ujifunzaji wa maarifa mapya, huendana na mambo mengi yanayomkuza na kumjenga mtu anayejifunza. mambo hayo hupitishwa katika lugha iliyomzunguka, utamaduni n.k.


Aidha, hoja yetu ya pili: HAKUNA ANAYEKATAA KUWA WATU WASIJIFUNZE KIINGEREZA. Labda hili hamlifahamu au mnalifahamu, ndivyo sivyo.

Kwa hakika sisi wote tungelipenda watu wafahamu Kiingereza. (Labda ndio maana watu binafsi wanawapeleka watoto wao katika shule za Kiingereza, hata kama watu hao ni watetezi wa hoja ya msingi ya upatikanajai wa maarifa).


Kwa taarifa yenu: Chama cha Walimu wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (CHAKAMA) kiliandika pendekezo, na likakubaliwa katika nchi zote wanachama. Pendekezo lilitaka Tanzania (kama kiongozi) iruhusu uanzishwaji wa Sekondari mmoja ya mfano ambapo Kila somo (KILA SOMO) litakuwa linafundishwa kwa Kiswahili!! Masomo yote ya sayansi, sayansi jamii n.k. yafundishwe kwa Kiswahili. Na tuwe na somo la Kiingereza kwa wanafunzi wote. Hoja ilikuwa ni kwamba, kwa kufanya hivyo, wanafunzi katika sekondari hiyo WATAKUWA WANA MAARIFA NA UELEWA WA MAMBO katika masomo yote. Watakuwa wamepata stadi zinazohitajika. Watakuwa WAMEJENGEWA ARI YA UVUMBUZI na UBUNIFU mambo ambayo yanahitajika kumfanya mtu awe mwanasayansi wa kweli.


Licha ya hayo, hoja ilikuwa ni kuwa: WANAFUNZI katika Sekondari hiyo WATAKUWA WANAELEWA KIINGEREZA NA KUKIZUNGUMZA Vizuri ZAIDI kuliko wanafunzi katika shule nyingine za kawaida nchini.


Tuliomba, na pendekezo likapelekwa kwa Waziri (aliyekuwapo wakati huo, miaka ya mwanzoni ya 2000) na Waziri akaKATAA KATA KATA, kuwa hataweza kuruhusu jambo kama hilo.


Kwa hiyo, Mwalimu mmoja kushindwa kukumbuka, (au kutokujua kabisa) neno la Kiswahili, na badala yake akalijua kwa Kiingereza, si hoja ya msingi katika mtiririko huu. Ninadhani ninaeleweka.


Katika Kiswahili kuna Taaluma nyingi. Kama Mhusika si mtu wa eneo la Msamiati, ni kwanini itarajiwe kuwa atajua, au anatakiwa kujua maneno yote katika Kiswahili kwakuwa anafanya kazi TATAKI? Mtu wa Fasihi kwa mfano, utakuwa unamwonea kumtaka ajue maneno ya Kiingereza katika Kiswahili au tafsiri yake. Kuna wanaoshughulikia taaluma ya tafsiri na ukalimani, hawa unaweza kuwatarajia wajue maneno toka lugha moja kwenda nyingine. Na hata wao si lazima maneno yote. Hivyo, ni kumwonea huyo Profesa wangu kuwa hakujua neno la Kiswahili akasema kwa Kiingereza.


Si vibaya, au dhambi kuzungumza Kiingereza. Tunachosema ni kuwa wanafunzi ili waelewe, wapate elimu na maarifa wafundishwe kwa Kiswahili. Huu ulikuwa uamuzi wa miaka ya 60. Kwa hakika mwaka 1962, ndipo azma ilipowekwa.


Tungelikuwa tulianza wakati huo na kuacha maneno matupu, leo, tungelikuwa na MAARIFA na MBADILIKO, na kama nchi za Asia za Malaysia, Singapore, Thailand ambazo ziliazimia kama sisi, wao wakatenda zaidi kuliko maneno. Sote tulikuwa chini ya Mkoloni huyo huyo mmoja.

KWEKA:

Ukweli
ni kuwa hata wale tunaokipigania kiswahili bado tuna wasiwasi nacho. Moyoni
mwetu hatujakikubali. Ni Mtanzania gani wa tabaka la kati ambaye anampika
mwanae awe mahiri katika lugha ya kiswahili kabla ya lugha ya kiingereza?
Katika nchi hii,kiswahili kina hadhi katika taasisi za umma tuu. Sekta
binafsi(rasmi) inatawaliwa na lugha nyingine. Ukoloni ulipanda fikra ya kubagua
na kupuuza lugha za wazawa. Athari ya fikra hizo kwetu iko wazi.  Profesa
mmoja(jina kapuni) wa kiswahili hapo UDSM alikua anahutubia mhadhara wa
kumbukumbu ya Chachage alafu `akashindwa` kusema jambo fulani kwa 
kiswahili maana msamiati wake ulikuwa mbali,lakini akalikumbuka kwa kiingereza.
Kisha akajicheka. Huyu ni nguli wa Kiswahili.


VYANZO CHA MJADALA:

http://groups.yahoo.com/group/Wanazuoni/message/17372

http://groups.yahoo.com/group/Wanazuoni/message/17322

VYANZO VYA PICHA:

https://udadisi.com/2012/07/tume-ya-kukusanya-maoni-ya-katiba.html

http://www.mjengwablog.com/2012/09/mabadiliko-ya-katiba.html