Tuitazame Katiba Mpya kama Chombo cha kuubadili
Mfumo Dhalimu uliopo
Richard Mbunda
(Makala haya yalitolewa katika gazeti la
Mwananchi katika ulingo wa Siasa mwaka 2014 wakati mchakato wa uandishi wa katiba
mpya unaendelea lakini haikuwekwa katika mtandao. Ni vyema sasa tukaiweka
katika mtandao ili iwe rejea ya baadaye)
Mchakato wa kuandika katiba mpya katika nchi yoyote
hugubikwa na mivutano inayoashiria kuwepo kwa maslahi ya makundi mbalimbali
katika nchi husika. Kundi lolote lililo na maslahi linatambua kuwa, kulala
wakati wa uandishi wa katiba ni sawa na ule usemi wa ‘cheka na nyani uvune
mabua’. Tunapaswa kutambua kuwa, mivutano hii haina mantiki hasi, kwa kuwa uwepo
wa maslahi yanayokinzana kutaifanya nchi kupata katiba nzuri kwa sababu mambo
ya hovyo hovyo ni lazima yatapigiwa kelele na kuchujwa.
vikundi na maslahi ya taifa ili katiba isitumike kutetea maslahi binafsi ya
watu wachache au vikundi fulani. Kwa mantiki hiyo basi, uandishi wa katiba unapaswa
kuzingatia utaifa zaidi kuliko maslahi ya vikundi.
Matumaini ya Katiba Mpya kwa Makundi Mbalimbali
Wadau wa katiba ya muungano wamekuwa na matumaini
mbalimbali. Kwa mfano, katika hotuba yake aliyoitoa kwenye uzinduzi wa Bunge
Maalum la Katiba, Rais [Mstaafu] Kikwete alitanabaisha kuwa kuna makundi yanayodhani
katiba mpya, na hasa katika mapendekezo yake ya mabadiliko ya muundo wa Muungano, yangewarahishia kushinda uchaguzi na kushika madaraka ya nchi. Kwa
vyama vya siasa, ambavyo malengo yake makuu ni kushika madaraka ya nchi hilo ni
tumaini sahihi kwao na wanapaswa kulizingatia ili kulinda umuhimu na uhai wa
vyama vyao. Kwa maana hiyo, vyama vya siasa vina haki ya kupigania kuwekwa kwa
mifumo sahihi ya kiutawala na usimamizi ili pawepo na ushindani wa haki wakati
wa uchaguzi.
Katika mijadala ya katiba, ndani ya Bunge Maalum na hata
katika majukwaa tumesikia matumaini ya pande mbili za Muungano katika katiba
mpya. Kwa upande wa Zanzibar, tumesikia matakwa yao, kuwa wanataka ushiriki
katika medani za kimataifa kama vile kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam,
kukopa kimataifa na kudhibiti biashara za kimataifa. Ingawa pia wapo wale
wanaodai mamlaka kamili ya Zanzibar katika muungano wa mkataba, madai ambayo,
kama yakizingatiwa, yatauweka muungano njia panda.
Katiba mpya imewapa pia watanganyika matumaini ya
kufufuliwa kwa Tanganyika yao ili iweze kutetea maslahi yao ndani ya muungano.
Wakati huohuo Wazanzibari wangependa Tanganyika ifufuliwe ili isiendelee kuvaa
koti la serikali ya Jamhuri ya Muungano
na kujinufaisha na nafasi hiyo. Hivyo basi, kwa baadhi ya makundi, katiba mpya
itakuwa na tija tu kama muundo wa serikali tatu kama ulivyopendekezwa na Tume
ya Jaji Warioba utazingatiwa. Kwa mtazamo wangu, tusijibane katika fikra hizo,
bali tuangalie ni jinsi gani katiba itaweka mazingira ya kuubomoa mfumo dhalimu
uliopo.
Matumaini ya Watanzania wa Kawaida
Matarajio ya wananchi wa kawaida, ambalo ndiyo kundi kubwa
nchini yamekuwa tofauti na wanasiasa wetu. Takwimu za Tume ya Mabadiliko ya
Katiba zinaonesha kuwa maoni ya wananchi wengi yalilenga zaidi masuala ya
utawala bora, matumizi ya rasilimali na maisha yao ya kila siku kuliko hata
miundo ya muungano ambayo wanasiasa wanaipigania. Wananchi wanakerwa na mfumo
uliopo ambao hauna uwajibikaji kwa viongozi na raia. Badala ya kufanya kazi kwa
bidii na kupata mapato halali, watu wengi wamekuwa wakiishi kwa ujanja ujanja
tu!
Wakati katika ngazi za juu kuna ufisadi wa kutisha, usemi wa ‘kila mbuzi
hula kutokana na urefu wa kamba yake’ umekuwa halali kwa watumishi wa Serikali
ambao wametumia nafasi zao kuomba rushwa ndogo ndogo kwa wananchi. Hizi rushwa ndogo
ndogo zimekuwa kero kubwa kwa wananchi kwa kuwa zinamkamua maskini huyu hata
kile kidogo alichonacho.
Vivyo hivyo, wakati Tanzania imejaliwa utajiri mkubwa wa
rasilimali kama vile madini, misitu, mbuga za wanyama na gesi, rasilimali hizi
zinaonekana kutokumsaidia mtanzania. Watu waliopewa dhamana ya kusimamia
rasilimali hizo wametuangusha kwa kujali maslahi yao binafsi. Matokeo yake ni
kuwa raia wa kawaida ameachwa katika maisha yasiyotabirika huku Serikali
ikiendelea kuongeza kodi katika bidhaa anazozitumia.
Mjadala umeibuka kwa muda mrefu sasa juu ya nini kikwazo
kikubwa cha maendeleo yetu kama taifa. Kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi mfumo
uliopo ndio kikwazo kikubwa kwa nchi yetu kupiga hatua. Lakini kwa upande mwingine kuna wanaoamini
kuwa tatizo letu kubwa ni uongozi.
Katika moja ya makala zake za wazi, M.M. Mwanakijiji
anatuaminisha kuwa adui mkubwa wa maendeleo yetu ni mfumo haramu uliotengenezwa
na utawala wa kifisadi. Kwa mujibu wa Mwanakijiji, “mfumo huu
una mchanganyiko wa mifumo midogo midogo ya kisiasa, kiuchumi, na kisheria
ambayo msingi wake ni ubinafsi, kutokuwajibika, kulindana, utawala wa hofu,
kubebana na kuvumiliana kwa kadri ya kwamba wanufaikaji ni kikundi cha watu
wachache walio katika utawala na wale wanaohusiana nao kwa karibu.”
Kutokana na
mrengo huu wa fikra, wakati tunatafuta mchawi wa maendeleo yetu tusianze
kushughulika na mtu mmoja mmoja bali tuungalie mfumo huu. Kwa maneno mengine,
kiongozi yeyote atakayeingia kufanya kazi katika mfumo huu, hawezi kuleta
mabadiliko ya kweli.
Mrengo huu wa fikra kama unavyodadavuliwa na ndugu
Mwanakijiji unashawishi kwa kiasi kikubwa. Lakini bado unaibua changamoto
kadhaa za kifikra. Kwa mfano, je tumeshafanya udadisi wa kutosha kujua kuwa
mfumo huu ulianzia wapi na umeota mzizi lini nchini Tanzania? Je, mfumo huu
ulikuwepo hata wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere? Kwa ajili ya kuibua
mjadala zaidi, ningependa kusema bayana kuwa ubinafsi, kutowajibika, kulindana,
utawala wa hofu, na kubebana haukuzaliwa na Tanzania. Sidhani kama waasisi
wetu walikuwa na utamaduni huu!
Hii ina maana kuwa, na ningependa kumuaminisha na ndugu
Mwanakijiji, kuna uhusiano mkubwa kati ya uongozi na mfumo uliopo. Kwa mfano, katiba yetu imempa Rais wa nchi
madaraka makubwa sana. Katika kifungu
cha 36 (1) kwa kuzingatia katiba, Rais ana mamlaka ya kuanzisha au kuifuta
taasisi ambayo anaona itasaidia au kudhoofisha utendaji wa serikali yake. Kifungu cha 36 (2) kinampa Rais mamlaka ya
kufanya uteuzi wa viongozi waandamizi katika kuendesha taasisi mbalimbali
ikiwemo zinazohusika na utungwaji wa sera. Wakati huo tukumbuke kuwa Rais
anapoingia madarakani anaenda kutekeleza sera zake kama alivyopewa ridhaa na
wapiga kura ambazo kimsingi zinaweza zikashabihiana na mfumo uliopo au
zikaubomoa kabisa. Uanzishwaji au ufutwaji wa Taasisi pamoja na uteuzi ni
baadhi ya silaha muhimu anazoweza kuzitumia Rais kuleta mabadiliko ya kimfumo.
Kwa mujibu wa Mwanakijiji chama kilichopo madarakani ndio
chanzo cha kuendelea kwa mfumo huu dhalimu. Na kwa maoni yake, tunaweza kuondoa
mfumo huu kwa kuking’oa chama hiki madarakani na kutoa nafasi kwa vyama vingine. Kazi kubwa ya uchaguzi imekuwa kusaidia mabadiliko
haya katika nchi nyingi. Uingereza inatupa mfano mzuri, ambapo, ingawa wao
hawana katiba iliyoandikwa, lakini wamekuwa wakiuondoa utawala usiowafaa
kupitia uchaguzi kwa ufanisi mkubwa. Lakini, je kama tatizo ni mfumo na sio
viongozi, utasemaje ukikiondoa chama fulani utapata suluhisho? Hayawezi kutokea
kama ya Rais Frederick Chiluba wa Zambia?
Kwa maoni yangu,vita hivi vinapaswa kupiganwa kila kona. Mosi,
tunahitaji uwepo wa taasisi muhimu kikatiba. Tume ya Jaji Warioba walifanya
kazi nzuri sana kutengeneza mifumo ya kiuwajibikaji ambayo wachambuzi wengi
wanaziangalia kama chachu za kuondoa huu mfumo dhalimu. Hata hivyo, maswali
mengi yameulizwa kuhusu kukosekana kwa TAKUKURU katika Rasimu ya katiba.
Taasisi kama hizo zilitakiwa kupewa meno ili ziweze kudhibiti utamaduni huu wa rushwa
ndogo ndogo zinazowakosesha haki raia.
Pili, viongozi wanaochaguliwa wanapaswa kuwa wenye nia thabiti ya kuliendeleza taifa na wanaouchukia
mfumo huu dhalimu. Viongozi ambao watakuwa wasikivu wa kilio cha
wananchi na walio tayari kuleta mabadiliko katika jamii. Tatu, tunahitaji
kuweka misingi ya uwajibikaji katika sheria zetu. Sheria hizo zizingatie pia mazingira
ya kisiasa yanayoheshimu ushindani wa haki na zinazowajali wananchi kwa ujumla.
Hatuna budi pia kukubali kuwa sisi wenyewe kama raia wa
Tanzania ni kikwazo kikubwa cha kupambana na mfumo huu dhalimu. Tumekuwa tukishabikia
ufisadi bila aibu na pengine, kwa utamaduni wetu mbaya wa kuishi kiujanja
ujanja, tumekuwa tukihamasisha uvunjaji wa sheria ili kukidhi maslahi yetu
binafsi. Hivyo basi, nafasi ya wananchi ni kubwa sana katika kubomoa mfumo huu kwa
kuwa ndio wanaochagua viongozi na ndio wanaoweza kushinikiza uwepo wa taasisi
za kiuwajibikaji. Mjadala na kutokukubaliana kuhusu muundo wa muungano kisibeze
jitihada ya kuundoa mfumo huu dhalimu.











