Katiba Mpya: ‘Ukikimbia Nchale, Ukisimama
Nkuki’?
Kitanzi kilichokuwa kimeufunga mchakato wa kutunga
Katiba Mpya kinaonekana kimefunguliwa. Hii ni baada ya kile kinachoonekana kuwa
ni maridhiano kati ya Rais Kikwete na kinachojulikana kama Kituo cha Demokrasia Tanzania (TDC). Maamuzi hayo yanaonekana yatapelekea Katiba Mpya ipatikane
baada ya uchaguzi mkuu wa 2015.
Huu unaonekana kuwa ni ushindi mkubwa kwa unaojiita
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Pia inaonekana ni ushindi kwa wanaharakati
wanaopinga namna ambavyo Bunge Maalum la Katiba (BMK) limekuwa likiendeshwa kimburuzo
chini ya Mwenyekiti Sitta na jinsi ambavyo Rasimu ya Katiba Mpya
iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba (TMK) iliyokuwa ikiongozwa na
Jaji Warioba imekuwa ikichakachuliwa.
Swali la kujiuliza ni: Je, maelewano haya ya wanasiasa
kule kwenye Ikulu ndogo mjini Dodoma na yale ya pale Ikulu kubwa jijini Dar es
Salaam yana tofauti gani? Kama chanzo kimojawapo kikuu cha kuvurugika kwa
mchakato wa kupata Katiba Mpya, kama baadhi ya wachambuzi walivyosisitiza toka
awali, ni kumwachia Rais awe na madaraka makubwa katika uteuzi wa TMK na BMT
pamoja na kwenye kutiririsha mwelekeo wa mjadala wa kitaifa, nini kitabadilika
sasa? Maamuzi ya mchakato wa Katiba Mpya ambayo inatakiwa kutenganisha
miingiliano na madaraka ya mihimili mikuu mitatu ya dola – Bunge, Mahakama na
Serikali – yanapofanyika Ikulu tutegemee nini kipya?
Rais ajaye 2015 ndiye atakuwa hana uchu wa kuhodhi
madaraka hayo makubwa ya kusimamia mchakato wa kutunga Katiba Mpya? Nini
kitamzuia? Mabadiliko mapya ya Sheria ya Kutunga Katiba? Nani atayapitisha
mabadiliko hayo? Bunge hili hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT)
linaloendeshwa na Spika Makinda ambalo lina wabunge wengi kutoka chama tawala
ambacho kimechangia kwa kiasi kikubwa kuteka nyara mchakato kutoka kwa wananchi?
Au baada ya uchaguzi Bunge litakuwa tofauti?
Uchaguzi Mkuu huo wa 2015 bila Katiba Mpya utaendeshwa
na Tume ya Uchaguzi iliyoboreshwa na kuwa huru (zaidi) kwa sababu wanasiasa kutoka
vyama vya upinzani wamekutana Ikulu na kukubaliana na Rais aondokaye kuwa iwe
hivyo? Rais huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala ambacho kinataka
kushinda tena ndiye atahakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki? Ama
marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi katika Katiba ya sasa ya mwaka 1977 ndiyo
yatakuwa mwarobaini?
Chama tawala kina makundi/mitandao ya marais
watarajiwa ambao wengi wao wanataka kushinda mwakani. Wao na wapambe wao
(wakiwamo wabunge wanaowaunga mkono) wana nguvu/madaraka na maslahi gani katika
hili la kuboresha Katiba ya sasa? Kama moja ya sababu zilizopelekea vyama vya
upinzani kudai Katiba Mpya, hasa baada ya uchaguzi tete wa 2010, ni vipengele vyake
vinavyohusu Uchaguzi Mkuu, je, wagombea kutoka chama tawala wanataka mabadiliko
hayo yatakayowarahisishia kazi wapinzani?
Mtanziko wa Katiba bado upo japo kitanzi kimelegezwa
kwa muda. Kupata Katiba mpya kabla ya Uchaguzi wa 2015 ni jambo ambalo sasa
linaanza kukubalika kuwa si kwamba ni gumu tu bali haliwezekani. Lakini hii
haimaanishi tutapata tu Katiba Mpya baada ya Uchaguzi wa 2015 hasa kama
michakato ya kisheria ya maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Tume
ya Uchaguzi itakuwa inafanywa na taasisi zilizojaa wajumbe au wabunge wa chama
tawala ambao maslahi yao makubwa ni kushinda ubunge au urais.
Jenerali Ulimwengu alienda mbele zaidi na kuhitimisha
hivi: “Ni dhahiri, na ushahidi upo, kwamba chama-tawala hakikutaka tangu mwanzo, hakitaki sasa na wala hakitataka kamwe kuandika Katiba mpya. Kisa? Chama hicho na wakubwa wake wanaona Katiba iliyopo sasa inawafaa wao na maslahi yao. Si maslahi ya nchi, bali maslahi ya wakuu walio madarakani leo.” Hitimisho
lake, japo haliutendei haki uwezekano wa mtu au kitu chochote kile kubadilika, linatukumbusha
kuwa ni hatari sana kuwaachia wanasiasa, hasa walio watawala au wanaotaka kuwa
watawala wetu, wawe na madaraka makubwa katika kuendesha mchakato wa kupata
Katiba ya Wananchi. Hilo ni kosa kubwa tulilolifanya.
Lakini tunajua kosa kubwa zaidi ni kurudia kosa.
Tumeshaona zaidi ya mara moja sasa jinsi ambavyo mikutano ya sharbati/juisi
Ikulu inavyoleta maridhiano/maelewano ya kisiasa yanayopelekea mchakato wa
kutunga Katiba Mpya ufuate mielekeo ya wanasiasa. Sasa jukumu ni letu
kuhakikisha kuwa tunatumia fursa hii ya mtanziko huu wa Bunge la Katiba kurudisha
mchakato huo kwa wananchi – kwenye Bunge la Wananchi la Katiba.
Profesa Shivji alipoongelea ‘Dhana na Maana ya Bunge
la Katiba’ alilalama hivi kuhusu kupoteza fursa hiyo adimu: “Ndiyo
maana, wachache wetu tulipendekeza tuwe na Bunge Maalum la kuchaguliwa na
wananchi moja kwa moja. Lakini watawala wetu, pamoja na watawala watarajiwa na
wengi wa wanaharakati, katika busara zao na kwa maslahi yao, hawakutilia
maanani pendekezo letu. Tumepoteza nafasi ya kipekee ya kihistoria ya kuwa na
Bunge Maalum la kuchaguliwa, jambo ambalo limetufikisha hapa tuliko.”
Ndiyo. Tumegota. Ila hapo tulipojifikisha sio mwisho
wa ‘safari ya matumaini.’ Japo tukisimamisha mchakato huu ‘ni shida’ na
tukiendelea nao pia ‘ni shida,” mtanziko huo kwa kiasi fulani umetusaidia
wananchi kukifanya kile kile ambacho mwanazuoni huyo wa Ukatiba amekuwa akisisitiza
miaka nenda rudi kuwa ndiyo msingi mkuu wa utungaji wa Katiba ya kidemokrasia:
Majadiliano Mapana ya Kikatiba ya Kitaifa. Hakika kama tunachohitaji ni Katiba tu
iliyoandikwa vizuri tunaweza hata kuwakodisha wanasheria waliobobea watuandikie
kama washauri wataalamu. Lakini hicho sicho tunachohitaji.
Tunachohitaji ni mchakato wa kina wa kitaifa wa
kujenga mwafaka kati ya wananchi. Huo mwafaka wetu sisi wananchi wenyewe ni
moyo wa nchi. Utakuwa na uhalali kwetu na utakutambulisha kwetu. Tutauona
wetu. Tutauhisi wetu. Tutalinda chetu. Tutatetea chetu. Mwafaka huo kati ya
mwananchi na mwananchi ndiyo Katiba ya Wananchi.