“Jambo la tatu linawagusa wananchi kwa karibu sana. Ib. 107(2)(h) inaeleza kwamba miongoni mwa madaraka ya Bunge ni ‘kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusisha rasilimali na maliasili zinazosimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.’ Jambo hili ni jema kabisa na la kulifurahia, angalau mikataba hii izungumzwe Bungeni kwa uwazi badala ya wananchi kuambiwa kwamba ni siri ya kibiashara. Lakini, rasilimali na maliasili – ardhi, mafuta, madini, gesiasilia, maji, mapori, n.k. – sio jambo la Muungano. Rasilimali na maliasili ni chini ya mamlaka ya Washirika na wao ndio watayasimamia. Katika hali hii, Serikali ya Muungano itaingia kwenye mikataba ipi na kuhusu rasilimali gani? Ni mfano mwingine wa wananchi kulishwa maneno matamu yasiyo na uhalisia. Ni haki hewa” – Issa Shivji (2013), Ukurasa wa 24, Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha [Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]
“Baada ya kuisoma Rasimu kwa kina, mimi nadhani kwamba masharti mengi ya Rasimu na muundo wake mzima ni matokeo ya mivutano mikali katika Tume. Bahati mbaya hatuna mwenendo wa majadiliano ya Tume wala taarifa yao rasmi, hata taarifa ya awali. Lakini usomaji wangu wa awali unaniambia kwamba Rasimu hii ni maelewano kwa maana ya compromise, na sio mapatano, au mwafaka, kwa maana ya consensus. Nijieleze kidogo. Katika maelewano au compromise, pande zinazokinzana hatimaye zinakubali kwa shingo upande ili kutokwamisha maamuzi. Pande zote zinapata kidogo na kupoteza kidogo, na kila upande huwa na mkakati wake wa kupata zaidi katika duru ya pili. Kwa hivyo, maelewano kamwe hayawezi kuwa kwa moyo safi. Maelewano au compromise, yanazaa uamuzi legelege. Mapatano au consensus, kwa upande mwingine, ni maafikiano yanayofikiwa baada ya mjadala mrefu, kila mmoja akilenga kuthibitisha hoja yake na kwa njia hii kusadikisha wenzake kwamba hoja yake ni sahihi. Baada ya kufikia uamuzi wa mwafaka, kila mmoja anatoka akiwa ameridhika na amefurahi. Katika compromise, kila mmoja anatoka amenuna. Ni wazi kwamba huwezi ukapata mwafaka fastafasta. Lazima utachukua muda” – Issa Shivji (2013), Ukurasa wa 7-8, Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha [Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]
“Hitimisho langu juu ya muundo wa muungano ni kwamba, mosi, ni tegemezi na, pili, ni dhaifu kwa sababu umejengwa juu ya msingi wa mchanga wa dhamira na nia nzuri badala ya msingi wa mawe ya nguvu za kikatiba zilizowekwa na wananchi wenyewe. Ni kama kwamba suala la Muungano ni ujirani mwema badala ya umoja wa nchi” – Issa Shivji (2013), Ukurasa wa 19, Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha [Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]
“Nilisema kwamba ninavyodhani mimi, masharti mengi ya Rasimu yalikuwa maamuzi ya maelewano kwa maana ya compromise na sio mwafaka kwa maana ya consensus. Baada ya uchambuzi wangu, ninadiriki kusema kwamba muundo wenyewe wa serikali tatu uliopendekezwa ni compromise kati ya wale waliosimamia serikali mbili na wale waliopigania muungano wa mkataba, kwa maneno sahihi, kuuvunja muungano. Wanaserikali mbili waliona afadhali kuwa na Muungano, hata kama ni wa serikali tatu, badala ya kuuachia uvunjike; wakajifariji kwa matumaini ya dhamira ya wananchi na nia ya viongozi. Wana-mkataba wakaona kuwa kwa wakati huu wakubali serikali tatu wakijua fika kwamba muundo wa serikali tatu hautadumu na vyovyote vile utavunjika. Nilisema pia kwamba compromise inazaa uamuzi legelege. Compromise juu ya muundo, kwa maoni yangu, imezaa muundo wa muungano legelege. Kuna maeneo mengi nimechambua na kudhihirisha kwamba yatazaa migogoro ambayo hatimaye inaweza kuuvunja Muungano. Kero za Muungano zitaendelea, safari hii kutoka pande zote mbili. Muungano ukivunjika hakuna mwananchi atakayenusurika, awe wa Tanganyika au wa Zanzibar” – Issa Shivji (2013), Ukurasa wa 37-38, Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha [Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]
“Kwa maoni yangu, kama tungekuwa na mtazamo wa kidemokrasia tungeweza kubuni muundo ambao unakidhi matakwa ya pande zote mbili bila hatari ya kuuvunja Muungano. Mimi binafsi nimewahi kutoa pendekezo la muundo mbadala. Mara ya kwanza niliwasilisha pendekezo langu kwa Baraza la Wawakilishi […] miezi michache iliyopita. Kwa muhtasari, nilipendekeza dola kamili mbili, la Zanzibar na la Muungano. Bunge la Muungano litakuwa na mabaraza mawili, Baraza la Wananchi na Baraza la Nchi. Wajumbe wa Baraza la Wananchi watachaguliwa moja kwa moja na wananchi wa pande zote mbili kutoka majimboni. Baraza la Nchi litakuwa dogo lenye, tuseme kama wajumbe 30, 15 kutoka Bara na 15 kutoka Zanzibar wakichaguliwa na Bunge la Zanzibar na wabunge kutoka Bara katika Baraza la Wananchi ilimradi wasiwe wajumbe wa bunge lolote lile. Na nilipendekeza orodha tatu – moja ya mambo ya muungano, nyingine ya mambo ya kushirikiana (concurrent matters) na orodha ya tatu ni juu ya mambo ya pamoja (joint interest). Kutokana na muda siwezi kufafanua; nia yangu ni kudhihirisha kwamba muundo mbadala unawezekana” – Issa Shivji (2013), Ukurasa wa 40-41, Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha [Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]