
Ngo! Ngo! Ngo! ndo mlio ulonishtua. Kuinuka kwenda kutazama nani anagonga mlango nakuta ola. Kufungua nikatazama kulia kisha kushoto nisione mtu. Nikajiambia labda naota. Ile nafunga mlango tu, kutazama chini naona sinia (tray) la chakula kikiwemo kiboksi cha chakula, chupa ya maji na matunda.
Mara ndio ikanipiga kichwani kuwa hii ndio hali halisi ya maisha yangu kwa takriban siku kumi. Baada ya kutafakari nikajua ndio masharti yaliopo. Mpaka sasa najiuliza hizo mbio za hao wahudumu kama za ‘Usain Bolt’ ili tu tusionane ni za nini hasa.
Ni vijimambo tu ambavyo vinatokea unapofungiwa ndani ya hoteli baada ya kurejea nchini Uingereza. Na kwa bahati mbaya licha ya kwamba dunia nzima kukumbwa na mtihani mkubwa wa mlipuko wa Uviko-19(Covid-19), wengi walidhani kwa sasa janga hili lingekuwa lishapoa.
Sikutarajia kwamba mwaka huu bado nitakuja kuandika tena makala kuhusu ugonjwa huu, mwaka jana nikiongelea zaidi suala la kufungiwa nyumbani ‘lockdown’ nilipotoka likizo na kurejea Uingereza.
Safari hii napo nilikuwa likizo tena nchini Tanzania na takriban wiki tatu hadi nne ya likizo yangu, taifa hilo lilipoteza aliyekuwa Rais wake, hatua iliyonilazimu kukatiza likizo yangu na kurejea kazini kuripoti tukio hilo la kusikitisha kwa takriban wiki nzima. Muda wote huo nilijitahidi kuendelea kuvaa barakoa japo idadi kubwa ya watu nchini humo wala hawakushughulika kabisa kuvaa.
Tukirejea baada ya likizo kukamilika hapo kikaanza kizaazaa kingine cha kuandaa safari ambapo kwanza lazima upime kuhakikisha iwapo una Covid-19 au la. Kama kuna jambo linalolitia tafrani basi ni kupima. Haiumi ila inakirihisha kidogo, ukizingatia unachokonolewa puani. Hizo chafya nilizopiga baada ya hapo hazielezeki na gharama ya kupima si ndogo pia.
Mbali na hapo nchi ya Uingereza imeweka masharti ya abiria wanaoingia nchini humo lazima kukaa hotelini kwa siku 10. Si abiria wa nchi zote hukumbwa na haya, bali ni zile tu zilizo kwenye orodha iitwayo ‘Red List’ (listi nyekundu). Baadhi ya nchi za Afrika Mashariki na Kati zilizopo kwenye orodha hiyo ni pamoja na Tanzania, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burundi.
Orodha hiyo inaonesha nchi zote ambazo raia wake wakiwasili Uingereza wana wajibu wa kukaa hotelini huku wengine wakipaita ‘jela’. Mbali na hayo watu wanaoruhusiwa kuingia ni wenye uraia wa Uingereza, Ireland na wenye ukaazi pekee.
Matokeo niliyapata siku ya pili tu na ndo ikanilazimu kuingia hatua ya pili, kutafuta hoteli ya kwenda kujiweka ndani ambapo napo lazima ulipe pesa si ndogo. Cheti cha matokeo na uhakika wa kupata hoteli ni uthibitisho unaotakiwa kuwa nao na kuonesha uwanja wa ndege kabla ya kusafiri. Bila kuwa na nyaraka hizo za kuonyesha malipo na hoteli utakayokaa basi hiyo safari sahau.
Safari yangu kuelekea Uingereza ikaanza na kutokana na Covid-19 ndege chungu nzima zilizuiliwa kuingia nchini humo. Hivyo basi, ndege niliyokwenda nayo sikuweza kurejea nayo kwani kwa wakati huo tayari shirika hilo lilizuiwa kuingia. Nilijikuta nashuka kwa muda (‘transit’) katika nchi mbili tofauti na safari ikawa na saa nyingi kuliko ilivyo kawaida. Hata hivyo, nilipowasili tu kwa kutambua nimetoka nchi iliopo kwenye ‘Red List’ basi unapata wa kukusindikiza.
Msindikizaji huyo huhakikisha anakutia ndani ya basi maalum linalokupeleka hotelini. Kwa kifupi wanahakikisha hukimbii na unaenda wanapotaka ufike. Na hapo ndio siku zangu 10 ndani ya kifungo kilipoanza.
Amini usiamini hata mguu nje ya mlango huwezi kuutoa. Unaposhushiwa chakula nje ya mlango lazima uhakikishe jirani yako hafungui wakati mmoja na wewe. Lazima upime tena Covid-19 hata kama ulionesha cheti kuthibitisha huna ulipowasili. Na kipimo hichi huchukuliwa mara mbili, siku ya pili na ya nane wakati ukiwa ndani. Kipimo hicho kinahusu kuchokonoa pua na koo.
Maelezo yote ya namna ya kujipima huachiwa nje ya mlango wako kwani ni jukumu lako mwenyewe kisha nawe unaacha nje ambapo hupitiwa baadae wewe ukiwa ndani. Matokeo yako huyapata kupitia barua pepe. Uombe Mungu usikutwe nayo kwani ukikutwa nayo utaongezewa siku nyingine 10 hivyo utakaa siku 20 na si bure bali unalipa pesa tele.
Almuradi kukaa ndani si kazi rahisi hata kidogo. Binafsi nilikuwa ndani ikiwa mwezi mtukufu wa Ramadhan, unajitahidi kufanya ibada zote, unasoma, unatazama televisheni kidogo na bado muda wa kufturu unakuwa haujafika kwani Magharibi ilikuwa takriban kwenye saa mbili unusu hadi tatu usiku. Utajibabaisha weeee, ila wapi muda hauendi.
Asante teknolojia kwani chakula nacho unaagiza tu kupitia simu yako, cha asubuhi, mchana na cha jioni. Mungu bariki ilikuwa Ramadhan maana nadhani ningevimba, kwani kazi kubwa ingenikumba ni kula tu. Jambo moja ambalo lilikuwa likinichekesha ni licha ya kuwaambia nafunga, walishika kuniletea mlo asubuhi na mchana, huku ikinikumba kazi kila siku kuwapigia waje kuchukua chakula chao.
Najua unajiuliza usafi wa ndani ulikuwaje. Hapo ndio usiseme, kwa hali ya kawaida hoteli hubadilisha mashuka na kusafisha kila siku. Ila huu mpango maalum kutokana na Covid -19 ukawa tofauti. Hawaji kabisa kwani, kama nilivyosema awali, hata hao wahudumu kuwaona mtihani. Ila baada ya siku tano wanakuwekea mashuka mapya na mataulo masafi nje ya chumba chako, utapambana mwenyewe kutandika.
Kwa hakika kwa mtu ambaye hajakaa gerezani, huu mpango unakufundisha kukaa kizuizini kuna maana gani. Mbaya zaidi hakuna ruhusa ya kutoka na wala kupata mgeni. Nilipotoka niliheshimu zaidi uhuru wa kuweza kutamba ninavyotaka.
Haya yote yameletwa na Covid-19 na naendelea kuomba virusi hivi vituachie. Kwa sasa idadi kubwa ya watu Uingereza wamefanikiwa kupata chanjo. Kwa hiyo matumaini ni kuwa miezi ya hivi karibuni maisha yatarejea kama awali.
Kupiga chanjo hapa nchini Uingereza ni hiari. Halikadhalila mijadala mingi kuhusu faida na athari za chanjo inaendelea. Licha ya hayo, wataalam wengi wanazidi kushawishi na kuelimisha wakazi wa Uingereza umuhimu wake.
Nimefarijika sana kuona Kamati Maalum aliyoiunda Rais wa Tanzania kwa ajili ya kufanya tathmini ya COVID-19 imegusia kwa kina suala la chanjo. Wakati Serikali inatekeleza mapendekezo yake, tuendelee kujikinga na kuwakinga wapendwa wetu. Tuvae barakoa, tuoshe mikono na tuwatunze walio wazee ambao wako hatarini zaidi kuambukizwa.
Sote tukishirikiana tutaudhibiti vilivyo ugonjwa huu uliouweka dunia yetu kifungoni.
Makala nzuri.
Ilikuwa vigumu kuudhubiti ugonjwa katika mazingira ya kuukana uwepo wake hapa Tanzania. Angalau sasa, tunaelekea kuzuri.
Pole sana na hongera kwa kutuhabarisha habar tusizozifahamu
Asante kwa kutushirikisha. Pole
‘Zuhura Yunus aonja
maisha ya kizuizini’
‘Covid-19 yamfungulia
Zuhura
Yunus pazia la kizuizini’
‘Zuhura Yunus asimulia
magumu aliyopitia kizuizini’
Kitandawili cha Covid 19
Nimemsoma Zuhura ila nami nitataka kuyaeleza ynagu juu ya Covid.
Kwa kweli Ugonjwa huu mie ninauita umeleta Fitna na Umasikini mkubwa kwa watu. Fitna kwetu sisi ambao kwenye wimbi la mwanzo la Corona kina sisi kutokana na umri ulivyokuwa umesonga mbele na kujiamulia kubakia nyumbani wengine walitunanga na kunena kuwa Waoga n ahata Imani zetu za dini ni dhaifu, wengine wakatuambia tumelewa na fikra potofu za nchi za magharibi na kujazwa uwoga na kutojitambua na Uafrika wetu.
Umasikini ulizidi na kila mara kusikia simu kwa watu mbalimbali nisaidie hichi nisaidie kile. Mara nyengine inabidi uzime simu na uwambie aila yako akibisha mtu hodi mwambie sipo. Umasikini uliwapiga watu pale tishio kutoka nchi za magharibi kuwa wakazi wa Afrika watapukutika kama nzige. Ilibidi kuhakikisha tunakusanya vyakula kuweka majumbani mwetu kukhofia isije ikawa Fungate nasi ikatukumba (Lockdown). Katika kipindi matumizi yangu yalikwenda nje ya mpangilio wangu wa kawaida ulikuwa ni wakati huo na huku nikiwafikiria watu wa kawaida wale ambao ‘’Tonge mkononi, Tonge kinywani’’ sikuwa naelewa wakipambana vipi na maisha. Nazungumza kama Mzanzibari nikijiuliz amaeneo mengine yalikuwaje?
Nilifikia nukta sitaki kuingia kwenye Internet, Kutotizama TV na kuzima TV nakusema Corona inaweza kunipa Mshtuko wa moyo.
Kilichonisaidia pekee ni vitu viwili navyo vile vitabu nilivyovinunua nakutovisoma niliweza kuvimaliza kuvisoma aidha nilifanya mafunzo 3 ya Online nakujiwekea Shuruti za kuwasha Computer yangu kuchukua masomo kisha kuizima, kwahayo nilifaidika kabisa.
Sasa tunaambiwa ni wimbi la tatu bado Waafrika tunatishwa. Dooh, Ulimwengu umeingia kwenye mtihani, tokomea weye CORONA.