Mheshimiwa Rais, kwanza nianze kwa kusema, hakuna mtu yoyote mwenye akili zake timamu atakayeulaumu uongozi wako kwa kuleta ugonjwa wa korona. Sio kosa lako! Ugonjwa huu hauna mjanja, umetoka ulikotoka, na umeenea kila mahala. Naamini tusingeweza kuuzuia kuingia nchini na umefika. Ila utawala wako kwa hakika utapimwa na kuhukumiwa kwa jinsi ulivyoratibu na kupambana na janga hili la korona.

Mheshimiwa Rais, kama ujuavyo, sehemu ya utangulizi katika Katiba ya nchi yetu unaanza kwa kusema, “KWA KUWA SISI Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani….” Hivyo, naomba niitumie ‘dhati ya moyo wangu’ na haki ya kujieleza kikatiba, kuongea na wewe kwa amani kuhusu uhuru na udugu. Naamini kwa dhati kabisa utayasoma maelezo yangu kwa kuwa katiba yetu pia imesema, “Kwa hiyo, Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha-(a) kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa.”

Mheshimiwa Rais, juzi nilipofiliwa na binamu yangu na kuamua kusema hadharani, watu wa karibu waliniambia, “Mishy hongera kwa ujasiri”. Kweli tumefika mahala kusema ‘umefiwa kunahitaji ujasiri’? Wote tunajua kuwa kufiwa kunauma sana na kifo hakizoeleki, ila kupoteza ndugu yako katika mazingira ambayo kifo chake kingeweza kuepukika kunauma zaidi.

Mheshimiwa Rais, inapofikia hatua ya, kunyang’anywa haki yako ya kuombeleza, kulia na kufarijiwa, maumivu yake hayahimiliki. Ni kwa sababu hiyo, nakuandikia waraka huu. Ninauandika nikiwa na maumivu makali ya kupoteza mpendwa wangu.

Mheshimiwa Rais, sisi ni Watanzania, hatualikani misibani. Ukisikia msiba unaungana na wafiwa kwenda kuzika. Misiba sio siri, kufiwa sio aibu, na kusema umefiwa haijawahi kuwa dhambi. Kwa mila na tamaduni zetu, misiba imekuwa mahala pa kusafiana nia, kupeana faraja na kujenga udugu wa dhati – Waswahili husema, akufaae kwa dhiki ndio rafiki.

Mheshimiwa Rais, ila sasa, kusema kuwa umefiwa ni dhambi, ni kosa, ni kitendo cha kijasiri. Tumeona kwenye taarifa za video zisizothibitishwa watu wakizikwa usiku, kama wachawi maana kwa mila zetu kukaa makaburini usiku ni uchawi. Wanaonekana wakizikwa bila staha na heshima stahiki za kiimani.

Mheshimiwa Rais, tumefika hapa kwa sababu hotuba yako ya tarehe 22 mwezi wa nne iligusia kuwa taarifa zinazotolewa na serikali si sahihi, na kuna haja ya kutoa zaidi taarifa za wanaopona na sio wanaokufa ili kuzuia taharuki. Wahenga walinena, mficha maradhi kifo humuumbua, na hakika, vifo vinatuumbua. Ni ukweli usio na chembe ya wahaa, kuwa hatuwezi kutatua tatizo kwa aidha kulikana au kulidogosha. Dhahama hii ya korona ni kubwa mno, sio tu kwetu, kila mahali.

Mheshimiwa Rais, msiposema ukubwa wa tatizo, wananchi watatafuta upenyo wa pa kusemea kwa sababu madhila yanapozidi mioyo ya binadamu huota kutu. Tuambiane ukweli, hata unapokuwa mchungu. Ukweli utatuweka huru na utatuleta pamoja kufanya kila linalowezekana kutafuta suluhu ya kupambana na korona na madhara ya kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Rais, huu ni muda wa kuunganisha taifa. Mimi ni Mtanzania na najua sifa moja kubwa ya Utanzania ni umoja wetu hasa tunapopambana na adui. Hivi sasa adui yetu ni korona, na sio wahanga wa korona. Watanzania tuna kiu na hamasa ya kuongozwa kwenye mapambano ya kweli kuiangamiza korona, kwa sababu maisha ya kila Mtanzania yana thamani ya pekee.

Mheshimiwa Rais, sijawahi kumuona wala kumsikia angalau Mtanzania mmoja ambae hayuko tayari kuhahikikisha vita hii dhidi ya korona tunaishinda. Tena wana wa Tanzania tupo tayari kupambana bega kwa bega mchana kweupe. Ila inashangaza kuona nguvu kubwa ya dola ikitumika kupambana na Watanzania wenye hofu ya kupoteza maisha yao, kipatacho chao, au ndugu zao.

Mheshimiwa Rais, hofu haiondolewi kwa vitisho, mitutu na pingu, huondelewa kwa serikali kuonesha nia ya dhati na ya dhahiri katika kupambana na janga hili. Hofu huondelewa kwa faraja na upendo wa kidugu. Watanzania wanastahili kulala wakiamini na kujua kuwa viongozi wetu na serikali wanapambana kwa kila hali kwa ajili yetu na kuhakikisha tuko salama.

Mheshimiwa Rais, hatuhitaji katika kipindi hiki kuwa na hofu juu ya serikali na watawala. Hatuhitaji kupambana na watawala na vyombo vya dola. Tunataka kuelekeza nguvu zetu kupambana na korona. Ndio utu, udugu na wajibu wetu wa pamoja.

Mheshimiwa Rais, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne, ardhi, siasa safi, uongozi bora na watu. Hakuna mapato bila watu. Na hata yakiwepo, nini thamani ya utajiri mbele ya uhai? Nani amezikwa na mali? Ni nani atapanda flyover kama wote tukiteketea?

Mheshimiwa Rais, mimi si mchumi, ila nawajua maelfu ya Watanzania wenzangu ambao hawana namna ya kupata kipato kwa sababu ya janga hili na kufungwa kwa mipaka mingi ya kimataifa. Katika muktadha huo, naamini mapato ya nchi yataendelea kuporomoka siku hadi siku. Kukataa kufanya jitihada stahiki kwa kuhofia kupoteza mapato ni kuwaambia Watanzania kuwa maisha yenu hayana thamani, na ni kulikuza janga maana uzoefu unaonesha kuwa tusipojifungia, dunia itatufungia. Tumeona kwa macho yetu kilichotokea wakati wa janga la Ebola kwa majirani zetu.

Mheshimiwa Rais, rais mwenzio wa Ghana aliwahi kusema, tunajua jinsi ya kufufua uchumi, lakini hatujui jinsi ya kufufua waliofariki dunia, jambo ambalo ni kweli. Dunia haina uhaba wa wabobezi kwenye taaluma ya kufufua uchumi lakini hakuna ushahidi wa kisayansi au wa kimazingira kuwa tunaweza kufufua wafu. Najua kupoteza Watanzania, 10, 100, 1000, 10,000 au hata 100,000 kati ya Watanzania takribani milioni 60 inaweza isiwe shida kitakwimu. Ila familia hizo zinazoondokewa na wapendwa wao, hawatakuja kupata baba mwingine, mama mwingine au mpendwa yoyote mwingine wa kuziba pengo hilo. Akiondoka ndio kaondoka na hapo ndipo penye wajibu wa serikali kuhakikisha haki ya kuishi kwa kila Mtanzania inahifadhiwa.

Mheshimiwa Rais, kama ulivyosema, sio kwamba maradhi mengine yameacha kuua kwa sababu ya korona, hapana, bado yanaendelea kuua. Mbaya zaidi, janga hili linafanya hata wenye maradhi ya ‘kawaida’ kuogopwa. Unyanyapaa huu unafanywa ndani ya sekta ya afya. Kimsingi, hata vifo vya maradhi mengine vitaongezeka. Ukijumlisha na korona, uhai utateketea na jamii itatetereka.

Mheshimiwa Rais, najua kila anayenifahamu atakayesoma ujumbe huu, kwanza atahofia usalama wangu. Ila najua siku ile, tarehe 25 mwezi wa kumi mwaka 2015 nilipopanga foleni kupiga kura, nilipigia kura haki yangu ya kujieleza, kulindwa na kuhifadhiwa kwa mujibu wa katiba. Nilipigia kura ishara ya uzalendo wangu. Leo hii, hapa, naandika haya nikiwa bado ninaamini uzalendo wangu ni kusimamia maslahi mapana ya nchi yangu na kupambana kwa jasho na damu na adui yoyote atakayeishambulia nchi yangu. Korona ameishambulia familia yangu na anaitesa nchi yangu, kama hilo litanitia matatizoni, basi na iwe hivyo.

Mheshimiwa Rais, nimalize kwa kusema, uhodari wa nahodha hupimwa kwenye dhoruba. Tuko kwenye dhoruba kali. Watanzania wanapambana na madhila mengi mno, kiuchumi, kijamii, kiafya ya mwili na akili. Wanastahili, kuongozwa, kwa uhuru, haki, udugu na amani. Utu ni bora kuliko kitu.