Kingunge Kayafuata au Kayakimbia Mabadiliko?
Na Muhidin J. Shangwe
Siku ya tarehe 4 Oktoba itakumbukwa kwa mambo mawili katika siasa za Tanzania. Ni siku ambayo mwanasiasa machachari Mchungaji Christopher Mtikila alifariki dunia kwa ajali ya gari. Ni siku ambayo pia mwanasiasa mkongwe nchini, mzee Kingunge Ngombale Mwiru alitangaza rasmi kuachana na chama chake cha CCM. Ikumbukwe kwamba mkongwe huyu alikuwa akishikilia kadi namba 8 ya uanachama, kielelezo kwamba yeye ni mmoja wa wanachama wa kwanza kabisa wa chama hicho kilichozaliwa tarehe 5 Februari 1977 baada ya kuviunganisha vyama vya TANU na ASP.
Kuna uhusiano fulani wa kifo cha Mtikila na kujiondoa rasmi kwa Kingunge kutoka CCM. Katika duru za siasa za nchi hii, jina la Mtikila ni kisawe (maneno mawili yenye maana moja, kwa kimombo synonym) cha siasa za upinzani. Ndiyo, Mtikila anafahamika sana kwa upinzani wake dhidi ya CCM na serikali yake, kazi ambayo ameifanya tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza mwaka 1992 kupitia chama cha Democratic Party (DP) ambacho alikuwa mwenyekiti wake.
Kwa upande wa pili, ukongwe wa Kingunge katika siasa za nchi hii akiwa mwanachama wa CCM unafahamika kiasi cha kuzaliwa neno “kingunge” (ambayo ni sawa au karibia na neno‘guru’, kwa lugha ya kimombo). Imefikia mahali kama mtu ni mzoefu/mkongwe au mahiri katika jambo fulani, kitu ambacho aghalabu huendana na umri mkubwa wa mhusika, basi watu humuita Kingunge. Wakiwa wengi huitwa Vingunge!
Miongoni mwa vijana neno“kingunge” humaanisha uzee, na wakati mwingine ukaaji madarakani kwa muda mrefu. Msanii wa muziki wa Hip hop (wengine huita wa kufoka foka) Nikki Mbishi katika wimbo wake uitwao Sauti ya Jogoo anaghani, nanukuu: “Furaha kwa mwenye hela masikini hoi Mwaisela, viongozi ni wale wale Kingunge na Malecela”. Matumizi ya Kingunge kwenye mstari huu yanawakilisha viongozi wanaokaa madarakani muda mrefu, hasa kwa kuzingatia kwamba wakati wimbo huu ukitoka mwaka 2011wakongwe hawa (yeye na Malecela) walishamaliza ngwe yao ya uongozi serikalini. Aghalabu Kingunge hutajwa kwenye muktadha wa uzee/ukongwe/umahiri/ukaaji madarakani muda mrefu.
Msimamo wa Mtikila kabla ya mauti kumfika na kitendo cha Kingunge kukiacha rasmi chama chake ni matukio yenye kuonesha ukinzani wa urithi wa wawili hawa. Mtikila ambaye jina lake kwa wengine lina maana sawa na upinzani kama tulivyoona hapo awali amefariki huku akiamini kwamba mgombea wa CCM ndugu Magufuli ana “nafuu” kuliko mgombea mkuu wa upinzani, Bwana Lowassa. Katika mahojiano yake na kituo cha Televisheni cha Star TV hivi karibuni Mtikila alisikika na kuonekana akitumia vigezo mbali mbali ikiwemo afya ya wagombea. Alisema mgombea urais wa CHADEMA/UKAWA hawezi kupewa dhamana ya taifa la watu milioni 46 kutokana na hali yake ya kiafya kuwa dhoofu.
Kwa kauli hii tunaweza kuhitimisha kwamba Mtikila amefariki akiamini kwamba ni Magufuli, mgombea wa CCM, anayestahili kupewa dhamana ya nchi hii. Tunatambua uwepo wa wagombea wengine wa urais kutoka vyama vingine lakini ni dhahiri mchuano mkuu ni baina ya wawili hawa.
Huko nyuma, Mtikila aliwahi kumtuhumu mgombea huyo kwa ufisadi na akaahidi kuzunguka nchi nzima kutoa “tiba”, akimaanisha kwamba kitendo cha mgombea huyo kukubalika miongoni mwa watu ni ishara kwamba Watanzania “wanaumwa” na yeye ana tiba ya maradhi hayo. Kwa tafsiri ya msimamo huu wa Mtikila, “kumkata” Lowassa ilikua ni kumkataa fisadi.
Nimejaribu kuhusianisha msimamo wa Mchungaji Mtikila kabla ya kukumbwa na mauti na kujiondoa kwa Mzee Kingunge kama jaribio la kuelezea “mabadiliko” yanayotokea katika siasa zetu kuelekea uchaguzi mkuu. Jaribio hili limesukumwa na tukio la msiba wa Mchungaji uliotokea siku ambayo Mzee Kingunge alitangaza kuachana na CCM. Msimamo wa Mtikila wa “kumfagilia” Magufuli, mgombea wa chama tawala huku yeye mwenyewe akiwa nembo ya siasa za upinzani, na kitendo cha Mzee Kingunge kuachana na CCM baada ya zaidi ya miongo mitano ya uanachama na kuamua “kufagilia” upinzani yote mawili ni ishara ya “mabadiliko”.
Na hakika uchaguzi wa mwaka huu umetawaliwa na kubadilika badilika, au kwa lugha nyingine tunaweza kusema undumilakuwili. Wapo waliosema hawahami vyama vyao wamehama, wapo waliosema fulani akipitishwa watahama mwisho wakaishia kuhama tena kwa kumfuata “fulani” yule yule ambaye hakupitishwa kwenye chama chao kama walivyotaka! Lakini wapo waliopita nchi nzima wakisema fulani ni fisadi, nao “wamebadilika” sasa na wanamnadi kwamba ndiye mkombozi na kielelezo cha mabadiliko! Haya ni “mabadiliko” katika ubora wake!
Lakini lengo hasa la makala haya ni kujaribu kutafsiri uamuzi wa Mzee Kingunge kukikacha chama chake. Mzee Kingunge katoa sababu kadhaa lakini linalojitokeza wazi ni la Bwana Lowassa kukosa nafasi ya kugombea urais kupitia CCM.
Ni hili la “kukatwa” kwa Lowassa linalopamba uamuzi wa mzee Kingunge kuachana na CCM. Mzee Kingunge alianza kumuunga mkono Lowassa tangu wakati wa harakati za kugombea urais ndani ya CCM. Amekaririwa mara kadhaa akimnadi Lowassa kama mtu mwenye sifa ya “kutuvusha” hapa tulipo kama nchi. Amerudia tena ujumbe huu wakati akitangaza kujiondoa CCM majuzi. Hajaishia hapo, ameenda mbele zaidi na kudai kwamba yeye sasa anaunga mkono vuguvugu la mabadiliko huku akiishutumu CCM kwamba si tu haiwezi kubadilika bali imeishiwa pumzi!
Kauli hii ni tofauti na ile aliyoitoa Lowassa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid wakati akitangaza rasmi nia yake ya kuwania urais kupitia CCM, kauli ambayo bila shaka mzee Kingunge alikuwa akiiunga mkono. Lowassa alisema pamoja na kwamba nchi inahitaji mabadiliko, alikuwa akiamini kwamba mabadiliko hayo yanaweza kuletwa na kusimamiwa na CCM. Kitendo chake cha kuhama CCM baada ya “kukatwa” ni ishara kwamba aliamini mabadiliko hayo yangeletwa na yeye na si CCM. Kwa mujibu wa fikra ya namna hii, Lowassa = mabadiliko na mabadiliko = Lowassa.
Hata kibwagizo cha UKAWA cha “Mabadiliko-Lowassa, Lowassa-Mabadiliko” ni ushahidi mwingine wa dhana hii kwamba kama Mtikila alivyokuwa ni kisawe cha upinzani, Lowassa amegeuka ghafla kuwa kisawe cha mabadiliko. Hili la kumtukuza mtu kiasi cha kumlinganisha na dhana ya pana na kubwa ya mabadiliko lina hatari yake, lakini si dhumuni la makala haya kujikita huko. Mwandishi Mimi Mwanakijiji ameandika juu ya hili.
Mtiririko huu wa matukio unawataka wale waliokuwa wakiamini mabadiliko ndani ya CCM chini ya Lowassa yangewezekana na sasa wanamuunga mkono Lowassa akiwa upinzani huku wakimnanga Magufuli kwamba hawezi kuleta mabadiliko maana sasa eti wamegundua “tatizo ni mfumo” kufafanua mkanganyiko huo wa kimantiki(logic).
Ukifuatilia mwenendo wa Mzee Kingunge utagundua kwamba na yeye anaamini Lowassa ndiyo mabadiliko. Leo anaposema CCM imeishiwa pumzi, swali ni tangu lini? Alipomuunga mkono Lowassa katika Safari ya Matumaini ndani ya CCM miezi michache iliyopita chama hicho bado kilikuwa na pumzi?
Kama hakikuwa na pumzi, kwa nini hakutuambia Watanzania? Kama CCM ilikuwa na pumzi wakati ule, pumzi imekatika lini? Je, ni baada ya “kukatwa” Lowassa? Ina maana pumzi ya CCM ilikuwa Lowassa? Kama ndivyo basi hii ni hatari kwa taasisi kubwa ya hadhi ya CCM!
Maelezo ya Mzee Kingunge kwamba anahama kwa sababu mchakato wa kumpata mgombea wa urais ulivurugwa unaibua maswali hasa ukizingatia kwamba yapo ambayo yamevuruga chama kwa ujumla, achilia mbali zoezi (dogo?) la uteuzi wa mgombea urais. Hili la kuvurugwa mchakato wa uteuzi si mara ya kwanza. Mwaka 1995 tunaambiwa kama si mchakato “kuvurugwa” na hayati Mwalimu Nyerere, Lowassa angeibuka “kidedea” kutokana na kuungwa mkono na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama. Mzee Kingunge hakujiondoa.
Hata baada ya kundi la mtandao kushika hatamu ya chama chake mwaka 2005 na “kuvuruga” chama bado mzee Kingunge hakujitoa. Na hapa labda mzee Kingunge aulizwe swali, ni namna gani “uvurugaji” na ukiukwaji wa katiba ya CCM wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM kule Dodoma ni matokeo ya siasa za kundi la mtandao ambalo alilifumbia macho na hakujiuzulu wakati likifanya “vitu vyake” ndani ya chama chake akipendacho?
Ikumbukwe kwamba kundi hili linatajwa kama moja ya sababu zilizoifikisha CCM hapa ilipo kutokana na “rafu” walizocheza wanamtandao. Kitendo cha mzee Kingunge kujiondoa CCM sasa ni sababu tosha kuamini kwamba anaachana na CCM kwa sababu ya “kukatwa” kwa Lowassa. Hilo tu. Basi.
Lakini vipi upande wa yanayoitwa mabadiliko ambao Mzee Kingunge ametangaza kuunga mkono? Mchakato wa kumpata mgombea wake ulifanyika kwa demokrasia? La hasha, kama tutaamini maneno ya Dkt. Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA ambaye amejiuzulu si tu nafasi yake hiyo bali siasa kwa ujumla kutokana na mchakato huo. Kwa mujibu wa Tundu Lissu, CHADEMA tayari ilishamteua Dkt. Slaa kuwa mgombea urais tangu mwezi Januari mwaka huu. Tunaambiwa kwamba Slaa aliandaliwa mpaka namna ya kuvaa kama Rais!
Kitendo cha “kumtosa” Slaa na kumkumbatia mgeni Lowassa hata kumpa jukumu la kupeperusha bendera ya chama kinaelezwa kwa ufasaha na maneno ya mwenyekiti wa CHADEMA Bwana Freeman Mbowe. Mbowe ameelezea kwa kauli yake kwamba kitendo hicho ni “kubadili gia angani”. Kauli hii pekee inaashiria udharura na uhitaji mkubwa (desperation), vitu ambavyo ni nadra kuendana na mahitaji ya demokrasia.
Vilevile Kitendo cha Mzee Kingunge kuikacha CCM kwa kile anachoita kusaka/kuunga mkono mabadiliko kunaibua upya mjadala wa dhana hii ambayo imetawala siasa kuelekea uchaguzi mkuu. Pande mbili kubwa zinazovutana, CCM na UKAWA, zote zinaimba kibwagizo cha mabadiliko. Kibwagizo hiki kimekuwa maarufu na kimejenga imani miongoni mwa Watanzania kiasi kwamba baadhi ya watu wanaamini nchi hii haitakuwa tena kama zamani, bila kujali nani atashinda uchaguzi. Kwamba ama Magufuli au Lowassa, mabadiliko ni lazima.
Awali ilionekana kwamba ajenda hii ni ya wapinzani, kabla ya CCM kugundua kwamba nao wanahitaji kuibeba ili waeleweke katika masikio na macho ya Watanzania. Punde Movement for Change (M4C), kampeni ya CHADEMA iliyoanzishwa miaka mitatu iliyopita “ikahodhiwa” na mgombea wa CCM aliyebadili maana yake na kuiita Magufuli for Change. Katika moja ya matangazo ya televisheni ya mgombea huyo wa CCM lipo tangazo linalomalizika kwa maandishi “Magufuli, mabadiliko yanakuja”. Mpaka sasa kumekuwa na vita juu ya uhodhi wa ajenda ya mabadiliko kiasi cha kuripotiwa kwamba CHADEMA wamefungua kesi kumshitaki Magufuli kwa “kuiba” kaulimbiu ya M4C!
Swali ambalo wengine wamekuwa wakijiuliza ni kwa namna gani “wagomvi” hawa wao wanyewe wanayaishi mabadiliko. Naam, wao wamebadilika kiasi gani hata watuhubirie mabadiliko? Ni dhahiri wamebadilika ingawa tafakuri tunduizi itahoji ni namna gani kubadilika huko kunaendana na mahitaji na maslahi mapana ya jamii ya Kitanzania.
Kwa UKAWA, kukosekana kwa sura za wanasiasa nguli wa kambi ya upinzani kwa maana ya Dkt. Slaa na Prof. Lipumba tayari ilitosha kuwa ishara ya mabadiliko. Kwamba sasa upinzani unaongozwa na makada maarufu na wakongwe wa CCM, mawaziri wakuu wawili (mmoja mstaafu mwingine aliyejiuzulu) ni mabadiliko!
Sina hakika mambo mengine yanayohusu uendeshaji wa vyama vya upinzani yameboreka kwa kiasi gani, hasa kwa yale ambayo kwayo vimekuwa vikiituhumu CCM. Ni namna gani vyama hivi, kwa mfano, vinaendeshwa kwa misingi ya utu, utaifa, haki, uadilifu, na misingi ya utawala bora na demokrasia? Ni namna gani sauti zinazokinzana na viongozi wa vyama zinasikilizwa? Majibu ya maswali haya yanahitaji makala nyingine.
Lakini isemwe tu kwamba kumekuwa na malalamiko juu ya namna vyama hivi vinavyoendeshwa, achilia mbali upatikanaji/uteuzi wa viongozi wake. Kwa CHADEMA, mifano ya namna makada wake wa zamani ndugu Zitto Kabwe na wenzie na hivi karibuni Dkt. Slaa “walivyoshughulikiwa” inaweza kutupa taswira ya yanayoendelea ndani ya chama hivyo kikuu cha upinzani. Kuna malalamiko kama hayo kwa chama cha CUF na vingine.
Kwa upande CCM, pengine kwa shinikizo kubwa kutokana na ukweli kwamba wako madarakani, wamejikuta wakilazimika kujionesha kwamba wame/wanabadilika, jukumu ambalo pengine wapinzani hawana. Hali hii ya kuichunguza sana CCM imevifanya vyama vya upinzani kukwepa jicho kali la wadadisi wa mambo na hivyo ubaya wao kutoonekana sana (slip under the radar). Hii ni bahati mbaya maana vyama vya upinzani vilitakiwa vijitofautishe na CCM kisera na namna ya uendeshaji wa taasisi ya chama cha siasa na macho ya wadadisi yavitazame na kuvihoji kwa yale watendayo.
Vyama vya upinzani vinatakiwa vijiendeshe kwa namna ambayo itajenga imani kwa wananchi kwamba wanastahili dhamana ya kupewa nchi. Kinyume na hili ni kutegemea kukata tamaa kwa wananchi kwa chama tawala ili kupata uungwaji mkono. Hili linaweza “kufanikiwa” kiasi kwamba likafanikisha malengo ya muda mfupi ya kuitoa CCM madarakani. Lakini kamwe haiwezi kuwa ndiyo mkakati wa muda mrefu kwa uhai na ustawi wa vyama husika.
Tangu CCM walipotangaza kampeni ya kujivua gamba miaka kadhaa iliyopita, wameonekana au walau wanataka waonekane kwamba wame/wanabadilika. Tumeshuhudia Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana akizunguka nchi nzima kukutana na wana CCM huku akihubiri falsafa ya kujivua gamba ambapo kwa nyakati tofauti ilimlazimu hata kukemea mawaziri “mizigo”. Kinana amesikika akisema wala rushwa, mafisadi, wazembe, walanguzi CCM si mahali pake na kuwataka waondoke. Amesikika pia akiahidi chama kitachukua hatua kali kwa makada wake wazembe ambao wameshika nafasi za uongozi serikalini.
Kinana pia ameonekana katika picha za mnato na video akijichanganya na “walalahoi” wa nchi hii. Zipo picha anaonekana akifyatua matofali na kuchanganya zege, akilima kwa jembe la mkono na kupanda mbegu, na hata akining’inia baada ya kudandia behewa la treni!
Tafsiri ya taswira hizi ni kuonesha dhamira ya chama kubadilika kwa kukirejesha kwa wenyewe, wakulima na wafanyakazi. Harakati hizi zilifikia kilele kwa “kumkata” Lowassa, mtu ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa nembo ya ufisadi, walau kwa mujibu wa tuhuma ambazo zimekuwa zikitolewa na wapinzani.
Ni katika muktadha huu, kwa wengine, kitendo cha kumkata Lowassa kimechukuliwa kama ishara ya uthubutu na ujasiri kwa upande wa CCM. Na hakika huo ndiyo ukweli. Ni dhahiri kwamba CCM walitegemea (anticipate) dhoruba itakayoambatana na “kukatwa” kwa Lowassa. Kitendo cha kujua matokeo yake lakini bado wakachukua uamuzi wa “kumkata” ni ujasiri wa kitaasisi ambao unategemewa kwa chama kikubwa na kikongwe kama CCM.
Hata hivyo, kwa wengine kama mzee Kingunge mchakato wa kumkata Lowassa ulifanyika kwa kukiuka Katiba ya Chama, hoja inayotiwa nguvu na kitendo cha baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM kutoka nje ya mkutano wakilalamikia “rafu” iliyokuwa ikichezwa. Kwa maneno ya Lowassa mwenyewe, mchakato huo ulikuwa ni “ubakaji” wa demokrasia.
Vyovyote vile, matokeo ya mchakato huo ni kupatikana kwa John Pombe Magufuli, mgombea urais ambaye CCM inamnadi kwamba ni mwadilifu, mchapakazi, na kama ambavyo kada maarufu wa CCM Mwigulu Nchemba hupenda kumzungumzia, mtu ambaye si “mpiga dili”. Tayari Magufuli ameanza kujigamba kwamba wabaya ndani ya CCM wanamkimbia. Anawananga wanaokimbia chama chake kwamba ni mafisadi ambao ameahidi “kulala nao mbele” na kuwashugulikia kwa “upole” kama atapata ridhaa ya kuwa rais.
Je, Mzee Kingunge anayakimbia mabadiliko haya na kuamua kupanda basi la mabadiliko la UKAWA ambalo dereva na kondakta wake ni makada wakongwe wa CCM, mawaziri wakuu wa zamani Fredrick Sumaye na Edward Lowassa? Ni kambi ipi kati ya hizi inawakilisha mabadiliko yanayoendana na mahitaji ya maslahi mapana ya Watanzania?
Yapo maswali mtu anaweza kutolea majibu papo hapo, yapo mengine yanatutaka kusubiri ili historia ije ihukumu. Lakini bado tunalazimika kutoa majibu ya sasa, kwa ushahidi uliopo sasa. Kwa upande wa CCM, ni lazima isemwe kwamba kuna dalili za kubadilika kuondokana na mtindo wa kufanya mambo kwa mazoea (business as usual). Dalili zipo. Lakini kazi kubwa iko mbele yao, wala si walichofanya huko nyuma, au kile kinachofanyika sasa.
Dhamira ya CCM kubadilika itapimwa baada ya uchaguzi, na hasa kama watashinda. Shinikizo la mabadiliko ni kubwa zaidi kwa CCM hasa ukizingatia “madudu” ambayo wameyafanya kwa miaka mingi sasa. Mimi si katika wale wanaosema CCM haijafanya kitu tangu Uhuru. Haiwezekani kuwa na chama chenye urithi (legacy) mkubwa ndani na nje ya mipaka ya nchi kama CCM halafu mtu aseme chama hicho hakijafanya kitu. Haiwezekani. Kama Mtanzania natambua yale ambayo nchi yetu, chini ya utawala wa CCM imefanikiwa. Na najivunia mafanikio yake. Si sahihi hata kidogo kubeza mafanikio hayo kwa sababu tu ya mahitaji yetu ya sasa.
Lakini ni dhahiri yapo “madudu” yaliyofanyika ambayo kama yasingefanyika nchi hii ingekuwa mbali zaidi kwa maendeleo. Kuna kujisahau/kubweteka ndani ya CCM na hivyo hasira na kelele za wananchi wanaopinga uwepo wake sasa zinaeleweka. Na wao wanalitambua hili, au tuseme wanaonekana kulitambua. Huhitaji kwenda mbali kufahamu hiki niandikacho, wewe msikilize Kinana kisha malizia na Magufuli.
Hata hivyo, pamoja na kuahidi mabadiliko hasa kupitia Magufuli, bado unapata hisia kwamba CCM hawatuelezi kwa kinaga ubaga walikosea wapi. Pamoja na kampeni ya “kujivua gamba”, bado watu wangependa kusikia zaidi kutoka kinywani mwa makada na wagombea wake wakikiri wazi kabisa, hadharani, ni wapi walikosea. Kwa sasa hili linafanyika kwa mtindo wa kutoa lawama kwa wale wanaoshutumiwa kuvuruga chama. Naungana na mwandishi mahiri Evarist Chahali anayewataka CCM watueleze Watanzania wapi ilipokosea.
Kwa upande mwingine imekuwa vigumu kuelewa mabadiliko yanayohubiriwa na UKAWA, hasa kwa kuzingatia sura ambayo umoja huo wa vyama vya upinzani umejivisha hivi karibuni. Mpaka sasa, ukiacha ushabiki na mhemko wa kisiasa, UKAWA hawajaweza kuwajengea wananchi imani kwa hoja ni kwa jinsi gani wanawakilisha mabadiliko. Tayari Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA Ndugu Tundu Lissu amekiri kwamba wamempokea Lowassa si kwa sababu ni mwanasiasa msafi (msisitizo ni wangu), la hasha, bali kwa sababu tu wanataka kumtumia kuleta “mabadiliko”.
Kwa maneno mengine, ni mabadiliko ambayo yanaletwa na wanasiasa ambao si wasafi lakini tutarajie siasa safi (na wao kuwa wasafi) wakishaingia madarakani! Na kama nia ya CHADEMA chini ya UKAWA ni kumtumia Lowassa, yeye naye ni lazima atakuwa na lengo lake la “kuwatumia” kufanikisha azma yake. Nitaacha wasomaji wajiulize ni azma gani. Jibu lolote laweza kuwa sahihi.
Ukiacha hayo, haieleweki kama umoja huo bado unasimamia lengo kuu la kuanzishwa kwake ambalo ni kupatikana katiba ya wananchi kama jina lake linavyosadiki. Na kama jibu ni ndiyo, ni namna gani zoezi hilo linaweza kusimamiwa na mtu ambaye alishiriki moja kwa moja kukwamisha katiba-pendekezwa ya Jaji Warioba jambo lililopelekea kuzaliwa UKAWA?
Kwa nini watu wasiamini kwamba waliopewa dhamana ya kuongoza mabadiliko ya UKAWA ni CCM B kama alivyosema rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi? Na kama watu hao ni CCM B, kuna haja gani ya kuchagua photocopy wakati original ipo? Kwa maneno mengine kwa nini kuandikia mate na wino ungalipo?
Mzee Kingunge amesikika akisema kwamba ni wakati wa watu wapya na fikra mpya kuongoza nchi. Ni kwa kiasi gani mtu aliyekabidhiwa dhamana ya kuongoza mabadiliko, Bwana Lowassa, ni mpya? Ni fikra gani mpya anazowakilisha? Ni kwa kiasi gani waziri mkuu mstaafu Bwana Sumaye ni mpya? Ni fikra gani mpya anazowakilisha? Yako wapi mabadiliko?
Maswali haya hayawezi kujibiwa kwa majibu rahisi ya kwamba eti lengo ni kuitoa CCM kisha mengine tutajua “mbele kwa mbele”. Na ni muhimu pia kutambua kwamba mabadiliko yenye tija kwa watanzania hayapimwi kwa kushinda uchaguzi. Kwamba mradi fulani kashinda tu basi ni ishara ya kuwepo/kutokuwepo mabadiliko.
Ni dhahiri kwamba yapo mengi ambayo ni vigumu kuyatolea ufafanuzi sasa lakini matokeo ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba yatatusaidia kupata majibu ya baadhi ya maswali yetu. Dkt. Slaa alihoji kama Lowassa ni rasilimali (asset) au kikwazo/mzigo (liability). Mimi nahoji je, Kingunge kayafuata au kayakimbia mabadiliko?
Tusubiri.