KIOO CHA TRUMP HAKIDANGANYI!

Muhidin J. Shangwe

Watanzania kama walivyo watu wengine duniani tumefuatilia uchaguzi wa Marekani ambao umemalizika kwa mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump, kumshinda mpinzani wake Hillary Clinton wa chama cha Democrats. Shauku na wajibu wa kufuatilia uchaguzi wa Marekani hutokana na sababu kadhaa, lakini kubwa ni kwamba utawala wa Marekani una athari kwa dunia nzima. Kwa mfano, mara tu baada ya Trump kutanganzwa mshindi tayari kuna hofu juu ya hatima ya Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris ambao umeungwa mkono na mataifa makubwa ikiwemo Marekani. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema lau kama Watanzania tungekuwa na nafasi ya kupiga kura Marekani basi tungeichangamkia kwa sababu matokeo yake yana athari kwetu! 

Lakini kuna sababu nyingine. Marekani ni taifa kubwa na la kupigiwa mfano katika nyanja mbali mbali hasa maendeleo ya kiuchumi, kijeshi, kisayansi na kiteknolojia. Marekani pia hupigiwa mfano kwa mfumo wake wa kidemokrasia ambao unaonekana umejengwa katika misingi ya haki na uhuru wa raia wake. Ni kwa sababu hizi, na nyinginezo, nguvu-laini (soft power) ya taifa hili ni kubwa. Nguvu-laini ni uwezo wa nchi fulani kuvutia nchi nyingine kwa sababu tu mifumo yake ya kisiasa, mienendo yake ndani na nje, na utamaduni wake huwafanya watu na serikali za mataifa mengine kuvutiwa hata kuwa tayari kuyafanya yale ambayo yanainufaisha nchi hiyo – wakati mwingine bila hata kuombwa kufanya hivyo! Nguvu-laini hii ni tofauti na nguvu-ngumu (hard power) ambayo ni matumizi ya nguvu za kijeshi au uchumi kufikia malengo – kwa maana ya kushurutisha wengine wakubaliane nawe hata kama hawapendi. 

Marekani ina vyote, nguvu-laini na nguvu-ngumu, hivyo basi, tunalazimika kufuatilia kinachojiri maana taifa hili ni kama “tembo ndani ya chumba” (elephant in the room) – huwezi kujifanya eti humuoni! Na kama kawaida, panapo washindani wawili basi “mashabiki” hugawanyika katika kambi mbili. Kinachofuata ni “ligi” isiyo rasmi kati ya “timu” mbili: kwa muktadha huu, ni Timu Trump v Timu Clinton. Hata kwa wale ambao ni neutral, kwa maana ya kutounga mkono upande wowote, kiuhalisia na kiubinadamu, hujikuta moyoni wakiunga mkono moja ya pande mbili. Kwa wale wenye “timu” wakati mwingine si kwamba wanavutiwa sana na mgombea mmoja bali wanaogopa zaidi matokeo ya mgombea mwingine kushinda. 

Ni kweli kwamba kampeni za uchaguzi wa Marekani mwaka huu zimekuwa ni kioja kifananacho na vipindi vya televisheni vyenye mzaha mzaha. Mapungufu ya wagombea wawili, Clinton na Trump, yameifanya Marekani kudharaulika kwa kiasi fulani na pengine kupoteza sehemu ya nguvu-laini yake duniani. Na kwamba sasa Trump ameshinda uchaguzi huo ni kioja kikubwa zaidi. Hapa China, Trump amekuwa akitumika kama kielelezo cha udhaifu wa mfumo wa demokrasia. Kwamba unawezaje kuwa na mfumo unaoruhusu mtu wa aina ya Trump kuwa mgombea wa urais, achilia mbali kushinda na kuwa rais? Swali hili naamini linaulizwa kwingineko duniani. 

Sababu za kuunga mkono “timu” moja hutofautiana. Siku mbili kabla ya uchaguzi nikiwa katika mkahawa wa chuoni kwangu kijana mmoja wa kizungu kutoka Canada alikuja kukaa nami meza moja. Tunafahamiana. Ni kijana mdogo tu wa miaka 21. Katika mazungumzo aliniuliza kuhusu uchaguzi wa Marekani na kama ninafuatilia yanayojiri. Nilimueleza kwamba, naam, nafuatilia. Kisha akaniuliza kuhusu Trump. “Unamuonaje?” Nikamjibu juu juu kwamba, he is not presidential, nikiwa na maana kwamba hana sifa za kuwa rais. Kisha nikamuuliza yeye swali hilo hilo, akasema yeye anataka Trump ashinde. Nilipohoji kwa nini akasema anampenda Trump kwa sababu “he does not give a f**k!” Hapa alikuwa anamaanisha kwamba Trump hajali!

Katika mazungumzo yetu pia aligusia hulka ya kutojali waliyo nayo watu wa Magharibi ya Mbali, akimaanisha Canada na Marekani. Akasema amejifunza mambo mengi tangu aje China, kwamba, kumbe dunia ni kubwa! Akasisitiza kwao dunia ni Canada na Marekani! 

Baada ya jibu hilo nikaona kuna umuhimu wa kumueleza kwa nini niliona Trump hafai kuwa rais. Nilimweleza kwamba kwanza kabisa ameonesha ni mtu asiye na ufahamu wa mambo mengi ya kisera kupitia mijadala mbali mbali aliyoshiriki. Ni mtu wa kusema jambo lakini hana mkakati wa kufanya jambo hilo, na wakati mwingine akibanwa hukimbilia kusema hiyo ni siri yake. Lakini kingine ni yale ambayo yalitoka kinywani mwake. Ni kauli nyingi za kuudhi na ukosefu wa heshima dhidi ya wanawake, watu wa mbari tofauti na wazungu, Waislam na hata watu wa tabaka la chini. Mawazo yake juu ya wahamiaji yanachefua, na ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico ni wazo la kijuha! Ukuta ni alama ya utengano. Zipo kuta zisizoonekana kama ubaguzi wa rangi, kitabaka na kadhalika. Lakini ukuta huu wa Trump utaonekana, ukitaka kuushika utaushika. Kweli ni mtu asiyejali! 

Tukaishia hapo. 

Uchaguzi umefanyika. Toba! Donald Trump ndiye Rais-Mteule wa Marekani sasa. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Van Jones, kutoka Shirika la Habari la CNN kwa usahihi kabisa anasema ushindi wa Trump hautokani na sababu moja. Zipo sababu za kiuchumi zitokanazo na kushindwa kwa mradi wa utandawazi, kitu ambacho kimewafanya watu wengi kukosa ajira na maisha kuwa magumu kwa ujumla. Wengine wamesema imetokana na wanasiasa wa Washington kushindwa kutimiza wajibu wao. Watu wamechoka. Wana hasira. Wameamua kutuma ujumbe kwa kumchagua mtu ambaye si mwanasiasa. Lakini kwa sababu Marekani ni jamii ya kimbari, suala la ubaguzi wa kimbari pia limetajwa. Imesemwa sasa wazungu wameamua kuchukua nchi yao! 

Isemwe pia kwamba kampeni ya Trump imeamsha hisia kali za utaifa wa Kimarekani ambao pia umechangia hisia za kibaguzi dhidi ya “wakuja” au kwa lugha nyingine wahamiaji. Vikundi vidogo vya kibaguzi vinavyojiita vya kizalendo vimepata nguvu kubwa wakati huu, shukrani kwa Trump ambaye amewaahidi “kuwarudishia nchi yao.” Moja ya vikundi hivi ni kile cha “Asimilia Tatu” ambacho kinaamini ni asilimia 3 tu ya Wamarekani wa sasa ndiyo damu yao ilishiriki vita vya ukombozi dhidi ya utawala wa Waingereza. Maana yake hao ndiyo “Wamarekani zaidi.” Wafuasi wa “Asilimia Tatu” wamekuwa wakifanya mazoezi ya kivita kuwa kutumia silaha nzito wakijiandaa kwa lolote ikiwemo kile kilichodaiwa na Trump kwamba kuna njama za yeye kuibiwa kura! 

Na Trump hajawaangusha watu wa aina ya Asilimia Tatu. Alitangaza siku ya uchaguzi kama siku ya uhuru wa Marekani, na wao wakaitika “we are taking our country back!” (tunairudisha nchi yetu mikononi mwetu!). 

Kaulimbiu kuu ya kampeni ya Trump ilikuwa kuirudisha Marekani katika hadhi yake ya ukuu (Make America Great Again!). Yapo maswali: Ni lini Marekani ilikuwa na ukuu? Kama ni miaka 30-50 iliyopita, nini ilikuwa hadhi ya watu wa makundi mbali mbali katika jamii ya Marekani kama vile wanawake na watu weusi? Je, kuifanya Marekani kuwa kuu tena kuna tafsiri gani kwa makundi haya na yale ya kihafidhina na kibaguzi? Maswali haya yatapata majibu kadiri muda unavyokwenda. 

Ushindi wa Trump umepokelewa kwa hisia tofauti na Watanzania. Wako waliofurahi na wako waliofurahi kupindukia! Hali kadhalika wapo waliofedheheshwa. Mimi ni mmoja wa waliofedheheka. Nimetaja sababu za maana ya uchaguzi wa Marekani kwa dunia. Baadhi yetu tuliamini taifa hili ambalo linaonekana limejengwa kwa misingi ya uanuwai (diversity), misingi ambayo imepata nguvu miaka ya karibuni kwa kumchagua Rais mwenye asili ya Afrika, watu wake wasingechagua mtu ambaye misimamo yake inaenda kinyume na uanuwai huo. Ni mtu ambaye aghalabu ametoa kauli zenye chembe chembe za kibaguzi, kejeli, dharau, ubabe, na mwenye kauli za kunyanyasa kijinsia. Lakini ah! Tulikosea. Wengine wametafsiri hatua kama hatua moja nyuma kwa nchi ambayo ilikuwa inaelekea kwenye mabadiliko makubwa ya kijamii. 

Baada ya ushindi wa Trump nimeanza kuwaza kuhusu Watanzania ambao wanamshabikia Trump. Je, kwa sababu ni mtu asiyejali? Ni kwa sababu wanapenda “sera” zake za kujenga ukuta kutenganisha Marekani na Mexico? Au ni kwa kudhibiti uhamiaji wa Waislam kuingia Marekani? Au wanasuuzwa moyo na kauli na mienendo yake ya kidume dume dhidi ya wanawake? Katika jamii yenye hulka za mfumo-dume, hii ni sababu ya kuvutia sana! Au ni ubabe na dhihaka dhidi ya watu wenye ulemavu? Au sasa wanaamini sera ya Marekani kwa Afrika na dunia itakuwa ya manufaa? 

Moja kati ya majibu niliyopata ni kwamba Trump “atatunyoosha” Waafrika! Ati wale viongozi wababe wa Kiafrika sasa wamepata kiboko yao na watakiona! Kumekuwa na kauli zinasombaa katika mitandao ya kijamii kwa muda mrefu sasa zikidaiwa kutoka kwa Trump, ikiwemo ile ya kwamba Waafrika ni wavivu, hawajiwezi na hivyo wanatakiwa kutawaliwa tena! Niseme kwamba sijawahi kuamini kauli hizi kwa sababu, pamoja na uzito wake, sijawahi kuziona zimeripotiwa na chanzo cha uhakika zaidi ya vyanzo vya kidaku. Kwamba Trump labda hakutoa kauli hizi lakini amesuuza waumini wa sababu hii ni kilelezo kingine cha matatizo tuliyonayo katika uwezo wetu wa kuchambua mambo! 

Lakini wapo wanaosema wanavutiwa na msimamo wa Trump na chama chake cha Republican kupinga masuala kama ya utoaji mimba na ndoa za jinsia moja. Hoja hii ya kihafidhina inasemwa kwamba ni miongoni mwa sababu zilizompa ushindi Trump baada ya kuvutia kura za waumini wa makanisa ya Kiinjili (Evangelicals). Pia kuna kundi la watu ambao “hawana habari,” wao wanampenda Trump kwa sababu tu ni wa chama pinzani na wao ni wafuasi wa vyama vya upinzani kwetu! Na wako pia wanaodai kwamba ni jambo zuri Trump kushinda kwa sababu unafiki na ujinga wa Wamarekani sasa utaonekana! Katika muda na sehemu tofauti, nami pia nimwahi kutamka sababu hii lakini si kama sababu ya msingi kumuunga mkono Trump bali kama namna ya “kufuta machozi” iwapo angeshinda. 

Ni wazi sasa kupitia Trump na mapokeo ya ushindi wake tunaweza kuona taswira yetu – ya kwamba sisi ni watu wa aina gani na tunaamini katika misingi ipi. Nihitimishe kwa kusema kwamba, kwa kupitia taswira hii tunayoiona kupitia kioo cha Trump, upo uwezekano wa akina Trump wetu kushinda chaguzi zijazo kwa kishindo! Si mwanamuziki Diamond Platinumz kaimba kwamba ‘kioo hakidanganyi’?