Kisa cha Wananchi Walioibagaza Demokrasia
Chambi Chachage
Sijui kwa nini leo nimekikumbuka tena kisa nilichohadithiwa na Bibi yangu, Mkunde wa Maore, nikiwa mdogo. Kinahusu watu waliokombolewa kutoka utumwani. Maisha yao mapya hayakuwa na watawala wa kiimla waliowazoea. Wakiwa na migongano walienda kwa waamuzi waliowasuluhisha hadi wakapatana.
Lakini siku moja wakaja juu wakidai na wao wanataka kuwa kama wenzao wa nchi jirani. Walichoshwa na waamuzi wapya ambao hawakuwa kama mwamuzi aliyewapa mikoba. Badala ya kuamua kwa haki, walikula rushwa na kupindisha hukumu ili wafaidike.
Kwa hakika ni sababu ya msingi kabisa kutotaka mafisadi wawe waamuzi. Lakini badala ya kutafuta waamuzi wazuri ili waendelee na mfumo huo huo ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa umegatua madaraka na hivyo kuwa wa kidemokrasia zaidi, wao walitaka mfumo wa kifalme. Eti mtoto akililia wembe mpe. Ila mwonye.
Basi mwamuzi wao mstaafu akakubali kwa shingo upande kuwatafutia mfalme. Ila akashauriwa awaonye. Bahati nzuri maonyo hayo yamerekodiwa katika historia yao. Yanasema:
Maonyo hayo hayakufua dafu. Wakaendelea kulilia wawe na mfalme mmoja wa kuwaamua na siyo waamuzi wengi. Tunataka “kuwa na mfalme juu yetu”, wakasisitiza, “ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu.” Sauti ya wengi ikawa sauti ya Mungu.
Huo uhuru wao wa maoni ukaheshimiwa. Ikawa wengi wape. Demokrasia hiyo waliyoichoka na hata kuibagaza ndiyo ikawapa kile kile walichokitaka. Wakasahau kuwa kuna wakati bibi na babu zao walishawahi kuwa chini ya himaya ya kifalme na kitumwa.
Wananchi hao wakajipatia Mfalme wao. Muda si mrefu wakaanza kulalamika mno. Yale yote waliyotahadharishwa kuwa yatatokea yakatokea. Lakini ndiyo hivyo tena, mfumo wa kifalme ukadumu.
Usiniulize kwa nini nimekumbuka kisa hiki. Nimeshajibu. Sijui.
Tuzingatie pia kwamba demokrasia inayohusisha wote nayo inazo kasoro zake pale walipogawanyika kwa misingi ya ubinafsi wa udini¸ukabila, n.k, na walio wengi wanapokuwa hawana uwezo tosha wa kufanya maamuzi yanayowahusu wote, na hapa ndipo inapofaa demokrasia ya wateule wachache walio na uwezo tosha wa kufanya maamuzi yanayowahusu wote kidemokrasi inapofaa.