BARUA YA SENSA YAIBUA MJADALA WA LUGHA YA KUFUNDISHIA!
HOJA YA RICHARD MABALA:
Wakati mjadala huu uliibuka miaka ya sabini nakumbuka Mjerumani aliyekuwa anafundisha Mzumbe Sekondari aliandika barua kwa Daily News. Ninavyokumbuka alisema hivi.
Yeye ni mwalimu na huko Ujerumani na shule yake iko kilomita kumi kutoka kwa mpaka wa Ufaransa. Hivyo wanafunzi wanavukavuka mpaka kila wakati.
Hivyo walipata wazo zuri sana la kukuza Kifaransa na Kijerumani. Waliamua kutumia Kifaransa kama lugha ya kufundishia. Bila shaka walikuwa na zana zote muhimu. Lakini baada ya miaka kadhaa ilibidi waache wazo hili zuri sana kwa sababu walifanya tathmini na kukuta kwamba
a) Kifaransa cha wanafunzi hakikuongezeka sana
b) Kijerumani chao kilishuka
c) Uwezo wao katika masomo mengine ulishuka
Ndipo hapo inabidi tutofautishe kati ya kufundisha lugha na kutumia lugha kama lugha ya kufundishia. Iwapo wanafunzi hawajafikia kiwango fulani katika lugha badala ya kujifunza mambo mengine wanakwama kabisa na hata ile lugha inadumaa.
Siongelei wachache waliofaulu vizuri sana katika mfumo uliopita na wanaofaulu hadi sasa. Wengi wenu mpo katika kundi hili. Nawaongelea vijana Watanzania walio wengi. hata TAMASHA (shirika langu) tulitoa kipande cha Kiingereza cha darasa la pili kwa wanafunzi katika shule 16 (mbilimbili katika wilaya 8). Matokeo yalikuwa kwamba robo tu waliweza kusoma na kujibu maswali bila shida. Darasa la pili si kidato cha pili. Wanaopenda kulaumu mfumo mzima wa elimu ni sawa na kweli mfumo umechangia sana sana sana lakini turejee mfano wa hapo juu.
Suala hili halikuanza leo. Mwisho wa miaka ya sabini kulikuwa na Tume ya Makweta iliyofanya uchambuzi wa kina juu ya hali ya elimu. Pamoja na mapendekezo mengine mengi ilipendekeza Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia. Hapo waingereza walihamaki na kushinikiza kiingereza kibaki na kuhonga kwa kuahidi kuleta vitabu vingi sana vidogovidogo kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kufikia kiwango kinachohitajika kuweza kusoma masomo yote katika lugha ya Kiingereza. (vingi vilijaa ubeberu kitamaduni kiasi kwamba nilichokozwa kuandika Mabala the Farmer na Hawa the Bus Driver ili watanzania angalau wasome vitabu vyenye muktadha wa Tanzania)
Waingereza walifanikiwa katika azma yao na pendekezo la tume lilibadilishwa. Lakini waingereza haohao walikuja kutambua (kimyakimya) kwamba bado wanafunzi walio wengi (na hii ni mwaka 1982 si mwaka 2012) hawakuwa na Kiingereza cha kutosha kukitumia kama lugha ya kufundishia (rejea utafiti wa Criper and Dodd nadhani 1984). Mwingereza kiongozi wa English Language Support Programme ndani ya British Council alianza kusema kwamba lugha ya Kiingereza inaanza kutumika kama silaha ya kuwanyima Watanzania walio wengi elimu ya sekondari. Alihamishwa haraka sana!!!!!
Kwa hiyo, pamoja na ubovu wote wa mfumo wetu, (nakubaliana na Matinyi) lugha ya kufundishia inachangia pia.
Naheshimu sana lugha ya Kiswahili na kuna sababu chanya kibao za kukitumia kama lugha ya kufundishia. Sielewi kwa nini hatujivunii kuwa na lugha ya taifa ambayo inaongelewa na karibu Watanzania wote na kukitumia barabara. Ninao uhakika tungefanya hivi tungeacha kulalamika kwamba vijana wetu wamezidiwa nguvu na nchi zingine. Badala yake wangekuwa na maarifa ya kuwashinda wenzao mara dufu.
Naheshimu sana lugha ya Kiingereza na nakubali pia kwamba ni muhimu sana ili watu waweze kupata maarifa kupitia kwa lugha hiyo. Ndiyo maana, kama mwalimu wa Kiingereza, nachukia sanasanasana Kiingereza kutumika kama lugha ya kufundishia maana najua kwamba kinabomoa lugha waliyo nayo badala ya kuiendeleza pamoja na kuwakatisha tamaa malaki ya wanafunzi.
Mwisho napenda kutumia mfano wa Japan. Hawajui Kiingereza. Hawajawahi kujua Kiingereza. Sijui hata kama wanafundisha Kiingereza darasani. Lakini walipotaka kuendelea wakatumia wataalam wao wasome kwa lugha zote, Kiingereza, Kirusi, Kijerumani n.k. Kisha wataalam wakarudi na kutafsiri kila kitu katika Kijapani na kukirahisisha ili kila mtoto Mjapan aelewe kwa lugha yake.
Kung’ang’ania kitu wakati ambao hakifanikiwi kunahesabiwa kuwa ni ukichaa. Sasa kung’ang’ania kitu ambacho kinazidi kuzorota … sijui
HOJA YA MOBHARE MATINYI
Tutazunguka weeee mpaka tutachoka lakini ukweli unabakia kuwa hivi, Kiingereza kwa watoto wa Tanzania huanza kama somo na si kama lugha. Somo hili hufundishwa kuanzia darasa la tatu hadi la saba. Kutokana na ubovu wa elimu yetu katika kila hali, yaani madarasa, walimu, vifaa, sera, n.k. watoto wetu wanapomaliza darasa la saba huwa hawajui Kiingereza kwa kuwa somo hili halina walimu mahiri au hakuna kabisa walimu. Tatizo la Kiingereza nchini mwetu ni tunda la kufa kwa elimu.
Inapofikia kidato cha kwanza hadi cha nne Kiingereza kinabadilika na kuwa lugha ya kufundishia huku mtoto huyo wa sekondari akiwa hakijui kwa sababu alipoteza muda bure wakati akiwa shule ya msingi. Hapo unaanza mgogoro mwingine mkubwa ambao unaongeza maumivu kwenye masomo mengine pia. Mhadhiri Kiputiputi aliyekuwa akifundisha Hisabati pale CBE aliwahi kufanya utafiti kwa majaribio na kubaini kwamba watoto wetu wana uwezo mkubwa zaidi wa kuielewa fizikia iwapo mwalimu atafundisha kwa Kiswahili. Huyu mtaalamu niliwahi kumhoji mwaka 1994 na amefanya kazi nyingine kubwa kukitafsiri kitabu cha fikizia cha kidato cha kwanza hadi nne kiitwacho Abott – nadhani tunakikumbuka wengi wetu hapa – amekiweka chote kwenye Kiswahili.
Hivyo, kutumia miaka mitano ya shule ya msingi bila kujua Kiingereza ni kosa kubwa na tatizo kubwa na jibu lake liko kwenye kufa kwa elimu yetu. Hapo sekondari pia hali ingeweza kurekebishwa lakini mambo si hivyo kwa kuwa huko nako kumeoza kabisa, hasa baada ya walimu wa fasta-fasta kuanza kufyatuliwa. Ukifika kidato cha tano na sita hali ni mbaya zaidi kwa Kiingereza kinakoma kuwa somo labda tu kama mwanafunzi anakichukua kama moja ya masomo yake makuu, mfano kwenye HGL au KLF. Aidha, ni wazi kuwa walimu wa sekondari nao hawakijui Kiingereza kwa hiyo balaa linakuwa kubwa zaidi. Shida hii inatokana na mfumo wa elimu kuwa mfu – kwa nini tushindwe kuvuna matunda ya somo moja la lugha kwa miaka yote hii?
Ni rahisi zaidi kupima hali kwa kutumia Kiingereza kwa sababu ni lugha ya mawasiliano na hatuna kipimio cha haraka haraka cha masomo mengine. Aidha, Kiswahili si kipimio kizuri kwa kuwa ndiyo lugha pekee ambayo kila Mtanzania analazimika kuimudu hata kama hakwenda shuleni kabisa. Hata hivyo, kidogo kidogo, siku hizi hali mbaya ya Kiswahili inakuwa na ni uthibitisho mwingine kwamba sasa elimu yetu siyo tu kwamba imekufa bali tunaizika. Hebu sikia redioni jinsi ugoro unavyozungumzwa, utasiki mtu anasema: Hii nyimbo yangu…………………….mwingine anasema – mipango tarajiwa????
Kwa hiyo huko tunakokwenda, Kiswahili kitakufa kabisa kiasi kwamba itabidi tuwe tunasema hivi: Kufa kwa Kiswahili ni matokeo ya kufa kwa mfumo wetu wa elimu. Kimsingi mimi binafsi nilishasema hivyo pale nilipohoji aina ya uandishi wa habari wa Tanzania unaotumia sentensi ndefu zenye maneno hadi 70 bila kuweka kituo chochote. Nililinganisha na magazeti ya Kenya – moja tu la Taifa Leo – na kisha nikalinganisha na habari zinazotafsiriwa kutoka mashirika ya nje kwa kuangalia kote kuwili, Tanzania na Kenya. Kiliibuka kitu cha ajabu kwamba Watanzania wanapotafsiri habari za nje sentensi zao zinalingana urefu na za Wakenya wanapotafsiri au wanapoandika wenyewe lakini Watanzania wanapokaa kuandika wenyewe yanatoka madudu ya ajabu. Hii yote ilihusu Kiswahili na nilitoa makala hii kwenye jarida na Baraza la Habari Tanzania liitwa SCRIBE. Ni matokeo ya kufa kwa elimu. Nimetoa mfano wa matokeo mabaya ya Hesabu kidato cha nne kwenye jukwaa jingine jana chini ya mjadala huu huu na bado tunaweza kupekua masomo mengine lakini kazi yake si rahisi kama Kiingereza.
Nadhani hofu ya baadhi yetu kwamba ukizungumzia suala la kufa kwa elimu yetu linavyohusiana na kuanguka kwa Kiingereza Tanzania basi wewe hukipendi Kiswahili ama una kasumba ama unataka kujenga hoja kwamba elimu ya Tanzania imekufa kutokana na Kiswahili – HAINA USAHIHI. Haya ni mambo tofauti kabisa na hayapaswi kuchanganywa. Mimi ni mmoja wa watu wanaounga mkono Kiswahili kutumika zaidI ya kinavyotumika hivi leo, lakini siwezi kuacha kusema kwamba elimu yetu imeua Kiingereza na kwamba sasa inaua Kiswahili pia na mwisho itaua kila kitu kama haijafanya hivyo tayari.
Elimu yetu mbovu ndiyo inayoua Kiingereza na si kwamba matumizi ya Kiswahili yameua elimu yetu…..ndiyo nisemavyo. Elimu hii mbovu itaua Kiswahili kabisa. Tujiandae.
HOJA YA ALDIN MUTEMBEI:
WaELIMISHE wanafunzi, wafahamu kile unachowafundisha.
Kisha, waache watumie lugha kuwasiliana.
Wanafunzi wetu wakifundishwa kwa Kiswahili, wataelimika. Na tutapata walimu wazuri ambao watafundisha masomo mengine yote vizuri zaidi.Watajifunza lugha ya Kiingereza vizuri zaidi.
Katika Chama cha Walimu wa Kiswahili Vyuo Vikuu Afrika mashariki (CHAKAMA) ombi lilitolewa kutaka kuruhusiwa kuwa na shule ya mfano, ambapo tutawafundisha wanafunzi wetu kwa kutumia Kiswahili masomo yote ya Sekondari. Ilisemwa kuwa Wanafunzi hao watakuwa na uwezo wa kuongea Kiingereza, Kukiandika na kukisikia MKUBWA ZAIDI kuliko wale ambao wanafundishwa kwa kutumia Kiingereza.
Tulitaka tulithibitishe hilo KWA VITENDO, lakini mpaka leo, bado “OMBI LINASHUGHULIKIWA”
Toka mwaka 2002/2003!!!
Kiingereza ni muhimu. Hilo halina ubishi. Lakini Kiingereza sio Historia au Jiografia au Hesabu.Mwanafunzi anapokwenda nje ya nchi haendi huko kuzungumza Jiografia au Historia. Anatarajiwa kuzungumza Kiingereza kuhusu Jiografia au Hesabu.
Basi na apewe nafasi ya kujifunza vizuri hiyo Historia, au Fizikia au Kemia yake na atumie lugha kuizungumzia.
HOJA YA ADAM LINGSON:
Niweke nyongeza ndogo kwa maelezo aliyotoa Mobhare kuhusu ushahidi wa kitaalamu toka kwa mtaalamu wa Hisabati, ndugu Kiputiputi. Kutokana na kutokuwa mahiri kwenye lugha ya Kiingereza (tuliyolazimisha/wa kufundisha kwayo) walimu wengi katika madarasa ya shule za sekondari za umma nchini, hufundisha kwa KISWAHILI kwa kiasi kikubwa. Hapa namaanisha MCHANGANYIKO SANA. Na hapa ndipo Lugha aliyopendekeza Chambi kipindi fulani inaleta mashiko (Kitu kama Kiswanglish).
Tukiondoka kwenye matamko ya sera kuwa lugha ya kufundishia itakuwa Kiingereza, ufundishaji wenyewe toka sekondari hadi chuo kikuu huwa kitu kama hiki (wengine mnakumbuka mengi zaidi):
MWALIMU: Archimedes’ principle of flotation states that…(anasoma au na ‘recite’ wakati mwingine kwa mbwembwe sana tu)…
When an object is immersed in a fluid, the up thrust on the object is equal to the weight of the fluid displaced… tumeelewana jamani? Yaani this means kwamba kitu kikizamishwa kwenye maji…. tumeelewana? sawa kabisa. Hiyo ndiyo kusema kuwa… weight yaani uzito wa kiasi cha maji kinachomwagika..sijui nini na nini…
Hapo mwalimu huyu kujiridhisha kuwa amefundisha na kueleweka lazima atwange kiswahili. Kama hivyo ndivyo, kuna haja gani ya kupoteza muda kufundisha kwa Kiingereza? Yanini kumpa kazi ya Ufasiri au na Ukarimani mwalimu?
HOJA YA RUBARA MARANDO:
Leo hii ni ukweli kuwa shule zetu nyingi za sekondari zinafundisha masomo yote kwa Kiswahili na wamebaki kuandika notsi kwa kiingereza ‘ili waelekezane vizuri’ lakn siwezi kuthibitisha uwepo wa matokeo chanya ya moja kwa moja ya uanzaji wa matumizi ya Kiswahili kiutendaji (jambo lipendekezwalo na tafiti).
Usisahau pia wengine hata hiki Kiswahili hatukuzaliwa nacho tumeanza kukijua vizuri sekondari sambamba na kiingereza lkn kilichotokea hapo kati mpaka leo najua Kiswahili kuliko kiingereza ambacho hata nakiogopa. Hilo naachia wataalamu kutueleza km naweza kujifunza Kiingereza kwa Lugha ya Kiswahili na kuwa mzuri kwenye kiingereza. Utabaini kuwa Kiswahili ni Lugha nayojifunza km Kiingereza, kunitendea haki inayozungumziwa na tafiti ni kunifundisha kwa Lugha yangu ( au mnafikir wote wako mijini?). Km inafkrika kuwa suluhisho ni Kiswahili kwa kabila zote kwanini Kiingereza kiwekwe kwenye mzani tofauti? [siyo ‘uzalendo’, ‘kujitawala’ kifikra n.k ndiyo hoja hapa??]
HOJA YA NYONI MAGOHA
Mimi nakubaliana na Matinyi kwamba hoja ya msingi katika tatizo zima ni kudorora kwa elimu yetu na lugha ikiwa sehemu ya maeneo yaliyoathirika. Ninachopenda kutofautiana mimi na walio wengi ni njia ya mkato wanayopendekeza kwamba elimu yetu itaboreka iwapo tutatumia Kiswahili kufundishia.
Sijasema Kiingereza ni lugha ya kitaalamu isipokuwa ningependa kuona hali halisi uwanjani ambako una mwalimu mbovu wa Fizikia au Baiolojia aliyejifunza kwa Kiingereza na sasa unamtaka afundishe somo asilolimudu kwa Kiswahili, nini kitatokea? Pili, sijui wenzangu lakini mimi katika shahada ya kwanza nimetumia mamia ya vitabu na majarida mbalimbali ya sayansi na teknolojia ya Kiingereza kwa miaka yote nilipokuwa chuoni. Bado kulikuwepo upungufu mkubwa wa vitabu muafaka, sasa huwa najiuliza itakuwaje hapo tutakapoamua kufundisha Kiswahili elimu ya juu na hali hii ambapo mishahara ya waalimu tu ni mgogoro?
Ushauri wangu ni kwamba tuliangalie suala la ubovu wa elimu yetu kwa mapana yake na kuacha kutumia njia za mkato. Lakini la msingi zaidi, sisi kama taifa tujiulize tulikosea wapi kuhusu suala zima la elimu na tufanye marekebisho. Kwa mfano uliotolewa na Matinyi, nchi ya ‘Mauritius’ pamoja na sababu nyingine (kama zile za kukataa masharti ya WB na IMF miaka ya 60 na 70) wamepiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii. Iwapo sijakosea ni ya kwanza au ya pili kwa ‘GDP’ katika Afrika. Wamewekeza kikamilifu katika elimu na wanatumia lugha tatu sambamba. Tukizungumzia ‘kasumba’ iwapo ipo kweli sawa lakini nchini ‘Mauritius’ mpaka leo hii, pamoja na wao kuwa na baraza lao la mitihani, bado mwanafunzi wa sekondari hulazimika kufanya mtihani wa ‘Cambridge’ ambao hutungwa na kusahihishwa nje ya nchi. Hii imewasaidia kuendeleza kiwango cha juu iwapo mifumo ya ndani inayumba. Sisi wazalendo tupo na Kiswahili chetu kinakufa wakati ujinga, maradhi na umasikini vinaendelea!
[…]
Ninachosisitiza mimi ni kuzingatia chanzo cha tatizo la msingi na siyo kuzibaziba viraka hapa na pale. Pamoja ni hilo ni kwamba tu sina muda wa kutosha lakini nikifuatilia kwa makini naamini nitakuta udhaifu mahala fulani kwenye hoja hizi. Labda nitahitaji kufuatilia zaidi lakini nachelea kushawishika na huo utafiti wa mwalimu wa kuhusu uwezo wa wanafunzi kuelewa Sayansi kwa lugha ya za Kiswahili na Kiingereza; alitumia wanafunzi wenye Kiingereza duni ili kutafiti uwezo wao wa kuelewa Sayansi kwa Kiingereza? Ni kweli unatumia walengwa wenye udhaifu mmoja kuthibitisha uimara mwingine kwa kuonyesha udhaifu ambao tayari upo? Ni vigumu sana kupata walengwa huru wa utafiti kama huu; wawe na uwezo sawa wa lugha zote mbili na uwezo sawa wa somo husika au la sivyo, unalinganisha nini?
Hata tukiamua kufundisha elimu yetu kwa Kiarabu na tukawa makini elimu itaboreka tu. Kwahiyo suala si lugha gani inatumika ila nini tunafanya ili kuhakikisha lugha yoyote tunayoitumia inaeleweka vizuri na kwamba taaluma yenyewe inatolewa vema.
Kulinganisha GDP yetu na ya nchi iliyofanikiwa kwa sababu ya ubora wa elimu si njia ya ‘mkato’ kama ile ya kusema “niliwasomea watoto hadithi ya Alfu Lela u Lela kwa Kiswahili na Kiingereza na nikawauliza ipi wameielewa vizuri wakasema Kiswahili…naam nikajua tatizo ni lugha ya Kiingereza”.
Nikasema kwamba nchi ya ‘Mauritius’ wana elimu bora japo wanatumia lugha mbili tofauti za kigeni na lugha yao moja ya ndani. Bado tunaona huo ni mlinganyo wa kivivu? Wakati mwingine kunukuu tu matokeo ya utafiti na kubeza hali halisi ya viashiria vya maendeleo ni dalili ileile niliyosema awali.
Haya mie napitia njia hii ya mkato…kuhoji mlinganyo wa mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Uvinza na yule wa Shule ya Msingi St. Peter’s ya Nottingham katika kuelewa historia ya Sir Winston Churchill.
[…]
Ningependa kusikia kutoka kwa mwalimu wa tiba au uhandisi anayepigia debe ufundishaji kwa kutumia Kiswahili. Nimeshasikia sana kutoka kwa waalimu wa lugha na wengineo. Kusema kwamba tutumie Kiswahili kwa sababu mwanafunzi ataelewa zaidi eti kwakuwa ni lugha aliyozoea siyo hoja yenye mashiko hapa bali ni dalili ya kuendeleza uvivu ambao tayari unatugharimu kwa sasa.
Wamarekani wameanza kujifunza Kichina kwa bidii siyo kwa sababu Kichina kitamu kuliko Kiingereza bali kwa sababu za kiuchumi. Kukua kwa uchumi wa China na biashara baina ya China na Marekani kumejenga soko kubwa la ajira kwa pande zote mbili. Ili mtu awe na ushindani mkubwa, basi awe na elimu ya biashara toka Marekani na nyongeza ya ujuzi wa tamaduni za Kichina ikiwemo lugha. Kwahiyo kwa Kiswahili kukua na kuendelea kukubalika kimataifa kutategemea maslahi ya kiuchumi au kisiasa katika eneo letu na siyo kwa sisi kuwa na madakitari au wanasayansi walosoma kwa Kiswahili. Wanachotaka kufanya wengi hapa ni kuhamasisha kuanzia kwenye matokeo kurudi kwenye chanzo!
HOJA YA ALEX KOBALYENDA
Mwl:Mbona umechelewa darasani na miguu imejaa matope? unaitwa nani?
Mwanafunzi:Alex Mugisha Kobalyenda,nilipitia shamba na mama
Mwl:Shamba!!??Una miaka mingapi?
Mtoto:IKUMI NEE MO
Mwl:Ikumi neemo maana yake nini!!!?(Darasa likicheka)
Mwanafunzi:mhhhh kumi na moja mwalimu
Mwl:(akiwa na hasira) nani amekwambia tunazungumza kilugha humu darasani?
Mwanafunzi:samahani mwalimu nilisahau
Mwl:Miaka kumi na moja uko darasa la kwanza,kwanini?
Mwanafunzi:nilichelewa kidogo kuanza nilikuwa namsaidia mama kumbeba byabato(mdogo wake)
Mwl:Hebu nenda huko kakae juu ya lile jiwe pale kwenye kona,halafu kuanzia sasa unapaswa kuongea English because I m your English Teacher,do you understand?
Mwanafunzi:CHEI (darasa likivunja mbavu)
Mwl:(akichekaa!)Hebu toka huko kakae nisije kukuchapa nikakuumiza….
Wandugu,let’s discuss hii hoja ya kuporomoka mfumo wa elimu kwa uhalisia.
Mfano huo hapo juu upo sambamba kabisa na mifano yoyote kati yetu mmoja anaweza kuutoa pale kijana wa chuo kikuu anaposimama mbele ya wenzake darasa kujieleza (presentation) na mengine kama hayo….hatakosea kama huyu mtoto ila maudhui ni yaleyale mwisho wa siku, KWANINI?
Ni kweli hoja ya msingi ni Kuanguka kwa elimu.nimefuatilia na kusoma kwa makini hoja mbalimbali hapa kutoka kwa wote wamechangia.Nashukuru sana na nimejielimisha kwa mengi.
Ningeomba kutoa mawazo yangu kidogo.
Kwa mtazamo wangu:
Umasikini+Sera zisizotekelezeka+Kuanguka kwa siasa ya ujamaa na kujitegemea+Mfumo mbovu wa elimu=Kuanguka kwa Elimu Tanzania.
Pamoja na majibu na maelekezo mazuri sana ya Mwl.Aldin mimi nadhani tungerudi nyuma zaidi kihistoria sio kwa lugha tu bali kwa kuangalia zaidi wapi tulianzia na kukosea.Kama alivyosema 1962 Mwl.Nyerere alihamasisha na kuhimiza matumizi ya kiswahili kama ‘lugha ya taifa’ Je kutokea pale matumizi hayo yamefanikiwa kwa kiasi gani na kurudi nyuma kwa kiasi gani ‘kiuhalisia’ na katika janja mbali mbali sio elimu tu
Elimu inategemeana sambamba na mambo mengi sana nadhani wote tunafahamu.
Sasa tukijikita zaidi kwenye lugha na kusahau kuangalia mfumo wote wakati tukiamini labda kila mmoja wetu anauelewa kwa undani maana inajulikana nadhani tutakuwa tunarudi kwenye ule ‘mkato’ au ‘uvivu’ bwana Nyoni na Rubara wamekuwa wanausema unatusumbua.
Wataalamu wanahitajika hapa kwenye hoja hii nadhani wachumi,watunga sera mbalimbali na wote wanaounda Mfumo wa Nchi kutuelimisha na kuboresha janja mbalimbali ili hiyo Elimu tunaipigania ifanikiwe.
Kwa mtazamo wangu kama mifumo hii ambayo ni mihimili ya kusaidia elimu bora haitawekwa sawa basi tutakuwa tunazunguka palepale tu kama alivyoelezea Bw.Matinyi
1.Umasikini
Ikumbukwe tulio mjini ni kama asilimia 20 tu ya watanzania wote.
Walio vijijini si kwamba tu hawana elimu bali pia hawajui hata hicho kiswahili cha kuongea tu achilia mbali kile fasaha cha darasani ambacho tulio wengi tungeambiwa tukitumie katika kuandika hapa tungekimbilia kiingereza….
kwa mwanakijiji bado yuko katika kutoka kwenye lugha yake ya kikabila kuhamia katika kiswahili.
Kiingereza kwao bado ni lugha ya ‘ahadi’
Je Umasikini huu ambao unaadhiri elimu kama kukosekana kwa maji,umeme,matibabu na umbali wa kufika mashuleni unakombolewa vipi?
Je Serikali yetu imedondoka kwenye mfumo wenyewe wa elimu au mfumo huu wa elimu uliopo hauna mihimili muhimu inayotegemeana nayo?
Lengo la ‘lugha ya uraia’ limetupelekea kupata elimu bora au ndio limetusimamisha?
je mipango ya maendeleo iendayo sambamba na malengo haya ya ‘lugha ya kitaifa’ ilitekelezwa na inatekelezwa kama itegemewavyo?
Nini hasa kifanyike pamoja na umasikini huu tulionao ambao haiwezekani kufutwa mara moja lakini kidogo kidogo tuboreshe mfumo wetu wa Elimu(naungana mkono na Mama Qorro kwamba lugha zote zinapaswa kwenda sambamba…
ila je hiyo mihimili mikuu ya kusaidia hili lifanikiwe ipo imara?) Kama Mwl.Aldin alivyotuelezea historia ya kiswahili na naamini amebobea zaidi katika sekta hii ila tungeomba twende zaidi ya lugha ili tuweze kuona je hizo tume za kina makwetta,vyama mbalimbali na hata bodi za hapo chuo kikuu dsm na vyuo vingine huwa zinakwama wapi?chanzo cha kukwama?nini tufanye kuweza kukikabili chanzo hichi kisitukwamishe?
Kwa haya machache nimejaribu elezea kwa upeo wa elimu niliyonayo nadhani wakati tunajaribu kujenga hoja ya maendeleo ya haraka yatafikiwa kwa lugha fulani tujaribu pia kuweka mikakati mbalimbali ya hatua kwa hatua kujitoa katika lindi kuu la umasikini ambalo ndio kiini kikubwa kwa kuanguka kwa mfumo mzima wa elimu.
Labda wataalamu hapa watupe mfano wa nchi mbalimbali masikini zilivyoweza kujikomboa pamoja na kuwa katika kiwango cha umasikini ambacho Tanzania kama nchi ipo.
Tusiangalie hapa mjini tu na sisi wachache tuliofanikiwa ingawa kwa elimu ambazo wote moyoni tunajua tumemaliza shule ila uelewa ukiwa bado kidogo….
(nikimuunga mkono Bw.Welwel aliposema angetamani sana kujua zaidi ya pale angejua na akiamini kama angefundishwa kwa lugha yake angeweza kuelewa zaidi na zaidi).
Lugha ni tatizo kweli na nakubaliana nalo ila nadhani kwa Tanzania tatizo ni zaidi ya hizi lugha tunaongelea…nini kifanyike kuondoa au kukabiliana na hayo matatizo?
Najua tunaweza kusema kuwa wakijiji wasubiri kwanza wakati sisi wa mjini tunapewa dawa ili tuweze kwenda kuwatibu ila nadhani kuporomoka huku kunaanzia kule kwenye asilia tunayotoka ambako ni huko kijiji hivyo ni bora wakati tunaongele mikakati yetu mbalimbali tujaribu kuoanisha pande zote hizi mbili ambazo kwa ngazi tofauti zote zimeadhirika kwa kiasi kikubwa
Tufute umasikini wa elimu,kama Mwl.Aldin alivyosema tusikate tamaa bali tupambane nalo hili suala na kuleta mabadiliko(nimependa kusikia mwaka 2009 mmepitisha wanaosoma kiswahili kuandika nasifu zao kwa kiswahili,hilo ni jambo zuri sana).
HOJA YA CHARLES MAKAKALA
Alex amenena vyema, tatizo letu ni zaidi ya lugha tunazoongelea. Hata hivyo naomba niende mbali zaidi, sekta inayozorota si ya elimu tu, hivyo tatizo ni kubwa zaidi. Naamini hata tukibadilisha lugha ya kufundishia ikibadilishwa kwa nia yeyote ile bado tutaendelea kushikana uchawi. Je, majirani zetu Kenya, Uganda, Rwanda, au Zambia wana matatizo tuliyonayo katika elimu kwa sababu ya kutumia lugha isiyo ya asili kwao kufundishia? Sijui, lakini jambo moja nina uhakika nalo: wanafunzi hawaendi sekondari bila kujua kusoma au kuandika ati kwa sababu ya shida ya lugha…
Wakati wa utawala wa kibaguzi wa watu weupe huko Afrika Kusini mfumo huo ulikuwa unasemwa kama chanzo ya matatizo mengi kwa watu weusi. Lakini pamoja na mabadiliko ya kisiasa yaliyofanyika makala hii ya BBC inaonyesha kwamba wakati watu wenye asili ya Asia wameongeza kipato chao kwa kiwango kikubwa, kipato cha watu weusi hakikubadilika hadi mwaka 2008. Mfano huu unadhihirisha kwamba mazingira yanaweza kubadilika na kutoa nafuu fulani lakini bado jamii ikashindwa kunufaika na nafuu hizo kwa sababu ya udhaifu ndani ya jamii hizo.
Nafikiri ili kuweza kuelewa matatizo yetu Wanazuoni tunapaswa kuvunja miiko ambayo inaweka mipaka kwa bongo zetu kufikiri. Pengine twaweza kuanza kwa kufikiri labda wengine wana ujuzi au elimu au nguvu fulani ya ziada kutuzidi kisha tuone mawazo hayo yanatupeleka wapi. Huwa napenda dhana ya ‘calculus friendly’ na ‘calculus challenged’ ya Ali Mazrui kwa sababu inatuonyesha jinsi gani tunapaswa kufikiri kuhusu jamii yetu dhidi ya nyingine bila kujiona tuna mapungufu ya kiasili. Mojawapo ya miiko hiyo ni ule unaotokana na falsafa ya ‘cultural relativism’- yaani tamaduni zote zina manufaa sawa kwa jamii husika. (This liberal let-all-feel-good idea can lead to a catastrophe if it is wrong.) Je, kuna dhana katika fikira zetu zinazotudhoofisha kiutendaji? Je, kuna ujuzi au elimu ambayo watu wa Asia wanao unaowafanya wafanikiwe huko Afrika Kusini, Marekani au Ulaya? Je, yawezekana sababu hizo ndizo zinazojidhihirisha katika jamii hizo hapa kwetu pia, na uzorotaji wa sekta mbalimbali nchini kwetu?
VYANZO:
MJADALA: http://groups.yahoo.com/group/Wanazuoni/message/16469
Nashukuru bwana Udadisi kwa kuyarejea machweo yaliyokuwa yanawapotea watanzania kwa kiwango cha kutisha.
Nimekuwa muamini wa Kiswahili ningali kinda, na ninaipenda sana lugha hii, najivunia sana na zaidi nimeathiriwa kuwachukia wale wachanganyao kiswahili na lugha ya kitumwa.
Tanzania tumeyumba na kuyumba huku binafsi naamini chimbuko lipo kwenye wapanga sera wetu na taifa kutokuwa na miiko stahiki.
Mimi naamini kiswahili/lugha ni sehemu ya kwanza kabisa katika utalii wa taifa, na ni chagizo la uchumi huria wa taifa lolote lile.
Kuna mambo mengi yanahitajika kfanywa ili kurudisha hadhi ya kiswahili na mswahili, kwanza kama taifa tubadili sera ya elimu yetu iwe ni yakulenga kujitegemea kuliko leo ni ya kulenga kuajiliwa, pili kama taifa tufumua mitaala yetu isimame kwa kiswahili kuanzia awali mpaka elimu ya chuo kikuu, hili linawezekana kwakuwa kiswahili kinautajiri wa maneno ya kutosha.
Jambo lingine la msingi nikuwa lugha hii isimamiwe na wizara ya mali asili au iundiwe wizara yake lakini itamkwe katika katiba mpya kuwa ni raslimali adhimu ya kitalii.
Baraza la kiswahili liwezeshwe ipasavyo kuliko leo lipo kama kijiwe cha wapagazi tu.
Katika maisha yangu nimetumia sehemu kubwa ya maisha kuishi Urusi na Uchina, na nimeshuhudia mtoto anazaliwa anaanza shule mpaka anakuwa Prof au Dr lakini anatumia lugha ya kirusi au kichina katika masomo na makuzi yake yote. Hili limesaidia kupata wataalamu wanaojua kweli wanachojifunza sio wanaokalili kile wanachokisikia.
Nikupongeze sana tena sana kutuletea marejeo mazuri yenye kutusimamisha nyoyo imara chini ya mwamvuli wa lugha adhimu ya kiswahili ambayo ni alama halisi ya mwafrika.
Asante kwa makala nzuri. Lakini umesahau kutoa chanzo ya picha inayosema lugha ni maisha. chanzo chake ni radiomrima.org. asante