Nilidhani “#SikilizaTogolani”: Kwa nini tutumie ‘msuli’ ilhali njia rahisi ipo wazi kabisa? itakuwa makala yangu ya mwisho kuhusu mjadala wa Lugha Ya Kufundishia (LYK). Imani hiyo ilitokana na ukweli kuwa nimeshaandika makala nyingi za LYK na sina hoja za ziada. Mwenye sikio amesikia. Na mwenye jicho ameona. Hivyo, kilichobaki ni misimamo tu.
Lakini leo wakati nafuatilia mjadala wa LYK ambao umepamba moto kwa siku tatu sasa katika mtandao wa twitter nimejikuta nikikumbuka maneno ya Dakta Neema Mduma wa Chuo kikuu cha Afrika cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) pale Arusha. Yeye ni gwiji wa kitu kinachoitwa kwa Kiingereza Machine Learning (ML) ambacho kwa tafsiri ya haraka ni Uelimishaji wa Mashine za Kikompyuta kwa kutumia mbinu za teknolojia ya kompyuta. Mhadhiri huyo wa NM-AIST anasisitiza tusipende kuchanganya ML na kitu kingine kinachoitwa Artificial Intelligence (AI) japo vinahusiana.
ML ni sehemu tu ya AI. Hiyo AI ndiyo pana zaidi na inajumuisha mfumo mzima wa hizo mashine za kikompyuta kuwa au kujengewa uwezo wa kuwa na akili za kujifunza, kufikiri, na hata kutenda kama wanadamu. Hizo mashine zinaweza kuwa kompyuter zenyewe, roboti au kifaa chochote ambacho kinaweza kutumia lugha ya kikompyuta kupangiwa/kuprogramiwa nini cha kufanya. Nimeamua kwa makusudi kutumia majina hayo ya Kiingereza ya ML na AI ili nisijiingize katika mjadala mwingine wa Kiswahili dhidi ya Kiingereza kama LYK. Ila hoja yangu bado inahusu LYK kwa kuwa, kianalojia ML na AI zinaweza kutusaidia kuelewa zaidi tatizo letu linalofanya huu mjadala wa lugha ukwame na kugota kwa zaidi ya miaka 40 sasa.
Akina Dakta Neema Mduma wanasema kuwa ili kuifundisha mashine kitu fulani basi unaiweka kwenye mazingira ambayo hicho kitu kipo ili ijifunze. Kwa mfano, kama unataka kuifundisha mashine iweze kutafsiri maneno ya Kiingereza kwenda kwenye Kiswahili na ya Kiswahili kwenda kwenye Kiingereza basi unaiweka sehemu ambapo hayo maneno yapo, yaani yanaandikwa na kutamkwa. Kwa kutumia lugha ya kikompyuta, mashine hiyo itatazama namna lugha hizo zinavyoandikwa na kutamkwa kwa namna anuwai na kisha kujifunza.
Sasa ili ijifunze vizuri zaidi au kabisa basi mashine hiyo inapaswa iwekwe kwenye mazingira yenye maneno au misamiati ya kutosha na yenye matumizi mengi. Kwa maana nyingine unailisha ‘akili’ yake, yaani programu ya mashine hiyo chakula cha kutosha cha maneno na matumizi yake mambalimbali katika muktadha tofauti tofauti. Ikitoka hapo ikakutana na neno fulani basi inatumia ‘lishe’ hiyo kulitambua na kulitolea tafsiri yake. Kwa kiasi kikubwa hivyo ndivyo ‘Google Translate’ inayotumika kutafsiri lugha kadhaa inavyojifunza kazi hiyo.
Ila si kumekuwa na malalamiko kwamba Google Translate au program za kutafsiri maneno kwenye TV hazikitendei haki Kiswahili? Ndiyo. Kwa sababu mashine zao za kikomputa hazijapata mazingira mazuri ya kutosha ya kujifunza Kiswahili, yaani kupata maneno mengi, maandishi mengi, na mazungumzo mengi ya lugha hiyo ili kuwa na akili ya kutosha kutafsiri mipangilio tofauti tofauti ya maneno hayo inapokutana nayo kwenye filamu au mtandaoni.
Lakini lugha zingine hasa kutokana na watu wao kujaza zaidi maneno na mazungumzo kwenye mitandao kumeifanya Google iwe na hazina kubwa ya kujifunzia. Hivyo, kwa mfano, ni rahisi kwa Google Translate kutafsiri kati ya Kifaransa na Kiingereza bila kuwa na makosa ya kiwango cha inapotafsiri kati ya Kiingereza na Kiswahili au Kifaransa na Kiswahili. Ila ipo siku hali itakuwa nzuri zaidi kama tutaendelea kutengeneza mazingira hayo kuongeza zaidi matumizi ya Kiswahili kwenye mitandao kupitia mijadala na machapisho.
Baada ya kusema hayo, swali lililobaki ni je, yana uhusiano gani na kutumia Kiingereza au Kiswahili kama Lugha Ya Kufundishia (LYK) masomo mengine shuleni na vyuoni. Uhusiano upo kwenye analojia ya mazingira na muktadha. Wanafunzi wengi wa shule na vyuo wamekuwa wanapata changamoto ya uelewa pale Kiingereza kinapotumika kwa kuwa kumekuwa na mazingira na muktadha duni. Kumekuwa na ufinyu wa Kiingereza. Kwa kiasi kikubwa Kiingereza cha walimu kimekuwa hafifu na kibovu.
Matokeo yake wanafunzi nao walio wengi wamekuwa na Kiingereza hafifu na kibovu. Hafifu huzaa hafifu. Mbovu huzaa mbovu.
Hapo ndipo tunapokutana na makundi makuu mawili katika mjadala ya LYK. Kundi linalosema twende hivyo hivyo na Kiingereza kilichopo kama LYK huku tukiimarisha mazingira na muktadha ya kujifunza badala ya kutumia Kiswahili kama LYK. Na kundi linalosema twende na Kiswahili kama LYK halafu tufundishe Kiingereza kama lugha na somo badala ya kuking’ang’ania kama LYK.
Makundi yote yanakubali kuwa mazingira na muktadha wa kujifunza na kufundishia Kiingereza siyo mzuri. Yanatofautiana suluhisho. Pia tafsiri ya masuluhisho.
Teknolojia za AI na ML zinatufundisha kuwa huwezi kufanikiwa vilivyo kujifunza bila muktadha na mazingira kuwa bora. Mashine za kikompyuta pamoja na uwezo wake mkubwa wa kuchakata data haziwezi kujua kutafsiri vilivyo kama data za kujifunzia hazitoshi au zina mapungufu. Na binadamu ni hivyo hivyo, huwezi kujua Kiingereza vizuri kama vitu va kujifunzia lugha hiyo havitoshi au vina mapungufu. Haba na haba siyo lazima zijaze kibaba. Chururu si ndondondo.
Profesa Kitila Mkumbo na Balozi Togolani Mavura wao wanasema tujaze tu kibaba na kukiongezea ubora ipo siku tutafika. Profesa Martha Qorro na Mwalimu Richard Mabala wanasema tunavyoendelea hivyo tunapoteza watu si haba, kibaba hakijajaa na kinaweza kutojaa, hivyo, tukijaze kwa mbinu tofauti ya kumfundisha mwanafunzi kwa lugha anayoilewa na hiyo asiyoilewa tumfundishe aielewe.
Sijui Dakta Neema Mduma atasemaje ila naamini atasema hakuna tofauti kubwa kati ya kuifundisha lugha akili ya mashine ya kikompyuta na kuifundisha lugha akili ya mwanadamu – kila unachokiingiza ndicho ukipatacho, kiingiacho ndicho kitokacho.
Garbage in, Garbage out (GIGO) – Uchafu ukiingia, Uchafu utatoka (UIUI).