Inasemekana Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kusema kuwa ‘Kiswahili ni lugha maskini’. Mimi sikubaliani na msemo huo. Naamini Kiswahili, kama lugha yetu ya taifa, inaweza kabisa kutumika katika mfumo wetu wa sheria, elimu na utawala tena wala haitachukua karne kufanya hivyo kama tukiamua kufanya hivyo leo. Lugha hii inajitosheleza na kama zilivyo lugha nyingine inakopa – wala haiombi au kuazima – maneno kutoka kwenye lugha zingine na kuyatumia kwa mujibu wa kanuni zake za kisarufi na kifasihi. Kukopa si ishara ya umaskini. Kuombaomba na kuazimaazima ndio ishara ya umaskini. Hata hiyo lugha ya Kiingereza haikukua kwa kutumia utajiri wa maneno yake yenyewe tu au kwa kutoa vizingizio vya umaskini wa lugha. Ilikua baada ya kuukataa uhodhi/ukiritimba wa lugha ya Kilatini. Hivyo Kiingereza kikapewa hadhi yake na kikakopa maneno kedekede ya Kilatini na Kiyunani/Kigiriki hasa yale ya kisayansi na kisheria. Sioni kwa nini tusifanye hivyo hivyo kwa Kiswahili hasa ukizingatia kuwa Kiswahili ambacho tunakitumia mtaani ambacho nakiita ‘Kiswanglishi’kukitofautisha na ‘Swanglish’ tayari kinafanya hivyo. Wananchi tunaotumia Kiswahili kila siku tumeshapiga hatua. Tatizo ni waliohodhi sera ya lugha. Kama wahenga wetu walivyotuasa, ‘nguo ya kuazima haisitiri matako’!