Zamani nilijiahidi kwamba siku moja nitatoa mhadhara kwa lugha ya Kiswahili Mombasa, Malindi, Lamu, Unguja au Dar es Salaam, au pengine popote ambapo Kiswahili kina mizizi yake. Nilipotunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu (PhD) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 2013, hotuba yangu ya shukurani niliitoa kwa Kiswahili. Nilifanya hivyo hivyo Chuo Kikuu cha Bayreuth, Ujerumani, mwaka 2014, nilipotunukiwa shahada nyingine kama hiyo.

Lakini hii ni mara yangu ya kwanza kutoa mhadhara Mombasa. Ahsanteni sana kwa kunialika na kwa kuifanya ndoto yangu kuwa kweli, hata kama naitoa hotuba hii kwa njia ya Zoom nikiwa California, Marekani.

Nitaanza kwa kusimulia hadithi.

Baada ya kuchapishwa kitabu changu kinachoitwa Decolonizing the Mind mwaka wa 1986, nilialikwa na BBC kushiriki katika majadiliano kuhusu Kiingereza. Mada ilikuwa ni swali: “Kiingereza Lugha ya Dunia?” Waliohudhuria walitoka sekta kadha wa kadha za viwanda, biashara, serikali na vyuo vikuu. Niliuandika mhadhara wangu kwa Gĩkũyũ, lugha yangu ya mama; lakini niliusoma kwa tafsiri yake ya Kiingereza. Wasikilizaji walishangaa niliposema kwamba Kiingereza hakifai kuwa lugha ya dunia, Kiswahili ndiyo lugha inayofaa!

Baada tu ya kumaliza kutoa mchango wangu, pazia moja lilifunguka, au lilifunguliwa, na aliyetokeza nyuma ya pazia hilo alikuwa ni mume wa Malkia Elizabeth wa Uingereza, Prince Philip, Duke of Edinburgh. Yeye ndiye aliyekuwa Mlezi wa Chama cha Lugha ya Kiingereza (Patron of English Union), na ambacho ndicho kilichotoa pendekezo la kufanywa majadiliano hayo. Wakati wote wa hotuba yangu, Prince Phillip alikuwa nyuma ya pazia.

Alipojitokeza akaja moja kwa moja mpaka pale nilipokuwa nimesimama. Nikafikiri: huyu jamaa anakuja kunikosoa kwa kusema kwamba Kiswahili ndiyo lugha inayostahili kuwa lugha ya dunia. Lakini hakunilaumu. Aliniambia kwamba kwa sababu yeye ni Mgiriki kwa kuzaliwa, yaani Kigiriki ndiyo iliyokuwa lugha yake ya mama, alifahamu yale niliyoyasema.

Lakini hata kama angenikosoa, nilikuwa tayari kujitetea. Ni kweli Kiingereza chazungumzwa na watu wengi duniani kushinda Kiswahili. Lakini Kiingereza kilienea duniani kwa mabavu ya ukoloni na ubeberu. Si Kiingereza peke yake. Katika aina zote za ukoloni, au hali zote za watu fulani kuwakalia wengine, lugha hutumiwa kama fimbo ya kuzipondaponda akili za wanaonyanyaswa. Mkoloni huwafanya anaowatawala wazidharau lugha zao za mama na wazikumbatie kwa dhati lugha za kigeni za hao watawala wa kikoloni.

Hivi ndivyo Waingereza walivyowafanya wenyeji wa Ireland. Nchi ya Ireland ilikuwa kama koloni la ulowezi wa kwanza wa Waingereza. Waingereza waliingia humo na wakaanza kunyakua mashamba na kuwakandamiza wenye nchi, lakini kwa miaka mingi wananchi wa Ireland waliendelea kuupinga utawala huo wa walowezi kwa njia mbalimbali.

Mwaka wa elfu moja mia tano na tisini na sita (1596), mwandishi  mmoja Mwingereza, aliyeitwa Edmund Spenser, aliandika kitabu kilichoitwa: A View of the Present State of Ireland, yaani “Mtazamo  wa Ireland kwa Wakati Huu”. Katika kitabu hicho, wahusika wawili Waingereza wanajadili njia bora za kukomesha upinzani na kuwashinda wananchi wa Ireland. Wakaona silaha bora na rahisi, yaani isiyo ya kutumia upanga na bunduki, ni kuwafanya wabadilishe wanavyojiita – yaani wabadilishe majina yao: kwa mfano kuwafanya waondoe “Mac” na waondoe herufi O’ kwenye mwanzo wa majina yao. Na pia kuwafanya watumie Kiingereza badala ya lugha yao ya mama, lugha ya asili ya Ireland.

Akasema mmoja wa wahusika:

Katika historia, imekuwa ndio mtindo kwamba wanaowatawala wengine, huwalazimisha kuongea lugha ya watawala.

Wale walowezi Waingereza walifanya hivyo kwa lengo la kuwalazimisha wenyeji wa Ireland kujisahau kabisa; na kwa kujisahau kilugha na majina, kutawarahisishia Waingereza kupata ushindi.

Waingereza walitumia sera hiyo hiyo kwa Waafrika waliowakamata na kuwafanya watumwa, na halafu kuwapeleka kwenye mashamba yao Marekani na Karibea, na kuwalazimisha kufanya kazi. Lugha zote za Mwafrika huyo zikapigwa marufuku katika mashamba hayo.  Watumwa wakipatikana wakiongea lugha zao za Kiafrika, walikuwa wakinyongwa. Hivi ni kusema kwamba mizizi ya lugha iliyowaunganisha na bara la Afrika ikakatwa.

Katika mwaka wa elfu moja mia nane na thelathini na nne (1835), Mwingereza mmoja anayeitwa Lord Macaulay alipendekeza sera mpya ya elimu India, nchi ambayo ilitawaliwa na Waingereza kwa miaka mingi. Alisema kwamba lazima Kiingereza kiwe lugha ya elimu, badala za lugha za wenyeji, kama vile Sanskrit. Nia ya kufanya hivyo, alisema, ni kuunda kitabaka kutoka kwa watawaliwa, ambacho, kwa miili yao, rangi za ngozi zao, mavazi, dini, zitabaki kuwa za Wahindi kabisa, lakini vichwa vyao, yaani mabongo yao, yatakuwa ya Mwingereza. Akaendelea kusema, tabaka hili la mwili wa Mhindi lakini bongo la Mwingereza, litasaidia au kufaulisha utawala wa ukoloni India. Watakuwa kama manyapara wa ubeberu.

Kote walikotawala duniani, Waingereza walifanya kama hivyo: walikandamiza lugha za wenyeji, na kukitukuza Kiingereza juu ya makaburi ya lugha za wenyeji. Kwa mfano, kote Marekani, Kanada, New Zealand na Australia, waliziangamiza lugha za wenyeji, na hata kuwaua wasemaji wengi wa lugha hizo.

Hata kwetu Kenya. Na ndipo ikawa kwamba mtoto akipatikana akiongea lugha yake ya kienyeji katika sehemu yoyote ya skuli, alichapwa viboko, au kulazimishwa ajiite yeye ni mpumbavu. Katika kitabu changu cha Decolonizing the Mind, nimeeleza vile tulivyoadhibiwa tulipokuwa skuli tukipatikana tunazungumza lugha zetu za mama, na tukilazimishwa kuvaa shingoni kibao kilichoandikwa: Mimi ni Punda.

Yote hayo ni kwa lengo la kumfanya mtoto aone aibu na kujidharau kwa kuongea lugha yake ya mama! Akiongea lugha ya mama, anapigwa makofi. Lakini akiongea Kiingereza, anapigiwa makofi!

Kwenye mchango wangu katika yale majadiliano yaliyoandaliwa na BBC, niliwaelezea sababu zangu za kupendekeza Kiswahili kiwe lugha ya dunia. Sababu mojawapo muhimu ni kwamba Kiswahili hakina historia ya ukoloni na ubeberu. Sababu hiyo ndiyo miongoni mwa sababu zinazonifanya nifurahie kuwa Kiswahili ni Lugha ya Taifa Kenya na Tanzania.  Na napendekeza iwe lugha ya mataifa yote ya Afrika Mashariki na bara lote la Afrika. Kiswahili hakijakuwa lugha ya ukandamizaji, wala ya ukoloni, wala ya ubeberu – kinyume na zile za Ulaya, kama vile Kifaransa, Kiingereza, Kireno na Kihispania, ambazo zinatiririka damu ya ukandamizaji.

Halafu, Kiswahili ni lugha ya Mwafrika. Asili yake ni Afrika. Ngoja tupate ushahidi kutoka kwa mshairi Abdilatif Abdalla. Nitanukuu kutoka majadiliano yake na wenzake kuhusu maneno “Kupelekea” na “Kusababisha”. Abdilatif aliyatanguliza maoni yake kwa kusema hivi:

Nilianza kukisikia Kiswahili tangu nimo tumboni mwa mamangu, ambaye alikuwa haijui lugha nyengine isipokuwa hii. Wala wazazi wake, na pia mababu wa mababu na manyanya wa manyanya wa wazazi wake, hawakuwa na lugha nyengine ya asili isipokuwa hii.

Huo ni ushahidi wa mzaliwa wa Mombasa, ambaye anakumbuka ukoo wake Pwani karne na karne  zilizopita. Kwa ufupi, Kiswahili ni lugha ya Mwafrika, haikuletwa Kenya na watu wengine. Ni kweli Kiswahili kimenoneshwa au kuathirika na maneno kutoka Kiarabu na lugha nyingine za kigeni ambazo wazungumzaji wake walikuja katika maeneo ya asili ya Kiswahili. Hilo ni sawa. Lugha zote duniani zina athari ya maneno kutoka lugha nyingine.

Zaidi ya Kiswahili kujulikana Kenya, Tanzania, Uganda, Msumbiji, Kongo, Rwanda, Burundi, kwa miaka mingi kimekuwa kinafundishwa katika vyuo vikuu vingi duniani. Mimi nafurahi kwamba Umoja wa Nchi za Afrika (AU) umekichagua Kiswahili kuwa lugha ya Afrika nzima. Kiswahili ni urithi wa Mwafrika. Ni titi la mama yetu Afrika. Na, kama msemo maarufu wa Kiswahili unavyosema:

Titi la mama li tamu, jingine haliishi hamu.

Ni matumaini yangu kwamba Swahili Heritage Trust itaendeleza, na kukuza, utumiaji wa Kiswahili kama lugha ya kawaida, lugha ya ushairi, lugha ya uvumbuzi, lugha ya demokrasia, lugha ya sayansi, lugha ya uchunguzi, na lugha ya kuwaunganisha Waafrika wa bara lote la Afrika. Ni matumaini yangu pia kwamba itaihifadhi na kuilinda historia ya Pwani na utamaduni wake.

Tukumbuke kwamba kwa karne na karne, Mombasa na miji mingine ya Pwani ya Afrika Mashariki, kama vile Sofala, Gedi, Pate, Lamu, Malindi, Unguja, Pemba, na Kilwa ilikuwa inajulikana sana; hata yule mwandishi, John Milton, aliitaja baadhi ya miji hiyo katika kitabu chake, Paradise Lost, kuwa ni vituo vya utamaduni na ustaarabu wa kesho.  Miji hii ndiyo iliyokuwa miji muhimu ya misafara ya biashara zilizounganisha miji yote iliyoko Bahari ya Hindi mpaka China ya Zamani. Ibn Battuta alitembelea Mombasa, Kilwa na Mogadishu. Lakini kabla yake yeye kulikuwa na wengine, kama yule mwandishi wa The Periplus of the Erythrean Sea.

Niseme tena. Lugha hii iliyo na historia ndefu kama hii ni urithi wetu Afrika. Lakini nataka kutoa onyo. Naona kwamba mawazo ya wengi wetu wasomi kuhusu lugha yameathiriwa na mfumo wa kuziweka lugha kwa viwango: kwamba kuna lugha ambazo ni lugha hasa, au ni muhimu zaidi, kushinda nyingine, au zina cheo cha juu; na kwamba hizo tu ndizo za ustaarabu na usomi.  Nawaomba mashabiki wote wa Kiswahili: tafadhalini tusifanye Kiswahili kikalie kile kiti kilichokuwa kinakaliwa na Kiingereza; kiti cha kujiona kama ni cha cheo cha juu, na kwamba lazima lugha nyingine zikipigie magoti. Tutupilie mbali ule mfumo wa viwango.

Kiswahili ni kama lugha nyingine za Kiafrika. Lakini kwa bahati ya historia, ndiyo lugha moja ya Afrika inayojulikana kwingi. Nikirudia tena: Kiswahili hakina historia ya ukoloni na ubeberu. Kwa hivyo, Kiswahili kina uwezo wa kusaidia mawasiliano kati ya mataifa mengi yaliyo na lugha tofauti za mama; yaani Kiswahii hakijaathiriwa na upumbavu wa ukoloni na ubeberu.

Kwa hivyo, tujivunie lugha za mama; tujivunie Kiswahili kama lugha ya taifa; na juu yake tukiongeza ujuzi wa Kiingereza au Kimandarin, au Kifaransa, au Kiyoruba, na kadhalika. Hizi zote zitatuongezea nguvu ya ujuzi na mawasiliano. Lakini msingi wetu ni lugha za mama na Lugha ya Taifa zima, yaani Kiswahili.

Basi napendekeza sera ya kila Mwafrika wa bara la Afrika kujua lugha yake ya mama; halafu ajue Kiswahili; halafu Kiingereza, Kifaransa, au Kireno. Baada ya hapo, mtu anaweza kujiongezea lugha nyingine kulingana na uwezo wake.

Kiswahili kinaweza kuwa lugha ya Umoja wa Afrika!

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Hatimiliki

Makala haya yanatokana na hotuba iliyotolewa na Ngũgĩ wa Thiong’o kwenye mkutano wa mtandaoni uliotayarishwa na Swahili Heritage Trust, Mombasa, tarehe 22 Juni, 2021, kusherehekea Siku ya Kiswahili. Picha zote zimetumika kwa hisani ya Abdilatif Abdalla na Ngũgĩ wa Thiong’o.