
Naomba mnisikilizeni tena msinidisi
Nijibuni kiuanazuoni wala msinitusi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi
Nawauliza wanazuoni nijibuni basi
Napaswa kufanyani niweze kupasi
Niwaige manyani kupigapiga utosi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi
Nawahoji wakinzani mnaoleta uasi
Niende mahakamani hatua kuiposi
Niwafuate wapinzani kununua kesi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi
Nawadadisi maskini msojali ukwasi
Niingie matatani kuwapigania waasi
Nichukue hatuani kuwapiga mabosi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi
Natoka kilingeni nimejawa utusitusi
Najiona limbukeni aogopaye bisibisi
Niingizeni tanuruni nisiupate uyabisi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi
© Chambi Chachage
Lipi likusumbualo, kalamu kuirukia
Au umekosa mlo, sasa umechukia
Lipi hasa ulonalo, unalolisumbukia
Kama shida ni uhuru, tushapata 61
Amani tulonayo, ni tunu ilotufikia
Usitake mapambano, shimoni tatumbukia
Sijeichokoza leo, kesho hutoifikia,
Kama shida ni uhuru, tushapata 61
Jaribu kujipa moyo, manani takusikia
Kuwa mtu wa maono, lengo utalifikia
Siwachukie vigogo, nchi wameitumikia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61
Siwatafute wanono, waweza kukuchukia
Mwisho wakakutoa roho, bure kwa kujitakia
Ogopa sana vigogo, chini watakufukia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61
Wale uwapiganiao, kesho watakukimbia,
Hawatoshiriki mgomo, Wala kukuimbia,
Tena watakaa kando, huku wakijitambia,
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61
We kula ugali wako, ukishiba tajitapikia,
Achana na nia yako, wengine kuhangaikia,
We jali maisha yako, wenye shida wajitakia,
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61
Chukua hatua zako, uone utapoangukia,
usitafute maneno, balaa likakufikia,
Mwombe sana Mola wako, ‘mana’ takushukia,
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61
Kama hawapendi jambo, hawawezistahimilia,
Madhari wanapata tango, shida wanavumilia,
Siku wakikabwa shingo, mabosi watasimulia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61
Shida zikiwakaba koo, watajua pa kukimbilia
Tena watafanya soo, mabosi watajililia,
Patakuwa ni padogo, mawe yatasimulia,
Kama shida ni 61, uhuru tushaupata?
© Ayub. R.
