Chambi Chachage

@Udadisi

 

Kumezuka mjadala mkali baada ya mahojiano kati ya mwanahabari nguli, Zuhura Yunus, na mtafiti gwiji, Thabit Jacob. Miongoni mwa wanamjadala katika vuta nikuvute hiyo ni mwandishi mbobezi, Maggid Mjengwa, ambaye ameishambulia vikali tafsiri thabiti ya takwimu zinazohusu sekta ya madini. Ili kuipa uzito hoja yake amenukuu hadi maandishi ya Profesa Seithy Chachage.

Lakini alichosahau rafiki yangu ni kuwa Profesa huyo huyo ndiye aliyewahi kuandika makala kuhusu Jinsi ya Kuhadaa kwa Takwimu. Wakati huo alikuwa akilenga jinsi takwimu za sekta ya utalii zilivyokuwa zinatolewa na kutafsiriwa katika namna ambayo zinaficha hali halisi nchini. Pia alitumia muda mwingi kwenye machapisho yake kuchambua hadaa za takwimu za madini.

 

Sasa nia yangu siyo kujiingiza moja kwa moja katika mjadala huo tete na tata ambao umemuibua hadi Waziri wa Madini, Dotto Biteko, kujibu mapigo. Azma yangu ni kuangalia jinsi suala la takwimu linavyoweza kutuhadaa au kutupambaza ama kutuondoa kwenye kiini cha tatizo. Tatizo kuu siyo takwimu, bali kuingiza masuala ya siasa hasa za kampeni kwenye tafsiri za kitakwimu.

Nitaanza na takwimu nilizooneshwa juma lililopita kuhusu mafanikio kwenye uuzaji wa madini ya dhahabu. Takwimu hizo hazikutolewa kama takwimu tu bali kama sehemu ya kupiga kampeni kutuonesha kufanikiwa sana kwa uuzaji wa dhahabu mwaka 2020 ukilinganisha na mwaka 2019.

 

Baada ya kutafuta sana kwenye tovuti rasmi ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) chanzo halisi cha takwimu hizo nikakipata. Katika toleo lake la Agosti 2020 la tathmini ya mwezi, BOT inaonesha kwenye ukurasa wa 11 pichani kuwa mauzo ya dhahabu nje ya nchi yalipanda kutoka Dola za Kimarekani milioni 1,446.4 mwaka 2018 wa fedha hadi milioni 1,785.3 mwaka 2019 wa fedha na mpaka milioni 2,728.7 mwaka 2020 wa fedha. Sasa mkanganyiko unaanza pale unapoenda kwenye majedwali ya BOT ya mwaka mzima.

 

Jedwali mojawapo pichani linaonesha kuwa mauzo hayo yalikuwa Dola za Kimarekani milioni 1,524.1 mwaka 2018 mzima na milioni 2,215.1 mwaka 2019 mzima. Kwa maana hiyo, mauzo yalishafikia zaidi ya bilioni 2 kabla hata ya mwaka 2020 wa fedha kama picha ya kwanza hapo juu inavyoashiria. Wataalam wa takwimu wanaweza kudai hilo jedwali linatuonesha makadirio ya awali tu ya BOT kabla ya kurekebishwa na kulinganishwa, kwa mfano, na takwimu mpya za Mamlaka ya Mapato (TRA) na/au kujumuishwa katika mwaka fedha.

Ila kabla hatujajaribu kuijibu hoja hiyo, hebu tuangalie na jedwali lingine pichani kutoka BOT. Hilo linaonesha kuwa hadi kufikia Juni 2020 mauzo ya dhahabu nje kwa mwaka huu yalikuwa yamefikia Dola za Kimarekani  milioni 1,326. Kwa maana nyingine, kati ya Juni na leo Septemba 2020, yaani kipindi cha miezi mitatu tu, mauzo hayo yanaweza kuwa yameruka hadi kufikia bilioni 2 na ushehe?

Uzuri wa jedwali hilo huko lilipotoka kwenye tovuti ya BOT pia lina takwimu za kila mwezi za miaka kadhaa iliyopita. Ukizijumlisha pia unapata takwimu zile zile za dola milioni 1,524.1 kwa mwaka 2018 mzima na dola 2,215.1 kwa mwaka 2019 mzima. Hapo ndipo ule msemo wa namba hazidanganyi unapoonekana. Sasa inakuwaje nambari zinaanza kutuchezea shere kwenye ripoti ya Agosti?

 

Au siasa za uchaguzi zimeingilia kati kiasi kwamba mafanikio ya kupanda kwa mauzo kati ya mwaka 2015 hadi 2019 wa fedha au mzima hayatoshi kutufurahisha wapiga kura hadi tuambiwe kuna mafanikio makubwa zaidi kati ya mwaka 2019 na 2020 wa fedha? Tena mno kabla hata mwaka 2020 mzima haujaisha?

Hali inakuwa ngumu mno hasa katika kipindi hiki ambacho wapo wenye hofu hata ya kujadili takwimu kutokana na Sheria ya Takwimu ‘mpya’ japo imerekebishwa rekebishwa sasa. Na hapo ndipo sisi wadadisi wa mambo tunapoona kwa nini mahojiano ya BBC Swahili yameleta ukakasi kwa wenye mamlaka japo wahusika walionesha kuwa kuna mafanikio kwenye sekta ya madini.

Pengine kosa lao kuu ilikuwa kuongeza neno “lakini” ama “ila”. Kuwataka wachambuzi waseme “ndiyo” au “hapana” badala ya “ndiyo” na “hapana” ni kuwaweka katika wakati mgumu mno. Ni kutaka waikane fani yao ya uchambuzi ambayo kwa kawaida hujikita kwenye kusimika mizania.

Takwimu zina raha yake kila mtu akiwa na fursa ya kuzichambua na kutoa tafsiri yake. Ila hayo mambo ya kulazimishana mtu aone bilioni 2 badala ya bilioni 1 ni karaha. Humfanya ahadae au apumbaze kwa kutumia takwimu. Na tena ni kutoitendea haki taaluma ya takwimu za kihisabati.

Magwiji wa takwimu wanajua kimahesabu ni kweli asilimia 16 ni mafanikio makubwa mno kuliko asilimia 0. Lakini pia asilimia 50 ni mafanikio makubwa kuliko asilimio 16. Hivyo, ni haki ya msingi kwa mchambuzi kusema kuna mafanikio ila siyo kama tuliyoambiwa tuyatarajie mwaka 2017. Wapo ambao tulitarajia hadi kununuliwa magari ya Noah nchi nzima ila wapi!

 

Dhahabu yetu ilipanda chati miaka 1990. Miaka ya 2020 ni fursa nyingine. Tusigombanie fito.

Vito vya kutosha kuutokomeza umaskini vipo. Ukiondoka takwimu zitaonesha. Hazitatuhadaa.