Harakati za kuwania urais zimepamba moto nchini. Nchi inaenda kushuhudia kwa mara ya kwanza uchaguzi wa vyama vingi. Wagombea wamedhamiria kushinda na si kushindana. Kila mmoja anaamini na amejiaminisha hivyo. Mtanange mkali hata hivyo uko kati ya Benjamin Mkapa na Naibu Waziri Mkuu wa zamani, Augustine Lyatonga Mrema; wengineo, kina Lipumba, Profesa mbuji wa uchumi, na John Cheyo, Bwana Mapesa, wanakimbizia vivuli vya wagombea hao wakuu kutoka vyama vya CCM na NCCR Mageuzi.

Wakati kampeni zilikuwa zimenakshiwa na kila aina ya tambo, propaganda na kejeli; nje ya ulingo huo wa siasa, yapo mengi mno yanayofukuta na kudhihiri. Kubwa kuliko lipo linalomsibu mfanyabiashara mashuhuri wakuitwa King Halfan King. Naye alikuwa miongoni mwa wachache waliokuwa na matamanio ya kuelekea ikulu. Yeye hakuwa mwanasiasa, bali alikuwa mfanyabiashara aliyetazamia kuitumia nguvu yake ya fedha kufanya ushawishi na uzengezi ilimradi aweze kufika ikulu. Ndoto yake hata hivyo inafifia kadri siku zinavyozidi kwenda. Muda haukuwa rafiki kwake, nao ukamtupa mkono, pale ambapo chama chake, CCM, kilipofunga milango, madirisha na mapazia ya kinyang’anyiro cha urais.

Wakati akitahayari kuhusiana na uchaguzi, ndipo hapo Bwana King akakutana na Christopher Marlone. Ndugu Marlone alikuwa na mpango kabambe utakaomuwezesha King kwenda ikulu, licha ya kwamba wagombea wa Urais walikuwa wamekwisha tangazwa na zoezi la kusajili wagombea wapya lilikuwa limeshafungwa mpaka uchaguzi mwingine. Mpango huo haukulenga kupitia mlango wa mbele na wala haukudhamiria kupitia mlango wa nyuma…mpango huu ulilenga kubomoa kabisa ukuta.

Ikiwa ndio ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, uchaguzi huo uliibua hisia kali sana ndani na nje ya nchi. Hamasa hiyo ilipelekea kuandaliwa mdahalo kati ya wagombea wa urais. Mdahalo huo ndio ambao Marlone alidhamiria kuutumia kama barabara ya King kuelekea ikulu, na yeye Marlone ndiye angekuwa mkandarasi mkuu. Wakati Marlone akiendelea kuichonga barabara hiyo itakayomsimika King ukuu wa nchi ya maziwa na asali, Tanzania, ndipo hapo sintofahamu juu ya mambo mbalimbali ilipoibuka na kumtoa Joram Kiango, mpelelezi maalum wa kujitegemea, kutoka mafichoni.

Barabara aliyokuwa akiichonga Marlone, haikuwa na punje la heri; haikuwa lami tamu ya kuteleza na kuliwaza, ilikuwa ni barabara shubiri iliyojawa damu na kede adha. Barabara hiyo ilianza kwa kushuhudia kifo cha Lilian, mpenzi wa King, na askari polisi ambaye alikuwa katika himaya na ulinzi mkali wa polisi. Safari ya King kuelekea ikulu ikaendelea kujawa na sintofahamu pale ambapo King alipojikuta akipelekwa Uingereza na Marlone kwa njia za magendo. Akiwa huko ndipo Marlone alipomueleza kinagaubaga kuhusiana na mpango wake kabambe wa kumpelekea ikulu. King alielezwa kuwa safari yake ya ukuu wa nchi ilihusisha ile siku maalum ya mdahalo wa wagombea urais. Marlone alimueleza King kuwa siku hiyo ndiyo ingekuwa siku ya mwisho ya safari ya maisha ya wagombea wote wa urais, katika uchaguzi huo. Wagombea hao walipaswa kuteketezwa wakati wa shughuli hiyo na hali hiyo na ombwe ambalo lingetokana na kitendo hicho lingezibwa na King.

Azma ya Marlone kumpeleka na kumsimika King ikulu ilikuwa ya dhati haswa. Uhodari na ujasusi wake haukuwa na shaka hata kidogo. Mipango yake yote ilienda na kutekelezwa kwa mafanikio makubwa, kama alivyopanga. Sasa zimebaki saa chache kabla ya kuelekea siku ya mdahalo. Si Joram Kiango wala mkuu yeyote yule wa vyombo vya upelelezi nchi waliweza kubaini kwa hakika mpango wa Marlone nyuma ya mapazia.

Je, Marlone atafanikisha azma yake na King hatimaye ataketi kwenye kiti kikuu cha nchi? Nini kitajiri? Je, hatimaye Joram Kiango atabaini yaliyojificha na kulifumbua fumbo hilo kuu?

Hakika hii ni riwaya ya kusisimua iliyoandikwa kwa lugha nyepesi, bunifu na yenye kueleweka na jamii yote ya waswahili. Unahimizwa kuweza kujipatia riwaya hii ya kurasa 146 tu, yenye jina Nyuma ya Mapazia iliyoandikwa na mwandishi nguli wa simulizi za kusisimua – Ben Mtobwa. Ninakusisitiza ufanye hivyo ilikuweza kutii kiu yako kama ambavyo nimeitii yangu. Kitabu hiki kinapatikana katika maduka mbalimbali ya vitabu nchini.

Kitabu kinachofuata ni Hati Nafsi kilichoandikwa na Lilian Mbaga. Je, wewe unasoma nini?