Mara nyingi nikiwasikiliza viongozi wa nchi-iwe marais, mawaziri na wakuu wa mamlaka mbalimbali pamoja na baadhi ya wanaharakati ninatatizwa na upeo walio nao juu ya suala la usawa wa kijinsia na ubaguzi wa kijinsia. Rais wa Zanzibar wa awamu ya nane, kwa mfano, toka aliposhika usukani, na tofauti na mtangulizi wake, amelivalia njuga suala la udhalilishaji wa kingono, hasa dhidi ya watoto. Hata hivyo, kwa vile aina ya udhalilishaji unaozungumziwa zaidi ni ule wa kingono madhila mengine ya kibaguzi wanayofanyiwa jinsi ya kike hususan hayamulikwi.

Tofauti kati ya maadhimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake inayoadhimisha mwezi wa Novemba kila mwaka na Siku ya Wanawake duniani inayoadhimishwa mwanzoni wa mwezi Machi ni katika kumulika upana na mseto wa ubaguzi, udhalilishaji, unyanyasaji, uhasi na dhulma dhidi ya jinsi ya kike. Mwanamke wa kawaida leo anapitia mchanganyiko wa hali hizi akipata msaada mdogo kutoka jamii yake au kutoka mamlaka husika.

Toka makala ya kwanza nimekuwa nasisitiza jinsi mitizamo hasi na ya kibaguzi inavyoigharimu jinsi ya kike haki, raha, uzima, ustawi, fursa na manufaa mengine mengi. Kisa nilochipitia wakati fulani kinaonesha namna kama wanawake tunakuwa hatarini kudhuriwa (vulnerability) kutokana na hali yetu ya kuwa wanawake. Siku kadhaa zilozopita nilipeleka gari langu kuoshwa. Niliuliza bei, nikataka kujua huduma walizonazo, mfano nilitaka pia nipigiwe hoverkunyonya taka na upepo kuondoa vumbi kwenye vipenyezi hewa (vents). Baada ya hapo nikataka kufahamu muda nitakaotakiwa kusubiri. Muda niliopewa nikaongeza mara mbili na nikamfahamisha nitakuwa nasubiri wapi akimaliza anifahamishe.

Miadi yetu ilikuwa gari lingekuwa tayari saa moja na nusu usiku lakini mpaka saa mbili usiku kimya. Kwa vile nlikuwa karibu sana nikamtuma mtoto akasikilize. Alipokuja na jibu kuwa gari tayari nikatoka kwenda kulifuata. Nilipofika sijakuta mtu. Wakati ninahodisha kuna mtu kando wa barabara akawashitua walioachiwa duka wanisikilize.

Wakaja vijana masharubaro. Wakati huo nafungua gari kujaribu kukagua lakini kwa vile giza lilikuwa limeingia nikataka wamulike kwa tochi. Vijana wakaja juu na majibu yao ya kisharubaro. Wakati nafungua nyuma ya gari nikauliza kama huko kumeoshwa. Kijana akajibu hakuosha kwani gari lilikuwa limefungwa. Lakini gari lilikuwa halijafungwa na nikamuonesha kuwa liko wazi. Akadai kajaribu kufungua kashindwa. Unajiuliza kwa nini hawakunifuata niwafungulie. Nikamuuliza kama injini imeoshwa akasema hajapewa maagizo hayo.

Kila niloliuliza sipati majibu ya kuridhisha ni ama sijaachiwa maagizo hayo au sijui. Ghafla akaja kijana mwingine akisogea nilipo kwa ubabe akiniambia nimekwenda pale nina “mawenge” na “maneno”. Akaja mpaka pale niliposimama akawa kanisimamia na akataka kunipita ila nafasi ilikuwa finyu kwa vile mlango wa kushoto wa nyuma niliposimama ulikuwa wazi. Akanipiga kikumbo huku akimtaka kijana aliyekuwa ananihudumia aachane na mimi. Nikahoji kauli yake kuwa hajui kuzungumza na maneno ya kutumia kama vile anazungumza na ‘mshikaji” mwenzake. Akaendelea kunipa lugha ya kibabe, akanijia usoni akijibizana kidogo aniingie maungoni. Kwa kifupi akawa kaingilia zoezi zima la ukaguzi wa uoshaji.

Yule kijana aliyekuwa anapewa amri alikuwa dhaifu hivyo akawa anamjali zaidi yule mwenzake kuliko mimi mteja. Kwa hadhi yangu kama mteja sijapata huduma bali manyanyaso. Wakati wale vijana wanaendelea na stizhai yao nikamuuliza kijana aliyewaita wenzake alipo, yaani yule aliyenipokea nilipoacha gari. Nikaambiwa katoka. Nikaomba apigiwe simu. Kwa makato nikaambiwa hapatikani mpaka baada ya saa tatu na nusu. Wakati huo ni saa mbili na nusu. Kwa hali ilivyokuwa inakwenda nikaona kuwa bora niepushe balaa niende nirejee siku ya pili nitakapomkuta aliyenipokea. Hivyo, nikasema nitarudi kesho lakini kwa vile walikuwa katika hali ya “kishikaji” soga lao limenoga huenda hawajasikia.

Nikarudi kwa jamaa zangu nilipokuwa nasubiri gari nikapakia mizigo niliyoitoa kabla sijapeleka gari kuoshwa. Nikawahadithia nini kimetokea na kuwaambia kuwa nitakuja kesho kulimaliza. Nimefika tu kwangu kuna simu imeingia namba ilikuwa ngeni kwangu. Nilipopokea mhusika akajitambulisha kuwa ni baba wa pale nilipoosha gari. Kwa vile ndio kwanza nimeingia nyumbani (na nilikuwa msalani) nikamuomba tuzungumze kesho. Akagusia salamu alizopewa na watoto. Mimi sikujua kuwa ni watoto wake nikijua ni wafanyakazi lakini kutokana na walivyonihudumia nikasisitiza bora tuonane kesho. Hapa alikuja juu akaanza kunitukana akiniita “muongo, malaya, mwizi, mshenzi na mzandiki”. Mwisho akanitishia akisema nitakutafuta ulipo. Utajuta nitakufanyia kitu kibaya hutasahau maisha yako”.

Kwa kweli nilipigwa na butwaa nikabaki namskiliza tu. Yeye mwenyewe akawa hajui kama bado nipo au sipo akaita “Hello? Hello?” Alipochoka na matusi yake akakata simu. Nilifadhaika sana lakini kutokana na muda ulivyosogea nikaona nisisumbue watu zaidi nitayashughulikia siku ya pili.

Kamwe sijafikiria kuwa lile aliloniambia mlinzi wa ninapolaza gari asubuhi iliyofuata lingeweza kutokea. Nilipokuwa najiandaa kutoka mlinzi alinifuata na kunihadithia yaliyojiri usiku huo. Aliniambia kuwa walikuja wanaume wapatao wanne wakitaka kulidhuru gari yangu. Wakati wote wakinikebehi “mwanamke” na kutaka kunitia adhabu eti nimeenda kuosha gari sijalipa. Mlinzi akatumia hekima na kumwita jirani yangu amsaidie na lile tifu. Bwana huyo katoka kwake masafa akaja kukabiliana nao na kufanikiwa kuwaondoa. Mimi hawajaniita maana hawajajua nini kingeweza kutokea.

Walipoulizwa chanzo cha zogo lote baba mtu akadai nimekataa kulipa pesa. Kiasi gani deni? Elfu sita! Jirani yangu akashangaa kuwa wamenifuata kote huku na kutaka kuvunja sheria kwa elfu sita? Akawapa pesa wakaenda zao.

Baada ya kuhadithiwa haya nikamwita mlinzi na kumfungulia gari aone hali ilivyo ndani kama limesafishwa au la? Ikumbukwe kijana tayari kakiri nyuma hajasafisha akidhani gari limefungwa. Lakini hata mbele sehemu mbalimbali gari halijaoshwa.

Nikapita kwa jamaa zangu kuwajuza kilichotokea. Walistaajabu. Walisema walitoa namba ya simu yangu kwa sababu alikuja baba mtu kistaarabu kuitaka ingawa walimuarifu kuwa nitarudi kumuona kesho. Baba huyo huyo alipotaka kujua ninaishi wapi alimfuata shemeji yangu na kudai anataka kununua gari yangu napatikana wapi? Akaambiwa maeneo ninapoishi. Kumbe akipanga yake na akanifuata.

Nimeamua kusimulia kisa kizima kwa urefu, mosi, kwa sababu wanawake wanakutwa wametupwa wameuawa bila ya kufahamu kisa au kiini cha mauaji na kwa vile hakijafanywa na mtu wa karibu kama mume au mpenzi inakuwa ngumu kuhusisha tukio la mauaji na kitu kilichotokea kama tukio la mimi kupeleka gari langu kuoshwa na mwenye biashara kutaka kunitia adabu akiambatana na genge la watu.

Pili, ninataka kusisitiza namna hadhi ya wanawake, uhasi dhidi ya wanawake na udhalilishaji wa wanawake unajengwa na kudumishwa. Nimegusia katika makala mengine namna mila, desturi, dini na tafsiri zake na hata sheria zinavyotumika kufanya hivi. Katika tukio hili tunaona dhahiri namna baba anavyowafunza watoto wake namna ya kumdhibiti mwanamke yoyote bila ya kujali anaweza kuwa nani kwake; au bila ya kujali uwajibikaji wao kwa yaliyotokea. Baba anayeweza kuwakokota watoto wanne kumfuata kibibi usiku kwake lazima afuatiliwe.

Binafsi kwa tukio hili ninaona kuwa kunaweza kuwa na watu katika sehemu nyeti au za huduma wanaonekana ni “watu wazima wenye heshima zao” kama alivyoamini mdogo wangu hivyo kuamini kutoa namba ya simu yangu kumbe ni wahuni tu. Ni kama fisi waliovaa ngozi ya kondoo. Wanasubiri fursa muafaka waoneshe makucha yao.

Tatu, ninataka kugusia na kusisitiza yale mambo yanayofanywa muda mwingi bila ya kutambua yanaweza kuhatarisha maisha, uzima au ustawi wa mwingine. Nilipokuwa ninasoma Marekani na nikifanya kazi katika kituo kilichokuwa kinashughulikia masuala ya ukatili, ikitokea tumemaliza kazi usiku mwenzangu akinirudisha nyumbani alikuwa haondoki mpaka ahakikishe nimeingia ndani nimewasha taa. Saa nyingine akitaka nimpigie au nimuashirie niko salama. Nilipomuuliza itifaki yote ya nini akaniambia kuwa mara nyingi wanawake wanashambuliwa wakiwa wanarudi kwao. Mtu anajibanza na kuwashtukizia wakiwa wanataka kuingia kwao. Akifanikiwa kuingia ndani naye ndio kazi inakuwa rahisi zaidi kwa mhalifu. Kutokana na kazi zetu hata sisi tungeweza kulengwa na mwenza mwenye hasira.

Funzo hilo nimelizingatia mpaka leo na kujaribu pia kulizingatia kwenye masuala mengine kama suala la mawasiliano. Mtu akitaka simu au anuani ya mtu kwanza lazma nimuulize mwenye namba kama nitoe au la maana hujui anamtaka kwa heri au shari. Ni sawa na wale wanaoomba kuazimwa simu halafu ikatumika kufanya uhalifu. Umempa simu kwa nia safi, mwenzako hajali taathira ya matendo yake na yuko tayari kukutia majaribuni kufanikisha lake. Mazungumzo mafupi yamemuwezesha mtu kujua ninakaa wapi kunifuata kuja kunidhuru pasipo waliotoa namba kushtuka kuwa wamehatarisha maisha yangu.

Nne, ni kuwa baada mambo yote haya kutokea na tuseme ningedhuriwa, chanzo cha suala zima kimewekwa nyuma. Baba mtu nimemkabidhi gari na nilimfahamisha nilipo. Kaondoka hajanifahamisha. Maagizo aliyoyatoa kwa watu wake siyajui. Wakati naacha gari hajanipa tanbihi kuwa sitamkuta na nifanye nini kama yeye hayupo. Hivyo, sikuwa na namna ya kujua nani ndiye kapewa dhamana ya duka kwani hakuna aliyenieleza hivyo nilipofika. Kuna kijana mmoja aliambiwa ajibu wakati nauliza maswali kuhusu usafi wa gari ila hilo halimaanishi kuwa kaaachiwa dhamana ya biashara.

Nimefanya jitihada kadhaa kutaka mhusika mkuu niliyefanya naye mapatano aitwe lakini vijana wakaona kwa nini ahangaishwa kwa ajili ya “mwanamke”! Ninasema hivi kwa sababu dakika 30 tu baada kutoka pale ghafla kapatikana na akaweza kunifuata mpaka ninapoishi na wanawe kuja kunitia adabu ilihali hawajastahili kudai chochote kwani hawajatimiza makubaliano ya kazi. Wametumia tu ubabe.

Hakika mlinzi na jirani yangu wametumia busara kubwa kulidhibiti genge la wahalifu la baba na vijana wake. Lakini unajiuliza iweje jambo limalizwe pasipo mhusika mkuu kuwepo? Najua kuwa lengo kuu la jirani yangu ni kuepusha shari kutokana na kile alichoniambia “watu siku hizi hawana muamana au mipaka hivyo bora kujinusuru badala ya kulumbana”. Hata hivyo, kutokana na uzoefu kuwa mara nyingi wanawake wanawekwa kando au kupigwa pande hata katika masuala yanayowahusu moja kwa moja ni vyema nikalimulika hili kusaidia katika uchanganuzi wa tukio hili kwa mtizamo wa kijinsia. Hali ni mbaya kiasi wapo wanaoona ili kunilinda bora nisihusishwe na hata kuonekana kwenye tukio ambamo mimi mhanga, ndiye mhusika mkuu!

Yapo mambo unaweza kuhadithiwa ukashangaa usiamini. Wenzetu wameendelea kwenye eneo la kukusanya ushahidi kutokana na kutumia zana mseto wa kukusanya ushahidi si tu maneno ya kuambiwa. Mji umesambazwa kamera za kunasa matukio mbalimbali. Vitendo vya baba na wanawe bila ya shaka ni vya kibabe hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa ni watu waliotanguliza ushari na si uungwana. Kitendo cha kumfuata mtu masafa kinaonesha nia ya kumdhuru hasa pale alipoambiwa mhusika atarejea siku ya pili. Kwa nini asisubiri kwanza?

Jibu langu ni kuwa kama mwanamke ilikuwa nikubali chochote kile walichoniamulia. Hakukuwa na sababu ya kunisikiliza au alau kufahamu mazingira ya kuondoka kwangu. Kama alivyoniambia kuli, “mwanamke ni wa kuambiwa tu!” kuwa ni shauri yangu, kukataa huduma mbovu ni kuwa muasi na jibu la kunikumbusha nafasi yangu ni kunitia adabu. Imefika hali mama anaadhibiwa na wanawe!

Matumaini yangu ni kuwa matukio kama haya yakitokea, ingawa ninakiri yanaweza kumkuta yoyote awe mke, mume, kijana, mzee, mtu mwenye ulemavu, mgeni na kadhalika, kuwa mchanganuo wa kijinsia utafanyika kuelewa mivutano (dynamics) inayotatiza suluhu kupatikana. Nina hakika mteja angekuwa ni wa jinsi ME asingefuatwa kwake kufanyiwa fujo. Nina hakika mwanamume asingepigwa kikumbo au kutukanwa matusi ya nguoni. Jamii imejikubalisha kuwa tabia kama hizi ni za kuwafanyia jinsi fulani tu kwani hawana namna ya kujibu. Au hata wakisema hawataaminika.

Utetezi wa haki, usawa, ustawi, uzima na uhuru wa jinsi ya KE unakwazwa na uhasi dhidi yao kwani uhasi na uhasama hutumika kama kitega uchumi kikuu kwa yeyote asiyethamini haki, utu na ustawi kudhalilisha wengine.