Kuvuna Viongozi wa Upinzani na Kisa cha Mtu Tajiri
Chambi Chachage
Kwa mara nyingine
uteuzi alioufanya Rais Magufuli umeibua mjadala mkali. Aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chama cha ACT Wazalendo, Mama
Anna Mghwira, kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kumepokelewa kwa
hisia tofauti: furaha, masikitiko, hasira n.k.
Mama huyo
aliyobobea katika taaluma ya theolojia atakuwa anakijua kwa undani kisa ambacho
Nabii Nathani alimsimulia Mfalme Daudi. “Palikuwa na watu wawili katika katika
mji mmoja”, Nabii alimsimulia Mfalme, “mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili
maskini.” Hivyo, yule “tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana; bali
yule maskini hakuwa na kitu, ila mwanakondoo mmoja mdogo, ambaye amemnunua na
kumlea; naye akakua pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake…akawa kwake
kama binti.”
Siku moja tajiri akapata
ugeni. Lo, badala ya kutumia utajiri wake mkubwa kumkirimu mgeni “alimnyanganya
yule maskini mwanakondoo wake.” Mfalme Daudi aliposikia hitimisho hili alikasirika
sana na kusisitiza kwamba mtu huyo asiye na huruma anapaswa kumrudisha yule mwanakondoo
mara nne.” Nabii Nathani akamjibu Mfalme: “Wewe
ndiwe mtu huyo.”
Nimekumbuka kisa
hiki usiku huu baada ya kusoma tamko la kumvua uwenyekiti wa ACT Wazalendo Mama
Mghwira ambaye alikaribishwa katika chama hicho kichanga, akalelewa katika
itikadi zake za Ujamaa wa Kidemokrasia hadi akagombea Urais mwaka 2015. Lepe la
usingizi likanipotea ghafla, ikabidi nimwazime Bibi yangu Biblia yake ili
ninukuu hicho kisa.
Hakika ni tamko
la kujitutumua mithili ya la Kijana Daudi dhidi ya Jitu Goliath. Kwa wachambuzi
wa kisiasa, ni muhimu kuzoea na kukubali kwamba matamko ya vyama hasa vile visivyotaka
ugomvi na Dola lazima yajaribu kuwa ya kidiplomasia. Hivyo, kama ilivyo ada,
ACT Wazalendo wanatoa matamshi ya kuuma na kupuliza au kukejeli kwa tafsida.
Lakini unaposoma kwa
jicho la tatu maneno kama haya yanayoelekezwa kwa Rais Magufuli ndipo
unapokikumbuka kisa cha mtu tajiri na mtu maskini: “Asichoke na asisite kuja kuvuna na
wengine maana tumeonyesha uwezo wa kutengeneza wengi wa aina hiyo.” Unabaki unajiuliza si ni hivi majuzi tu Kiongozi
wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alihojiwa na gazeti la The Citizen kwa barua pepe na kusema kwamba wao kama “chama
kichanga” wako “hatarini” na “kwa
kila mwanachama” wanayempoteza “ni pigo kubwa na hasa anapokuwa ni kiongozi”?
Wakati unatafuta
majibu unakutana na ujumbe wa leo wa Kiongozi wa Chama huyo uliokuwa kwenye ukurasa
wake wa Facebook ukisema: “Unajua
uimara wa vyama kwenye Mitihani kama hii inayotukuta sisi.” Hakika huu ni mtihani mkubwa hasa ukizingatia kwamba mmoja wa waasisi wa chama hicho, Profesa Kitila
Mkumbo, amekitosa chama kama yule nahodha aliyejitosa baharini kwenye ile Zilipendwa ya
wanamuziki wa Mlimani Park Orchestra. Hicho kilichokuwa
kichwa cha chama sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.
Ujumbe huo wa
Facebook wa Zitto Kabwe pia una maneno haya yanayoashiria kwamba teuzi hizi mbili
ni mapigo makubwa: “Wanachama 400,032 wa ACT Wazalendo mliotapakaa nchi nzima
msiingie kwenya malumbano na nyumbu.” Wanaofuatilia siasa za vyama vingi nchini
wanajua kwamba wanaofananishwa na nyumbu ni wafuasi wa CHADEMA ambako Zitto
Kabwe, Kitila Mkumbo – na hata Anna Mgwhira – ndiko walikotokea. “Asili ya
kuanzishwa kwetu”, ujumbe huo unasisitiza kuhusu hao mahasimu wao wa kisiasa, “ni kuukataa
unyumbu.”
Pamoja na kwamba
ujumbe huo umekwishafutwa
kwenye Facebook ya mhusika, kwa wachambuzi wa Saikolojia ya Siasa hiyo ni
ishara ya taathira ya uteuzi alioufanya Rais Magufuli. Unabomoa nguvu ya chama pekee cha
upinzani chenye itikadi mbadala kwa uliberali mamboleo na hivyo kufifisha demokrasia ya vyama vingi. Wapo wanaodai ni hatua ya aina yake na
inalenga kuleta ‘mseto’ unaonesha utayari wake wa kufanya kazi na wapinzani. Lakini
Wadadisi tunaona maneno yafuatayo ya Rais yanaashiria kwamba lengo lake ni kuwapa
nafasi ambazo zitawafanya wawe chini ya mamlaka yake ya kidola:
Demokrasia ya
Kibunge inayotenganisha mihimili ya Dola inafanya kazi kwa uthabiti pale ambapo Bunge
lenye Meno linaisimamia Serikali kijasiri. Hivyo, Serikali inayopambana na
ufisadi kwa dhati inapaswa kuwa tayari kuhakikisha kuna wapinzani mahiri
watakaoisakama Bungeni kwa ukweli na uwazi ili itekeleze majukumu yake vilivyo.
Na ndiyo maana Wadadisi wa Mambo tuliwahi kudai kama tungekuwa Rais Magufuli, tungesema
na kutenda hivi wakati wa kuteua:
Ila Rais wetu hapangiwi.
Anashauriwa tu. Na kama Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi alivyodadavua Bungeni: “Tutunze heshima ya Rais
akiwa Mkuu wa Nchi. Tutunze heshima ya Rasi akiwa Amiri Jeshi. Lakini inapokuja kwenye nafasi ya Ukuu wa Serikali,
serikali isimamiwe.”
Rais Magufuli katukumbusha
kwamba Mama Mghwira alikuwa na dhamiri na utashi wa kuweza kukataa uteuzi. Tunaomfahamu tunajua
ilikuwa ni vigumu kukataa. Na ndiyo maana
wachambuzi wa siasa kama mgawanyo wa mamlaka na rasilimali tunasisitiza kwamba, kuna mstari mwembamba kati ya hiari na shurti. Je, kweli chama maskini kimeridhia tu kumpoteza Mwenyekiti wake?
Chama tajiri nacho, je, kinataka kuua Upinzani ili kishike hatamu?




