Hatima ya zaidi ya asilimia 52 ya Watanzania inategemea mitizamo ya wale wanaopewa dhamana ya kusimamia masuala mbalimbali— ya umma na ya binafsi. Wanaharakati wanafahamu vyema kuwa unaweza kuwa na sheria nyingi na nzuri. Unaweza kuwa na mahakama na taasisi nyingine za kusimamia haki. Lakini kama wale wanaohudumu katika taasisi hizo au wale ambao wanategemewa kutimiza azma ya kisheria ya haki, basi sheria hizo zinakuwa hazina maana wala tija.
Mitazamo yetu inaweza kutufanya tukawa wapofu kwa hata yale ambayo ni dhahiri. Kuna mambo lukuki yanafanywa kila siku, tena hadharani lakini tunayaona ni kawaida au hatubughudhwi nayo kutokana na nani anayefanya na mtazamo wetu juu ya lile linalofanywa uko vipi. Itoshe tu kusema kuwa mitazamo yetu kwa ujumla wake ni ya kibaguzi.
Hii ni kwa vile kwa kiasi kikubwa mitazamo hiyo inaakisi ufahamu wetu juu ya nini kukitukuza, nini kukibeza? Nini kukithamini, nini kukidhalilisha? Kipi bora, kipi ni duni?
Ubaguzi uliokithiri ni ule wa kijinsia. Mbali na kukinyima kitu chochote ambacho kinaashiria au kutambua jinsi KE uhalali au heshima wengi wetu tunahalalisha ubaguzi huu kwa njia mbalimbali. Wako wanaodai ni kawaida; au ndio matakwa ya kimaumbile; au ndivyo maandiko yanavyosema; au ndivyo mila na desturi zetu zinavyoagiza…ilimradi sababu za kutukuza jinsi ME na kudhalilisha jinsi KE hazikauki kwani ni harakati za makusudi za kuuhami mfumo wa manufaa.
Nitajaribu kuonesha mifano kadhaa ambapo mitazamo fulani inaakisi ubaguzi wa kijinsia ninaouzungumzia na pia kuakisi yale mambo yanayothaminiwa katika jamii kutokana na nani anahusishwa na jambo hilo. Suala la mazingira limepata umuhimu wa kipekee siku za karibuni hasa baada ya nchi nyingi kupitia majanga yanayoaminika kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo ni moja ya vyanzo au dalili za uharibifu wa mazingira na ikolojia.
Ninaposikiliza vipindi, hasa vya redio na kidogo vya runinga, kuhusu uharibifu wa mazingira ninaona kuna mtiririko fulani wa simulizi juu ya masuala ya mazingira— iwe utunzaji wake, iwe uharibifu wake. Suala la kupanda miti kwa mfano limekuwa ni la kitaifa. Moja ya sababu kuu ya kupanda miti ni kupata uhakika wa mvua. Nyingine ni suala la nishati hasa kwenye kaya. Suala la ukataji miti litahusishwa na kuni za kupikia.
Hata hivyo, kuni anayotumia mama kupikia haisababishi uharibifu unaozungumziwa. Kuni zinazotumika katika viwanda, kwa kutengezea mikate ya boflo ya biashara, au magogo yanayokatwa kwa ajili ya mbao ndio hasa yanayosababisha uharibifu wa mazingira lakini kwa vile yanahusu viwanda vikubwa na uwekezaji mkubwa hili halipigiwi kelele sana kwa vile linaonekana kuchangia kiuchumi hata kama halina uendelevu. Anayekata kuni kwa upande wake anaweza kukata tu tawi ambalo litachipua tena. Lakini kwa vile shughuli hiyo si kubwa uhifadhi huo wa mti hauonekani kuwa nyeti katika kutunza mazingira.
Inafaa tuhoji kwa nini wanasakamwa wanotumia kuni haba tu?
Mfano mwingine ni suala la uchafuzi wa mazingira ambalo mara nyingi hutokea katika ngazi ya jamii. Kumekuwa na taarifa mbalimbali, tena za muda mrefu, kuhusu uchafuzi wa mazingira unaofanywa na baadhi ya shughuli za kibiashara. Uchimbaji wa madini, kwa mfano, ni suala linaloibuka mara kwa mara na linawahusu wachimbaji wadogo na makampuni makubwa. Mara nyingi serikali haipepesi macho kuwafungia wachimbaji wadogo wanaposhukiwa kutumia kemikali hatari au kusababisha athari za maumbile za mazingira mfano mashimo.
Hatua dhidi ya makampuni makubwa mara nyingi huchukua sura ya kuraiana, kubembelezana na hata kuziba masikio na kufumbia macho baadhi ya malalamiko ya jamii. Ni kwa vile tu mwekezaji mkubwa anaonekana kuchangia uchumi hata kama anatorosha madini na mapato mengi pia. Ila mchimbaji mdogo anaonekana ni mchafuzi tu ingawa shughuli zake ndizo zinazochangia pato la jamii yake moja kwa moja.
Kazi kubwa imefanywa na Lawyers Environmental Action Team (LEAT) kuibua baadhi ya uharibifu huu. Tena kwa ushahidi na hoja. Lakini mara nyingi wakikosolewa kama wachochezi na si kupongezwa kwa uzalendo wa kulinda urathi wa mazingira na utii wa sheria.
Kuna uchafuzi unaotokea pia katika ngazi ya makazi yetu. Uchafuzi huu mara nyingi huhusisha taka ngumu na laini. Ukifuatilia vipindi vya redio vingi utabaini kuwa wanawake hulaumiwa sana kwa kutupa pampers ovyo. Kwa vile vazi hilo huhusishwa na malezi ya watoto basi ni kawaida kulaumiwa mama na si baba. Pampers ni taka ambayo ni rahisi kuhamishwa na baadhi ya wakati kunguru au wadudu wengine wanaburuta taka wanapokuwa wanatafuta rizki. Mbali na wanajamii viongozi wa dini nao wako mstari wa mbele kuwalaumu wanawake kuhusu uchafuzi unaohusishwa na ulezi, hivyo inaonekana ni suala la jinsi ya kike.
Je, kuna kiongozi wowote wa kiserikali au dini au jamii anayekemea na kuchukua hatua juu ya uchafuzi unaofanywa na wanaume wengi kama shughuli ya kila siku ya kuwapatia rizki? Kwenye mazingira yangu ninaona vitu vingi vinafanywa na wanaume vinavyohatarisha mazingira. Lakini kamwe sioni mamlaka kuchukua hatua, viongozi kuvikemea au hatua za urekebu kufanyika.
Kitu cha kwanza ninachokiona kila siku nikiamka alfajiri ni vijana wa kiume wanaosha si chini ya gari kumi nyingi zikiwa ni taxi. Shughuli hii hufanyika kwenye sehemu ambayo watu hupita kwa miguu. Hivyo, mbali ya kadhia ya kuzibwa njia pia waoshaji huchafua sakafu kwa kuijaza tope. Kwa vile wanapata kipato unatakiwa unyamaze usiwakosoe.
Kwa vile wanaume wengi wanakaa maskani ni wazalishaji taka wakubwa mitaani. Kuna uharibifu unatokana na kelele iwe kutokana na mziki unaopigwa kwa sauti kubwa; au maongezi yaliyonoga juu ya mambo yasiyo ya msingi kwa kwetu sote kama mpira. Shughuli za kila siku mfano kula na kunywa pia husababisha taka ikiwemo za plastiki ambazo hazirejelesheki bila ya kusahau vipande vya sigareti vinavyonyonywa katika harakati ya mtu kuonekana DUME.
Gereji bubu na hata za halali nazo zinachafua mazingira mitaani mwetu. Mafuta machafu yakiingia ardhini yananyonywa na ardhi na kubaki muda mrefu. Sehemu yoyote inayoendesha gereji inakuwa na uoto hafifu haipendezi. Pia inakuwa chafu.
Ninamalizia na karaha ya manukato yanayohanikiza mitaani ya choo kikubwa na kidogo. Kuta za nyumba yangu zimesharabu mikojo kwani nyumba yangu imegeuzwa choo cha walinzi cha wawekezaji wakubwa wanaoendsha maduka na hoteli jirani yangu. Kwa vile wengi wao ni wanaume wakojozi hawathubutu kusogea kuwakojolea lakini mimi ninapaswa kuheshimu haja ya chululu hata kama inachafua nyumba yangu.
Kutupa taka ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Adhabu na Sheria inayohusu Tawala za Mikoa lakini sijawahi kuona mtu akikamatwa kwa kukojoa nje. Wala sijawahi kusikia kiongozi katika ngazi ya serikali, chama au dini wakikemea haya kama wanavyokemea pamperszinazotupwa na mama wasiowajibika. Nimelalamika miaka na kamera zinanasa kila kitu lakini hakujanaswa mhalifu wa kojo dume.
Imewahi kutoa Zanzibar wanawake kupigwa kwa kuvaa nguo zisizostahili. Wanaume vikojozi kutwa wanaonesha maumbile yao na kusababisha karaha kubwa na hawafanywi kitu. Wanawake wanaoshukiwa kujiuza hulaaniwa na kuvamiwa mara kwa mara lakini kamwe husikii hayo wakifanyiwa wanaume wanaotukana matusi ambayo yanalaani sehemu nyeti za jinsi KE ingawa matumizi ya lugha ya matusi ni jinai.
Imekuwa kawaida siku hizi vijana kutukana kama sehemu ya maongezi ilihali Kiswahili kina msamiati wa kutosha. Lakini kwa vile wanaofanya ni vijana wa kiume au wanaume wa makamo halionekani ni jambo kubwa au la kuchukuzia hasa ukizingatia kinachodunishwa au kudhalilishwa ni mtima wa uwana-jike. Msimamo uliotamalaki ni kuwa utegemee kutukanwa au kusikia matusi ukienda sokoni au kwenye mnada wa samaki utadhani matusi ndio kitoweo ulichofuata.
Kushindwa kukemea haya au kuyasema katika ngazi husika ikianza ngazi binafsi, kaya, mtaa, na madiwani au wawakilishi na kwenye mamlaka husika inathibitisha hoja yangu ya nini kinatukuzwa na kuthaminiwa na nini kinabezwa na kudharauliwa. Kwamba kwa muda mrefu hakuna anayehoji ‘unafiki huu’ na kuendelea kupima masuala yanayofanana kwa mizania tofauti (double standards). Huu ni ushahidi tosha kuwa mitazamo ya kibaguzi imezoeleka, imetamalaki na kudumishwa hata pale inapokera wengine au kuvunja sheria za nchi bila ya hatua ya maana na ya kudumu kuchukuliwa.
Hakika mitazamo hasi na ya kibaguzi inatukuzwa zaidi ya misingi ya utu, adabu na sheria.
Makala nzuri sana, Salma.
Asante Dada Salma. Asante mno, kulisemea hili la jamii kudumisha mifumo kandamizi kwa kupima vitu vifananavyo kwa mizania tofauti.