Mara kwa mara watu mbalimbali wamekuwa wanahoji dhamira ya wanaharakati wanaotetea matumizi ya Kiswahili kama Lugha ya Kufundishia kwenye shule na vyuo vyetu. Hivi karibuni nilikumbana tena na hoja ya aina hiyo. Ifuatayo ni sehemu ya maelezo yangu kuhusu kwa nini mimi binafsi natetea ufundishaji huo. Maelezo hayo yanatokana na jibu nililolitoa kuhusu swali hili: Utetezi wa Kujifunza kwa Kiswahili: Uzalendo au Unafiki wa Wajuao Kiingereza?

Sijawahi kupinga Kiingereza na wala sitakipinga ndio maana, kama inavyodaiwa, nakitumia sana. Nachosisitiza ni upatikanaji wa maarifa/ufahamu ulio sanjari/sambamba na ujuaji wa lugha husika. Hili linawezekana kunapokuwa na ufundishaji mzuri wa lugha husika pamoja na ufundishaji bora kwa kutumia lugha ambayo wanafunzi wanaielewa na kuitumia zaidi kwenye mazingira yao ya kila siku ili wahusianishe kile walichojifunza na mazingira wanayopambana nayo kila siku hatimaye waweze kuyabadili ili kuleta maendeleo yanayoendana na muktadha wa jamii yao .

Nachopinga ni hii dhana ‘potofu’ kuwa njia nzuri (na ya lazima?) ya kujifunza Kiingereza katika mazingira yetu ni kwa kukitumia kufundishia ilhali hatujui kukitumia vizuri kwa maongezi na maandishi. Je, hivyo ndivyo hao wazazi wetu wanaotumiwa kama mfano walivyojifunza Kiingereza vizuri kabla hatujaleta hii ‘sera ndumilakuwili ya lugha’? Tukitaka kuwa kama wao tuandae walimu wanaojua kufundisha Kiingereza kama lugha ya pili ili tuweze kukiongea vizuri na kukiandika. Hivyo ndivyo wao walivyoandaliwa na hakika kuna tofauti kubwa kati ya wale waliosoma kabla ya mabadiliko ya sera na wale waliofuatia.

Pengine inaonekana mimi ni mwandishi mzuri wa Kiingereza kutokana na hizo safu/makala zangu ila, laiti ingejulikana, msingi wangu wa Kiingereza sio mzuri kiasi hicho hivyo huwa napata shida sana kwenye suala la sarufi na tungo. Nilibahatika tu kidogo kukaa ng’ambo kwa mwaka mmoja hivi nikiwa mdogo ndipo hapo walau nilipata kauwezo ka ziada ka kuweza kujua Kiingereza kiasi kwa kutumia uzoefu wa asili (‘intuition’) lakini bado mpaka leo sentensi zangu hazijanyooka na nakatika sana hata nikiongea hivyo natumia muda mwingi sana kuziweka sawa ninapoandika. Mtu anaweza kuuita utetezi wangu wa Kiswahili unafiki ila mimi naongea kutokana na uzoefu wangu na uhalisia wa maisha niliyoishi hapa Tanzania hasa wakati nasoma Shule ya Msingi Mlimanina ya Sekondari Azania ambazo zote zilikuwa ni za Serikali.

Mfano naopenda kuutumia kuhusu jinsi ambavyo nilimaliza shule bila kujua maana ya spishi (‘species’), unadhihirisha kuwa sizungumzii suala hili kwa sababu najua Kiingereza na sitaki wengine wakijue. Kwa kuhitimisha nauweka mfano huo, na tafsiri yake, kutoka kwenye makala yangu ya Kiingereza kuthibitisha kuwa hili ni suala ambalo limeniathiri na kila ninapoenda kwenye shule zetu na naposoma vitu walivyoandika wanafunzi na jinsi wanavyoongea Kiingereza ‘kilichovunjika’ sana na hivyo kutoeleweka basi huwa najiuliza sana kwa nini tunawafanyia hivi watoto wetu kana kwamba ELIMU = KIINGEREZA = UTANDAWAZI = MAARIFA = MAENDELEO:

One day my teacher wrote this definition on the blackboard: “Species are groups of organisms that can interbreed to produce fertile of spring.” I knew the meanings of fertile and spring. But I couldn’t figure out how they fit in. Anyway, I memorized and reproduced it in the examination. As you can guess, I got it right.It was only later, much later, when I came to know what species are. Actually, they produce fertile offspring. I don’t know whether it was my teacher’s fault or mine. What I know is that as a boy I frustratingly tried to breed fish. But, alas, they produced infertile offspring! I didn’t know why. What a missed opportunity to relate what I was taught with what I practiced! I wonder if my teacher taught what she knew.Teaching is primarily about imparting knowledge. When you teach someone to cook ugali what matters mostly is that s/he ends up knowing how to cook ugali. Language is only a medium to facilitate knowledge exchange. And the efficient medium is the one that knowledge users know reasonably well. Could it be that we have politicized language at the expense of professionalizing it. Are we trying too hard to know the form to the extent that we ignore the content?

Tafsiri/Maelezo: Siku moja Mwalimu wangu aliandika maana ya neno spishi ubaoni. Maana aliyoandika niliinakili kama ilivyo. Siku ya mtihani nikaiandika vivyo hivyo. Nikapata vema. Lakini nilikuwa sijui maana hasa ya spishi japo nilikuwa najua maana ya maneno yote ambayo mwalimu aliyatumia kuelezea maana ya spishi. Nilikuja kugundua miaka mingi baadae kuwa kumbe kuna maneno mawili aliyotumia mwalimu kimakosa maana yalipaswa kuunganishwa na kuwa neno moja. Sina hakika kama mwalimu alilijua hilo na kuwa alikosea kwa bahati mbaya. Ila niligundua kuwa neno alilotumia lilisababisha nipate tafsiri hii ya kimakosa ‘Spishi ni kundi la wanyama wanaozalishana na kuzaa rutuba ya majira ya kuchipua’ badala ya tafsiri hii sahihi ‘Spishi ni kundi la wanyama wenye uwezo wa kuzalishana na hivyo kuzaa watoto ambao na wao wana uwezo wa kuzalishana wakikua.’ Cha kusikitisha ni kuwa kipindi nilipokuwa nikifundishwa spishi ndicho kipindi nilipokuwa nafuga samaki na kuna samaki walikuwa kamwe hawazalishani ila sikujua kwa nini. Je, hiyo haikuwa fursa nzuri ya kujifunza kwa vitendo kile kilichofundishwa na Mwalimu wangu wa Biolojia shuleni? Je, sikuipoteza fursa hiyo kwa sababu ya kufundishwa kwa Kiingereza bila kupata ufahamu/maarifa halisi ya kile kilichofundishwa, yaani, spishi? Mpaka leo najiuliza kama kweli Mwalimu wangu alikuwa anajua anachokifundisha kwa Kiingereza. Kufundisha kunahusisha zaidi suala la kutoa maarifa. Unapomfundisha mtu kupika ugali kilicho muhimu ni ajue kupika ugali. Lugha ni chombo tu cha kuwezesha kusambaza maarifa na kubadilishana taarifa. Na chombo kinachofanya kazi hiyo kwa ufanisi ni kile ambacho watumiaji wanakielewa vizuri zaidi. Kuna uwezekano kuwa tunaingiza siasa nyingi kuliko utaalamu husika kwenye hili suala la lugha. Je, tunajaribu sana kujua fani kuliko maudhui yake?

Lugha ni maarifa. Maarifa si lugha. Tutumie Lugha ya Kiswahili kukuza, kuhifadhi na kusambaza maarifa.