Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama ambacho kimeiongoza Tanzania tangu kilipoanzishwa. Kuanzia mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar zilipoungana kuunda Tanzania hadi mwaka 1977, vyama tawala vilikuwa ni Tanzania African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP). Kuungana kwa TANU na ASP mwaka 1977 ndiko kulikozaa CCM. Hivyo, Watanzania hawajawahi kutawaliwa na chama kingine chochote zaidi ya hivyo toka Tanganyika ilipopata Uhuru mwaka 1961 na Mapinduzi kufanyika Zanzibar mwaka 1964.

Kuanzia mwaka 1965 vyama vingi vilipofutwa hadi mwaka 1992 viliporuhusiwa tena, TANU na ASP – na baadaye CCM –vilikuwa vyama pekee vya kisiasa vilivyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria. Kila aliyetaka kufanya siasa wakati huo ilibidi afanye hivyo kupitia vyama hivyo tawala. Hivyo, kwa miaka 30 sasa Watanzania wamekuwa na uchaguzi wa chama wakitakacho lakini CCM imeendelea kubaki madarakani.

Katika Sayansi ya Siasa, Tanzania huwekwa na wasomi katika kundi la nchi zinazojulikana kama “Competitive Authoritarian” [Imla-Shindani] kwa maana kwamba ingawa vyama vingi vimeruhusiwa na uchaguzi wa kuchagua viongozi huwa unafanyika, chama kilicho madarakani kinafaidika na matumizi ya vyombo vya dola na mali ya umma kwenye kufanya siasa na hasa nyakati za uchaguzi.

Mifano ya nchi za namna hii ni kama Zimbabwe ambako mwaka 2008, baada ya mgombea wa upinzani, Morgan Tsvangirai kuonekana ameshinda, Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe ilikaa kwa takribani mwezi mzima bila kutangaza matokeo – huku vyombo vya dola vikitumika kufanya kazi ya kukamata, kupiga na kutesa viongozi na wafuasi wa upinzani mpaka uchaguzi uliporudiwa.

Tuliona pia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 Zanzibar ambako aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huku kukiwa na taarifa kwamba chama cha upinzani cha Civic United Front (CUF) kilikuwa kimeshinda uchaguzi huo.

Hata hivyo, ni makosa kudhani kwamba CCM imebaki madarakani kwa sababu tu ya faida ya kutumia vyombo vya dola na mali ya umma kwenye siasa. Chama hicho kinabaki kuwa miongoni mwa vyama vya siasa vilivyosukwa vema kiitikadi na kimtandao – kikiwa kimefika maeneo yote ya Tanzania, bila ya kuwa na eneo moja tu ambalo ni ngome yake.

Zimbabwe African National Union – Patriotic Front (ZANU–PF) inajipambanua kwa kuwa na ngome yake katika maeneo yenye watu wa kabila la Washona, National Resistance Movement (NRM) imetapakaa Uganda lakini inajulikana ngome yake iko Magharibi mwa Uganda na Kenya hakuna chama chenye itikadi bali ni muungano wa vigogo wa makabila tofauti wenye ngome katika maeneo yao hivyo wanaounganisha nguvu zao wakati wa uchaguzi ili watawale.

CCM iko nchi nzima, haina kabila linaloweza kujidai kwamba chama ni chake, kinatoa fursa kwa watu wa makabila madogo kuwa viongozi wakubwa – awe Mzanaki, Mndengereko, Mmakua au Mkwere, wote wana nafasi. Na pamoja na kwamba chama kimoja kimekaa madarakani, lakini marais sita tofauti wamekaa madarakani na hivyo angalau kuna taswira ya chama kinachofanya mabadiliko kila wakati kutokana na zama.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni – na kwa watu wanaofuatilia mitandao ya kijamii, ushawishi wa chama tawala unaonekana kupungua hasa miongoni mwa vijana. CCM yenyewe inafahamu hali hii na ndiyo sababu hata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kampeni haikuwa inahusu “Chagua CCM” kama ilivyozoeleka, bali “Hapa Kazi Tu” na “CCM ya Magufuli”. Ni wazi wataalamu wa mikakati ndani ya chama hicho waliona kwamba kusema chagua CCM pekee hakungetosha kuongeza kura.

Kwa nini ushawishi wa CCM umepungua na sasa kinahitaji kutumia nguvu zaidi kubaki madarakani kuliko ilivyokuwa zamani? Nini hasa kimesababisha hali ya sasa? Pengine, namna nzuri zaidi ya kujibu swali hili ni kuanza kudadavua kwanza kwa nini CCM ilipendwa huko nyuma?

Seti Benjamin wa Azimio la Arusha

Hakuna namna nzuri ya kueleza mapenzi waliyokuwa nayo Watanzania – hasa vijana kwa TANU na baadaye CCM – kuliko tukio la kifo cha kijana wa miaka 22, Seti Benjamin Mpinga, aliyefariki wakati akitembea kwa mguu kutoka Arusha hadi Dar es Salaam kuunga mkono Azimio la Arusha mnamo mwaka 1967.

Seti alifia njiani wakati akitaka kutimiza ndoto yake ya kuunga mkono kutangazwa kwa Azimio la Arusha kunakotajwa kama mojawapo ya matukio muhimu zaidi katika ujenzi wa taifa la Tanzania. Seti hakuwa kijana pekee aliyetembea kwa mguu – maelfu walifanya hivyo, lakini kifo chake kinabaki kama alama ya kujitoa kwa vijana kwa wakati huo.

Lakini waliotembea kwa miguu hawakuwa vijana au wananchi masikini peke yao. Ziko picha zinazomwonesha aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Julius Nyerere, akitembea kwa miguu kutoka Butiama kwenda Mwanza. Ni picha inayoonesha namna viongozi walivyokuwa kwenye mstari mmoja na wananchi.

Lakini, kwa nini Seti na wenzake waliunga mkono Azimio la Arusha? Ni kwa sababu lilitoa dira iliyoonesha mwelekeo wa kutengeneza taifa lenye usawa, haki, umoja na mshikamano. Ni Azimio lililofuta dhana ya mkubwa na mdogo au kutawala na kutawaliwa. Kubwa zaidi, lilifanya Watanzania wajione wanamiliki hatima ya maisha yao, uchumi wao na taifa lao.

Kwa hiyo Azimio liliwafanya Watanzania – hasa vijana, wajione wana fursa sawa. Ni muhimu kukumbuka kwamba Tanzania Bara ilikuwa huru kwa takribani miaka sita tu na wengi wa vijana na watu wazima waliokuwa hai wakati huo walikuwa wameonja adha ya ukoloni na kutawaliwa.

Ndiyo sababu, Nyerere – katika mojawapo ya hotuba zake kali kwa wafanyakazi wa Tanzania, aliwahi kuhoji wanamgomea nani kufanya kazi ilhali viwanda ni vyao? Kama kuna ‘ndumba’ iliyowahi kufanywa na TANU/CCM katika miaka yake 30 ya kwanza madarakani ilikuwa ni kuondoa dhana ya kuna ‘sisi na wao’ na badala yake kulikuwa na picha ya usawa na umoja.

Nimetoa mfano hapo awali wa fursa za watu kuwa viongozi mpaka katika ngazi za juu kabisa bila kujali dini, makabila wala jinsi(a) zao. Hili lilikuwa muhimu kwa sababu kila mmoja ndani ya Tanzania alijiona ana nafasi ya kufika katika ngazi za juu kabisa za mafanikio – kwa juhudi na maarifa yake.

Ilikuwa bahati pia kwamba mpaka kufikia mwanzoni mwa miaka ya 2000, Tanzania haikuwa na tatizo kubwa la ajira kwa vijana. Serikali ilikuwa na mashirika mengi ya umma yaliyokuwa yakitoa ajira kwa wingi na haikuwa kawaida kukuta kijana mwenye elimu walau ya sekondari kuwa hana ajira mitaani. Katika historia ya dunia, hakuna nchi yenye mgogoro na vijana wake wakati ajira ni jambo la uhakika.

Uwepo wa vyombo vichache vya habari vilivyodhibitiwa na serikali pia ilikuwa faida kwa CCM. Udhibiti huu ulimaanisha kwamba kwa kiasi kikubwa taarifa zilizokuwa zikiandikwa magazetini au kusomwa redioni zilikuwa ni zile tu ambazo ziliruhusiwa na chama na serikali na hakukuwa na namna ya kupata habari au mtazamo tofauti.

CCM ina wenyewe

Miongoni mwa nyimbo mashuhuri za kisiasa kuwahi kutungwa na hayati Kapteni John Komba na kundi la Tanzania One Theatre (TOT) ulikuwa ni ule usemao “Chama Cha Mapinduzi kina wenyewe”. Tafsiri iliyokuwa kichwani kwake pengine haikuwa tafsiri ambayo ilikuja kupokewa na wengi. Kwa walio nje ya mfumo, kauli hiyo ilichukuliwa kwamba CCM si tena chama cha wote – kina wenyewe. Lakini swali la kujiuliza wenye CCM ni akina nani?

Jibu lipo katika mabadiliko yaliyoanza CCM baada ya Mkutano Mkuu mashuhuri wa CCM wa mwaka 1992 ambao wasomi mashuhuri kama Profesa Issa Shivji wameueleza kama mkutano ulioasisi “kutunguliwa kwa Azimio la Arusha”. CCM ikaingia rasmi katika mfumo wa uchumi wa soko na iliyokuwa miiko iliyosimika usawa baina ya watawala na watawaliwa ikawekwa kando.

Mabadiliko – mengine ya lazima kulingana na nyakati, ikiwamo kuruhusu mfumo wa vyama vingi na vyombo huru vya habari na kuanguka kwa dola ya Urusi iliyosababisha dunia kuwa na mbabe mmoja tu – Marekani, ambaye kusambaza demokrasia ya kiliberali duniani kote ndiyo ulikuwa wajibu wake mkuu, yamekuwa sehemu kubwa ya matatizo yanayoifanya CCM isipendwe

Pamoja na mambo mengine, Azimio la Arusha lilifuta dhana iliyojulikana kwa jina la Wabenzi – neno lililokuwa likitumika kueleza kada ya viongozi wa serikali waliokuja baada ya Uhuru waliokuwa wakitumia magari aina ya Mercedes Benz kwenye shughuli zao za kikazi na binafsi. Badala ya Benz, sasa ‘wakubwa’ wanatambulika kwa ‘mashangingi’ au ‘Vieti (V-8)’ na misafara mikubwa yenye ulinzi mkali.

Wakati Nyerere alichukia hata kuona bunduki – mmoja wa wasaidizi wake aliwahi kunisimulia namna Mwalimu alivyosikitika siku ulipofanyika uamuzi wa kuruhusu askari kulinda benki kwa bunduki, siku hizi fasheni ni viongozi kulindwa kwa mitutu na silaha hata katika ziara za kuzungumza na wanavijiji.

Wenye CCM – kwa maana ya wimbo wa Komba na TOT, imekuja kutafsiriwa kama wale wenye fursa za kisiasa na kiuchumi, matajiri wanaofadhili wanasiasa na viongozi wenye ukwasi, wanaoendeshwa kwenye magari ya kifahari na kulindwa na ulinzi mkali.

Bomu la ukosefu wa ajira

Wakati fulani, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipata kuurejea msemo maarufu kuwa “mtu mwenye njaa, ni mtu mwenye hasira”.  Masharti ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwenye miaka ya 1980 yalisababisha serikali kushindwa kuendesha viwanda vyake na kufikia miaka ya 1990, ubinafsishaji ulifanya mashirika na makampuni Mengi ya umma kufa.

Wakati ajira za serikalini zikishuka, idadi ya vijana wanaomaliza elimu katika vyuo vikuu nchini imekua kwa kasi huku Tanzania ikiwa mojawapo ya nchi zenye viwango vya juu vya kuzaliana. Matokeo yake ni kwamba sasa, takwimu zinaonyesha ukosefu wa ajira sasa umefikia asilimia 10 – ingawa kuna wanaoamini huenda tatizo ni kubwa zaidi.

Ukosefu huu wa ajira umeibua kundi kubwa la vijana wenye hasira na msongo. Vijana ambao wana elimu, wana nguvu na ari ya kufanya kazi lakini hawana kazi wala namna ya kupata kipato cha maana. Katika historia ya Tanzania tangu Uhuru, hakujawahi kuwa na wakati ambapo kundi kubwa la vijana wenye elimu wana matatizo ya kupata ajira kama ilivyo sasa. Na kama hawana ajira, maana yake wana njaa. Na kama wana njaa, kama nimemnukuu Kinana sawasawa, maana yake ni kwamba wana hasira pia.

Vijana hawa wanaona maendeleo katika nchi nyingine kupitia televisheni na mitandao ya kijami. Matarajio yao kwa viongozi na ndoto zao ni makubwa kuliko waliyokuwa nayo vijana wa enzi za Seti Benjamin. Uwepo wa vyama mbadala vinavyotaka kuingia madarakani, pia kumetoa fursa ya watu kusikia mawazo mengine ya namna ya kuongoza nchi.

Bahati mbaya nyingine kwa CCM ni kwamba kwa hulka, mwanadamu ni kiumbe anayetaka mabadiliko. Kama kuna kitu kingine cha uhakika kwa mwanadamu – kuondoa maneno ya Benjamin Franklin ya kifo na kodi, basi kitu hicho ni kiu ya mabadiliko. Wakati mwingine, kuna watu wana kiu tu ya kuona chama kingine tofauti na CCM kikitawala. Kundi hili linafanana na lile lingine ambalo linatamani tu kuona CCM ikibaki madarakani kwa vile wamekizoea na hawana uhakika na maisha bila CCM.

Mustakabali wa CCM

Faida ya kwanza kwa CCM ni kwamba pamoja na changamoto zote zilizo mbele yake, bado iko madarakani. Nje ya madaraka, ‘dawa’ ya kujifufua na kutaka kurudi tena madarakani ingekuwa tofauti na hizi ambazo nataka kupendekeza kwenye makala haya.

Mosi, ni muhimu kwa CCM kujikita katika sera zitakazochochea ukuaji wa uchumi na ajira. Kama tatizo hili la ajira ambalo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amewahi kulieleza kama bomu linalosubiri kulipuka, litazidi kukithiri, mustakabali wa CCM huko mbele ya safari utakuwa kwenye hatihati.

Pili, ni muhimu kwa viongozi na wanachama kuanza kuondoa ile dhana ya chama kina wenyewe. Viongozi wanatakiwa kuanza kuonekana waungwana, wasio na kauli za kukera au kuudhi zinazoonyesha kutojali shida za wengine. Wanatakiwa kuonesha kukerwa na kero za wananchi kwa kupambana nazo na mara zote kuchochea umoja na si migawanyiko.

Katika siku za karibuni, kuna matamshi na kauli za viongozi hadharani na kupitia kwenye mitandao zinazoonesha hawajui nini hasa kinawasibu wananchi au wananchi wanataka kusikia nini katika wakati husika.

Jambo la tatu naliona hapa Uingereza sasa. Waziri Mkuu mpya, Liz Truss, alikuwa mwanasiasa mshari wakati akipanda ngazi kisiasa. Tangu amekuwa Waziri Mkuu – na baada ya misukosuko mikubwa kwenye wiki zake za kwanza, ameanza kupunguza mashambulizi dhidi ya wapinzani wake hasa wale wa ndani ya chama. Ninachokiona ni kwamba hakuna sababu ya kupigana vita vya ndani kwa ndani miongoni mwa wanachama wa chama kimoja.

CCM mara zote kimekuwa chama chenye makundi ya ndani kwa ndani lakini uimara wake umekuwa kwenye kuyaweka pamoja na kuhakikisha yote yanahisi yanatendewa vema kwenye chama. Ni muhimu kuondoa minyukano ya kuita wengine pengine Mtandao, Wakuja, Sukuma Gang na majina mengine. Mwalimu Nyerere alipata kuasa huko nyuma kwamba CCM ikipasuka, pengine huo ndiyo utakuwa mwisho wake. Kama CCM inataka kuendelea kudumu madarakani ni muhimu ikalinda makundi yake yote ya ndani.

Nne, ni kuhusu matumizi ya vyombo vya habari. Katika vuguvugu la mabadiliko katika nchi za Kiarabu barani Afrika, ushindi wa chama cha Bharatiya Janata (BJP) nchini India mwaka 2014 dhidi ya chama kikongwe cha Congress, mapinduzi ya Sudan miaka miwili iliyopita na ushindi wa Barack Obama mwaka 2008 – jambo moja linajitokeza kwa kujirudia; matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii.

Mustakabali wa CCM utaimarishwa na namna itakavyoitumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kwa ujumla kwa faida yake. Katika dunia ya sasa, kupoteza udhibiti wa suala nyeti katika mitandao ya serikali kunaweza kusababisha kuanguka kwa utawala ndani ya muda mfupi. Kama CCM itapata namna ya kufikisha hoja zake na kuteka hadhira mitandaoni, itabaki kuwa salama.

Tano, ni suala hili la kupanda kwa gharama za maisha linaloendelea sasa. Uingereza na nchi nyingine za Ulaya tayari zimetangaza uwezekano wa kuwepo kwa mgawo wa umeme na hatari ya kupanda kwa bei za mafuta. Hii maana yake ni kwamba – kama hali itaendelea namna hii ya Vita ya Ukraine, hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika miezi michache ijayo.

Kama mafuta yatapanda bei zaidi na nchi wahisani kuingia katika taabu kiuchumi, ni wazi nchi nyingi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, nazo zitaingia katika taabu kubwa. Sikuwa nimezaliwa kwenye miaka ya 1970 wakati bei za mafuta zilipoleta anguko kubwa la uchumi lakini tayari wachumi na wanahistoria wa Ulaya wanazungumzia kurejea kwa nyakati zile.

Katika taifa ambalo tayari lina changamoto zake tayari, ni muhimu kwa CCM kujiandaa na hali ngumu zaidi kiuchumi katika miezi michache ijayo. Ni muhimu kujua hali ikiwa mbaya zaidi ni hatua zipi zitachukuliwa na namna gani taarifa zitafikishwa kwa wananchi.

Ikrari, nawaonea huruma wale waliovaa viatu vya kuongoza CCM na Serikali wakati huu. Pengine wanafanya makubwa kuweka mambo sawa. Lakini lawama na malalamiko yanaendelea kila uchao; na labda wanajiuliza; pamoja na yote haya – kwa nini wanatuchukia namna hii?

Nimejaribu kutoa sababu chache.