Yapata mwaka mmoja toka tumpoteze yule mchambuzi mahiri, Lionel
Cliffe. Uchambuzi wake wa migongano ya maslahi Tanzania bado unahitajika
leo. Hebu tuurejee
kwa kina.
Katika uchambuzi huo, Cliffe anaanza kwa kusisitiza kuwa mabunge
mengi katika nchi za Jumuiya ya Madola yalimzuia Mbunge kulipigia kura au kuliongelea
suala ambalo ana maslahi binafsi nalo. Lakini baada ya uhuru baadhi ya mabunge
yaliamua kuondoa zuio hilo linaloaibisha. Inaonekana alikuwa anamaanisha kuwaaibisha
waheshimiwa.
Wabunge wa Tanzania, mwanazuoni huyo anaendelea kusisitiza,
hawakuwahi kuzuiwa kiasi hicho ama ‘kivile’. Kanuni za Kudumu za Bunge zilikuwa
zimewazuia tu kuongelea masuala ambayo wana maslahi binafsi ya kifedha bila kuweka wazi aina na ukubwa wa maslahi hayo.
Rekodi alizozipitia mtafiti huyo zinaonyesha kuwa katika kipindi hicho inaonekana
hakukuwa na maslahi yaliyowekwa wazi wala mgongano wa tafsiri ya kanuni.
Hata baada ya Azimio la Arusha kuleta mwongozo wa viongozi na
sheria iliyowalazimu wabunge kuorodhesha maslahi yao ya kifedha kwa Spika, bado
utekelezaji wake ulikuwa ni mgumu. Japo sheria hii pia iliwahusu wake za
wabunge, mtafiti huyo anasisitiza kuwa haikuwagusa ndugu wote, hivyo, baadhi ya
wabunge walitumia kipindi cha mpito kusajili maslahi yao binafsi kwa ndugu zao
au kuanzisha makampuni ya muamana (trusts/waqfs)
kwa manufaa ya watoto wao. Pamoja na hayo, sheria ilizuia sana migongano ya
maslahi.
Jambo moja ambalo uchambuzi huu wa kihistoria unatukumbusha
ni kuwa mgongano wa maslahi binafsi wa kifedha unaweza kuwa na uhusiano wa
karibu sana na (unaoonekana kuwa ni) mgongano wa maslahi binafsi usio wa
kifedha. Unaweza usipate hata senti moja lakini ndugu, mfanyakazi au hata
rafiki yako akapata kitita cha pesa. Pia wote mnaweza msifaidike kiuchumi ila
kwa namna moja au nyingine mkanufaika kijamii n.k. Mtaji wa kijamii (social capital) nao ni faida tu kama
ulivyo mtaji wa kifedha (financial
capital).
Mheshimiwa mbunge huwezi kujipatia umaarufu mkubwa wa kisiasa
(political capital), unaoweza hata
kukufanya uwe Rais 2015, kwa kulivalia njuga sakata la ufuaji wa umeme wa
dharura bila kuwa wazi kuwa wewe na ndugu zako mna kampuni binafsi ya
uzalishaji wa umeme. Ndiyo, mbunge huwezi kulisemea hilo bila kueleza kuwa wewe
au wasaidizi wako wananufaika kwa namna fulani na malipo yatokanayo na kesi
lukuki za sakata hilo.
Suala hili haliwahusu wabunge wetu tu. Linatuhusu sote tulio/tutakaokuwa
katika nafasi za kufanya maamuzi yanayogusa umma japo pia yanagusa maslahi
yetu binafsi ama ya watu walio karibu nasi. Anahusika yule jaji pale wa shindano
lile anayejuana na mshiriki au mmiliki wa kikundi cha washiriki wale. Yule
mjumbe wa bodi ya kuamua vitabu gani vitumike ilhali rafikiye anamiliki kampuni
ya uchapishaji anahusika. Huyu, huyo na yule.
Nani anayenufaika au kutonufaika na mgongano wa maslahi? Ni
mimi. Ni wewe. Ni sisi. Jukumu la kuyaweka wazi maslahi binafsi, yawe ya
kifedha au yasiwe ya kifedha, ni la nani? Ni lako. Ni langu. Ni letu. Maslahi
ya nchi ni ya nani? Ni yangu. Ni yako. Ni yetu.