Nilipomsikiliza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe akiwasilisha matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi jana [10/12/2009], roho iliniuma lakini sikushangaa.

Najua nchi yetu inakabiliwa na changamoto nyingi katika utoaji wa elimu ya msingi kwa wote. Baadhi ya changamoto hizi ni za kawaida kama uchache wa rasilimali kulingana na mahitaji, lakini baadhi yake zinatokana na kutokuzingatia mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji ya UPE ya kwanza, na mengine ni muendelezo wa historia hiyo hususani maandalizi ya walimu chini ya mipango ya UPE, MMEM na MMES.

Matatizo mengine ni kama ilivyo katika taasisi nyingine za umma: usimamizi mbovu, kukosa uzalendo kwa baadhi ya wasimamizi na watendaji kunakopelekea kuwepo kwa mazingira na mianya mingi ya rushwa na ufisadi; pamoja na walimu kuvunjika moyo kutokana na masilahi yao kutokuzingatiwa kwa wakati. Pamoja na matatizo haya na mengine mengi, lipo hili la lugha ya kufundishia.

Nalizungumzia tena suala la lugha ya kufundishia kutokana na kuwa mwaka huu kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma, kiwango cha kufaulu somo la Kiingereza ni hafifu (asilimia 35.4), tofauti na Kiswahili ambacho waliofaulu ni asilimia 69.08. Na wizara yetu bado inang’ang’ania kufundisha masomo yote ya sekondari kwa Kiingereza!

Hivi tatizo ni nini hasa? Ni wanataaluma kushindwa kuwaelimisha wanasiasa kuhusu sayansi ya ufundishaji wa lugha za kigeni na jinsi ya kujenga mfumo na stadi za mawasiliano ya lugha mbili au ni wanasiasa, kudhani kuwa kwa kuwa tu nao ni wasomi hata kama si wa fani ya lugha basi wanayo tiketi ya kuisemea taaluma ya ufundishaji wa lugha na ukuzaji mitaala ya lugha kiasi cha kupingana na matokeo ya tafiti za wataalamu wa fani hiyo?

Kwa takribani miongo miwili sasa kumekuwa na malumbano kati ya wanataaluma wa lugha na wanasiasa kuhusu lugha ya kufundishia. Mimi niliufuatilia mjadala huu hadi ukanikirihi. Ushauri wangu kwa wanataaluma ya lugha ambayo pia ni fani yangu ikawa kuwa tujaribu kupambanua jinsi mfumo wa lugha mbili unavyojengwa.

Kimsingi, malumbano ya lugha ya kufundihia iwe Kiswahili au Kiingereza yanaficha ukweli kuwa, mtoto anaweza kujifunza na kutumia lugha nyingi kwa wakati mmoja. Kinachogomba ni jinsi lugha hizo zinavyofundishwa na kutumiwa katika mawasiliano. Kimsingi lugha ngeni inakuwa rahisi kujifunza kama una msingi mzuri wa lugha unayoitumia kwa mawasiliano ya kila siku, na lugha ambayo haitumiki katika mawasiliano nje ya darasa inapaswa kufundishwa kwa kutumia matini mengi yanayoasili au kuwakilisha mazingira halisi ya mawasiliano.

Kwa mfano, mazungumzo anuai yaliyonaswa katika kanda, matumizi ya redio, televisheni na vitabu vingi vya hadithi zenye maudhui yanayohusu nyanja mbalimbali za maisha na mazungumzo ya kawaida ya watu wa rika mbalimbali walio katika mazingira anuai yanaweza kutumika. Matini haya yanapaswa yasindikizwe na mazoezi mengi ya kusikiliza(uelewa), kuongea, kusoma na kuandika (ufasaha), kwa kutumia fani anuai za nathari, fasihi na wizani. Mambo haya hayazingatiwi vya kutosha katika ufundishaji wa Kiswahili na Kiingereza lakini tofauti na Kiingereza, Kiswahili kinatumika zaidi ndani ya jamii, hivyo wanafunzi wanatokea kukimudu zaidi.

Laiti wanasiasa wangewataka wanataaluma watunge mtaala mzuri wa matumizi ya lugha mbili, na kuwahakikishia kuwa katika mtaala huo mhitimu atamudu vizuri mawasiliano kwa Kiingereza na Kiswahili bila kujali ni lugha ipi kati ya hizo inatumika kufundishia, nadhani mustakabali wa elimu yetu sio katika lugha tu, bali masomo yote ambayo ni vigumu kuyaelewa kama lugha ‘haipandi’ kama vile hisabati na masomo mengine ya kinadharia ungekuwa bora kuliko ilivyo hivi sasa.

Wenzetu katika Ulaya ya kale walifanikiwa kufanya mapinduzi makubwa katika sayansi na teknolojia pale tu walipoanza kutumia lugha za kinyumbani badala ya Kiyunani na Kilatini katika fani zote za kisanaa na kisayansi—kipindi hiki walikiita ‘renaissance’ (mwamko). Vivyo hivyo mafanikio ya hawa ‘Duma’ (Tigers) wa Asia ya Kusini Mashariki tunaowasifia sana yaliambatana na uhamishaji wa matini ya taaluma zote kuwa katika lugha zao na kuzitumia lugha zao kufundishia hadi vyuo vikuu.

Hii haina maana kuwa Wanazuoni wa Ulaya hawakuendelea kuzamia na kubobea katika Kiyunani na Kilatini au ‘Duma’ wa Asia katika Kiingereza na lugha nyingine za Ulaya, la hasha. Hii ndiyo maana ya ‘bilingualism’ kama mfumo wa lugha mbili unavyojulikana kitaaluma. Ingefaa wataalamu wetu wa ufundishaji wa lugha za kigeni wachukue muda wa kutosha kuulewesha umma na hususani umma wa wanasiasa jinsi ‘bilingualism’ inavyojengwa.

Lakini kama wasemavyo Waswahili, sikio la kufa halisikii dawa. Je, sisi ni sikio la kufa?

Kazi kwenu wazalendo maana mwenye macho haambiwi tazama!

© Demere Kitunga, 11/12/09