MAISHA YA DK. REGINALD ABRAHAM MENGI YALITUGUSA WENGI KWA NAMNA NYINGI
NA
RONALD B. NDESANJO
Asubuhi ya Mei 2 Watanzania wengi waliamka na habari za simanzi kufuatia kifo cha Dk. Reginald Abraham Mengi kilichotokea huko Dubai-Falme za Kiarabu. Si kawaida yangu kuandika taabini pale watu maarufu wanapotangulia mbele ya haki. Ila kwa Dk. Mengi imenilazimu kufanya hivyo. Nitafafanua hapa.
Dk. Mengi ni mmojawapo kama si Mtanzania pekee (mweusi/mwafrika) ambaye amepata mafanikio makubwa sana kiuchumi tangu tupate Uhuru na pengine hata kabla ya hapo. Kwa kipindi chote cha historia ya uchumi wa Tanganyika (na baadaye Tanzania), mafanikio makubwa ya kiuchumi yalikuwa yakihusishwa (kuwahusu) zaidi Watanzania wenye asili ya Kiasia hasa Waarabu na Wahindi. Kutokana na mafanikio yake makubwa kiuchumi, Dk. Mengi alionekana ni shujaa kwa kuvunja desturi hii na kujipambanua kuwa “anaweza.”
Binafsi nadhani kuweza huko ni jambo liliompa Dk. Mengi upekee wa aina yake. Hivyo, naweza kusema kuwa watu wengi tulimtazama Mtanzania huyu kwa namna ya pekee kidogo. Katika taabini hii nitaeleza, japo kwa ufupi, namna nilivyomtazama na kumfahamu.
Katika kipindi cha uhai wake nilibahatika kumuona ana kwa ana mara mbili tu. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2000 (kama nakumbuka vizuri) kule mjini Moshi-Kilimanjaro. Wakati huo Dk. Mengi alikuwa amekuja kufunga msimu wa mashindano ya mpira wa wavu ya Bonite (Bonite Volleyball Championship). Mashindano haya yalianzishwa mwishoni mwa miaka ya themanini chini ya udhamini na usimamizi wa kampuni ya vinywaji baridi ya Bonite, mojawapo ya makampuni aliyokuwa akiyamiliki.
Mara ya pili kumuona Dk. Mengi ilikuwa ni takribani miaka saba baadaye, wakati huo nikiwa mwanafunzi wa shahada ya kwanza pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Siku hiyo alikuwa mgeni mualikwa katika kongamano la masuala ya ujasiriamali liliokuwa limeandaliwa na baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho. Nakumbuka mmojawapo wa waratibu wa kongamano hilo alikuwa ni Ndugu Jokate Mwegelo ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani.
Wakati ule Mheshimiwa Jokate alikuwa tayari anajihusisha na masuala ya ujasiriamali pamoja na kuwa mwanafunzi wa shahada ya kwanza pale UDSM. Nadhani lengo la kumkaribisha Dk. Mengi lilikuwa ni kutaka kupata uzoefu wake katika biashara. Pengine lilikuwa na kuwapa wanafunzi hamasa ya mambo ya ujasiriamali.
Miongoni mwa wageni wazungumzaji alikuwepo pia mwandishi maarufu wa riwaya nchini na mjasiriamali, Erick Shigongo. Nakumbuka wakati wa hotuba yake Ndugu Shingongo alionesha hamasa kubwa ya kufanikiwa zaidi kiuchumi kwa kumwambia maneno ya kimombo Dk. Mengi kuwa anamfuata huko aliko (kiuchumi); ….“I am coming brother”…. Sijajua amefika hatua gani katika safari yake ya kumfuata mwenzake kwenye mafanikio ya kiuchumi na kijasiriamali. Wacha nirejee kwa Dk. Mengi.
Tangu mwishoni mwa miaka ya themanini na nusu ya kwanza ya miaka ya tisini niliifahamu zaidi (kwa kusikia) chapa ya Industrial Promotion Projects(IPP) kuliko hata mwenyewe Ndugu Mengi (wakati huo hajawa Dakta). Hii ilikuwa hasa kupitia matangazo ya redioni ya bidhaa zilizokuwa zikitengenezwa/kuzalishwa na makampuni mbalimbali ya IPP. Kilichokuwa kikinivuta zaidi ni kile kibwagizo cha lugha ya kimombo cha “IPP Cares for You” ikimaanisha “IPP inakujali” kilichokuwa kikisindikiza tangazo la kila bidhaa ya IPP.
Binafsi nadhani huu ulikuwa ubunifu wa hali juu katika ujenzi wa chapa (brand building). Kwa kiasi kikubwa, dhana ya “kujali” ndiyo ilikuja kuwa msingi wa “falsafa” ya Dk. Mengi hasa katika mambo ya jamii; “mtu anayejali wengine” kama alivyokuwa akijinasibu mwenyewe na wengi walivyokuwa wakimtazama. Sina hakika kama mambo haya mawili yalikuwa na uhusiano ama ilitokea kwa bahati tu (coincidence).
Kati ya mwaka 1994 na 1995 kulitokea kile ninachoweza kukiita “Mapinduzi ya Sekta ya Habari” kufuatia kuanzishwa kwa vyombo binafsi vya habari hasa vituo vya redio, televisheni na magazeti. Kati ya hivi zilikuwa ni Radio One Stereo (Sasa Radio One) na Independent Television (ITV). Wakati ule kituo maarufu (cha redio) kilikuwa ni Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Ujio wa vyombo vipya ulileta hamasa kubwa kutokana na mpangilio wa vipindi ambao ulionekana wa kisasa na wenye mvuto hasa kwa vijana.
Japo nilikuwa nina umri mdogo sana wakati ule bado nakumbuka vyema jinsi watu walivyokuwa wanafurahia vipindi hasa vya muziki mpaka kufikia hatua ya kurekodi katika kanda za kaseti. Mimi ni mpenzi wa Muziki wa Hip Hop na hasa wa wasanii nguli kama Marehemu Tupac Shakur wa Marekani. Mara ya kwanza kumsikia Tupac Shakur ilikuwa ni kupitia Radio One Stereo. Bahati mbaya ndipo alikuwa amefariki kwa shambulizi la risasi.
Nakumbuka watangazaji maarufu wakati ule walikuwa ni DJ Rankim Ramadhani na Misanya Dismas Bingi (wote hawa wameshatangulia mbele ya haki). Hawa niliwafahamu kwa sababu walikuwa wanafanya vipindi vya usiku muda ambao tuliweza kukamata mawimbi ya redio. Hizo ni zama za “Chombeza Time.”
Upande wa televisheni ya ITV nako mambo yalikuwa moto moto. Bado nayakumbuka sana yale matangazo ya bidhaa za IPP kama sabuni ya Revola. Kuna wakati ulizuka uvumi kuwa wale mabinti warembo waliokuwa katika matangazo yale walikuwa watoto wa Dk. Mengi. Ni katika kipindi hicho ndiyo nilianza kumsikia mtu aliyekuwa nyuma ya IPP, Radio One Stereo na ITV; Reginald Mengi, tajiri mkubwa Tanzania na Mtanzania mzaliwa wa Machame, Kilimanjaro.
Kati ya mwaka 1997 na 2000 “nilibahatika” kusoma katika Shule ya Sekondari ya Lyamungo iliyoko Machame Wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro. Shule hiyo ilikuwa kijijini Lyamungo jirani kabisa na kijiji cha Nkuu alikozaliwa Dk. Mengi. Pamoja na mambo mengine, shauku yangu kubwa baada ya kufika shuleni ilikuwa ni kupaona nyumbani kwa Mengi; tajiri mkubwa kabisa wa Tanzania na “mzawa” haswa! Nilikuwa nimefahamishwa na wanafunzi wenzangu wanaotokea maeneo ya Machame kuwa nyumbani kwa Mengi hapakuwa mbali toka shule yetu ilipo na siku muafaka ikifika nitapaona tu.
Hatimaye siku yenyewe ikawadia. Ilikuwa ni safari ya kwenda shambani eneo la Maili Sita pembezoni na barabara kuu ya Moshi-Arusha. Safari ilianzia kijijini Lyamungo kupitia Nkuu, Makoa, Machine Tools (kilichokuwa kiwanda cha vipuri vya mashine) na hatimaye Maili Sita. Tulipofika kijiji cha Nkuu nikakaa tayari kupaona kwa Mengi. Punde nikaoneshwa uzio wa bogavilia (bougainvillea) ambao kwa ndani nadhani kulikuwa na ukuta. Ndani ya uzio kulikuwemo nyumba ya kifahari hasa ukizingatia mazingira na aina ya nyumba zilizokuwepo maeneo ya jirani. Pia niliona gari la kifahari (nadhani ilikuwa Mercedes Benz ile) katika eneo la maegesho.
Niliweza kuyaona yote haya kwa sababu nilipanda juu kabisa kwenye bomba za lori la shule. Kwa kweli ilikuwa siku ya kipekee kwangu kwani hatimaye nilipaona alipozaliwa tajiri mkubwa mzawa wa Tanzania. Nakumbuka niliporejea nyumbani wakati wa likizo niliwatambia sana wenzangu kuwa nimeshapaona nyumbani kwao Mengi na shule yetu iko kijiji cha jirani na hapo.
Sasa nizungumzie kidogo kuhusika kwa Dk. Mengi katika harakati za uhifadhi wa mazingira nchini Tanzania; jambo ambalo binafsi nililiona la kipekee na kupongezwa pengine kwa sababu ni eneo ninalifanyia kazi. Kati ya mwaka 1997 na 2006 Dk. Mengi alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Karibu robo tatu ya uwenyekiti wake, sheria ya mazingira inayofanya kazi sasa na kusimamiwa zaidi na NEMC ilikuwa haijatungwa (sheria imeanza kufanya kazi mwaka 2005).
Kwa kiasi kikubwa shughuli za/na uwepo wa NEMC vilianza kujulikana zaidi baada ya sheria hii kuanza kufanya kazi. Kabla ya hapo ni watu wachache walifahamu juu ya baraza hili na shughuli zake. Katika kipindi cha uongozi wake, Dk. Mengi alitumia nafasi na ushawishi wake kutia hamasa ya uhifadhi wa mazingira. Nakumbuka NEMC ilitajwa na kufahamika sana kipindi hicho. Nakumbuka mwaka 2004 nilipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea masuala ya mazingira baadhi ya jamaa zangu walikuwa wakinikejeli kuwa nataka kuwa kama Mengi; wakimaanisha kujihusisha na mambo ya uhifadhi wa mazingira.
Mnamo mwaka 2000 wakati Dunia inaingia katika karne ya 21 mpango kabambe wa Shirika la Umoja wa Mataifa wa Malengo ya Milenia ulianza rasmi. Lengo mojawapo ilikuwa ni uhifadhi endelevu wa mazingira. Hapa nchini Tanzania ilianzishwa kampeni kabambe ya Kitaifa ya upandaji miti (pamoja na mambo mengine) chini ya kitengo cha mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Dk. Mengi alikuwa mstari wa mbele katika kampeni hiyo. Mbali na ushiriki wake kama mwenyekiti wa NEMC, amefanya kazi ya uhifadhi wa mazingira kwa takribani miaka 30 kupitia Kampuni ya Bonite aliyokuwa akiimiliki. Jambo hili ni somo muhimu sana kwa wafanyabiashara na makampuni makubwa kwani linawakumbusha kuwa wanao wajibu (na sio hisani) wa kustawisha mazingira ya kijamii na kiikolojia katika maeneo wanamofanya biashara zao au kuvuna malighafi zinazotumika katika shughuli zao za uzalishaji.
Katika kipindi cha karibu miongo mitatu, hivi ndivyo nilivyomtazama na kumfahamu Dk. Reginald Abraham Mengi.