Majibu ya Magufuli na Kazi ya Kikatiba ya Wanahabari

Chambi Chachage

Hatimaye Rais Magufuli amekidhi kiu ya wananchi tuliokuwa tunasubiri kwa hamu atangaze Baraza jipya la Mawaziri. Mjadala mkali kuhusu uteuzi wa baadhi ya ‘wale wale’ wa ‘CCM ni ile ile’ unaendelea mitandaoni, runingani na ushorobani. Kujikita katika kujiuliza kwa nini huyu, huyo ama yule yupo au hayupo kunaweza kusababisha tusahau kujadili kwa kina jambo lingine muhimu sana linalohusu haki ya kikatiba lililotokea wakati wa utangazaji huo.

Kwa mara ya kwanza toka ateuliwe kuwa Rais, tumepata fursa ya kumsikiliza akiulizwa maswali ya ‘papo kwa hapo’ na waandishi wa habari. Tukumbuke kuwa kutokana na sababu za kisiasa, wakati wa kampeni hatukupata fursa ya kumwona Rais Magufuli katika ule Mdahalo wa Wagombea Urais ulioandaliwa na taasisi ya Twaweza na kuendeshwa na mwanamawasiliano Maria Sarungi Tsehai. Pia hatujui kwa nini hatukuweza kumsikiliza akihojiwa na BBC Swahili Dira TV katika vipindi vya mfulululizo vya kuwahoji wagombea viliyoendeshwa na mwanahabari Zuhura Yunus.

Nafasi ambayo angalau tuliipata ni ile ya kusoma mahojiano yake ya kimaandishi na gazeti mojawapo linaloheshimika nchini. Hata fursa hiyo haikukidhi hitaji la tuliotaka kumsikia Magufuli akijibu kwa uwazi maswali magumu ambayo yamekuwa yanawasumbua wadadisi kwa muda. Mmoja wa waasisi wa gazeti hilo alikuwa na haya ya kusema kuhusu mchakato huo wa kujitahidi kumhoji:

“Kwa mfano, gazeti hili lilipata fursa ya kumhoji siku za hivi karibuni, na akaelekeza apelekewe maswali kabla ya siku ya mahojiano. Pamoja na kupeleka maswali kabla ya mahojiano, alishindwa kujibu maswali aliyoyaona kama nyeti. Mojawapo ya maswali yaliyomshinda ni lile lililohusu “uuzaji” wa nyumba za serikali (uuzaji ambao kwa kweli haukuwa uuzaji bali ugawaji). Swali hilo lilimshinda kujibu pamoja na kuwa alikuwa amekwisha kupelekewa maswali kabla ya mahojiano” – Jenerali Ulimwengu (30 Septemba 2015: http://www.raiamwema.co.tz/magufuli-anakikimbia-chama-chake-au-chama-kinamkimbia#sthash.RWSF2xlM.dpuf)

Baada ya kurejea historia, ama muktadha na usuli, huo kwa ufupi, tujikite katika tukio la leo kama lilivyorekodiwa katika vyombo vya habari. Hapo tunamwona Rais Magufuli akianza na maneno haya: “Waheshimiwa sana Waandishi wa Habari, nimewaiteni kwa ghafla sana ili kukwepa yale mambo ya ‘breaking news’. Kwa hiyo ‘breaking news’ zina-‘break’ sasa hivi…” Kisha tunamwona Rais wetu akiongelea jinsi gani ambavyo kumekuwa na ‘speculations’ (minon’gono/utabiri) kuhusu Baraza la Mawaziri na kukikiri kuwa sisi wanananchi tumesubiri kwa muda mrefu. Pia tunamwona akitambua hitaji letu – ama haki haki yetu – ya kujua/kufahamu.

Maneno hayo ya awali yanadhihirisha kwamba Rais anaelewa fika kuwa kupashana kwa uwazi na ukweli habari za uhakika husaidia kuzima min’ong’ono. Pengine ndiyo maana baada ya kutangaza Baraza lake dogo la Mawaziri, linalomjumuisha Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, kama Waziri wa Habari n.k., akamalizia kwa kusema: “Labda kuna maswali kidogo, moja, mbili.”

Sasa hapo ndipo tunapoona kile ambacho ama ni uwezo mdogo wa waandishi wetu wa habari kuuliza maswali muhimu au ni umahiri wa Rais ‘kupotezea.’ Watetezi wa wanahabari wanaamini ‘kuuliza si ujinga’ kama walivyonena Wahenga wetu. Ila watetezi wa Rais wanaamini kuwa hakuna muda wa kupoteza, hivyo, wanahabari wafanye kazi yao kwanza (homework), maana sasa “hapa kazi tu.”

Tuanze na haya maswali na majibu yaliyokuwa kifungua pazia:

Mwanahabari: Katika kutaja hizi Wizara na Mawaziri kuna baadhi ambazo hukutaja na kusema bado hujapata hao mawaziri. Tungependa kujua tatizo ni nini hasa? Wabunge wa Jamhuri ya Muungano kutoka chama chako hawana sifa au nini hasa kimetokea?


Magufuli: Mimi nakushukuru swali lako. Umeniuliza….Mimi nilitegemea ungeniuliza kwa nini sikuteua siku hiyo hiyo nilipoteuliwa. Nimeamua nianze na hawa. Hao waliobaki wanne nao wataingia baadaye. Kwa hiyo subira yavuta heri. Usiwe na haraka.

Jibu hili katika medani ya siasa na stratejia ni zuri sana kwa kuwa halimpi muuliza swali kila kitu kilichopo ‘jikoni’ au kile kinachoendelea ‘nyuma ya pazia.’ Lakini kwa kufanya hivyo pia linaweza kuchochea zaidi ‘minong’ono (speculations). Kwa mfano, wapo wadadisi wa mambo ambao wanaamini kwamba kuna uwezekano kwamba Rais anataka kufanya kile ambacho Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amefanya, yaani, kusimamia Wizara fulani mwenyewe. Pia wapo wachunguzi wa mambo ambao wanaona hii ni ishara kwamba kuna msuguano wa ndani kwa ndani ‘chamani/serikalini’ kuhusu nani hasa anatakiwa kuwa Waziri wa Wizara nyeti sana ya fedha (hasa ukizingatia huko ndiko Rais alipoanza nako alipofanya ziara ya kushtukiza na pia ndipo ambako kunalengwa na ule upelelezi wa taasisi ya uchunguzi wa matukio ya kifisadi ya Uingereza ijulikanayo kwa kifupi kama SFO).

Pia inafanya watu wajiulize iweje kiongozi mwenye uzoefu wa hali ya juu katika kuendesha Wizara ya Ujenzi atumie muda mwingi kumtafuta ‘mrithi’ wake. Hali kadhalika inafanya watu wahoji ni kwa nini Waziri wa Elimu asubiriwe hivyo ilhali hii ni Desemba 2015 na kuna kazi ya ziada ya kutimiza ahadi ya elimu bure kwa shule za Msingi na Sekondari ifikapo Januari 2016.

Tunapokuja kwenye swali la pili kuhusu Wizara gani zitaungana na TAMISEMI kuhamia Dodoma ambako ndipo yalipo Makao Makuu ya nchi yetu, Rais anatoa jibu hili linalofanana na kile alichokuwa akikisema wakati wa Kampeni: “Kuhusu Dodoma tutatekeleza yaliyopo kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi.” Katika aya ya 151 ya ilani hiyo yenye kichwa cha habari cha ‘Kuhamia Makao Makuu Dodoma’ tunakutana na maneno haya ambayo kwa kiasi kikubwa yanazima min’ongono (ama matamanio) ya Magufuli, Ikulu Kuu na Wizara zote za Serikali kuhamia huko hivi karibuni:

Chama Cha Mapinduzi kinatambua jitihada zilizofanywa na Serikali za kuunganisha mji wa Dodoma na mikoa mingine kwa njia ya barabara zalami. Aidha, baadhi ya majengo ya Serikali yameendelea kujengwa Dodoma likiwemo jengo la Bunge, Benki Kuu, Hazina, Chuo Kikuu cha Dodoma na Shirika la Nyumba la Taifa limejenga nyumba kwa ajili ya makazi ya wananchi. Katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani hii ya 2015-2020, Chama Cha Mapinduzi kitaielekeza Serikali kufanya yafuatayo:-


(a) Kutunga Sheria itakayoutambua mji wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi;


(b) Kusimamia azma ya Serikali ya kuhakikisha majengo yote ya Wizara za Serikali yanajengwa Dodoma badala ya Dar es Salaam; na


(c) Kuongeza kasi ya kupima viwanja kwa ajili ya makazi, viwanda na taasisi na kuendelea kuiweka miundombinu ikiwemo maji, umeme na barabara.

Pengine swali la tatu kuhusu ‘Semina Elekezi’ na jibu lake ndilo limekonga sana nyoyo za walio wengi. Hapa tunamwona Rais ambaye (‘mpaka sasa’) ameonesha nia ya dhati na ujasiri wa wazi wa kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Umma/Serikali akisema bajeti ya semina hizo (“zaidi ya shilingi bilioni 2”) zitaelekezwa kwenye shughuli “muhimu zaidi” za kimaendeleo. Itakumbukwa kwamba wafaidika wakuu wa semina hizo zilizoasisiwa na Rais wa Awamu ya Nne hotelini Ngurdoto mjini Arusha, Jakaya Kikwete, walilazimika kuachia ngazi, miaka miwili na ushee tu baada ya ‘kupigwa msasa’, pale aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu kwa kashfa ya Richmond mwaka 2008 na hivyo kupelekea Baraza la Mawaziri kuvunjwa na kuundwa ‘upya’.

Swali la Mhariri Manyerere Jackton wa gazeti la Jamhuri kuhusu gharama zilizookolewa kwa kupunguza ukubwa wa baraza nalo lilipelekea Rais ampe ‘kazi’ ya ziada ya kwenda kupiga mahesabu. Pia lilitupa fursa ya kujua kwamba, kumbe, Magufuli alijiandaa kwa maswali yanayohusu miundo ya mabaraza ya mawaziri kwa kuja na kabrasha lenye takwimu za mabaraza mbalimbali duniani.

Pamoja na kwamba swali lifuatalo lilitoka ‘nje ya mada/tukio’, ni dhahiri kwamba tunahitaji kupata jibu hilo na huu sasa ni wakati mwafaka kwa mhusika ama msemaji rasmi kutupasha habari:

Mwanahabari: Mheshimiwa Rais, wakati unaongea na Wafanyabiashara ulitoa siku saba; wale ambao walikuwa wamekwepa kulipa kodi walipe zile hela. Na kumbukumbu zinaonesha siku saba zimetimia, zile hela zimesharejeshwa?


Magufuli: Swali lako nenda kamuulize Kamishna Msaidizi wa TRA

Ukakasi unajitokeza (zaidi) pale wanahabari walipojaribu kuhoji mantiki ya idadi ya manaibu waziri kwa kuzingatia uunganishaji wa wizara na vigezo vilivyotumika kuwarudisha mawaziri kadhaa kutoka kwenye Baraza lililopita. Yafuatayo ni majibu waliyopewa:


Magufuli: Kafanye utafiti kwanza uangalie hiyo Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia sera, Bunge, ajira, vijana, walemavu, tumeunganisha Wizara ngapi… tumeweka Manaibu Waziri wawili. Utapata jibu lake.


Magufuli: Kwanza kwa sababu umekosea hata kupiga hesabu, kafanye hesabu vizuri. Kwa awamu iliyopita Mawaziri waliorudi ni saba sasa umesema kumi. Kwa hiyo, ukirudi huko ukapiga vizuri hesabu zako, utaelewa ni vigezo gani nilivyovitumia.


Ingawa kimahesabu, Waziri kama Profesa Mwijarubi Muhongo hakuwa kwenye Baraza lililopita, kimantiki ni sehemu ya lililowahi kuwa Baraza la Mawaziri la Rais Kikwete kabla ya kulazimika kujiuzulu kutokana na sakata endelevu la akaunti ya Tegeta Escrow. Hivyo, wanahabari wanahitaji kujua kwa nini amerudi. Vivyo hivyo wanastahili kujua kwa nini Dakta Hussein Mwinyi amerudi hasa baada ya zile kadhia ya ulipukaji wa mabomu Mbagala na Gongo la Mboto. Pia wanataka kujua imekuwaje Dakta Harrison Mwakyembe karudi ukizingatia kuna ‘utumbuaji majipu’ katika Wizara aliyekuwepo kabla, yaani ya Uchukuzi n.k.

Lakini pia ukitumia mantiki ya kwamba hata waliokuwa Manaibu Mawaziri nao walikuwa ni sehemu ya Serikali ya Awamu ya Nne, unajikuta na majina mawili tu ambayo yanaonekana kuwa mageni miongoni mwa Waziri kamili – Nape Nnauye na Dakta Augustine Mahiga. Ila hata wao wamekuwa sehemu ya tawala zilizopita kwa kushika nyadhifa kubwa kwenye medani za itikadi au intelijensia na diplomasia katika chama au serikali. Ndiyo maana kuna kiu ya kujua ni vigezo gani hasa vimetumika au ni ‘suluhu tu ya kichama.’

Cha kushangaza pia ni kwamba wanahabari, wakiwamo wanawake waliouliza maswali leo, hawakuibua swali zito la usawa/uwiano wa kijinsia. Hesabu za haraka haraka zinaonesha kuwa mawaziri kamili wanawake ni watatu tu kati ya mawaziri kamili kumi na tano ambao wamekwishatangazwa. Na hiyo ni sawa na takribani asilimia 20 tu. Na ikitokea, kwa ‘bahati iliyoje’, mawaziri wanne waliobakia wote wakawa wanawake basi hiyo asilimia itapanda kiasi na kuwa asilimia 36 na ushee. Ila tukiwajumlisha na manaibu wao basi idadi ya wanawake inakuwa ni nane kati ya thelathini, hiyo ikiwa ni takribani asilimia 26. Wale wanne waliosalia nao wakiwa wanawake basi idadi hiyo itakuwa ni kumi na mbili kati ya thelathini na nne, ikiwa ni sawa na asilimia 35 na ushee. Katika jamii ambayo wanawake ni wazalishaji na walishaji wakuu licha ya uwepo wa ‘mfumo dume’, kaulimbiu ya ‘hapa kazi tu’ inawahusu na hakika wanastahili kujulishwa ni kwa nini hizo asilimia ziko hivyo.

Wahenga walinena kuwa ‘nyota njema huonekana asubuhi’ na ‘dalili ya mvua ni mawingu’. Kipindi hicho kifupi cha maswali na majibu kati ya Wanahabari na Rais kinaweza kutupa mwelekeo wa huko tuendako. Japo madai ya Katiba mpya yanazidi kusahaulika katika kipindi hiki cha mwamko wa ‘Magufulika’, tukumbuke kuwa hata hii Katiba ya Mwaka 1977 tuliyonayo inasisitiza kwamba:

“Kila mtu… anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii” – Ibara ya 18 (d)

Lakini pia Ibara ya 18 (b) ya Katiba hiyo tuirekebishayo inasema:

“Kila mtu… anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi”

Kupewa taarifa ni haki. Na kutoa habari ni kazi. Hapa hakikazi tu.