Na Abdilatif Abdalla
Nami nambe, niwe kama waambao
Niupambe, upendeze wasomao
Niufumbe, wafumbuwe wawezao
Kuna mamba, mtoni metakabari
Ajigamba, na kujiona hodari
Yuwaamba, kwamba ‘taishi dahari
Memughuri, ghururi za kipumbavu
Afikiri, hataishiwa na nguvu
Takaburi, hakika ni maangavu
Akumbuke, siku yake ikifika
Roho yake, ajuwe itamtoka
Nguvu zake, kikomoche zitafika
Afahamu, mtu hajuwi la kesho
Hatadumu, angatumiya vitisho
Maadamu, lenye mwanzo lina mwisho
———————————————-
*Shairi limechapishwa kwa idhini ya Abdilatif Abdalla
**Katuni imetumikwa kwa idhini ya Masoud Kipanya
Comments are closed.
Yote I walaza chali, ina ghururi dunia. Ahsante Abdulatif
Duh! Huyu mamba hatari!!
Nguvu ya Mamba ku’ mai
Mamba anenwae hapa ni yupi?
Tuelezwe au aulizwe malenga Abdulateef Abdalla huyo mamba ni nani? Kwani hapa Taswira iliopo ni mtu ila kafafanishwa na Mamba, suala huyu Mamba ni nani? Naomba nifumbuliwe Kitandawili.